32. MWANA ASO MTEMBEZI
Kwa jina Mwanzamkwao, ulo mwingi wa mbawazi,
Mgawa haki kigao, ni barika ya Azizi,
Ukwapi hata utao, ziumane beti hizi,
Mwana aso mtembezi hachi kusifia kwao.
Hachi kusifia kwao, mwana aso mtembezi,
Maneno kila uchao, mamaye ndiyo mjuzi,
Humsifu kwa matao, aupikavyo mchuzi,
Mwana aso mtembezi hachi kusifia kwao.
Hachi kusifia kwao, yamemziba maozi,
Hatoki nyumbani mwao, thama kangiwa ubozi
Angauza wapitao, apate masimulizi,
Mwana aso mtembezi hachi kusifia kwao.
Hachi kusifia kwao, yamemlevya malezi,
Amepigwa mzumbao, mengine hajamaizi,
Walisema mtu kwao, sikuacha utembezi,
Mwana aso mtembezi hachi kusifia kwao.
Hachi kusifia kwao, ja vile msimaozi,
Aliyeona mng'ao, unapo andama mwezi,
Haumwishi mshangao, kwenye yake maongezi,
Mwana aso mtembezi hachi kusifia kwao.
Hachi kusifia kwao, nafanya ukomelezi,
Ni mvuli niwambao, mfungue masikizi,
Msambe ino ni mwao, nafanya uelekezi,
Mwana aso mtembezi hachi kusifia kwao.
MKANYAJI
HAMISI A.S KISSAMVU
kutoka (Baitu shi'ri)
MABIBO * DSM.(
)