esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 555
TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), imejipanga kuanza kutoa huduma za mionzi kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kusoma picha za X-Ray.
Kupitia huduma hiyo, mashine za kisasa zitafungwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya kupokea picha zitakazotumwa kutoka katika hospitali mbalimbali nchini na madaktari bingwa wa mionzi watazisoma na kurudisha majibu kwa muda mfupi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alibainisha hayo juzi wakati akikagua chumba hicho maalum cha kusomea picha za X-Ray katika taasisi hiyo. Alisema kuwapo kwa chumba hicho na mashine za kisasa kutawezesha mgonjwa kupata majibu ya tatizo alilo nalo ndani ya muda mfupi na kuanza kupatiwa matibabu.
"Badala ya kuweka picha katika chumba cheusi katika mfumo ambao unatumika sasa, madaktari wetu wataanza kutumia kompyuta kusoma picha hizo zitakazotumwa kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi," alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Respicious Boniface, alisema wana madaktari bingwa wa mionzi ambao wana uwezo wa kutoa huduma hizo kwa ufanisi na wapo tayari kwa ajili ya kufanya kazi kwa saa 24.
Naye daktari wa mionzi, Mechris Mango, alisema kitengo hicho kinaweza kusoma picha 300 za X-Ray kwa siku na kurudisha majibu kwa mgonjwa kwa muda mfupi.
"Kitengo chetu tunapokea picha za X-Ray ambazo tunatumia teknolojia ya kompyuta kuzisoma na kurudisha majibu muda mfupi, urahisi wake ni kama kupokea ujumbe mfupi wa maneno na kurudisha majibu kwa uharaka huo huo," alisema Dk. Mango. Alisema picha zitakazotumwa ni zile ambazo madaktari wameshindwa kuzisoma kwa urahisi, hivyo kutakiwa kutumia utaalamu zaidi kusoma kutoka katika kitengo hicho kuziandikia ripoti ya majibu ya tatizo lililobainika.