Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,482
MBUNGE WA Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF)
Tuesday, Desemba 16, 2014
MBUNGE WA Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), amesema ni vigumu vyama vya siasa vilivyopigania Uhuru kuondolewa madarakani kirahisi kwani vyama hivyo vina nyenzo za kushinda uchaguzi kwa gharama yoyote.
Mnyaa aliyasema hayo katika mahojiano Maalumu na Majira mwishoni mwa wiki akiwa mjini Mbeya. Alifafanua: "Ujio wa vyama vingi vya siasa katika nchi nyingi za Afrika, umegubikwa na ukiritimba wa vyama tawala kuhodhi vyombo vya dola ili viwasaidie kwenye chaguzi zinazoendelea katika nchi hizo."
Alisema fursa pekee ya ushindi kwa vyama vya upinzani ni kuondokana na ubinafsi, tamaa ya madaraka, na badala yake ni kujenga umoja utakaoweza kukiondoa chama tawala madarakani.
Alitoa mfano kuwa, nchi za Afrika zilizofanikiwa kuviondoa vyama vinavyoshika dola madarakani kama Kenya, Zambia na Malawi, vyama vya upinzani vilifanikiwa baada ya kuunda umoja wao na kuviondoa vyama vilivyopigania uhuru.
"Tumeshuhudia Kenya KANU ikianguka, Zambia UNIP kikiondolewa madarakani…hapa kwetu UKAWA ukiimarishwa CCM itaong'oka," alisema Mnyaa ambaye pia ni Mjumbe anayewakilisha Bunge kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Aliongeza kuwa, tatizo la ubinafsi katika vyama vya upinzani ndilo linalosababisha vyama hivyo kuendelea kushindwa kwenye chaguzi mbalimbali zinazoendelea, hivyo upo uwezekano wa CCM kuendelea kuwepo madarakani kwa miaka mingi ijayo kama wapinzani hawatabadili mtazamo wao kwenye jamii.
"Yapo matumaini makubwa ya UKAWA kufanya vizuri, tumejipanga vyema kwa mikakati na tutasimamisha mgombea mmoja wa Urais ambaye hatutamweka hadharani kwa sasa."
"UKAWA imeweka mipango mizuri ya mgombea wa Urais ambaye hawezi kuwekwa bayana mapema ili kuepuka hujuma za chama tawala," alisema Mnyaa.
Chanzo: Majira