Lonestriker
JF-Expert Member
- Oct 8, 2010
- 640
- 241
Wakati fulani nikiwa mdogo baba yangu alirudi nyumbani na suruali nzuri sana ya dangrizi kama zawadi yangu katika sherehe yangu ya kuzaliwa zaidi ya miezi miwili mbele.
Marufuku ilitoka nisijaribu kuivaa kwa namna yoyote ile kabla ya siku lengwa kuwadia. Yalikuwa mateso makubwa ya Kisaikolojia , nilibaki kuikodolea macho kila uchao .
Nilikuwa nikiwaza muonekano wangu na mikogo mbalimbali kwa ndugu na rafiki zangu. Mashabiki, wanachama na wadau wa Yanga SC wameingia katika umbwe hili juu ya usajili iliofanywa na klabu yao juu ya mlinzi wa kati toka nchini Togo, Vicente Bossou.
Si lazima kila anayesajiliwa aingie kikosi cha kwanza nakuanza kuvuma lakini vilevile shaka huja pale unapomsajili mchezaji na kumweka kando kwa takribani mechi tano mfululizo katika ligi ukizingatia thamani ya mchezaji .
Usajili kiufundi, mbinu na kimfumo hufanyika kukidhi hitaji fulani la timu kwa mashindano yaliyopo ili kutengeneza maelewano mazuri ya timu kiushindani.
Ina maana mtogo huyo hakuwa chaguo la kocha? Au ni usajili kwa mahitaji ya baadae? Au bado embe hilo halijakomaa vyema basi linaendelea kuvundikwa?
Mwisho wa siku mwalimu ndio atakuwa na majibu sahihi lakini tujiulize, Nadir , Yondani, Twite na Pato Ngonjani hawa wote ni walinzi wazuri wa kati.
Kuna nafasi ya mtogo huyo kucheza na ilihali tuliona uzito wake katika mechi za kirafiki? Hata hivyo, jibu linalotoka vinywani mwa viongozi mwa Yanga ni kuwa bado utimamu wake wa mwili hauko sawa.
Lakini hapo nawaza miili ya Ngoma na Kamusoko ilikuja na viongeza-nguvu gani kiasi cha kufunguka moja kwa moja? Tuendelee kuisubiri suruali yetu , siku ya sherehe ikifika tutaivaa .
Ikitupwaya tukae kimya, ikitubana tunyamaze kabisa lakini ikitutosha vyema tuinue bega moja kwa mikogo.
Chanzo soka360