Fortunatus Buyobe
JF-Expert Member
- Nov 9, 2011
- 463
- 1,128

MMILIKI wa Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), Robert Kisena ameingia katika kashfa mpya, safari hii akidaiwa kuvamia kiwanja cha mfanyabiashara mwenzake, Alex Msama.
Mbali ya kuvamia eneo hilo lililoko Mbagala Kokoto jijini Dar es Salaam, Kisena anadaiwa pia kuvunja amri ya mahakama ya kusitisha ujenzi katika eneo hilo hadi kesi ya msingi itakapomalizika.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa sasa, umebaini kuwa mgogoro huo wa ardhi unaligusa Jeshi la Polisi ambapo inadaiwa kuwa baadhi ya vigogo wanamlinda Kisena kiasi cha kuwa na jeuri ya kuvunja amri ya mahakama.
Tanzania Daima ilipofika eneo hilo wiki iliyopita, ilishuhudia mafundi wa Kisena wakiendelea na kasi ya ujenzi, huku baadhi ya askari polisi na mabaunsa wakilizingira kwa ulinzi.
Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi, Msama ndiye mmiliki halali wa eneo hilo ambalo awali lilikuwa mali ya Benki ya Nyumba (THB).
Tayari Mahakama Kuu imeshatoa zuio la kutoendelea na shughuli zozote za ujenzi katika eneo hilo hadi hapo kesi ya msingi itakapomalizika.
Kwa mujibu wa hati za mahakama zilizobandikwa kwenye kuta za jengo linaloendelea kujengwa, zuio la kwanza lilitoka Desemba 3 mwaka huu.
Diwani afichua siri
"Zuio hilo liliwekwa na wafanyakazi wa Manispaa ya Temeke, lakini wasimamizi kutoka UDA walipowaona waliwatisha kwamba aliyevamia eneo hili ana nguvu kubwa, hivyo waangalie wasije wakahamishiwa Tandahimba.
"Desemba 6, aliweka tena zuio lingine (Stop Order) ya Mahakama Kuu iliyokuwa inasema kuwa atakayeonekana katika eneo lile akamatwe, lakini pamoja na zuio hilo, mafundi wa Kisena waliendelea na ujenzi kama kawaida huku polisi wakishindwa kuchukua hatua," alisema Diwani wa Kata ya Mbagala, Hadson Kamonga.
Diwani huyo akizungumza na gazeti hili, alisema kuwa eneo hilo lina mgogoro ambao upo mahakamani ila anashangaa kuona UDA haina karatasi inayoonyesha kuwa eneo hilo ni la kwao.
"Cha kushangaza zaidi ni pale tunapoona UDA waliovamia hapa hawana karatasi yoyote inayoonyesha kuwa ni eneo lao kihalali, lakini Msama anazo, sasa tunashangaa UDA wanatoa wapi jeuri ya kudharau amri ya Mahakama Kuu.
"Eneo hili lina mgogoro mkubwa ambao upo mahakamani, na inaonekana sheria inadharauliwa, yaani mtu anatumia jeuri tu kudharau amri ya mahakama, hii ni mbaya, mimi nashauri kuwa sheria ichukue mkondo wake ili haki itendeke," alisema diwani huyo.
Kisena analitaka eneo hilo kwa ajili ya kujenga ofisi na kituo cha mabasi ya UDA.
Akifafanua zaidi, diwani Kamonga alisema wakati wakitambua kuwa eneo hilo ni mali ya Msama, hivi karibuni Kisena alivamia kinguvu na kupaki magari yake na kuanza ujenzi wa ofisi zake kibabe.
Alisema baada ya Msama kusikia hivyo, alikwenda kuvunja sehemu iliyokuwa imejengwa.
"Mimi nilishangaa baada ya Msama kupeleka polisi hati zake za umiliki ili watende haki, walimkamata na kumuweka ndani kwa madai kuwa eneo lile ni la Kisena, lakini aliachiwa kwa dhamana.
"Msama alihoji kwanini mali yake imegeuka kuwa ya Kisena, ndiyo polisi wa kituo kile wakamwambia Kisena amefungua kesi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi pale Wizara ya Mambo ya Ndani akidai kuwa lile ni eneo lake," alisema Kamonga.
Kauli ya Kisena
Alipohojiwa juu ya tuhuma za kuvamia eneo hilo na kukaidi amri ya mahakama, Kisena alimtaka Msama wakutane naye kujadili na kufikia muafaka wa mgogoro huo.
"Mimi nafikiri Msama akitaka jambo hili limalizike vizuri, aje tuzungumze, akitumia vyombo vya habari itakula kwake," alisema Kisena.
Mmiliki huyo wa UDA alisema mgogoro uliopo katika eneo hilo ni kati ya Msama na wenzake, lakini sio na UDA, hivyo hata zuio hilo halihusiani na kampuni ya UDA.
Msama naye afunguka
Kwa upande wake, Msama alisema kuwa eneo hilo ni lake, analimiki kihalali, lakini alishindwa kuzungumza kwa undani kuhusu mzozo huo kwa kuwa kuna kesi Mahakama Kuu.
"Eneo hili ni langu, lakini kuna kesi ya msingi Mahakama Kuu kati yangu na African Relief Committee of Kuwait na kuna zuio la Mahakama Kuu ambalo limezuia mtu yeyote katika viwanja hivyo, PLOT 141/3/141/4, asijenge wala kufanya shughuli yoyote katika viwanja hivyo hadi kesi ya msingi itakapokwisha.
"Kimsingi tunaheshimu amri ya mahakama tukisubiri kesi ya msingi iishe, lakini Kisena amekuwa akiendelea na ujenzi kwa makusudi kabisa bila kujali amri ya Mahakama," alisema.
Msama pia alisema mahakama imetoka zuio jingine linalosema mtu yeyote atakayefanya shughuli yoyote katika eneo hilo akamatwe na kufikishwa mbele ya Mahakama Kuu, jambo la kushangaza Kisena ameendelea kudharau mahakama na anaendelea na ujenzi na polisi wanatoa ulinzi kwa wafanyakazi wa kampuni yake.
Alisema anaamini sheria itachukua mkondo wake ili kuhakikisha mgogoro huo unamalizika na ukweli kubainika.
Source: Tanzania daima