Zapa RadioFm
Senior Member
- Feb 12, 2016
- 112
- 171
MKURUGENZI ILALA AKUBALIANA NA MAAGIZO YA MEYA.
Sakata la wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu wamachinga kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala limegonga vichwa kwenye vyombo vya Habari kuanzia tarehe 06/05/2016 ya wiki iliyopita.
Sakata hilo lilianza Mara baada ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala bwana Isaya Mngurumi kutangaza kuwa ndani ya siku mbili wamachinga waondoke katikati ya jiji la Dar es salaam hasa maeneo ya Kariakoo na Karume. Maamuzi hayo ya Mkurugenzi yalipingwa na Madiwani wa Ilala, hususani Madiwani wa UKAWA kwa madai kuwa maeneo husika wanakopelekwa wamachinga lazima kwanza miundombinu ile ya lazima, iboreshwe kwa kiwango cha kuridhisha.
Baada ya Madiwani kupinga tamko la Mkurugenzi, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala mhe. Charles Kuyeko alitoa agizo kwa Mkurugenzi kuwa asitishe zoezi la kuwaondoa wamachinga kwa nguvu, zoezi ambalo lilikuwa lifanyike kuanzia Jana tarehe 09/05/2016. Mhe. Kuyeko alimtaka Mkurugenzi atekeleze maazimio ya baraza LA Madiwani la kukamilisha ukarabati wa miundombinu katika masoko ambayo wamachinga watapelekwa.
Maagizo ya mhe. Kuyeko na madiwani yaliungwa mkono na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam mhe. Paul Makonda. Hatua hiyo ya Mkurugenzi ya kufanya maamuzi ya kukurupuka bila hata kumshikisha Meya ambaye kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kiuongozi, Meya ndiye Msimamizi na Msemaji mkuu wa Manispaa ya Ilala, yalimfanya mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kuitisha kikao, kikao ambacho kiliwashirikisha Mstahiki Meya, Naibu Meya, Mkurugenzi na wenyeviti wa kamati za kudumu za Baraza la Madiwani ili kujadili sakata hilo la wamachinga. Katika kikao hicho Makonda alimkemea Mkurugenzi na kumtaka aache kufanya maamuzi yanayoihusu Manispaa bila kujua. Ili Ilala ipate maendeleo ni lazima tushirikiane viongozi wa kiserikali na viongozi wanaowakilisha wananchi alisema Makonda.
Katika kikao hicho Mkurugenzi alikiri kosa na kuahidi kushirikiana kwa dhati na Meya na Madiwani kwa ujumla. Na katika kuonyesha ushirikiano huo Leo kwa pamoja wameongea na waandishi wa habari na kueleza mwelekeo wa suala la wamachinga kwa Manispaa ya Ilala.
Katika mkutano wa Leo na waandishi wa habari Mkurugenzi ametoa tathimini ya ukarabati wa miundombinu ya masoko ambayo wamachinga watapelekwa ambapo alisema miundombinu hiyo imekamilika kwa asilimia kubwa, hivyo wanaweza kuanza kuhamia katika masoko hayo.
Aidha, Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala mhe. Omary Kumbilamoto akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari alisema Mara baada ya kikao na mkuu wa Mkoa hapo Jana, Meya alimwagiza yeye (Naibu Meya) akajiridhishe na ukarabati wa miundombinu katika masoko husika. Baada ya kutembelea masoko hayo alikuta ukarabati ukiendelea kufanyika hivyo kwa sasa wamachinga wanahaki ya kuhamia.
Mhe. Kuyeko alijiridhisha na hatua ya uboreshaji wa miundombinu ya masoko hayo alisema sasa anawataka wamachinga waanze kuhamia maeneo hayo kuanzia sasa bila kusubiria kuhamshwa kwa ngumu. Wamachinga tunawapenda, ni walipa Kodi wetu hivyo nawaomba waondoke katikati ya jiji kwa hiyari yao, na Manispaa itashirikiana nao kwa kila hatua.
Imetolewa Leo 10/05/2016
Na Alex Massaba
Katibu wa Meya Manispaa ya Ilala.