USITISHA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA STASHAHADA (DIPLOMA)
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuutaarifu umma kuwa imesitisha mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma
stashahada (Diploma) kuanzia mwaka wa masomo
2018/2019 kama ilivyotangaza awali.
Itakumbukwa kuwa tarehe
10 Mei mwaka huu, HESLB ilitoa mwongozo unaosimamia utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo
2018/2019. Mwongozo huo, pamoja na mambo mengine, unaeleza kuwa HESLB itaanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na kuwa mwongozo kuhusu utaratibu wa kuomba mikopo hiyo ya wanafunzi wa stashahada ungetolewa baadae.
Hatua hii imechukuliwa ili kuhakikisha kuwa kiasi chote cha
TZS 427.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka
2018/2019 zinaelekezwa kwa wanafunzi wenye mikopo hivi sasa na waombaji wapya wahitaji ambao wana sifa za kujiunga na kozi za shahada tu ambao ndiyo walengwa wakuu.
Hivyo basi, tunatoa wito kwa wanafuzi wote wenye sifa za kujiunga na masomo ya shahada katika taasisi za elimu ya juu na ambao ni wahitaji wa mikopo kuhakikisha wanasoma kwa makini mwongozo wa utoaji mikopo na kuuzingatia.
Kwa takwimu za mwaka
2017/2018, takribani maombi
10,027 ya mikopo yaliyowasilishwa Bodi ya Mikopo yalikuwa na upungufu kama vile kutosainiwa, kutokuwa na viambatanisho sahihi n.k.
HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na pia kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika.
Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Jumapili, Juni 3, 2018