Ahahahahahhahaha niko makini
RIWAYA: DAMU YA MWANAMWALI
MTUNZI: ALLY KATALAMBULA
SIMU: 0687750295 AU 0762 439947
SEHEMU YA 11
“Nambie Issa?”
“Mkeo amefika gesti, yupo na hawara wake.”
“Eeeeh!!” nilihamaki
“Ndiyo, kafika yupo na bwana wake, fika fasta basi eneo la tukio tumalize kazi,” Issa alisisitiza, nilihisi kitu ndani ya kifua changu kikilipuka kama bomu.
SONGA NAYO...
KITENDO cha kuambiwa mke wangu alikuwa gesti na mwanaume mwingine kilinishitua sana.
“Nakuja fasta Issa,” nilimwambia na kukata simu.
Sikuwa na habari tena na simu ya mama ambayo nilikuwa nimeihold, jambo pekee lililokuwa akilini mwangu ni kufika gesti ya Madrid na kushuhudia uchafu anaofanya mke wangu Nasra Mfaume.
Bila kuwaaga wafanyakazi wangu, nilikurupuka na kutoka nje ya duka, nikaona nikitumia gari langu naweza kuchelewa eneo la tukio, nilichofanya ni kuchukua bodaboda.
Dakika kumi na tano badaye, nilikuwa Kinondoni, niliwasiliana na Issa akanieleza mahali walipokuwa wamebana, walikuwa kwenye glosari moja iliyokuwa mita kama 100 kutoka kwenye gesti aliyokuwa mke wangu.
“Umechelewa sana Faraji,”Issa alinipokea na lawama.
“Samahani Issa, mambo ya foleni, si unajua mji wetu huu.”
“Unajua madhara ya kuchelewa hivi, inawafanya wagoni wetu wapate wasaa wa kufanya malovee,” Issa aliniambia, maneno yale yalikuwa mkuki wa moto kifuani.
“Kwa hiyo unataka kusema, hadi wasaa huu mke wangu na hawara wake watakuwa wamekwishavunja amri ya sita?”
“Kwa muda huu watakuwa wako katikati ya raha ya penzi, hawajamaliza bado,” Issa alisema, hakujua kabisa kama maneno yale, yalikuwa ni sawa na ncha ya sindano kwenye kidonda.
“Sasa tufanyaje?” niliuliza kwa sauti ya unyonge.
“Ngoja niwastue jamaa ili tuingie”
“Jamaa gani”
“Polisi na mwenyekiti wa mtaa.”
“Kumbe hao nao wanahusika?”
“Ndiyo, kwenye mchakato huu inaweza kutokea jinai, polisi na mwenyekiti watasimama kama mashahidi kama ikitokea hali hiyo.”
Baada ya Issa kuwasiliana na watu hao, muda mfupi baadaye mzee mmoja, aliungana nasi. Jumla tukawa watu watatu kwa maana ya waandishi wa habari wawili, mimi na yule mzee ambaye badaye nilimtambua kama mwenyekiti wa mtaa.
Tulizipiga hatua kuikabili gesti ile. Tulipofika mapokezi Issa na mwenyekiti wa mtaa wakajitambulisha kwa binti aliyekuwa mapokezi. Msichana yule aliposomewa tuhuma za nyumba ile kuwa chaka la uzinzi na uasherati kwa wake za watu, hakufanya ukaidi kutoa ushirikiano.
Tuliongozana naye hadi katika chumba alichokuwa mke wangu na bwana wake. Tulipokewa na sauti za mahaba zilizotokea ndani. Miguu yangu nilihisi ikishiwa nguvu.
Mwili ukaninyong’onyea, na kadiri mambo yale yalivyozidi kunisibu, ndivyo kelele za mke wangu aliyekuwa akishughulikiwa ndani, zilivyozidi kuingia ndani ya ngoma ya masikio yangu.
Nikapepesuka kulia na kushoto na bila kutarajia nikajikuta ninaketi kitako sakafuni. Issa na wale waandishi wengine ambao muda ule walikuwa na kamera zao tayari kwa kurekodi kila kitu, wakajikuta katika fadhaa baada ya kuniona nimekaa chini.
“Jikaze bro” Issa akanihimiza, aliongea kwa sauti ya kunong’ona.
Pamoja na kujihakikishia kwamba nilikuwa nimekaa, ajabu bado nilikuwa nahamu ya kuketi, hadi leo huwa nashindwa kabisa kuelewa ile hamu ya kuketi ilikuwa imelenga kuketi wapi zaidi.
“Simamaaa!” Issa akanong’ona tena, safari hii kwa ukali, na muda huohuo mwandishi mwenziye alinifikia na kuninyanyua wima.
Nilikuwa katika mateso makubwa, kitendo cha kusikia sauti ya mke wangu akiwa anafanya mapenzi na mwanaume mwingine ilikuwa ni adhabu nzito mno maishani.
“Gonga mlango” mwenyekiti wa mtaa alimwamrisha yule mhudumu wa kike.
Wakati anataka kugonga, mara akasita.
“Vipi?”Issa aliyekuwa tayari kwa kufutoa picha, alimaka.
“Mlango upo wazi!” mhudumu akasema.
“Eeh!” tukashangaa
“Upo wazi.”
Baada ya mhudumu kusisitiza kwamba mlango ulikuwa wazi, tukio lililofuatia ilikuwa ni kusukuma mlango na kuingia kwa ghafla.
Lahaulaa!!.... Sikuamini macho yangu.
SURA YA SITA
Nasra Mfaume. Mwanamwali wa Kipemba. Mke wangu wa ndoa. Muhibi wa moyo wangu. Alikuwa amekunjwa na mwanaume mrefu mwenye misuli, wakiwa kama walivyozaliwa, walikuwa wakifanya mapenzi. Jamaa alikuwa amemkunja mke wangu kwa mtindo ambao mimi sikuwahi kumfanyia mwanamke huyo hata siku moja.
Nilijikuta nalia kama mtoto mdogo aliyetelekezwa na mzazi wake. Mke wangu mrembo. Niliyempenda kwa dhati. Alikuwa amenipa pigo takatifu.
Baada ya kuona wameingiliwa, walishituka mno. Hawakutegemea kabisa uvamizi ule. Wakiwa kwenye hali ya kuzubaa na taharuki kubwa, Issa na wenzake walikazana kufotoa picha.
Yule mwanaume alikuwa wa kwanza kugutuka na kuona alitakiwa afanye kitu ili kijificha na aibu ile. Haraka, alivuta shuka na kujifunika. Hata hivyo, alikwishachelewa sana. Picha nyingi zilikwishaingia kwenye kamera za waandishi.
Mke wangu naye baada ya kugundua alitakiwa ajistiri, akavuta shuka jingine na kujifunika.
“Tusameheni jaman,” hatimaye jamaa akaongea kwa fadhaa.
Kauli hiyo ilikuwa ni mthili ya petroli katika moto. Iliniudhi sana. Hasira zilinipanda. Nikiwa katikati ya kilio. Nilimsogelea na kumtandika ngumi mbili za uso.
Kufumba na kufumbua, uso wake ukajaa damu. Tukio hilo likamliza mke wangu kwa hofu. Naye akaanza kuomba msamaha. Kitendo hicho kikachochea chuki. Nilitamndika teke la tumboni. Akatapika chipsi kuku alizolishwa na yule bwana.
Mambo yote hayo yalikuwa yakirekodiwa na wale waandishi wa habari chakaramu.
Ndugu msomaji. Nakusihi sana, kama unatabia za kutembea na wake za watu, acha kabisa kamchezo hako. Naijua hali utakayokukuta siku utakapofumaniwa. Nakuhakikishia ndugu yangu, kama umezoea kula vya watu, ipo siku utakamatwa. Usiombe.
Haijalishi una nguvu nyingi, pesa, ama mamlaka katika serikali. Ukifumaniwa na mke wa mtu, ndugu yangu...Utapata tabu sana. Hutowezi kabisa kupambana na mwenye mali. Na siyo siri. Pamoja na sifa zote ulizonazo, lakini mbele ya mume aliyekufuma na mkewe, huna la kufanya. Unaweza jikuta unauawa na mwanaume dhariri, ambaye hajai kiganjani mwako. Waswahili husema:
‘Mke wa mtu ni sumu’
Jamaa pamoja na mwonekano wa mwili wa mazoezi, umarufu, sanjari na fedha zilizompa kiburi hapa mjini, wasaa ule alikuwa zoba, mpole kama kobe.
Baada ya lile teke la tumbo nililomtandika Nasra na kumfanya ajitapikie matapishi, nilimgeukia huyo njemba mwenye misuli thabiti. Nikaendelea kumshushia kipigo cha mbwa koko. Wandishi wa habari wakazidi kurekodi kadiri walivyoweza. kufumba na kufumbua utitiri wa watu wakajaa kwenye gesti ile.
Askari polisi walinituliza kisha wakawataka watu wale wavae nguo. Gumzo kubwa kuzunguka gesti, ilikuwa ni juu ya fumanizi.
Baada ya mke wangu na mtu wake kuvaa nguo, walitolewa nje na kupakiwa ndani ya defender la polisi, wakati mambo yote yanafanyika picha ziliendelea kufotolewa.
Mimi, mwenyekiti wa mtaa, pamoja na mhudumu wa gesti, tukatakiwa kuongozana na polisi wale.
Kwa pamoja tuliingia ndani ya gari la polisi na safari ya kuelekea Kituo cha Osterbay ikaanza.
Baada ya kuwasiri, mke wangu na yule bwana waliingizwa kwenye ofisi za wapelelezi. Mimi nikabakia nje,walichukuliwa maelezo mule ndani, muda mfupi badaye wakatolewa, ikawa zamu yangu kuhojiwa na kutoa maelezo.
Nilitoa maelezo mbele ya askari mpelelezi, nikamueleza kila kitu juu ya usaliti wa mke wangu hadi kumfumania.
“Huyo mwanamke ni mkeo au alikuwa mkeo?” askari kanzu akauliza, baada ya kumpa maelezo.
“Ni mke wangu”
“Mbona yeye anasema wewe siyo mume wake ila ulikuwa mume wake kwa kuwa mlishapeana talaka kitambo sana?”
“Anasema mimi siyo mume wake?” niliuliza kwa mshangao
“Ndiyo. Kwa mujibu wa maelezo yake, anasema mlikwishaachana muda mrefu tu, ila wewe ndiyo unamng’ang’ania” askari yule alinipasha. Nilishusha pumzi ndefu nikaumia sana moyoni.
“Sasa nisikilize kwa makini,” yule mpelelezi aliongea huku akiwa amenikazia macho ya kipolisi.
“Kisheria hakuna kesi ya fumanizi, kwa sababu tendo hilo limefanywa kwa makubaliano ya watu wazima. Neno makubaliano ndiyo linatofautisha na kesi ya jinai iitwayo ubakaji,”aliweka kituo kisha akaendelea kunieleza:
“Kimsingi kama mke wa mtu amefumaniwa linakuwa ni shauri la madai lenye lengo la kudai fidia au kuvunja ndoa na kutoa talaka.”
“Unaweza kufungua shauri mahakamani kwa kudai fidia kwa kudhalilishwa au kuvunja ndoa yenu kwa kuiomba mahakama isimamie utoaji wa talaka,” alihitimisha.
“Nini mantiki ya kunieleza yote hayo?”
“Swali zuri,” alisema. Akaendelea:
“Nataka utambue, katika tukio la wewe kumfumania mkeo, watuhumiwa hawana kesi ya kujibu, hivyo jeshi la polisi, litawaachia huru.”
UKO DAR ES SALAM ? NIKULETEE NAKALA YA KITABU HIKI LEO LEO?
WEKA NAMBA YAKO HAPA CHINI. BEI NI ELFU KUMI (10,000/=)
SIMU YANGU NI 0687750295 AU 0762 439947
WASOMAJI WA MWANZA:
VITABU VINAKUJA SIKU YA JUMAPILI, KAMA BADO HUJAWEKA ODA NI WAKATI WAKO SASA, ACHA NAMBA YAKO HAPO, AU NITUMIE INBOX AMA KWA NAMBA ZANGU HAPO JUU