Mji wa Wathesalonike

Mji wa Wathesalonike

Bujibuji Simba Nyamaume

Platinum Member
Joined
Feb 4, 2009
Posts
77,961
Reaction score
165,352
Wathesalonike walikuwa wakazi wa mji wa Thesalonike, mji uliokuwa katika jimbo la Makedonia ndani ya Dola ya Rumi. Leo, mji huo bado upo na unaitwa Thessaloniki, ukiwa mji wa pili kwa ukubwa nchini Ugiriki baada ya Athene.

Historia ya Thesalonike inaanza karibu mwaka 315 KK, wakati Kassanda, mmoja wa majenerali wa Aleksanda Mkuu, alipounganisha vijiji kadhaa na kujenga mji mpya. Aliupa jina la Thessalonike, kwa heshima ya mke wake aliyekuwa dada wa Aleksanda Mkuu. Tangu mwanzo, mji huo ulikusudiwa kuwa kitovu cha biashara na utawala, na ndani ya muda mfupi ukawa miongoni mwa miji muhimu zaidi katika Makedonia.

Kilichoufanya mji huu ukue haraka ni eneo lake. Thesalonike ulijengwa kandokando ya Bahari ya Aegean, ukiwa na bandari kubwa iliyopokea meli kutoka Asia, Misri, Italia na Ugiriki. Pia ulipitiwa na Via Egnatia, barabara maarufu ya Warumi iliyounganisha Mashariki na Magharibi. Hivyo, kila siku mji huo ulijaa wafanyabiashara, askari, viongozi wa serikali, mabaharia na wasafiri kutoka mataifa mengi. Thesalonike ukawa mji wa watu wa tamaduni tofauti, lugha tofauti na biashara kubwa.

Kama ilivyo kwa lmiji mingine iliyochangamka kipindi hicho,Masoko yalijaa bidhaa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, na bandari yake ilikuwa chanzo kikubwa cha utajiri. Watu wengi walikuwa wafanyabiashara, mafundi, mabaharia na watumishi wa serikali ya Kirumi. Kwa sababu ya biashara hiyo, Thesalonike ulikuwa mji wenye maisha ya pilika pilika nyingi na ushindani mkubwa.

Lakini pamoja na maendeleo hayo yote, hali ya kiroho ilikuwa tofauti.

Wakazi wengi waliabudu miungu ya Kigiriki na Kirumi kama Zeus, Dionysus na Kaisari wa Rumi, ambaye pia aliheshimiwa kama mtawala mwenye mamlaka ya kidini. Kulikuwa pia na ibada za sanamu, sherehe za kipagani na maadili yaliyokuwa mbali na mafundisho ya Mungu.

Hata hivyo, ndani ya mji huo kulikuwa na jamii kubwa ya Wayahudi waliokuwa na sinagogi lao, jambo lililompa Paulo nafasi ya kuanza kuhubiri Injili.

Baada ya kutoka Filipi, Paulo aliwasili Thesalonike katika safari yake ya pili ya umisionari (Matendo 17:1-9). Kama ilivyokuwa desturi yake, alianza kuhubiri ndani ya sinagogi kwa Sabato tatu mfululizo.

Kwa kutumia Maandiko aliwaonyesha kwamba Masihi alipaswa kuteswa, kufa na kufufuka, na kwamba Yesu ndiye Kristo.

Mahubiri hayo yaligusa mioyo ya watu wengi. Baadhi ya Wayahudi waliamini, lakini walioitikia kwa wingi zaidi walikuwa Wayunani waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wenye heshima katika jamii. Ndani ya muda mfupi, kanisa la Thesalonike likaanza kukua.

Lakini kadiri Injili ilivyozidi kuenea, ndivyo upinzani ulivyoongezeka.
Viongozi wa Kiyahudi waliingiwa na wivu, wakakusanya kundi la wahuni na kuanzisha fujo mjini. Walimtafuta Paulo na Sila ili wawakamate, lakini hawakuwakuta. Badala yake walimkamata Yasoni, aliyekuwa amewakaribisha nyumbani kwake.

Walimshitaki mbele ya viongozi wa mji wakisema:
"Watu hawa waliougeuza ulimwengu wamefika hapa pia." (Matendo 17:6)

Kutokana na hali hiyo, Paulo aliondoka usiku kuelekea Berea ili kuokoa maisha yake. Ingawa alikaa Thesalonike kwa muda mfupi, mbegu ya Injili aliyopanda iliendelea kukua.

Baadaye, akiwa Korintho, Paulo alipata habari kwamba waamini wa Thesalonike walikuwa bado wanasimama imara pamoja na mateso yao. Ndipo akaandika Waraka wa Kwanza wa Wathesalonike, ambao tunaamini ni mojawapo ya vitabu vya kwanza kabisa kuandikwa katika Agano Jipya.

Katika waraka huo, Paulo hakuwakemea sana kama alivyofanya kwa Wakorintho au Wagalatia. Badala yake, aliwapongeza kwa sababu walikuwa mfano wa imani, upendo na matumaini.

Aliwaambia:
"Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiilipokea lile neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu." (1 Wathesalonike 1:6)

Baadaye aliandika Waraka wa Pili wa Wathesalonike kwa sababu baadhi ya watu walikuwa wameanza kufundisha kwamba siku ya Bwana ilikuwa tayari imefika. Wengine hata waliacha kufanya kazi wakidhani Yesu angerudi mara moja tu.

Paulo aliwasahihisha kwa upendo. Aliwaambia wasidanganywe na mafundisho ya uongo, waendelee kufanya kazi kwa bidii, waishi maisha matakatifu na wamngojee Kristo kwa uvumilivu.

Kanisa la Thesalonike halikuzaliwa katika mazingira ya amani. Lilikua katikati ya mateso, vitisho na upinzani mkali. Lakini tunaona, waamini hao hawakurudi nyuma.

Walibaki waaminifu kwa Kristo, wakijua kwamba thawabu yao ilikuwa mbinguni kuliko duniani. Ndiyo maana Paulo aliwaandika: "Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiilipokea lile neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu." (1 Wathesalonike 1:6).

Hii inaonyesha kuwa mateso si ishara ya Mungu kukuacha, bali mara nyingi ni sehemu ya safari ya imani.
Hata leo, kuna Wakristo wengi wanaodhani kwamba kumfuata Yesu kunamaanisha kutokuwa na majaribu.

Lakini Biblia inasema, "Wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa." (2 Timotheo 3:12). Imani ya kweli haionekani pale mambo yanapokwenda vizuri, bali pale unapobaki mwaminifu hata unapopitia majaribu, kukataliwa au dharau kwa ajili ya jina la Yesu.

1000010086.jpg
 
Amina.... Sana mtumish¡¡¡
Be blessed......
Sema leo watu wanamfuata YESU,,, iliatatue changamoto zao tu! na wahubiri wengi wanawaaminisha ukimpokea YESU kila kitu kitakuwa sawa..... bila kuwajenga kiimani namna ya kumtumaini MUNGU kama watu wathesalonike¡¡¡
 
sidhani kama kuna watanzania wengi huko maana siku hizi hawatoi scholarship
 
Back
Top Bottom