Mjadala Z`bar wapasua kichwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mjadala Z`bar wapasua kichwa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by abdulahsaf, Mar 21, 2011.

 1. a

  abdulahsaf JF-Expert Member

  #1
  Mar 21, 2011
  Joined: Aug 31, 2010
  Messages: 859
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  Mwinyi Sadallah

  20th March 2011
  Mjadala wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano umeendelea kupasua vichwa wanasheria na vigogo wa Zanzibar, ambapo jana imeelezwa si sahihi Rais wa Zanzibar kula kiapo kutetea katiba hiyo, wakati amechaguliwa kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
  Hayo yameelezwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ibrahim Mzee wakati akiwasilisha mada kuhusu katiba za Tanzania na Zanzibar changamoto juu ya mianya na utata uliopo, katika mjadala wa katiba mpya uliofanyika mjini Zanzibar.
  Alisema Rais wa Zanzibar anachaguliwa kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar kwa kuitumikia Zanzibar, lakini bado katiba ya Muungano inamlazimisha kuapa kutetea na kuilinda katiba hiyo.
  Mzee alisema kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano asiyekuwa na Wizara Maalumu wakati Zanzibar iliungana na Tanganyika kama mataifa mawili yenye sifa sawa kitaifa.
  “Rais wa Zanzibar anachaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na sio sahihi kulazimishwa kuapa kutetea katiba ya Muungano,” alisema Katibu huyo huku baadhi ya wajumbe wakipiga makofi katika kongamano hilo.
  Alisema katiba ya Muungano imempa mamlaka Rais wa Muungano kuchagua Mawaziri kwa kushirikiana na Waziri Mkuu na kuwapangia kazi baadhi ya Wazanzibari katika wizara yoyote hata kama haihusiki na masuala ya muungano.
  Katibu huyo wa Baraza alisema kwamba utaratibu huo ni sehemu ya utata uliopo katika katiba hiyo na kutoa mfano Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi ambayo inaonekana ni ya Muungano kuna baadhi ya mambo yanahusu upande mmoja peke yake.
  Alitoa mfano katika Wizara hiyo kuna Jeshi la Magereza na Kikosi cha Zimamoto ambayo hayahusiani na Zanzibar, lakini Waziri wake anatoka Zanzibar na kusimamia mambo yasiyokuwemo katika mambo ya Muungano.
  Alitoa mfano mwengine Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuwa mbali na kupewa Waziri kutoka Zanzibar kuna jeshi la Kujenga Taifa, ambalo halimo katika masuala ya Muungano.
  Katika mada yake hiyo alisema mkanganyiko mwingine unajitokeza katika suala la Jumuiya ya Afrika Mshariki, kwa vile yapo mambo ambayo Zanzibar ilipaswa kunufaika moja kwa moja bila ya kupitia serikali ya Muungano.
  Aliyataja mambo ambayo hayamo katika mambo ya Muungano ni Utalii, Afya na Kilimo ambayo yanahitaji kujadiliwa na kuwekewa utaratibu mzuri, kwa maslahi ya Zanzibar.
  Alieleza kwamba katiba hiyo pia inaudhaifu katika kutoa mamlaka makubwa ya Tume ya Uchaguzi ambapo inaelezwa baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo hakuna chombo chochote chenye uwezo wa kuhoji matokeo hayo.
  “Tume ya Uchaguzi kuwa na mamlaka kuliko chombo chengine hiyo ni kasoro kubwa ya Katiba”, alisema Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
  Aidha, alisema kwamba katiba ya Muungano imeweka kinga kubwa kwa Rais kutoshitakiwa akiwa madarakani na baada ya kuondoka, jambo ambalo alisema linahitaji kuangaliwa katika mchakato huo wa marekebisho ya Katiba.
  Alisema viongozi katika mataifa mbali mbali wanapokuwa madarakani wanakawaida ya kujisahau na kuwepo kwa sheria kama hizo kunaweza kusababisha matumizi mabaya ya madaraka.
  “Nafuu katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inaruhusu Rais akiwa nje ya madaraka kushitakiwa, tofauti na katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inazuia Rais kushitakiwa akiwa madarakani na hata akiondoka madarakani,” alisema.
  Aidha, alisema haikuwa muafaka kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano kueleza Makamo wa Rais kama atafukuzwa madarakani anapoteza na sifa ya kugombea Urais wa Zanzibar.
  Alisema hata utaratibu wa kuthibitishwa na Bunge, makamo mpya wa Rais pale inapotokea aliyekuwepo amefariki dunia sio mzuri kwa vile wabunge humjadili na kumthibitisha kwa muda mfupi, jambo ambalo huwanyima wananchi na vyombo vya habari kumchunguza uwezo wake wa kiutendaji na uadilifu.
  Alishauri inapotokea hali kama hiyo jina na makamo wa Rais litangazwe na lithibitishwe na Bunge baada ya muda wa miezi miwili ili wananchi wapate nafasi ya kuangalia kumbukumbu zake katika masuala ya uadilifu na uwajibikaji.
  Wakichangia mada hiyo wajumbe wameshauri kuwepo Tume tafauti mbili za kukusanya maoni ya Katiba ya Muungano ili Zanzibar isifunikwe na Tanzania Bara ambayo ina idadi kubwa ya wakaazi.
  Wakili mkongwe Mahakama Kuu Zanzibar, Awadh Ali Said alisema kulingana na mazingira ya Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuna haja iunde tume yake ya kukusanya maoni na Zanzibar iwe na mjadala wake.
  Alieleza kwamba iwapo mjadala huo wa katiba utafanyika kwa jumla Zanzibar haitanufaika na lolote na badala yake Tanzania Bara watoe maoni yao na Zanzibar watowe maoni yao juu ya katiba mpya.
  Wakili huyo alisema Zanzibar ina kero nyingi ndani ya muungano ikiwemo suala la Afrika Mshariki ambapo kuna mambo yapatayo 14, ambayo hayapo katika orodha ya mambo ya Muungano.
  Ahmed Omar Khamis alishauri tume itakayoundwa isiwe ya ujanja ujanja kama tume zilizotanguliwa na badala yake maamuzi yatakayotolewa na wananchi yatekelezwe kwa vitendo.
  Hata hivyo, aliunga mkono wazo la kuwepo tume mbili katika ya Tanzania Bara na Zanzibar na kila moja ifanye kazi katika sehemu moja.
  Naye mwanaharakati, Rashid Yussuf Mchenga alisema wakati umefika Zanzibar iwe na mamlaka ya kisheria kusajili vyama vyake vya siasa, badala ya vyama hivyo kulazimishwa kuwa na sura ya Muungano.
  Alisema serikali ya Zanzibar ndiyo pekee duniani isiyokuwa na vyama vyake vya siasa, licha ya kuwa na hadhi ya nchi na kutaka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wawe imara katika kusimamia maslahi ya Zanzibar.
  Kongamano hilo limetayarishwa na kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC) kwa kushirikiana na chama cha wanasheria Zanzibar, (ZLS) jumuiya ya waandishi wa habari ya (Wahamaza) na taasisi ya Utafiti ya Bahari ya Hindi, (ZIORI) Zanzibar.
   
Loading...