Ni robo fainali ya ushindani, mvuto mkubwa Chalenji
Monday, 06 December 2010 21:41 0diggsdigg
Mshambualiaji wa timu ya taifa ya Zanzibar Heroes, Sabri Ramadhan Mzee akiwania mpira wa juu na beki wa Rwanda, Eric Gasana pamoja na kipa Jaen Luc Nayishimiye wakati wa mechi ya makundi ya Kombe la Tusker Chalenji kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Sosthenes Nyoni
ROBO fainali ya michuano ya Kombe la Tusker Chalenji inaanza leo kwa michezo miwili ambapo katika mpambano wa awali, vigogo wa soka kutoka kusini mwa Afrika, Zambia au Chipolopolo watakabiliana na Swala wa Ethiopia.
Mpambano unaotarajiwa kuwa mkali wenye ushindani utafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 8 mchana, ukifuatiwa na ule ambao utaikutanisha timu ngumu ya Ivory Coast (Elephants) dhidi ya Malawi, maarufu Flames, ambayo pia imeonyesha mchezo wa kuvutia.
Kikubwa zaidi, ni mchezo huo baina ya timu hizo ambazo zote zimealikwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), unaorejesha kumbukumbu ya mechi ya mjini Abidjan mwaka juzi, ambapo Ivory Coast iliichakaza Malawi 5-0.
Katika mchezo huo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika na Kombe la Dunia mwaka 2010, mashabiki 20 walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa kwa kukanyagana kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny.
Ikiwa na nyota wake, Didier Drogba, Salomon Kalou na wengineo wengi, ambao hata hivyo hawashiriki fainali hizi za Chalenji, Ivory Coast ilitoka jasho katika mchezo wa marudiano mjini Blantyre kwa ushindi wa bao 1-0 ambao uliikatia tiketi ya fainali hizo zilizochezwa Angola na Afrika Kusini.
Kwa vyovyote vile, mchezo huo wa leo utakuwa wenye ushindani mkubwa kutokana na kasi ambayo Malawi inacheza, dhidi ya ubabe, nguvu za vijana wa Ivory Coast.
Chipolopolo imefanikiwa kuingia robo fainali baada ya kujikusanyia pointi saba zilizotokana na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Kilimanjaro Stars, sare ya bao 1-1 ilipocheza na Burundi pamoja na kipigo cha 6-0 kutoka kwa timu dhaifu ya Somalia.
Ikiwa na mpachika mabao kinara wa michuano hiyo, Felix Sunzu(21)ambaye pia aliyewahi kuichezea Konkola Blades ya nchini humo, Chipolopolo imeonyesha nia yake ya kutwaa ubingwa wa michuano na dola 30,000 baada ya kuongoza Kundi A lililokuwa na Kilimanjaro Stars, Burundi na Somalia.
Kocha wake, Mario Bonetti ambaye ni raia wa Italia alisema juzi kuwa ni vigumu kutabiri mwelekeo wa kikosi chake kwa sasa, lakini ameapa kupigana kufa au kupona ili waweze kuvuka hatua hiyo.
"Hii ni soka bwana unakuwa na malengo, lakini huwezi kumhakikishia mtu kwamba utafanya kile, lakini tumejiandaa kuikabili Ethiopia ili tuvuke hatua hii na hili ndilo muhimu kwa wakati huu,"alisema Bonetti.
Ikitokea Kundi C, Ethiopia ' swala' ilibebwa na idadi kubwa ya mabao matatu na kuitupa nje Burundi iliyokuwa na mabao mawili licha ya timu hizo kulingana kwa pointi, nne.Wahabeshi hao ambao wameonyesha kuwavutia mashabiki wengi kwa kandanda yao ya pasi nyingi walianza kwa kuadhibiwa na Uganda mabao 2-1 kisha ikaitungua Kenya, Harambee Stars, mabao 2-1 na kufuatia na suluhu ya 0-0 dhidi ya Malawi.
Ivory Coast iliyokuwa kundi B na inayoonekana kuwa na chipukizi wengi pengine kuliko timu nyingine yoyote inayoshiriki michuano hii imefikia hatua hiyo baada ya kujikusanyia pointi sita ikiwa imezisulubu Zanzibar Heroes 1-0, Sudan 3-0 na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Rwanda.
Kocha wa Ivory Coast, Kouadio Georges ambaye kikosi chake kitaikabili Malawi alisema mpaka kuwa hadi wakati huu vijana wake wameimarika kiasi cha kutosha tayari kwa mpambano huo ambao ameuita ni vita isiyotabirika.
Malawi,'The Flames' itashuka katika kipute hicho ikijivunia rekodi ya kutopoteza mchezo ambapo ikitokea Kundi C ilikoibanjua Kenya 3-2 na kufuatia na sare mbili ikiwa ni ile ya bao 1-1 na Uganda sambamba na bao 1-1 dhidi ya Ethiopia.