1994 Mara ya mwisho Tanzania kutwaa Kombe la Chalenji
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 3rd December 2010 @ 23:59 Imesomwa na watu: 55; Jumla ya maoni: 0
MICHUANO ya Chalenji ilianza Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam na inashirikisha nchi 12.
Michuano hiyo inashirikisha nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Lakini mwaka huu kuna nchi tatu zimealikwa ambazo si wanachama wa Cecafa, ambazo ni Ivory Coast, Zambia na Malawi.
Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars' ipo Kundi A pamoja na Zambia, Somalia na Burundi, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rwanda, Ivory Coast, Sudan na Zanzibar, huku Kundi C likiwa na nchi za Uganda, Malawi na Ethiopia.
Katika mchezo wa ufunguzi Jumamosi Kilimanjaro Stars ilifungwa bao 1-0 na Zambia, wakati siku iliyofuata Zanzibar iliifunga Sudan mabao 2-0. Waamuzi wanaochezesha michuano hiyo na nchi wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Issa Kagabo (Rwanda), Rassas Librato Sabit (Sudan), Israel Mujuni (Tanzania Bara), Dennis Bate (Uganda), Ramadhan Kibo (Zanzibar) na Bamlak Weyesa Tessema (Ethiopia).
Waamuzi wasaidizi ni Charles Nizigiyimana wa Burundi, Gebre Silassie Solomon (Ethiopia), Wamalwa Elias Kuloba (Kenya), Theogene Ndagijimana (Rwanda), Hamis Chang'walu (Tanzania Bara), Bugembe Hussein (Uganda), Medany Mustafa (Sudan) na Bashir Arab (Somalia).
Kipigo ilichokipata Stars Jumamosi kiliwashtua wadau wa soka kwa kiasi kikubwa, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo Jan Poulsen kidogo alirekebisha mambo hivyo Jumanne Stars ikaifunga Somalia mabao 3-0, angalau ikawapa matumaini mashabiki.
Kwa ujumla matokeo ya mchezo wa kwanza kwa Zanzibar Heroes nayo yaliwapa matumaini mashabiki ingawa nayo Jumatano iliwaudhi baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka
kwa Ivory Coast.
Ni miaka 15 sasa imepita, Tanzania ikiwa inafanya kazi ngumu na isiyo na mshahara katika soka kwenye michuano hiyo kwa maana ya kuwa msindikizaji. Ni kazi ngumu kwa kweli, kuwa msindikizaji tu kila mwaka, huku ukishuhudia wenzio wakibeba vikombe na mamilioni ya pesa.
Inauma na pengine inasikitisha na kushangaza pia hasa kutokana na tathmini za makocha mbalimbali wa ukanda huu kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na wachezaji wengi wenye
vipaji.
Pande zote yaani Tanzania Bara na visiwani ambazo hushiriki kama nchi mbili tofauti kwenye michuano hiyo, zimeshindwa kufanya lolote kwenye michuano hiyo inayofanyika kila mwaka katika nchi inayokubaliwa kuandaa.
Mara ya mwisho Tanzania Bara kufurahia michuano hiyo ni mwaka 1994 pale Kilimanjaro Stars ilipoutwaa ubingwa huo, baada ya hapo imekuwa hadithi mpaka leo.
Kabla ya hapo, Kilimanjaro Stars imewahi kuwa bingwa wa michuano hiyo mwaka 1974, huku Zanzibar Heroes ikijitutumua na kutwaa ubingwa mwaka 1995.
Tanzania ilionekana kupata ahueni kidogo ilipofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani michuano iliyofanyika Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka jana.
Lakini pamoja na Tanzania kuonekana ndio timu iliyokuwa pamoja muda mrefu na kucheza mechi nyingi za kimataifa, lakini iliishia hatua ya makundi na kurudi zake nyumbani.
Nasema hivyo kwa sababu michuano hiyo ilikuwa ikishirikisha wachezaji wanaocheza ligi
ya ndani, lakini kwa upande wa Stars haikuwa na wachezaji wanaocheza ligi za nje, hivyo walikuwa na uzoefu na michuano ya kimataifa, kwani kikosi kilichoenda Ivory Coast karibu
chote ndicho kilichokuwa kikicheza mechi za awali kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika zilizofanyika Ghana.
Sasa huu ndio wakati kwa timu ya Tanzania Bara na Zanzibar kuleta sherehe nyumbani, Watanzania wamechoka kulalama kila kukicha. Kocha Mkuu wa Tanzania Bara, Jan Poulsen
anaiongoza nchi kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo tangu alipowasili Agosti mwaka
huu.
Watanzania bado wana mapenzi na timu yao ni vile tu imekuwa ikiwakatisha tamaa kila inapodhaniwa kwamba inafanya vizuri kumbe ndio huvurunda hapo ndipo kila mmoja
anapoona uchungu.
Aidha Zanzibar Heroes ipo kwenye michuano ya mwaka huu ikiwa chini ya kocha Stewart Hall ambaye pia ni mara ya kwanza kukiongoza kikosi cha timu hiyo.
Kama nilivyosema Zambia, Malawi na Ivory Coast zinashiriki michuano hiyo kama timu mualikwa ili kutoa changamoto kwa timu mwanachama wa CECAFA. Hata hivyo mwaka 1981
Zambia na Malawi zilikuwa miongoni mwa wanachama wa CECAFA kabla ya kujitoa mwaka 1994.
Nchi hizo zilijitoa baada ya kuundwa kwa Shirikisho la Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA). Baadaye Rwanda, Burundi, Eritrea na Djibouti zilijiunga na CECAFA mwaka 1995 na kufanya idadi ya wanachama wake kufikia 11.
Nawaombea heri wachezaji wa Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes wajue Watanzania wapo
nyuma yao, hakuna lisilowezekana panapokuwa na juhudi za kutosha. Wafanye kile ambacho
Watanzania wengi wanataka wakifanye, nacho ni ushindi na kuhakikisha kombe haliondoki.
Kikubwa ni kwamba Stars na Zanzibar Heroes zinakutana na nchi ambazo inazifahamu vyema, hivyo hazitawasumbua sana. Ingawa soka huwa halitabiriki, lakini kwa kiwango
kilichooneshwa na wachezaji wa timu hizo kama watabadilika kidogo basi kombe halitaondoka.
Wachezaji watambue Watanzania nia yao ni kubakisha kombe nyumbani, ili walishike na si kuliona likipandishwa kwenye ndege na kuondoka. Ifuatayo ni orodha ya mabingwa wa Kombe la Chalenji tangu mwaka 1973.
Mwaka Mshindi 2010 ?
2009 Uganda
2008 Uganda
2007 Sudan
2006 Zambia
2005 Ethiopia
2004 Ethiopia
2003 Uganda
2002 Kenya
2001 Ethiopia
2000 Uganda
1999 Rwanda B
1997 Uganda
1996 Uganda
1995 Zanzibar
1994 Tanzania
1992 Uganda
1991 Zambia
1990 Uganda
1989 Uganda
1988 Malawi
1987 Ethiopia
1985 Zimbabwe
1984 Zambia
1983 Kenya
1982 Kenya
1981 Kenya
1980 Sudan
1979 Malawi
1978 Malawi
1977 Uganda
1976 Uganda
1975 Kenya
1974 Tanzania
1973 Uganda