Msondo na Sikinde watuonyeshe udugu wa wanamuziki
Juma Kasesa
AHLAN wasahlan mpenzi msomaji wa safu hii ya Jamvi la Kulonga, ikiwa ni Ijumaa nyingine tunapokutana kwa lengo la kuchambua na kujadili hili na lile yaliyojiri katika anga ya burudani na sanaa kwa ujumla.
Leo katika safu hii ningependa nizungumzie mpambano wa kukata na shoka unaotarajiwa kufanyika leo baina ya bendi mbili kongwe za muziki wa dansi nchini ambazo ni Msondo Ngoma zamani (JUWATA Jazz) ‘Baba ya muziki' na Mlimani Park Orchestra zamani DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae' ambazo zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Jamvi la Kulonga limeguswa na mpambano huu kwakuwa unagusa hisia za mamilioni ya Watanzania ambao ni wapenzi na wadau wa muziki wa dansi kutokana na ubora na uimara wa bendi tangu zilipoasisiwa baada ya Tanzania kupata uhuru.
Sikinde na Msondo ndizo bendi za muziki wa dansi ambazo ni kongwe zilizodumu hadi leo katika kuenzi na kuutunza muziki wa asili wa Tanzania kulinganisha na bendi nyingine chipukizi ambazo zimekuwa zikipiga muziki ambao una vionjo vyenye asili ya nchi na majirani zetu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Hoja ya Jamvi hili leo ni kutaka kuzipa changamoto bendi za Msondo na Sikinde kuwa zinatakiwa kutumia mpambano wao huu kuonyeshana kuwa wanamuziki ni ndugu na wanaweza kushirikiana jukwaa moja katika kuimba na kucheza, jambo linaweza kuwa ni urithi kwa bendi chipukizi za muziki huo.
Pengine kabla Jamvi hili halijaingia kwa undani kujadili hoja hiyo ya ushirikiano wao kindugu ni vyema tukazifahamu bendi hizo kwa kifupi, wapi zilipotoka na wapi zilipo sasa, ambapo kwa wasiofahamu Mlimani Park Orchestra iliasisiwa mwaka 1978 na ilijulikana hivyo kutokana kuwa na maskani yake pale Mlimani Club mitaa ya Mwenge jijini Dar es Salaam chini ya mmiliki wa Tanzania Transport and Taxi Services.
Mwaka 1983 waliokuwa wamiliki wa bendi hiyo walifilisika na na hatimaye bendi hiyo ikachukuliwa na Dar es Salaam Development Corporation (DDC) na hapo ndiyo ikaanza kuvuma kwa jina la DDC Mlimani Park Orchestra ikiwa chini ya wanamuziki galacha na waasisi, Muhidin Maalim Gurumo, Abel Baltazar, Hassan Rehani Bitchuka, ambao walitokea JUWATA Jazz Band huku Cosmas Thobias Chidumule, Michael Enoch ‘King Michael' na mpiga gitaa la solo mahiri, Joseph Batholemeo Mulenga, wakiwa wametwaliwa kutoka Dar International.
Bendi hii ilivuma na nyimbo mbalimbali ambazo ziliiwezesha kupata mialiko mbalimbali ya kimataifa ambapo `miongoni mwa nyimbo hizo ni ‘Fikiri Nisamehe', ‘Mtoto Akililia Wembe', ‘Mnanionyesha njia ya Kwetu', ‘Nawashukuru Wazazi', ‘Majirani Huzima Redio', ‘Ramadhani', ‘Maneno maneno ya nini', ‘Gama', ‘Celina' ‘Barua' ‘Mume Mlevi' ‘Neema' ‘Dunia kuna Mambo' ‘MV Mapenzi' namba moja na namba mbili hizi nyimbo zote zikiwa ni kabla ya waasisi hao kuondoka na kurejea.
Kwa muda wote huo ilikuwa chini ya Shirika hilo la Maendeleo Dar es Salaam DDC kabla halijawatosa miaka miwili iliyopita na bendi hiyo sasa ikiwa inamilikiwa na wanamuziki wenyewe na sasa kujulikana kwa jina la Mlimani Park Orchestra, ikiwa inaendelea kupiga muziki wenye asili ya Tanzania ambao washindani wake ni Msondo Ngoma.
Jamvi hili linakukumbusha kuwa Msondo Ngoma nayo kwa nyakati tofauti baada ya kuasisiwa mwaka 1964 ikiwa imepitia katika miliki ya taasisi moja ya wafanyakazi lakini ikibadilishwa majina kulingana na nyakati zilivyokuwa zikienda.
Bendi hiyo iliasisiwa kwa jina la National Union of Tanganyika Workers (NUTA ) na kuitwa NUTA Jazz, ikiwa chini ya gwiji la muziki wa dansi nchini Muhidin Maalim Gurumo, sambamba na Mabruki Khalfan, Joseph Mulenga, Ahmed Omary, Mohamed Omary, Epimakus Mkundika na Rashid Abdallah.
NUTA Jazz ilifanikiwa kutamba na nyimbo mbalimbali na miongoni mwa nyimbo hizo ni Magdalena', ‘Maneno ya Mwalimu', ‘Nipeleke kwa baba', ‘Nimuokoe nani', ‘Viva Flerimo' ‘Maneno ya Wazee Yote Sawa', ‘Rehema Umefeli Shule kwa Kisa Gani', ‘Ashibaye', ‘Bahati', ‘Gloria', ‘Hamida', ‘Sikutarajia kashfa', kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa JUWATA Jazz, OTTU Jazz na Jumuiya ya Wafanyakazi ilipojitoa umiliki wa bendi hiyo ikaitwa Msondo Ngoma chini ya umiliki mpya wa wanamuziki wenyewe.
Baada ya kuzielezea kwa kifupi bendi hizo ni vyema nikarudi katika hoja iliyonisukuma kuandika Jamvi hili ambayo ni kuzitaka Msondo na Sikinde kutuonyesha undugu wao leo kwa baaadhi ya wanamuziki ambao waliwahi kupitia kwa nyakati tofauti katika bendi kupanda jukwaani na kuimba nyimbo ili kuwa uhondo mashabiki wao.
Bendi hizi kwa pamoja zimepata bahati kubwa ambayo wanapaswa kuitumia ambayo ni kuona mwasisi wa bendi hizo mtunzi na mwimbaji Muhidin Maalim Gurumo akiwa bado yupo akiendelea na shughuli za muziki, japokuwa miezi kadhaa iliyopita hali yake kiafya ilitetereka.
Gurumo ameshiriki kuanzisha NUTA Jazz na baadae kuitosa na kwenda kuiasisi Mlimani Park Orchestra na baadaye kurejea NUTA, lakini si Gurumo peke yake yupo mtunzi na mwimbaji mwingine, Hassan Rehani Bitchuka, ambaye naye ameimba kwa mafanikio na bendi zote hizi mbili kwa nyakati tofauti lakini sasa akiwa amepiga kambi na Sikinde.
Kuwepo kwa Gurumo na Bitchuka, wanamuziki ambao wametoa mchango mkubwa katika medani ya muziki wa dansi kutokana na ubora wa tungo zao na sauti, kuna chagiza mpambano wao wa leo kuwa mzuri, hivyo mashabiki wanachotarajia kuona baada ushindani kumalizika hatua ya kwanza, kitakachofuata ni Bitchuka kusimama jukwaa la Msondo na kuimba baadhi ya nyimbo alizowahi kuziimba, hali kadhalika kwa Gurumo kwa Sikinde.
Jamvi la Kulonga linaamini mashabiki wa bendi hizo na wadau wa muziki wa dansi wanataka kusikia vibao kama ‘Celina', ‘Barua', ‘Pata potea', na nyinginezo za Sikinde vikiimbwa na Gurumo huku Bitchuka naye akifanya hivyo katika nyimbo kama, ‘Demokrasia ya Mapenzi', ‘Usia wa Baba', ‘Nidhamu ya Kazi'.
Mpambano wa huu ni changamoto kwa bendi nyingine za muziki wa dansi nchini kufikiria kufuata nyayo za wakongwe hao katika kuenzi na kutunza muziki wa dansi wenye vionjo vya asili ya Tanzania.
Jamvi la Kulonga linaamini kabisa bendi zote zipo imara kuonyeshana ufundi katika kutunga na kuimba kutokana na uwezo walionao wanamuziki wa pande zote mbili, ingawa Sikinde imepata pigo juzi baada ya aliyekuwa mwanamuziki wake tegemeo Shabani Dede kujing'atua ndani ya bendi hiyo na kujiunga na mahasimu wa bendi hiyo, Msondo Ngoma.
Lakini licha ya Dede kujiunga na Msondo bado kuna vichwa vingi ndani ya Sikinde vinavyoweza kutoa upinzani kwa Msondo, lakini pia kwa mahasimu wao nao wamepata ahueni baada ya Gurumo ambaye alikuwa mgonjwa katika siku za hivi karibuni kupata nafuu, ambapo mwanzoni mwa wiki alianza mazoezi na wanamuziki wenzake, jambo linalotarajiwa kuleta faraja kwa bendi hiyo.
Tusubiri tuone kitakachojiri. Kwa leo nalikunja Jamvi, tukutane Ijumaa ijayo katika kuchambua na kujadili haya na yale katika anga ya burudani na sanaa.
Tuwasiliane kwa barua pepe:
jkasesa@hotmail.com, simu 0715-629298.