Liverpool yafuzu kucheza 32 Europa League
Friday, 03 December 2010 19:42 0diggsdigg
MILAN, Italia
KLABU za Liverpool, Paris St Germain, Besiktas, Dynamo Kiev, Sparta Prague na Villarreal zimekata tiketi ya kucheza 32 bora kwenye michuano ya Europa League juzi.
Huku Ulaya ikikabiliwa na hali mbaya ya hewa, idadi kubwa ya mabao ilishuhudiwa katika mechi hizo.
PSG ilishinda 4-2 nyumbani dhidi ya Sevilla, ambao wanashindana na Borussia Dortmund kusaka nafasi ya pili zitakapokutana Desemba 15 kwenye mchezo wa Kundi J.
Dortmund iliikaribia Sevilla baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Karpaty Lviv. Besiktas ilikata tiketi yake kutoka Kundi L baada ya ushindi mgumu wa 2-1 dhidi ya CSKA Sofia ya Bulgaria wakati Rapid Vienna ilishindwa 3-1 nyumbani na Porto, ambayo tayari imekata tiketi.
Dynamo Kiev ilishinda 4-1 dhidi ya BATE Borisov ambayo ilishavuka na hivyo nayo kufuzu , ikimaanisha kuwa sare ya AZ Alkmaar ya bao 1-1 dhidi ya Sheriff Tiraspol katika mchezo wa Kundi E haukuwa na maana.
Milan Jovanovic, ambaye ni nadara kutumika katika mechi za Ligi Kuu England aliipa uongozi Liverpool dhidi ya Steaua Bucharest kwa kichwa safi kipindi cha kwanza, ingawa Eder Bonfim alisawazisha, pointi ilitosha kuwakatia tiketi mabingwa hao mara tano wa Ulaya.
"Ilikuwa kazi kubwa kwa wachezaji kuhimili vishindo na aina ya soka iliyochezwa na Steaua," alieleza kocha Roy Hodgson akizungumza na waandishi wa habri baada ya mchezo huo.
"Ni mafanikio kwetu, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba tumekuwa na msimu mgumu, kiasi cha kuwatumia wachezaji wasiozoeleka kucheza Ligi Kuu."
Palermo nje
Mabao lukuki Kundi K ambako mchezaji wa kimataifa wa Uruguay,Edinson Cavani alifunga matatu, hat-trick kwenye sare ya 3-3 ya Napoli dhidi ya Utrecht, ambako mshambuliaji Ricky van Wolfswinkel alifunga mawili lakini hayakusaidia.
Sare hiyo inaamanisha kuwa Napoli ni timu pekee ya Italia ambayo bado inasaka nafasi katika hatua hiyo ikiwa pointi mbili nyuma ya Steaua, mchezo wa mwisho utakuwa nyumbani dhidi ya klabu hiyo ya Romania, Desemba 15.
Palermo ikiwa na wachezaji tisa ilitolewa licha ya mara mbili kuongoza dhidi ya Sparta Prague na kumaliza kwa sare ya 2-2 kisiwani Sicily. Dorin Goian alitolewa kwa kadi nyekundu na Javier Pastore pia alifuata dakika za majeruhi.
CSKA Moscow ambao tayari wamefuzu walishangilia uenyeji wa nchi yao kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Lausanne ambayo imetolewa kwa mabao mawili ya Tomas Necid , kutoka Kundi F.
Stefan Scepovic aliipa sare Club Bruges ya bao 1-1 dhidi PAOK Salonika na kuwasaidia vinara wa Kundi D, Villarreal kusonga mbele kwa 3-0 dhidi ya Dinamo Zagreb nchini Hispania.
Makundi A-C na G-I, mechi zao zilichezwa Jumatano, huku mabingwa mara mbili Ulaya, wakiwa timu kubwa pekee kutupwa nje.