Polisi Arusha yaongoza netiboli Morogoro
Imeandikwa na John Nditi, Morogoro; Tarehe: 19th February 2011 @ 23:45 Imesomwa na watu: 21; Jumla ya maoni: 0
TIMU ya Netiboli ya Polisi Arusha inayoshiriki Ligi Daraja la Pili ngazi ya Taifa katika mashindano yanayofanyika mkoani Morogoro imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika kundi B baada ya kuifunga timu ngumu ya Ruvu JKT mabao 25-17.
Mchezo huo wa kundi hilo ulifanyika jana asubuhi, ulitawaliwa kwa majigambo tambo na shamrashamra kutoka kwa baadhi ya wachezaji na mashabiki wa timu hizo kufuatia jezi zilizovaliwa na wachezaji wa pande hizo.
Timu ya Polisi Arusha ilivalia jezi za rangi nyekundu zinazotumiwa na timu ya soka ya Simba, ambapo Ruvu JKT yenyewe walivalia jezi za rangi ya njano ambazo pia huvaliwa na timu ya Yanga hali iliyosababisha ushangiliaji kuwa ni wa Yanga na Simba.
Hata hivyo mchezo huo ulikuwa wa vuta nikuvute na ufundi mwingi kutoka kwa wachezaji wa pande zote ambapo hadi mapumziko Polisi Arusha ilikuwa mbele kwa mabao 12-9 ya wapinzani wao.
Timu hizo katika kipindi cha pili zilicheza kufa na kupona, lakini vijana wa Polisi Arusha walikitawala kipindi hicho kwa kuongeza mabao mengine 13 dhidi ya 8 ya wapinzani wao.
Hadi mchezo huo unamalizika Polisi Arusha walijipatia mabao hayo 25 -17, hata hivyo Ruvu ilipata pigo baada ya mshambuliaji wao mahiri kuumia kabla ya mapumziko.
Mshambuliaji na mfungaji huyo mahiri wa timu hiyo, Jawa Iddi aliumia mkono wa kushoto ambapo kipindi cha pili alicheza dakika chache na kutoka nje na nafasi yake ilichukuliwa na Zainab Lukindo.
Katika mchezo mwingine ulikuwa na ushindani mkubwa uliofanyika awali ulikuwa ni kati ya timu ya Mzinga na Alliance One , zote za mkoani hapa ambapo timu ya Mzinga ilishinda mchezo huo kwa kuifunga Alliance One mabao 23- 19.
Hadi timu hizo zilizochuana vikali katika kipindi hicho cha kwanza zinakwenda mapumziko zilikuwa sare kwa mabao 11- 11 .
Kwa upande wake nahodha wa timu ya Ruvu JKT Anna Masaga akizungumzia mchezo dhidi ya wapinzani wao alisema ulikuwa mzuri na wamefungwa kutokana na makosa madogo madogo yaliyojitokeza.
Hata hivyo alisema wanashukuru kushika nafasi ya pili katika kundi lao hilo, baada ya kushinda michezo mitatu na kufungwa mmoja na Polisi Arusha, ambapo alizitaja timu walizozifunga ni Tandahimba mabao 40-20, Black Sisters mabao 47- 10 na Tigo kwa mabao 30-14 .
Naye Nahodha wa timu ya Polisi Arusha, Jackline Kishimbo, alisema ligi hiyo imekuwa na ushindani ambapo katika mchezo huo na Ruvu JKT waliweza kutulia na kufanya mashambulizi ya kujipanga hasa katika kipindi cha pili na kuibuka kidedea.
Kwa mujibu wa Nahodha huyo, kufuatia matokeo hayo, Polisi Arusha imeongoza kundi hilo baada ya kushinda michezo yake yote kwa kuzifunga timu ya Tigo mabao 25-14, Tandahimba 25- 6, Black Sister mabao 35-6 na Ruvu JKT kwa mabao 25-17.
Hivyo alisema kuwa wanasubiri utaratibu mwingine wa waandaaji wa mashindano hayo kuweza kupangwa kwenye hatua ya robo fainali.