Azam yapania kuishusha Yanga
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 19th February 2011 @ 23:59 Imesomwa na watu: 95; Jumla ya maoni: 0
AZAM FC leo inawania kuishusha miamba ya soka nchini Yanga na Simba na kukalia kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara endapo itaifunga JKT Ruvu katika mechi ya vuta nikuvute inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Yanga ndio inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 34 na Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32.
Ushindi wa leo kwa Azam utaifanya ifikisha pointi 35 sawa na Yanga lakini itaongoza ligi kwa kuwa na uwiano mzuri wa mabao kulinganisha na Yanga.
Kabla ya mechi ya leo, Azam inaongoza ikiwa na tofauti ya mabao 19 huku Yanga ikiwa na 18 na Simba ikiwa na 14, hivyo ushindi wowote leo utaifanya izidishe tofauti ya mabao na hivyo kupata nafasi ya kuongoza.
Mechi ya leo inatarajiwa kuwa kali na ya vuta nikuvute kutokana na timu hizo kusumbuana zinapokutana, katika mechi ya mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya bila kufungana.
Akiizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Azam Stewart Hall alisema anatarajia atashinda leo ili aongoze ligi.
"Tangu nimekuja nimekuwa nikitamani kuwa juu ya Yanga na Simba na nadhani leo ni muda muafaka wa mimi kufanya hivyo,"alisema.
Mechi nyingine itakayochezwa leo ni kati ya Kagera Sugar itakayoikabili Afican Lyon kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
Kagera Sugar iko nafasi ya tano kwenye msimamo ikiwa na pointi 25 na Lyon ni ya nane ikiwa na pointi 17, timu hiyo haifanyi vizuri sana kwenye ligi hali inayodhaniwa kuwa Kagera inaweza kuibuka na ushindi kirahisi leo.
Aidha kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Toto Africans itaikaribisha kibonde wa ligi hiyo AFC yenye pointi 11 ikiwa mkiani. Toto iko nafasi ya saba ikiwa na pointi 17.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma kutakuwa na mechi kati ya Polisi ya huko na Majimaji ya Songea ‘Wazalizombe'.
Polisi iko nafasi moja kutoka kwenye ukanda wa kushuka daraja, iko nafasi ya 10 ikiwa na pointi 14 na Majimaji iko kwenye ukanda wa kushuka daraja ikiwa na pointi 11 katika nafasi ya 11. Endapo ikifungwa leo, itazidi kujipalia makaa isirudi kwenye ligi msimu ujao.
Msimu huu zitashuka timu mbili na kupanda nne ili kufanya ligi ya timu 14 badala ya 12 kama misimu iliyopita.