Taifa Stars yaenda Misri
Imeandikwa na Betram Lengama; Tarehe: 3rd January 2011 @ 07:34
TIMU ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars' ilitarajiwa kuondoka leo alfajiri kwenda Misri kwa ajili ya kushiriki kwenye michuano maalumu ya soka ya Mto Nile ambayo inajumuisha mataifa tisa itakayoanza kutimua vumbi keshokutwa jijini Cairo.
Kwa mujibu wa kocha Msaidizi wa kikosi hicho cha Stars Sylvester Marsh timu hiyo ilitarajiwa kuondoka nchini leo saa 12 alfajiri kwa ndege ya Egypt Air ikiwa na kikosi cha wachezaji 23 ambao waliitwa kambini kwa ajili ya kujiandaa na michuano hiyo.
Kocha Marsh alibainisha kuwa hakuna mchezaji aliyechujwa kwenye kikosi hicho ambacho kinajumuisha wachezaji wazoefu na wasio na uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa. Wachezaji ambao walitarajiwa kusafiri leo ni Makipa: Juma Kaseja (Simba), Shaaban Kado (Mtibwa) na Said Mohamed(Majimaji).
Walinzi ni Shadrack Nsajigwa (Nahodha), Stephano Mwasika , Nadir Haroub ‘Cannavaro' (Yanga), Aggrey Morris, (Azam),Kelvin Yondani, Juma Nyosso, (Simba).
Viungo: Idrissa Rajabu (Sofapaka, Kenya), Nurdin Bakari, Abdi Kassim ‘Babi', (Yanga), Shaaban Nditti (Mtibwa) ,Jabir Aziz (Azam) na Rashid Gumbo kutoka Simba aliyechukua nafasi ya Henry Joseph aliyeondolewa kwenye kikosi hicho.
Washambuliaji ni Salum Machaku (Mtibwa), Mrisho Ngassa (Azam), Nizar Khalfan, (Vancouver Whitecaps- Canada), Godfrey Taita (Kagera Sugar), Athumani Machuppa, (Vasuland IF -Sweden), Jerry Tegete, (Yanga) Said Maulid(Onze Bravos-Angola) na Ali Ahmed Shiboli (Simba).
Ratiba ya michuano hiyo inaonesha kuwa Stars itafungua pazia la michuano hiyo kwa kuumana vikali na wenyeji Misri keshokutwa usiku majira ya saa moja wakati Kenya ' Harambee Stars' itaivaa Sudan saa kumi jioni.
Awali ilitangazwa kuwa kikosi hicho cha Stars kilikuwa kiondoke jana lakini badala yake jana walitangulia viongozi na wanahabari, Kocha Mkuu wa Stars Mdenmark Jan Poulsen anatarajiwa kuungana na kikosi hicho huko Cairo akitokea kwao ambako alikuwa kwenye mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka.
Michuano hiyo ambayo ni maalumu kwa ajili ya uhamasishaji wa utunzaji wa maji wa Mto Nile kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo mbali na Tanzania inashirikisha timu kutoka nchi zilizopo kwenye Ukanda wa Ziwa Victoria na Mto Nile ambazo ni Kenya, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Ethiopia, Sudan na wenyeji Misri.