Miaka 81 ya Sekondari Azania (Azania Alumn Day)

Tresor Mandala

JF-Expert Member
Aug 20, 2010
37,581
78,920
View attachment 247181
SERIKALI na wadau wa sekta ya elimu wanatakiwa kuboresha shule kongwe zilizopo hapa nchini kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kulifikisha Taifa hapa lilipo.

Wasomi wengi waliostaafu, wanasiasa, wabunge na viongozi waliopo sasa madarakani wengi wao walisoma kwenye shule hizo ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi hasa za kitaaluma, hivyo kupoteza umaarufu wake.

Ikumbukwe tu kwamba shule ni sehemu ya kumwandaa kijana ili baadae aweze kukabiliana na changamoto za mazingira yanayomzunguka.

Ukizitaja shule hizo za zamani ni lazima Azania Sekondari iwepo kwani ni shule ambayo May 2 mwaka huu itatimiza miaka 81 tangu ianzishwe mwaka 1943.

Nyingine ni Tambaza, Jangwani na Zanaki.

Historia ya Azania
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu maadhimisho ya miaka 81 ya Shule ya Sekondari Azania, Mkuu wa Shule, Benardi Ngozye anasema shule hiyo ilianzishwa na watu ambao walikuwa ni jamii ya Wahindi Weusi waliotokea nchini India, ambapo wakati huo ilikuwa ikiitwa Government India Primary School – Mtendeni.

Mwaka 1939 shule hiyo ilibaddilishwa ikaitwa Government India Secondary School, ambapo baada ya mji kukua ikagawanywa mara mbili ya wasichana ambayo ni Jangwani kwa sasa na wavulana – Azania.

Ngozye anasema mwaka 1952 wavulana walihamishwa kutoka Mtendeni wakajengewa shule yao ambapo iliandikisha wanafunzi sita tu wa Kiafrika ndipo jina la Azania likazaliwa.

Anasema shule hiyo wakati ikianzishwa asilimia 95 ya walimu walikuwa si Waafrika na shule ilibaki kuwa ya wavulana hadi mwaka 1967 ilipotaifishwa wakaandikishwa wasichana 15 lakini baadae iliendelea kuwa ya wavulana pekee.

Taaluma
Mkuu wa shule hiyo ambaye pia aliwahi kusoma shule hiyo mwaka 1984/85 anasema kulikuwa na wanafunzi wachache lakini walimu walikuwa ni wengi kitu ambacho kiliwafanya wanafunzi kufanya vizuri.

"Wakati tunasoma hapa wanafunzi waliokuwa wamechaguliwa kutoka shule za msingi ni wale ambao ni ‘Cream' wenye uelewa mkubwa kimasomo.

"Isitoshe shule hizi enzi hizo zilikuwa ni chache, ulikuwa ni msimu au wakati wa ujamaa kwa kuwa uchumi wa nchi ulikuwa ni mzuri hivyo serikali ilikuwa na uwezo wa kumudu shule hizo," anasema Ngozye.

Anasema tofauti na ilivyo sasa ambapo ongezeko la watu limechangia Azania na shule nyinginezo kuzidiwa na idadi ya wanafunzi wakati walimu wakipungua kutokana na kutopandishwa vyeo na mishahara duni.

"Bajeti ya Wizara ya Elimu inaonekana haikidhi mahitaji ya walimu ipasavyo, hivyo Serikali inapaswa ijitahidi kuongeza walimu na kuwalipa mishahara mizuri ili watimize wajibu wao.

"Shule hii tangu nilipoingia hapa mwaka 1999 nilikuwa mwalimu wa kawaida, idadi ya wanafunzi katika darasa moja walikuwa 500 lakini kadri siku zinavyozidi kwenda walikuwa wakiongezeka kwa kuhamia, hivyo darasa hilo hujikuta siku ya kumaliza linakuwa na wanafunzi wengi zaidi," anasema Ngozye.

Anaongeza kuwa sababu kubwa inayofanya shule hiyo kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ni kuwa karibu na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwani wanafunzi wenaokabiliwa na maradhi mbalimbali huja kusoma hapa ili kuwa rahisi kwao kupatiwa huduma ya matibabu.

Anasema kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi, miaka ya nyuma ilikuwa na wanafunzi wakorofi kutokana na utovu wa nidhamu.

"Hali hii ilichangia pia kushusha kiwango cha elimu katika shule hii, mfano mwaka 2012 wanafunzi wengi wa kidato cha pili walifeli kutokana na utovu wa nidhamu ambapo kwa sasa nimeweza kudhibiti hali hiyo," anasema.

Anaongeza kuwa wapo wanafunzi ambao wanachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza lakini hawajui kusoma wala kuandika.
Anasema hili ni tatizo kubwa ambalo limezidi kufanya shule iwe na matokeo mabaya katika siku za karibuni.

"Kuna wanafunzi walishawahi kuja hapa hawajui K.K halafu mtihani wa kidato cha pili hawachujwi hali hii ilifanya kuwa na matokeo mabovu kwenye mitihani ya kidato cha nne.

"Pia walimu kuhamishiwa kwenye shule za kata imechangia kushusha viwango vya taaluma kwani licha ya idadi ya watoto kuongezeka walimu wamezidi kupunguzwa.

Waliosoma Azania;
Generali Devis Mwamunyange – Mkuu wa majeshi nchini;
Suleiman Kova – Kamishna Kanda maalumu ya Dar es Salaam;
Jobu Msuya – Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani,
Cleopa David Msuya.
Eliakimu Maswi – Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini;
Emmanuel Nyalali – Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na
John Mongela – Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Tatizo la utoro
Mkuu wa shule anasema katika vitu ambavyo vimechangia kushuka kwa taaluma shuleni hapo ni utoro ambapo kuna utoro wa rejareja, jumla na wa msimu.

Ngozye akizungumzia utoro uliokithiri wa reja reja anasema kwamba wapo wanafunzi wanaokuja kwa wakati mfano anaweza kuja asubuhi anaingia kwenye vipindi vya masomo na vingine haingii.

Utoro wa jumla ni ule ambao mwanafunzi anaweza kuacha kufika shule kwa kipindi cha mwezi mmoja bila kutoa taarifa. Hata hivyo, uongozi wa shule umeweka sheria ndogo inayowabana wanafunzi endapo siku 90 akionekana hajafika shule anafukuzwa.

Akizungumzia utoro wa msimu huu unasababishwa na wazazi kugombana, ambapo mmoja wao akiondoka watoto wanakosa sehemu ya kuishi hivyo huanza kutangatanga.

"Utakuta mtoto anakaa mhula mmoja haonekani shule wala hakuna taarifa zozote, baadaye mzazi au mlezi mmoja wao anakuja na kutoa taarifa za kutokuelewana au kufariki dunia.

"Ili kuepusha jambo hili wazazi au walezi wanapaswa kutoa taarifa endapo kuna matatizo yametokea," anasema.

Changamoto
Azania inakabiliwa na tatizo kubwa la miundombinu chakavu ya majitaka hali inayochangia wanafunzi kushindwa kujisaidia kwa kuhofia afya zao.

Mkuu wa shule anasema bomba la kusafirisha maji taka kuelekea baharini limezidiwa kwani ni la miaka mingi hivyo kutokana na ongezeko la watu katika eneo hilo uchafu hausukumwi ipasavyo hali inayosababisha hatari ya magonjwa ya mlipuko hasa katika msimu wa mvua.

"Hali hii pia imechangia kwa kiasi kikubwa watoto kutoroka shule… wengine ni watanashati hivyo wakiona wanasoma katika mazingira kama yale hawatakubali kuja shule," anasema.

Anasema shule ina majengo ambayo ni ya miaka mingi hivyo yanahitaji kukarabatiwa kwa kupakwa rangi na kubadilishwa mabati kwani mengine yanavuja msimu wa mvua.

Ngozye anasema shule pia inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati na viti ambapo katika kukabiliana na changamoto hiyo aliwaita wazazi wenye watoto wanaosoma hapo kisha wakachangia zaidi ya milioni hivyo tatizo hilo likapunguzwa.

"Tunashukuru wazazi na wadau wa elimu ambao wanajitolea michango yao kwa ajili ya kuendeleza Azania kwani mtoto anayesoma hapa atakwenda kufanya kazi na jamii atahudumia kila mtu katika sekta atakayokuwa," anasema Ngozye.

Anatoa rai kwa wadau wa elimu kwamba katika kuchangia maendeleo ya shule si wajibu wa wazazi wenye watoto wanaosoma tu au kwa wale waliomaliza tu bali ni kwa kila mtu anayeguswa kwani shule ni ya kila mtu.

ALIYEKUWA MKUU WA KWANZA MWAFRIKA
MTANZANIA lilifika hadi nyumbani kwa Mwafrika wa kwanza anayejulikana kwa jina la Abdulrahmani Mwalongo, ambaye aliongoza shule hiyo kuanzia mwaka 1966 hadi 1971.

Mwalongo ambaye ana zaidi ya miaka 80 sasa anaishi Temeke Mwembeyanga mtaa wa Ruvuma, anasema mwaka 1956 alikuwa anasoma Chuo Kikuu cha Makerere na baada ya kuhitimu alirudi nyumbani na kuanza kufundisha, shule ambazo alifundisha kabla ya Azania ni Songea, Tabora na Chuo cha Ualimu Mpwapwa.

"Nilikuwa mwalimu mzuri wa masomo ya Hesabu, Biashara na Kilimo na masomo yangu wanafunzi wangu walikuwa wanafanya vizuri," anasema Mwalongo.

Akizungumzia taaluma katika Shule ya Azania enzi hizo Mwalongo anasema, wanafunzi walikuwa wana uwezo mkubwa katika masomo kwani kulikuwa na mwanafunzi mmoja alikuwa anapata alama ‘A' masomo yake yote.

"Kipindi hicho wanafunzi waliokuwa wanasoma hapo ni watoto wa Wahindi, Mabalozi na shule ilikuwa ni ya mchanganyiko co - Education, pia kulikuwa na Bwalo, hosteli moja na nyumba ya mwalimu, kulikuwa na maabara tatu ya Kemia, Baiolojia na Fizikia kwa kweli palikuwa pazuri sana," anasema.

Chanzo: MTANZANIA
 
Back
Top Bottom