Miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika: Abdul Sykes, Japhet Kirilo na Earle Seaton the Meru land case, 1952

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,915
30,259
MIAKA 60 YA UHURU WA TANGANYIKA 1961: ABDULWAHID SYKES, JAPHET KIRILO, NA EARLE SEATON - THE MERU LAND CASE 1952

Japhet Kirilo na Earle Seaton wameandika kitabu, ‘’The Meru Land Case,’’ kuhusu mgogoro wa ardhi ya Wameru ambayo ardhi yao ilichukuliwa na Wazungu bila fidia.

Mimi nimekieleza kisa hiki kufuatana na jinsi Abdulwahid Sykes akiwa kiongozi wa TAA alivyokishughulikia akishirikiana na Earle Seaton na Japhet Kirilo kwa nia ya kuongeza ufahamu wa mkasa huu.

Naweka hapo chini kipande kidogo kutoka kitabu cha maisha ya Abdul Sykes:

Wakwanza aliyekaa kushoto ni Japhet Kirilo na Wanne waliosimama ni Abdul Sykes.
Baada ya Dr Kyaruzi kuhamishiwa Nzega nafasi ya rais ikawa wazi.

Abdulwahid akakaimu nafasi hiyo sasa akiwa katibu na kaimu rais wa TAA. Mgogoro wa ardhi ya Wameru ulikuwa umekwishaanza lakini bado haujalipuka kuwa suala lililowahusu Watanganyika wote.

Umoja wa Mataifa ulipotuma ujumbe wake wa pili kuzuru Tanganyika mwaka wa 1950, Wameru waliwasilisha rasmi malalamiko yao kwa ujumbe huo.

Abdulwahid aliwaomba wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria washirikiane na TAA katika kutatua baadhi ya matatizo yanayokabili jamii ya Waafrika.

Abdulwahid alifadhaishwa na wajumbe Waafrika katika Baraza la Kutunga Sheria pale waliposhindwa kuipinga Wilson Report ambayo ilipendekeza kuondolewa kwa wananchi wa Meru kutoka kwenye ardhi yao.

Katika barua aliyoiandikia Meru Citizenís Union, Abdulwahid, kwa niaba ya makao makuu ya TAA, aliwahakikishia watu wa Meru kuwa tatizo lao llilikuwa tatizo la Watanganyika wote.

Abdulwahid aliamua kutumia mgogoro wa ardhi ya Wameru kuwaunganisha Watanganyika wote dhidi ya serikali ya kikoloni.

Uamuzi wa serikali juu ya mapendekezo ya TAA kwa Constitutional Development Committee ulikuwa bado umo akilini mwake.

Alitambua kwamba uamuzi wa Gavana ulikuwa ni mpango wa muda mrefu wa kuwadhalilisha Waafrika katika utumwa wa daima.

Abdulwahid sasa akiwa na ghera kubwa alianza kufanya kazi ya kuwahamasisha watu wa Tanganyika chini ya vuguvugu la kuunganisha umma dhidi ya utawala wa Waingereza.

Abdulwahid aliwasiliana na Earle Seaton mjini Moshi kutaka ushauri wa kisheria juu ya tatizo la Meru. Seaton alikuja Dar es Salaam na kukutana na Abdulwahid na uongozi wa TAA.

Ilikubaliwa na pande zote mbili kuwa makao makuu ya TAA, Meru Citizens Union ikiongozwa na Japhet Kirilo na Seaton lazima waunganishe shughuli zao katika kesi hiyo na kwa pamoja watume rufaa yao kwenye Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa huko New York.

Kwa sasa uongozi wa chama cha TAA ulitambua kwamba nusura yao ilitegemea uwezo wao wa kudhibiti na kushawishi matukio na maamuzi ndani ya Baraza la Kutunga Sheria.

Ili kuweza kufanya hayo shinikizo lilitakiwa kuwekwa katika Baraza la Udhamini huko New York, nchini Amerika na siyo katika Ofisi ya Makoloni pale London Uingereza.

Tawi la chama cha TAA la Tabora lilichukua changamoto hiyo kwa kupitia juhudi za Kandoro aliyeuona mgogoro wa ardhi ya Wameru kama jukumu lake binafsi.

Kandoro aliitisha mkutano wa matawi ya TAA ya Mwanza, Kigoma na Tabora kujadili suala hilo.

Mwanza iliwakilishwa na Bhoke Munanka, Mzee Mkama Mlaji na Mohamed Kihaka Kitenge; kutoka Kigoma mjumbe aliyekuja alikuwa Jumanne Mawimbi na Tabora iliwakilishwa na Sheikh Kinana, Kandoro na George Magembe kama rais wa TAA tawi la Tabora. Mkutano wa Tabora uliahidi mshikamano wa pamoja na watu wa Meru katika mapambano dhidi ya walowezi.

Mgogoro wa ardhi ya Meru ni wa pekee katika historia ya Tanganyika. Ilikuwa kupitia katika mgogoro huo ndiyo Mtanganyika, Japhet Kirilo, akifuatana na Earle Seaton kama mkalimani na mshauri wa sheria, kwa mara ya kwanza alizungumza mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa huko New York, na kuonyesha udhalimu wa ukoloni.

Mnamo November, 1952 Kirilo alizungumza mbele ya Kamati ya Nne ya Baraza Kuu.

Watu wa Tanganyika sasa walikuwa wanayachukua mapambano yao toka mipaka yao hadi kwenye kumbi za Umoja wa Mataifa, mjini New York kutafuta haki.

Lakini Kirilo alirudi mikono mitupu.

Rufaa ya mgogoro wa ardhi ya Wameru ilitupiliwa mbali. Kirilo aliuhakikishia Umoja wa Mataifa kuwa watu wake kamwe hawatachukua silaha kuikomboa ardhi yao kama Wakikuyu wa Kenya walivyojaribu kufanya.

Kwa kweli hapakuwa na sababu ya kutoa kauli hii, kwa kuwa uhakikisho wa kutokuwepo mapambano uliwafanya walowezi washushe pumzi na kujiona wako salama.

Tangu mwanzo wa mgogoro wazalendo nchini Kenya kama Fred Kubai na Kung'u Karumba walikuwa wakitoa ushauri kwa Meru Citizens Union kwa kuwa wao walikuwa na ujuzi zaidi wa matatizo ya walowezi kuliko watu wa Tanganyika.

Kwa mtazamo wa juu juu mtu anaweza kudhani kuwa Abdulwahid alikuwa akipata kipigo kutoka sehemu zote alizojaribu kuipenyeza TAA kutoka mwaka wa 1948 katika enzi za chama cha makuli, kufikia marekebisho ya katiba hadi kumalizikia kwa mgogoro wa ardhi ya Wameru.

Kushindwa huku si kwa sababu TAA ilikuwa ina viongozi dhaifu au ilikuwa haiuingwi mkono na umma.

TAA ilikuwa haifanikiwa katika madai yake kwa sababu serikali ya kikoloni ilikuwa imeamua kutosikiliza lolote kuhusu matatizo ya Waafrika.

Matokeo ya hali hii ilimfanya Abdulwahid aamue kuwa njia iliyobakia ya Tanganyika kujitoa katika makucha ya Waingereza ni kuuandaa umma wa Tanganyika chini ya chama cha siasa.

Mara tu baada ya Kirilo kurejea kutoka New York, mpango wa kuanzisha chama cha siasa cha kushirikisha umma wote ulianza.

Uongozi wa TAA Makao Makuu ulianza kampeni ya nchi nzima kuueleza umma matokeo ya safari ya Kirilo kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa ardhi ya Wameru na vilevile kuchangisha fedha za kupeleka msafara mwingine katika Umoja wa Mataifa kuueleza umoja huo kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya udhamini na Watanganyika walikuwa sasa na haki ya kudai uhuru wao.

Kamati ya TAA ya watu watatu iliyowajumuisha Kandoro, Kirilo na Abbas Sykes iliundwa kwa ajili hiyo.

Ally Sykes akiwa mweka hazina msaidizi wa TAA aliombwa ampelekee Kirilo hawala ya posta Usa River kama nauli ya kumwezesha kusafiri hadi Dodoma kujiunga na ile kamati ya watu watatu.

Kulikuwa hakuna huduma ya fedha katika posta ya Usa River na fedha zile zilikaa hapo kwa muda bila ya kuchukuliwa hadi hapo zilipopelekwa posta ya Arusha mjini ambako Kirilo alizichukua.

Kuanzia tarehe 26 Septemba, 1953 kwa takriban mwezi mmoja ile kamati ilitembelea na kuhutubia mikutano ya hadhara, ikikusanya fedha Dodoma, Mwanza, Bukoba, Ukerewe, Tarime, Musoma na Shinyanga.

Rais wa chama cha TAA, kanda ya ziwa, Paul Bomani aliipokea ile kamati ya watu watatu na kuhutubia mikutano pamoja nao katika jimbo lote.

Bomani aliwaambia wanachama wa TAA na wananchi wote mjini Mwanza kuhusu umuhimu wa kuchanga fedha kwa kusudio hilo.

Picha ya kwanza ni Earle Seaton, picha ya pili Waasisi wa TANU waliokaa wa kwanza kushoto ni Japhet Kirilo, 1954 na picha ya nne kulia ni mwandishi na kushoto ni Abdulwahid Ally Sykes wakiwa nje ya nyumba ya Japhet Kirilo USA River.

Abdul alimpeleka mwandishi kwa Kirilo lakini bahati mbaya alikuwa amesafiri kwenda Nairobi.

Kirilo akimpenda sana Abdul wa kuwa alikuwa akimkumbusha rafiki yake Abdul Sykes muasisi mwenzake wa TANU na mtu aliyemsaidia sana wakati wa Mgogoro wa Meru.

Screenshot_20211126-221052_Facebook.jpg
 
Back
Top Bottom