Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,743
- 2,601
Chama cha Mapinduzi kinaadhimisha miaka 49 tangu kilipoanzishwa Februari 5, 1977 baada ya kuunganishwa vyama vya TANU iliyokuwa Tanganyika na ASP iliyokuwa Zanzibar. Kwa hiyo CCM ni zilezile TANU na ASP zilizopambana wakati wa ukoloni.
Ni miongoni mwa vyama vikongwe vya ukombozi barani Afrika vikijumuisha vyama saba vikuu vilivyounda Umoja wazamani wa ukombozi Kusini mwa Afrika (FLMSA), ambavyo ni ANC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia), MPLA (Angola), FRELIMO (Msumbiji), ZANU-PF Zimbabwe), na BDP (Botswana).
Ukifuatilia mwenendo wa vyama hivi kwa sasa vimepoteza mwelekeo, lakini baadhi yake vimebaki madarakani kwa nguvu za Dola na matumizi ya majeshi kuwalazimisha wananchi kuvipenda, wakati havina tena mvuto.
Sababu kubwa ni kwamba, wakati vinapigania uhuru, vilitoa ahadi kwa wananchi kwamba vitarejesha matumaini yaliyochukuliwa na Wakoloni na kwa wakati huo walikuwa ni Wazungu. Waliwaaminisha Waafrika kuwa mchawi wa matatizo yao ni Mzungu, hivyo kuwaondoa Wakoloni lilikuwa ndio suluhisho.
Lakini Wakoloni walipoondoka, viongozi wa vyama hivyo wakarithi tabia zilezile za wakoloni, wakajitajirisha, wakawasahau tena wananchi. Kwa muda mrefu matumaini ya wananchi kwa wa vyama hivi yametoweka, kilichobaki sasa ni kuendelea kubaki madarakani kwa nguvu za Dola.
CCM inalindwa na nafuu ya kuwa madarakani?
Hapo ndipo ilipofika CCM leo, kubaki kwake madarakani ni kwa sababu tu ya nguvu za Dola. Hayo ni maneno aliyoyasema aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally (sasa ni waziri wa Mifugo na Uvuvi), alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa vyombo vya habari vya IPP, Machi 7, 2020 jijini Dar es Salaam.
Alisema chama kinapokuwa madarakani kinakuwa na faida ya kuwa madarakani (incumbency advantage) na endapo chama hicho kikishindwa kuitumia hiyo faida hiyo itakuwa ni hasara kwake.
Your browser is not able to display this video.
Wakati Dk Bashiru akihimiza matumizi ya Dola kubaki madarakani, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliwahi kuwaasa wana CCM kutotegemea Jeshi la Polisi kutekeleza shughuli zake.
Kikwete alitoa kauli hiyo Novemba 14, 2012 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM uliofanyika kwa siku tatu mfululizo katika Ukumbi wa Kizota mjini Dodoma.
Kikwete aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, alisema kitendo cha wanaCCM kuishi katika siasa kwa kutegemea Jeshi la Polisi hakipaswi kukubaliwa kwani kimepitwa na wakati.
“Mnaishia kulalamika tu kila siku, eti wanatukana halafu mnaishia kusema ndiyo kawaida yao…au utasikia mtu anasema eti Serikali haipo! Kazi ya Serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu,” alisema Kikwete na kuongeza:
“Sasa mnataka wakisema Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi wawafuate, au wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wakawakamate? Kama wakisema hatujafanya kitu ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni barabara, shule na mambo mengine.”
Licha ya kwamba hakuwataja moja kwa moja, kauli za Rais Kikwete zilikuwa zikielekezwa kwa uogozi wa Chadema ambao kimsingi kinaonekana kuwaumiza vichwa CCM.
Huku akirudia mara kadhaa maneno hayo alisema, “Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli.”
Uchaguzi mkuu Oktoba 29
Ukirejea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 utaona kabisa kwamba CCM leo ni kwamba imepoteza kabisa mvuto kwa wapiga kura hasa vijana na ndio maana waliandamana kuupinga uchaguzi ule uliokuwa ukilalamikiwa kwa kutozingatia misingi ya demokrasia.
Tulimsikia Rais Samia Suluhu Hassan wakaati wa kampeni, akijitangaza kuwa yeye ni Amiri Jeshi Mkuu na atahakikisha hakutakuwa na maandamano bali watu watakwenda kupiga kura. Aliitumia kauli hiyo kwa karibu mikutano yake yote.
Kwa maana nyingine, Rais Samia alikuwa akijitapa kuwa Amiri Jeshi Mkuu aliyezungukwa na majeshi yote, wakati huo huo anaomba kura. Kwa hali kama hiyo, vyama vingine vilikuwa na wagombea wasio na chochote hawakuwa na cha kujitapa kwa wapiga kura.
Kwa vyama kama CHADEMA waliopinga mfumo mzima wa uchaguzi, Mwenyekiti wao, Tundu Lissu alikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uhaini yasiyo na dhamana.
Tulishuhudia vikosi vya majeshi vikifanya mazoezi na kupiga kwata barabarani, kutisha wananchi.
Yaani uchaguzi uligeuzwa kuwa zoezi la kijeshi, watu watake wasitaki ni lazima watii amri ya kwenda kupiga kura.
Lakini ilipofika siku ya kupiga kura, idadi ya wapiga kura ilikuwa ndogo sana. Ni kama watu walikuwa wameususia ule uchaguzi. Ilipofika saa 5 asubuhi, maandamano yalilipuka jijini Dar es Salaam na yakasambaa katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro, Njombe na Iringa.
Waandamanaji walichoma moto vituo vya kupigia kura, walichoma vituo vituo vidogo vya polisi, ofisi za Serikali za Mitaa, Vituo vya mabasi ya mwendokasi na magari. Kwa ujumla uchaguzi kwenye mikoa hiyo ulivurugwa kabisa.
Lakini cha kushangaza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliendelea kutangaza matokeo, sijui waliyapataje kwenye maeneo yaliyokuwa na vurugu. Matokeo yakawa kwamba Rais Samia ameshinda kwa asilimia 97.6 ya kura milioni 31.91.
Wakati huo huo, waandamanaji walikabiliwa kwa nguvu ya risasi, hali iliyosababisha mauaji na majeruhi. Mpaka leo Serikali inaogopa kutaja idadi ya watu waliouawa kwenye maandamano, maana ni aibu.
Maoni ya waangalizi
Hata ukiangalia ripoti za waangalizi wa uchaguzi utaona, kulikuwa na walakini katika uchaguzi huo. Kwa mfano ripoti ya waangalizi wa SADC (SEOM), waliokuwa wakiongozwa na Richard Msowoya, Spika wa zamani wa Bunge la Malawi, alisema pamoja na mengine, kulikuwa na idadi ndogo ya wapiga kura iliripotiwa, na katika baadhi ya vituo hakukuwa na wapiga kura kabisa.
Pia alisema kulikuwa na tuhuma za udanganyifu wa kura kutokana na kura za mafungu zilizokuwa zimepangiliwa vizuri kwenye masanduku ya kura zikiashiria watu walipiga kura nyingi kwa wakati mmoja, pamoja na ukosefu wa waangalizi wa ndani katika vituo vingi.
Aligusia pia suala la kufungwa kwa mtandao wa intaneti kulizuia SEOM kupata takwimu kamili za upigaji kura na kuhesabu na waangalizi wengi hawakuweza kushuhudia kufungwa na kuhesabiwa kwa kura kutokana na matukio na vitisho vya vurugu katika baadhi ya maeneo.
Ripoti za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, Mtandao wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (EHORN) na ile ya Chama cha African National Congress cha Afrika Kusini pia vilikosoa mwenendo wa uchaguzi huo.
Thabo Mbeki
Taasisi ya Thabo Mbeki ya nchini Afrika Kusini nayo ilitoa ripoti yake Novemba 23, 2025 ikikosoa uchaguzi huo.
Taasisi hiyo ilieleza kusikitishwa na uvunjifu wa amani uliojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu nchini humo, ikisema kuwa imekosa ‘serikali halali’.
Kulingana na taasisi ya Thabo Mbeki, matokeo ya urais na ubunge nchini Tanzania, hayaakisi matakwa ya Watanzania wenyewe.
Mbali na taasisi hiyo, Rais wa zamani wa Botswana, Seretse Ian Khama, akizungumza katika kongamano la African Renaissance lililofanyika Lukenya University nchini Kenya Novemba 10, 2025, alisema “hamtambui Rais Samia Suluhu Hassan kama kiongozi halali wa Tanzania.”
Alieleza kuwa uchaguzi wa mwaka 2025 ulitawaliwa na vitisho, vifo, na ukandamizaji wa wananchi waliopinga utawala, akisisitiza kuwa mazingira hayo hayakuruhusu demokrasia ya kweli.
Hata hivyo, mara kdhaa Rais Samia amesikika akitetea uchaguzi huo, akisema wanachi walijitokeza mapema kwenda kupiga kura kabla maandamano hayajatokea.
Seretse Ian Khama
Rais Samia Suuluhu Hassan alijibu maoni ya waliohoji uchaguzi huo mara kadhaa na hata alipozindua Bunge la Jamhuri ya Muungano, Jovemba 14, 2025, Rais Samia alisema utaratibu wa kuongeza vituo vingi vya kupigia kura ulisaidia sana kupunguza msongamano katika vitu hivyo.
“Jambo lililowafanya baadhi ya waangalizi wa uchaguzi kudhani wananchi hawakujitokeza kupiga kura.”
Ushindi bila shamrashamra
Licha ya ushindi huo wa Rais Samia, bado sherehe za kumwapisha zikafanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, ambapo walialikwa watu mashuhuri tu, wakiwa marais na viongozi wa nchi wa nchi jirani.
Kwa nini Rais aliyeshinda kwa asilimia 97.6 asije kuapishwa kwenye uwanja wa wazi kama ilivyozoeleka? Maana yeye ndiyo rais anayependwa Zaidi na wananchi kuliko marais wote waliopita.
Kwa ushindi huo, tungetarajia kuoa Rais Samia akiandaliwa maandamano makuwa kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Tanga. Mbona kimya?
Rais Samia aliingia madarakani Machi 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, hayati Rais John Magufuli, ambapo wananchi walipata matumaini makubwa ya kupatikana kwa utawala unaojali demokrasia na uhuru wa maoni. Lakini tunachokishuhudia ni kinyume chake kabisa.
CCM itajisafishaje?
Katika maazimio ya kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM cha Novemba 5, 2025 kilichoongozwa na Rais Samia, wajumbe walikubaliana pamoja na mengine walikubaliana chama kujitathmini na kujiopanga kubeba dhima ya kuliongoza Taifa.
Hapa kwa kweli CCM inapaswa kujitathmini upya kama bado inakubalika kwa wananchi. Achana na huo uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, ambao hata matokeo hayaeleweki yamepatikanaje, chama kijiulize, huko mitaani wanakichukuliaje?
Angalau jambo moja, Rais Samia ameunda Wizara inayoshughulika na masuala ya vijana. Hii ni kwa sababu wanaona kabisa vijana ndio wamepoteza hamu na chama chao, kwa hiyo wanajaribu kuwavutia kwa kuwapa wizara, kuwapa motisha hapa na pale, mikopo, ajira za hapa na pale. Lakini hiyo ndio imetosha?
Jambo la muhimu kwa chama hicho ni kukubali makossa kwa yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na kukubali kubeba lawama kwa kuwawajibisha watendaji waliosababisha yatokee. Toba ya kweli ya chama hii itarejesha Imani kwa wananchi.
Bila kufanya hivyo, CCM italazimika kuiongoza nchi hii kidikteta kwa mtutu wa bunduki, kwani wananchi hawatakubali kuburuzwa kwa mambo wasiyoyataka.