Miaka 32 ya CCM na visheni iliyokwenda kombo! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Miaka 32 ya CCM na visheni iliyokwenda kombo!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Feb 11, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Feb 11, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 60,393
  Likes Received: 39,800
  Trophy Points: 280
  Miaka 32 ya CCM na visheni iliyokwenda kombo!

  Johnson Mbwambo Februari 11, 2009
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo​

  WIKI iliyopita chama tawala cha CCM kiliadhimisha miaka 32 tangu kizaliwe. Katika wiki ya maadhimisho hayo, tulisikia tambo za hapa na pale kuhusu uimara wa chama hicho na maendeleo ambayo kimeyaleta hapa nchini.

  Buddha, aliyeishi kati ya mwaka 536 BC na 483 BC, alipata kunukuliwa akisema “believe nothing, no matter who said it unless it agrees with your own reason and your own common sense” (usiamini chochote, na haijalishi nani kakisema; labda kiwe kinakubaliana na kile unachokiamini wewe na kile ambacho, kwa mtazamo wako, ndiyo ukweli).

  Kwa msingi wa kauli hiyo ya Buddha, nina hakika Watanzania watapima wenyewe tambo za vigogo wa CCM tulizozisikia wiki iliyopita na watafanya tathmini zao wenyewe wanazoziamini moyoni kuhusu wapi kilipotoka chama hicho na wapi kinapoelekea.

  Lakini kwa mtazamo wangu, CCM ni kama chama kongwe cha Afrika Kusini cha ANC; yaani kilitoka kuzuri na kutenda mema kwa wananchi wake; lakini sasa kinaelekea kuzimu kwa sababu ya kuwatosa wanyonge.

  Najua wapo watakaokerwa na kauli hiyo, lakini naomba hao niwarejeshe katika kauli za mwisho mwisho za mwasisi wa CCM, Mwalimu Nyerere kuhusu chama hicho alichokianzisha, akakilea, akakipa visheni na misheni, kikachanua; lakini, kabla hajafariki Oktoba 14, 1999, kikapoteza kabisa mwelekeo wake.


  Akiwa ameudhiwa na mwelekeo wa chama hicho, Mwalimu alipata kutamka kwamba “CCM si mama yangu”. Kwa hakika, Mwalimu hakuficha kuonyesha hisia zake kwamba kama kungekuwa na chama kingine cha siasa nchini ambacho ni imara na anachokubaliana nacho ki-sera na katika visheni yake, angeihama CCM na kujiunga nacho.

  Ni bahati mbaya kwamba Mwalimu hakuishi miaka mingi kukiona chama cha aina hiyo kikitamalaki nchini, lakini naamini hisia zake hizo bado ni hisia za Watanzania wengi tu ambao bado wamebakia kuwa wanachama wa CCM kwa sababu tu hawaoni pa kwenda, na si kwamba wanaridhishwa na chama hicho!

  Kwa hiyo, wale wanaotaka kuiamini kauli iliyotolewa wiki iliyopita na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa kwamba CCM kimekuwa imara zaidi; niwakumbushe tu kufanya rejea ya kauli ile ya kale ya Buddha – believe nothing, no matter who said it unless it agrees with your own reason and common sense.

  Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa
  Kuna vigezo vingi vinavyopaswa kutumika katika kuzipima tambo hizo za Msekwa kuhusu CCM, lakini kwa kuwa kimekuwa chama tawala tangu kianze (miaka 32 iliyopita), kigezo kikuu kinakuwa ni namna ambavyo serikali yake inawahudumia Watanzania kuyafanya maisha yao yawe bora zaidi.

  Natujiulize (kwa mfano): Ni kweli CCM imeyafanya maisha ya Watanzania walio wengi kuwa bora zaidi – miaka mitano au kumi iliyopita?

  Katika kujaribu kulijibu swali hilo, hebu tuuangalie mfano ambao watawala wenyewe, mwaka jana, walitupatia kuhusu hilo.

  Mnamo Oktoba 3, 2008 Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo alitangaza takwimu mpya za hali ya umasikini nchini. Takwimu hizo zilitokana na utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu nchini unaoitwa “Household Budget Survey”. Takwimu hizo mpya zinaonyesha kuwa Watanzania walio masikini wameongezeka na kufikia milioni 12!

  Kwa mujibu wa takwimu hizo, wastani wa pato la Mtanzania kwa mwezi ni Sh. 14,000 tu; yaani Sh. 460 kwa siku! Sasa natujiulize; Ni wapi katika Tanzania hii ambapo mtu anaweza kupata mlo mmoja tu kwa siku uliokamilika kwa Sh. 460?

  Kama jibu ni hakuna, sasa tambo kwamba CCM kimekuwa imara zaidi ina mshiko gani? Maana uimara wa CCM unapaswa upimwe kwa kuangalia pia ufanisi wa serikali yake katika kuboresha maisha ya Watanzania. Je, CCM kimekuwa imara kwa sababu serikali yake imeongeza idadi ya masikini Tanzania hadi kufikia milioni 12?!

  Lakini hata ukiangalia suala la ufanisi wake katika vita dhidi ya ufisadi na rushwa, CCM cha sasa ni hovyo zaidi kuliko ilivyopata kuwa huko nyuma.

  Si siri, kwa mfano, kwamba chama hiki kimeshindwa, au hakina nia ya kweli, kukomesha rushwa katika chaguzi zake. Na kwa sababu hiyo, viongozi wake wengi na wale wanaoingia serikalini, ni wale walioshinda kupitia chaguzi hizo za rushwa.

  Kwa hakika, tumefika mahali ambapo baadhi yetu tumeshaanza kujenga fikra kwamba watawala wetu wanapenda hali ya umasikini izidi kuendelea kutamalaki kote nchini – vijijini na mijini; kwani kwayo; ndiyo huweka mazingira yanayowawezesha kushinda uchaguzi kirahisi.


  Mantiki hapa ni kwamba kwa kuwa uchaguzi ni rushwa, kiasi kiwango cha umasikini kinavyokuwa kikubwa ndivyo pia wagombea watakavyolazimika ‘kununua’ kura kwa pesa kidogo.

  Mathalan; mtu mwenye hali nzuri kidogo kimaisha huwezi ‘kununua’ kura yake kwa doti moja tu ya kanga! Huyu utapaswa umpe labda Sh. 100,000 wakati kwa masikini Sh.10,000 tu (au hata pilau tu) zinatosha!

  Hiyo ndiyo hali inayokuwepo katika chaguzi za CCM, na ndiyo pia hali inayojitokeza wakati wa uchaguzi wa wabunge na rais. Na wenyewe wameizoea kiasi kwamba hawakuona hata haya, mwaka 2005, walipochota mabilioni ya pesa za EPA na kuyatumbukiza katika kampeni zao za uchaguzi.

  Matokeo ya hali hii ni kwamba tunapata viongozi waovu right from the start. Viongozi wa namna hiyo, wanaoingia madarakani kwa njia hizo ovu, wakishashika hatamu za uongozi, ufisadi kwao ni mbele kwa mbele!


  Kwa maneno mengine, CCM ya sasa imeacha kusimamia suala la maadili, na matokeo yake kada ya viongozi sasa imejaa mafisadi. Kugombea uongozi si tena ni kutafuta fursa ya kutumikia wananchi na kuboresha maisha yao; bali ni kutafuta njia ya mkato ya kujitajirisha!

  Ndiyo maana, kama Buddha alivyotuasa, tunapaswa kusemezana na nafsi zetu na kujiuliza: Kama hali ni hiyo, je, tambo hizi kwamba CCM imeimarika zaidi inatoka wapi wakati serikali yake inakumbwa na kashfa nzito mno za kifisadi kuliko kipindi chochote katika historia ya taifa letu?

  Sitaki kuzungumzia kwa undani kuhusu kashfa hizo za ufisadi; kwani itakuwa ni marudio tu, na wala sitaki kuzungumzia tambo nyingine kama vile kuboresha elimu kwa kujenga utitiri wa shule hizi za sekondari za kata zisizo na walimu, vitabu au maabara.

  Lakini hata ukienda kwenye masuala ya utawala bora, CCM ya sasa ni ya hovyo kuliko ya miaka ya nyuma. Ndani ya miaka 15 iliyopita tumeshuhudia kanuni na miongozo ya chama hicho ikiwekwa pembeni ili ‘kuwalinda’ maswahiba au ‘kuwatosa’ wanaoonekana ni maadui.

  Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumeshuhudia siasa za kulindana (mtandao syndrome) zikitawala na kushamiri ndani ya chama hicho na ndani ya serikali yake, mambo ambayo enzi za Mwalimu Nyerere yasingeweza kutokea.

  Nimalizie tafakuri yangu hii kwa kuikumbusha CCM kwamba wakati wa enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, CCM kilikuwa kweli kweli ni chama cha wakulima na wafanyakazi; lakini sasa ni chama cha masikini na matajiri ila wakati wa uchaguzi, masikini ndio wapiga kura na matajiri ndio wagombea. Niikumbushe pia kwamba masikini na matajiri, kamwe, hawawezi kuwa na visheni moja ndani ya chama hicho.

  Ukiniuliza mimi ni kitu gani CCM na serikali yake bado inajivunia, jibu langu ni amani na utulivu. Kwamba pamoja na umasikini mkubwa wa Watanzania wengi katika nchi yenye mabilionea kibao, bado nchi yetu ni ya amani na utulivu kuliko nchi nyingi za Afrika.

  Kama hivyo ndivyo, basi, ni wajibu wa CCM na serikali yake kuilinda amani kwa nguvu zake zote; maana ndicho kitu pekee kikubwa ambacho chama hicho kinajivunia katika miaka 32 ya kuanzishwa kwake.

  Na kwa mtazamo wangu, njia bora ya kuilinda amani hii ni kuhakikisha haki inatendeka kwa wote, na kwamba pengo kati ya matajiri na masikini linapunguzwa kwa kasi. Vinginevyo, CCM itapoteza hata hicho kitu pekee inachojivunia katika miaka yake 32!

  Niseme tu kwamba baadhi yetu tulifarijika hivi karibuni baada ya kupata habari kwamba Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliandaa mkutano wa faragha kule Zanzibar ambapo wajumbe wengi walikiri kwamba ilikuwa ni makosa kulifuta Azimio la Arusha kwa kuweka Azimio la Zanzibar.

  Tuombe Mungu tu kwamba mkutano huo wa siri wa UVCCM wa Zanzibar, ni mwanzo wa mchakato wa kurejesha nchini misingi ya Azimio la Arusha, azimio ambalo lilihakikisha kwamba angalau Watanzania wengi wananufaika na keki ya taifa.

  Tafakari.
   
 2. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #2
  Mar 23, 2009
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 201
  Trophy Points: 160
  CCM haifai hata kupewa uongozi wa nyumba kumikumi,imeshapoteza dira ,haina muelekeo wa kurudi katika mstari wa uongozi bora,maana mihimili yote ya uongozi wao imejaa wizi na kashfa kubwa kubwa za mabilioni ya shilingi kupotea tokea historia ya wizi ambayo ilishamiri wakati wa Mkapa na kudhihiri wakati wa Kikwete ni ushahidi wa wazi kuwa leo hii ,ubadhirifu huo umo ndani ya kiongozi mmoja mmoja ,kila alie kiongozi hufikiria njia za kukwiba na sio za kuongoza ,wachache waliomo ndani ya CCM hawawezi kuepuka wizi huu ikiwa wataendelea kuwemo ndani ya Chama hicho ni lazima wakiache mkono na kutafuta kwengine ,kubaki humo humo hakutasaidia chochote kwani wamezidiwa na kupoteza nguvu za kuwawajibisha wahusika ,mambo ya kuambiana wakutane katika vikao vyaoChama vya wabunge kusawazisha na wengine kusema tuzungumzie kitaifa ndani ya Bunge zima ,ni kuonekana kushindwa kuchukuliana hatua za kisheria ,ile nguvu ya Watawala kwa kuwajibika kisheria na kuwawajibisha wengine ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wahusika wa uhujumu uchumi kwa haraka hazipo, serikali inaonekana kwenda mbio sana katika kuhangaika na wahujumu uchumi.
  Serikali ingeweza moja kwa moja kuzuia dhamana ,Raisi angeweza moja kwa moja kuzuia dhamna lakini wahusika ni marafiki na wafadhili kesi zinaonekana zinazorota kwa visingizio hivi na vile.
   
Loading...