Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,618
- 9,611
MFANYABIASHARA Antony Mandawa (58) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 30 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwanafunzi na kumsababishia ujauzito.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Rashid Chengula. Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa Mandawa ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Isanga jijini Mbeya, alishtakiwa na Jamhuri kwa makosa mawili ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza kinyume na kifungu namba 130 (2) e na 131 (1) ya kanuni ya adhabu.
Kosa la pili ni kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo, kinyume na kifungu namba 60 A (3) cha Sheria ya Elimu sura ya 353 na marekebisho yake kifungu namba 22 (3) cha sheria namba 2 ya mwaka 2016.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Chengula alisema mshtakiwa anahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 kwa kosa la kwanza ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya Sh milioni mbili.
Kosa la pili mtuhumiwa huyo alihukumiwa kutumikia jela miaka 30 kwa kosa la kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo, ambaye pia amemsababisha akatishe masomo yake na vifungo hivyo aliviamuru kwenda pamoja.
Hakimu Chengula alisema Mandawa alitenda kosa hilo Februari mwaka jana na mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyekuwa akisoma shule ya Upili Samora na kumsababishia ujauzito huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kwa mujibu wa Hakimu Chengula jamhuri kupitia mashahidi wake, akiwamo muathirika wa tukio hilo bila kuacha shaka, mfanyabiashara huyo amefanya makosa yote mawili hivyo kumtia hatiani na kumpatia hukumu hiyo.
Awali katika utetezi wake, mshtakiwa Mandawa alikana kutenda kosa hilo, huku akikosoa mwenendo wa shauri hilo kwa madai kuwa muathirika alichelewa kutoa taarifa akidaiwa kuripoti baada ya siku 30.
Aidha, alidai kuwa yeye ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na kujitetea kuwa mwanafunzi anayedaiwa kubakwa hajaathirika hivyo mahakama inathibitishaje kama kweli alimbaka, hata hivyo mahakama ilisema utetezi wa mshtakiwa hauna mashiko ya kutomtia hatiani.
Shauri hilo lilikuwa likiendeshwa na mawakili wawili wa serikali ambapo miongoni mwao ni Davice Msanga ambaye aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
HabariLeo