Miaka 20 ya Viagra na mchango wake kwa wanaume

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
pic+viagra.gif


Kabla ya Viagra kuingia sokoni, ukosefu wa nguvu za kiume ulimaanisha fedheha, aibu na wakati mwingine ndoa au uhusiano kuvunjika. Leo hali ni tofauti, dakika 27 baada ya kumeza kidonge kimoja cha bluu, heshima inarudi ndani ya nyumba.

Miaka 20 iliyopita, kampuni ya utafiti wa dawa nchini Marekani, Pfizer ilipewa kibali cha kuingiza sokoni dawa za kuongeza nguvu za kiume ikifahamika kwa jina la Viagra. Kidonge hicho chenye rangi ya bluu kimepata umaarufu duniani kwa kubadilisha maisha ya wanaume wengi wenye tatizo la kukosa nguvu za kiume.

Kwa taarifa tu ni kwamba, Viagra wakati huo ikiitwa sildenafil ilitengenezwa kwa ajili ya kutibu shinikizo la juu la moyo na maumivu ya kifua, lakini ikaleta matokeo tofauti wakati wa majaribio.

Matokeo yake wakati wa majaribio ilisababisha kusisimka kwa mwili na sehemu za siri za mwanaume kusimama na tangu hapo, ikatajwa kuwa ni mapinduzi halisi kwa maisha ya wanaume, ikabadilisha maisha ya wengi wao waliokuwa na shida hiyo na ikawaongezea kujiamini kwa miongo miwili sasa.

Pamoja na kuwa dawa hiyo haikuleta matokeo tarajiwa, watafiti hao wakaona hiyo ni nafasi muhimu ya kuifanyia majaribio kwa namna ambayo ilitoa matokeo haya mapya.

Wakabadilisha aina ya majaribio kwa kuwatumia wanaume pekee wenye umri wa miaka 40 kwenda juu na matokeo yakawa chanya kwamba iliwasisimua na kusimamisha sehemu zao za siri.

Mpaka sasa mabilioni ya dozi yameuzwa duniani kote na inadaiwa imesaidia kubadilisha maisha ya wanaume hasa ambao umri ‘umesogea’.

Katika miongo miwili, wanaume wapatao milioni 30 ndani ya nchi 120 wametumia dawa hizo ingawa wapo ambao wananunua mtandaoni na madukani bila kufuata ushauri wa madaktari.

Kwa Marekani pekee, wanaume 10,000 huwa wanaandikiwa na daktari kila siku watumie dawa hizo.

Moja kati ya malalamiko ya Kampuni ya Pfizer ni uwapo wa Viagra feki sokoni, hali ambayo imeshusha mauzo yao duniani kwa kiasi kikubwa pia kusababisha usugu kwa baadhi ya watumiaji kwa kuwa haziwapi matokeo chanya.

Miaka mitano iliyopita, mauzo ya Viagra yalikuwa dola 2.1 bilioni lakini mwaka 2017 yalishuka karibu nusu yakiwa dola 1.2 bilioni.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Pharma mwaka 2011 ulionyesha asilimia 80 ya Viagra zinazouzwa mtandaoni ni feki.


Nini hutokea mwanamume anapotumia dawa za kuongeza nguvu za kiume?

Jarida la Human Reproduction linasema huchukua kati ya dakika 27na 30 uume kusimama mara baada ya mwanamme kumeza kidonge cha hicho.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Viagra haiwezi kumsaidia mwanamme kufika kileleni kama hana uwezo huo.

Baada ya mshindo mmoja, kwa mwanamme ambaye hajatumia Viagra anaweza kukaa dakika 20 hadi nusu saa kabla ya kusisimka tena kwaajili ya mshindo wa pili, lakini akitumia atapumzika kwa dakika 10.


Chanzo cha upungufu wa nguvu za kiume

Pombe, maradhi na ulaji wa vyakula usio na mpangilio mzuri ni baadhi ya mambo yanayotajwa kusababisha upungufu wa nguvu za kiume.

Daktari bingwa wa upasuaji wa tumbo na kifua wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Maurice Mavura anasema tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume lipo ingawa waathirika wengi hawafiki hospitali.

Anasema pengine walishindwa kujitokeza kwa kuhofia unyanyapaa au kuona aibu.

Dk Mavura anasema kutokana na sababu hizo, ni vigumu kueleza idadi ya wenye tatizo la nguvu za kiume kama wameongezeka ama wanapungua.

Daktari Anna Sarra wa Muhimbili pia, anasema tatizo hilo ambalo kitaalamu linaitwa Ericticle Dysfunction, husababisha na mambo mengi ikiwamo maradhi.

Anayataja maradhi hayo ni pamoja na kisukari, shinikizo la damu, uti wa mgongo na kuharibika kwa mishipa kutokana na upasuaji.

Dk Sarra anasema ili mwanaume amudu kushiriki tendo la ndoa, anatakiwa mfumo wake wa damu uwe kwenye mzunguko unaotakiwa, pia ubongo, mishipa ya fahamu na homoni.

“Kutokana na kuugua maradhi niliyotaja, kuna dawa pia zinazochangia kupunguza nguvu za kiume. Zipo ambazo husababisha homoni kushindwa kuwa katika mfumo wake wa kawaida, hivyo kumletea athari mwanaume,” anasema na kuongeza:

“Kuna baadhi ya miili ya watu inatambua sukari kama adui, hivyo husababisha kuchomwa sindano ya DM I, kwa kawaida hupatwa na ganzi, wengine hupatwa matatizo ya kisaikolojia, hivyo hupoteza hisia za mapenzi,” anasema Dk Sarra.

Dk Sarra anasema mtindo wa maisha wa baadhi ya wanaume, ikiwamo unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara na dawa za kulevya za aina zote huchangia tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Anasema mtindo wa ulaji wa vyakula bila kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na tiba lishe, hasa ulaji wa nyama nyekundu ni miongoni mwa sababu zinazochangia upungufu wa nguvu za kiume

Pia, wanaume wenye umri kati ya miaka 40 na kuendelea ndiyo hukumbwa na tatizo hilo.

Hata hivyo, anasema wapo wengine ambao si wengi sana wenye umri chini ya miaka 40 nao hukumbwa na tatizo hilo.


Viagra zipo nchini na kwa kiasi gani?

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), inatambua uwapo wa dawa hizo za kuongeza nguvu za kiume na nyingine nyingi.

Msemaji wa Mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza anasema dawa hizo zipo nchini na zinauzwa katika maduka mbalimbali ya dawa za binadamu.

“Viagra ni jina tu dada yangu, zipo madukani za majina mbalimbali na huuzwa kwa watu kulingana na taarifa ya daktari kama inavyoshauriwa kitaalamu,” anasema Simwanza.

Akizungumzia kiasi cha dawa hizo kinachoingia kwa mwaka nchini, anasema hawezi kufahamu kwa kuwa wafanyabiashara tofauti huziingiza, na wao kama mamlaka inakuwa vigumu kutambua kwa haraka.

“Ninaweza kutazama katika orodha ya wafanyabiashara ambao tunawakagua kila mwaka, hata hivyo siwezi kufanya hivyo kwa sababu ni siri ya wateja,” alifafanua

Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) haiingizi dawa hizi kwa kuwa haijawahi kupata maombi kutoka kwa wateja wake ikiwamo Serikali.

Msemaji wa MSD, Eti Kusiluka anasema wao hawaingizi dawa hizo ila wanaweza kufanya hivyo iwapo Serikali au wauzaji wa dawa zikiwamo hospitali binafsi zitawaagiza.

“Sisi hatuleti dawa bila kuagizwa, sasa hatujawahi kuagizwa na wateja wetu lakini ikitokea wakatuagiza,tutazileta,” anasema Kusiluka.


Serikali yafafanua kutoagizwa kwa dawa hizo

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja amesema huwa hawaagizi dawa za aina fulani kama hazihitajiki.

Akifafanua sababu za kutoagiza dawa za kuongeza nguvu za kiume, Mwamaja anasema inatokana na ukosefu wa takwimu sahihi za uhitaji kwa kuwa huenda wengi hawaendi hospitali wanapokuwa na matatizo hayo.

“Sisi tunanunua dawa muhimu kwa kuangalia ambazo zitawasaidia wagonjwa wanaohitaji, hatujaona ukubwa wa tatizo hilo. Lakini wapo watu wanafika hospitali wakidai hawana nguvu za kiume, lakini daktari anapomchunguza anagundua ni matatizo mengine,” anasema.

Hata hivyo, aliwasihi wanaume wenye matatizo hayo kufika katika hospitali za Serikali ili kuisaidia kupata takwimu sahihi na wao wenyewe kujua matatizo yanayowasumbua.

“Waache kufanya uamuzi kwa utashi wao, wengine wanakimbilia madukani kununua dawa au kutumia za kienyeji, huenda hawana matatizo lakini wanayatengeneza kwa kutumia bila kupata ushauri wa daktari,” anashauri Mwamaja.


Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom