Mhasibu kizimbani kwa kughushi sahihi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MHASIBU wa Kampuni ya Tasu, Machafu Chokoma (59) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka mawili, likiwemo la kughushi sahihi na kujipatia Sh milioni 1.8 kwa njia ya udanganyifu.

Chokoma alifikishwa mahakamani hapo mwishoni mwa wiki iliyopita na kusomewa mashitaka na Hakimu Wilberforce Luhwago wa mahakama hiyo.

Wakili wa Serikali Sakina Sinda, alidai mshitakiwa alighushi saini ya Kaimu Mhasibu wa kampuni hiyo, George Kambute, kwenye hundi No.504642.

Kwa mujibu wa madai hayo, hundi hiyo iliyoghushiwa ilionesha kuwa Kimbute amesaini ili atoe fedha hizo kutoka akaunti yenye namba 015007803600 jambo si la kweli.

Sinda aliendelea kudai kuwa, Oktoba 22 mwaka jana katika Benki ya CRDB Tawi la Lumumba, Dar es Salaam, Chokoma alijipatia Sh milioni 1.8 kwa njia ya udanganyifu kutoka katika akaunti hiyo kwa kutumia hundi ya kughushi iliyoonesha imesainiwa siku hiyo hiyo.

Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Luhwago aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 23 mwaka huu itakapotajwa tena.

Mshitakiwa aliiachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Yahaya Hamis (22) anayedaiwa kuiba Sh 270,000 katika eneo la Mtaa wa Muheza, amewekwa rumande katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo baada ya kukosa wadhamini.

Hamis ambaye alipandishwa kizimbani jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Flora Mujaya, aliwekwa rumande baada ya wadhamini wake kushindwa kufika mahakamani.

Awali Karani wa Mahakama, Lucy Rutabanzigwa alidai kuwa, Juni 8 mwaka huu saa 9 mchana katika eneo hilo la Muheza Hamis alidaiwa kuiba fedha hizo mali ya Joshua Zarrow.

Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi Juni 27 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Hata hivyo Hakimu Mujaya alisema dhamana ya Hamisi ipo wazi endapo atapata wadhamini wawili watakaosaini hati ya Sh 130,000.

Katika Hatua nyingine, mkazi wa Kariakoo, Said Abeid (27) amefikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na mashitaka ya wizi wa simu yenye thamani ya Sh 25,000.

Mbele ya Hakimu Mujaya, Karani Rutabanzigwa alidai kuwa Mei 3 mwaka huu saa 12 jioni katika eneo la Mkunguni, Abeid aliiba simu aina ya Nokia yenye thamani hiyo mali ya Msafiri Mashamu.

Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi Juni 27 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
 
Back
Top Bottom