Mh.Rais Magufuli unaanza "kutuangusha" tuliokuunga mkono na kukutetea mitandaoni, zingatia haya machache ili ututie moyo

barafu

JF-Expert Member
Apr 28, 2013
6,726
32,819
Ni hakika kuwa,yale matumaini makubwa ambayo wengi wetu tulikuwa nayo juu ya serikali ya awamu ya tano,sasa yameanza kupungua.Siyo kwamba wengi tumekosa imani kabisa na serikali ya JPM,ila tumeanza kupunguza matumaini yaliyotokana na nguvu nyingi tulizowekeza katika kuwaaminisha watu kuwa uongozi wa awamu ya tano ni mwanzo wa suluhisho ya matatizo mengi yaliyokuwa yanalikumba Taifa.

Tulio wanachama wa JF,tunafahamiana kwa aina ya maandishi na misimamo,wengine katika harakati za kampeni na mwanzo wa utekelezaji wa sera za serikali ya awamu ya Tano,hatukuficha "hisia" zetu,tulipita humu kujibu hoja na wakati mwingine kuanzisha mijadala ya kuitia moyo serikali ya JPM na wasaidizi wake.Hii ni kwa sababu,tuliona mwanga mkubwa ktk kuelekea Tanzania mpya ya uwazi,uwajibikaji,utawala bora,ufanisi,uadilifu na umoja wa kitaifa.

Hatua za mwanzo za JPM kuelekea Tz mpya zilitupa moyo,hata tulio mbali na nyumbani,mara kadhaa tuliporudi nyumbani,tuliendelea kuwaaminisha wanaotuzunguka kuwa "huyu hasa ndio wakala wa Tanzania mpya".Mzalendo wa kweli asiyeona haya katika kupigania maendeleo ya Taifa lake.

Mimi kama mwana Jf na Mtanzania niliyekuwa nyuma ya JPM,nilianzisha mijadala mingi ya kumtia moyo wakati wa harakati zake za Makinikia na msimamo wake juu ya madini yetu,nilikuwa bega kwa bega na Rais wangu katika jitihada zake za kufufua shirika la ndege la Tanzania(ATCL).

Tulianzisha mijadala kama hii Tupunguze "kuisimanga" ATCL, haijengi zaidi ya kukatisha tamaa Katikati ya sauti nyingi zenye upinzani wa hoja nzito ndani ya Jf kama hizi Zitto: Tumepigwa cha juu katika ununuzi wa ndege mpya wengi tulipambana kuutetea uamuzi huo wa JPM na kumtia moyo.

Kwenye "vita" vyake dhidi ya madini na vito vya thamani,wengine tulimtia moyo Rais wetu kwa kubadilishana maarifa na watu kuwa mambo haya lazima tuwe nyuma ya Rais wetu bila kumuacha peke yake,tulianzisha mijadala hii Tujipange: Kutaifishwa mzigo wa almasi Airport ni mwanzo wa vita ya kibiashara kati ya Tz na De-Beers ili kumtia moyo.Alipogusa kule kwa watu wa Barrick,tuliwatia watu moyo kwa mijadala kama hii Vita dhidi ya mabepari wa madini inahitaji umoja, ilimshinda Dr Williamson wa Mwadui na Mwl Nyerere

Lakini kwa sasa,kuna mambo "anatuangusha",sisi watetezi wake ndani ya mitandao na nje ya mitandao tunaanza kupata wakati mgumu,maana uhalisia wa kauli zake ktk majukwaa,hauakisi hali halisi ya maisha ya kila siku na matendo ya serikali yake.Kama wakati alithamini mchango wetu bila hata kutufahamu kwa sura,anapaswa pia kuona na kusikia malalamiko yetu bila kujua sura zetu wala bila kuwa na wazo kuwa "Tunatumika".

Tunakutana na raia na tunaona malalamiko yao,iwe wale walio ndani ya nchi au wale walio ugenini wakitafuta maisha.Malalamiko haya asiyapuuze,na kupitia jukwaa hili,nami kama raia niliye nyuma ya Rais wangu,ambaye najitahidi kuwa katikati ya hisia za siasa za kivyama,ninamuandikia Rais wangu kile ambacho hakina unafiki sababu hakuna nalotegemea kupata kwake la "hisani" kama nitakuwa "nampamba" tofauti na hali halisi ya walio wengi.

Utawala Bora.Malalamiko yamekuwa mengi sana katika eneo la utawala bora,toka kuzimwa kwa bunge mubashara na kuzuiwa kwa mikutano ya siasa,kumezua maswali mengi sana kwa wadau na hata raia wa kawaida.Jambo hili Rais asilichukulia kama ni dogo,lina athari zake kubwa sana ambazo zinaweza kuwa ni hasi kwa uongozi wake.Kuzuia bunge kuonekana moja kwa moja na wananchi,kumepunguza kiasi cha watu waliokuwa na imani nae kati ya mwaka 2015 wakati wa uchaguzi hadi kipindi cha July 2016 serikali ilipoamua "kubana matumizi" kwa kuzima bunge.Swali kwa wengi ni kuwa,kama "Mubashara" ni gharama na kupoteza muda wa wananchi kufanya kazi,mbona matukio ya muhimili mmoja wa dola ambao ni serikali, yanayohusu Rais yanaonekana mubashara?Lifanyie kazi hili Rais wangu.

Uwazi katika Utekelezaj wa majukumu ya serikali.Serikali imejinasibu kupambana na ufisadi na mafisadi,imejinasibu kupambana na rushwa na wala rushwa,lakini ajabu ile misingi yote ya uwazi katika kukabiliana na ufisadi na rushwa imefifishwa.Sasa hapa kweli kuna dhamira ya kweli ya kupambana na haya mambo?Serikali imeamua kujiondoa katika mpango wa OGP (Open Gvt Parternership).

Mpango wa OGP ulitoa uwezo kwa wananchi kuwa na haki ya kupata nyaraka na taarifa za utendaji wa serikali.Nguzo za OGP ni uwazi wa viongozi serikalini,ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji.

Uratibu wa OGP ngazi ya Taifa ulihusisha AZAKI kama Tanganyika Law Society,Foundation of Civil Societies na kwa upande wa serikali,Wizara mbili zenye unyeti mkubwa kama Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi zilihusishwa.Hii ni kwa sbabu,historia ilionyesha hizi ndizo wizara zinazoongoza kwa ufisadi na rushwa.

Lakini sasa serikali imejitoa kwenye OGP,serikali imeonekana kuwa na mahusiano mabaya na Asasi za Kiraia kama TLS mpaka "kuingilia" chaguzi zake.Jambo hili linakatisha tamaa na kuleta manung'uniko katikati ya jamii.

Kupitia Bunge,serikali ilimtuma Waziri wa Utawala bora kutishia kuivunja halmashauri ya Ujiji kwa sababu tu,madiwani wake na mbunge wake wamejiunga katika mpango wa OGP.Sasa serikali inayopinga ufisadi,inakuwaje kinyume na halmashauri inayoingia ktk mpango wa OGP ambao ni msingi wa kupinga rushwa na ufisadi?Hii inakatisha sana tamaa.

Kupitia bunge,serikali imeamua kupeleka mswaada ambao umekuwa sheria,ili kuzuia mambo ya madini na mikataba yake kujadiliwa bungeni,na hivyo kuipa nafasi serikali kufanya mikataba na kanuni za sheria za madini bila kujadiliwa kwa kina bungeni.Sasa sheria hizi za nini kama tulilalamika wazungu wa makinikia wanatuibia?Serikali hiyohiyo imetunga sheria inayomzuia hata Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu Serikalini (CAG) kukagua mahesabu ya Migodi.Hali hii imefanya hata CAG mwenyewe kulalamika.Sasa vita hivi vya kuyarudisha madini kwa wazawa,vitafanikiwa vipi bila kuwa na CAG mwenye kuijulisha serikali wapi inapoibiwa?

Mambo haya yote yanakuvurugia Mh.Rais na sie watetezi wako tunaanza kupata wakati mgumu,maana maneno yako,nia unayotusadikisha haiendani na matendo yako.Na sisi wengine tulifundishwa kuamini zaidi matendo kuliko maneno.Sasa matendo hayatushawishi kuwa nia ya maneno yako ipo sambamba na matendo yako.

Wale waliofukuzwa kazini wakiwa wamebakiza miezi,mwaka au miaka miwili sababu ya vyeti feki nao wanalia ktk vifua vyao,hao wanalia sababu kuna mmoja kama wao wanasikia amesamehewa kisa ni "mchapaka kazi".Sasa wale walimu waliofundisha miaka zaidi ya 30,wakiwajuza watoto silabu na hesabu kwa miaka yote,tena katika mazingira magumu huko vijijini huku wakiwa na mishahara duni,nani aliwaona na wao uchapakazi wao ili awaache na vyeti vyao "feki" wamalizie miaka yao na mafao yao?Hawa nao wanahuzunika,tunapokutana nao,tukiwaambia wewe ni Rais wa wanyonge wanakataa

Jambo linalotupa shida tunapojadiliana na wenye "akili zao"(sio wale fuata upepo),ni kuhusu uwazi katika ununuzi wa ndege na pia katika ulipaji wa deni la ndege iliyokuwa imekamatwa Canada.

Mpaka sasa tumepata ndege tatu aina ya Dash8-Q400,tuna matarajio ya kupata CS300(Jet engine) na Boeing 787-800(Dreamliner).Hizi tumeambiwa ni "Cash" bila mkopo,lakini wakati tunazinunua kwa ajili ya shirika letu la ATCL,tunajua kuwa tunadaiwa na tuna madeni ambayo hayaelezeki.Na ndio maana kwa kujua hilo,serikali imeamua "kuzimilikisha" ndege hizo kwenye "agency" nyingine ya serikali ya Tanzania Gvt Flight Agency(TGFA) ili zinaporuka hata nje ya nchi zisizuiliwe kama ile ya Canada,sababu ATCL inanuka madeni.

Mpaka sasa harufu ya madeni ya ATCL imesababisha umoja wa mashirika ya usafiri wa anga duniani (IATA) kuindoa ATCL katika wanachama wake sababu hailipi madeni na hainekani kuwa na uwezao wa karibu wa kulipa madeni hayo.Sababu hizi zilipaswa kuifanya serikali kumuagiza CAG kuikagua ATCL,ili hizo pesa za "cash" tunazowekeza kwenye ndege za ATCL tujue zitatuletea faida gani.Ukimya wa kulikwepesha shirika ambalo ndio linashika "kiki" kwa sasa kwa kuwekewa pesa nyingi za mabilioni ya ndege mpya,inaleta picha hasi kuwa nia yetu ya kupambana na ufisadi na rushwa,inaweza kuwa ni maneno tu bila vitendo.Haya yote,Mh.Rais wangu mpendwa yanatupa kazi ya kukutetea huku mitaani.

Usalama kwa raia umepungua sana Mh.Rais,wanaoonekana kukuosoa ni ama wanakufa,wanakamatwa au wanapotea bila maelezo.Hii inatisha sana raia na kujenga picha hasi juu ya utawala wako.

Hili la Tundu Lissu siwezi kulijadili,maana kila anayelisema anaonekana yupo chama cha upinzani.Hili la kijana Ben Saanane siwezi kulisema sana,ila watu wanalisema sana sana.Hili la Abdul Nondo na Kakobe halijaachwa tu,lipo katika vifua vya watu na hasa watu wa Ujiji na Kigoma kwa ujumla.Kuna zile maiti za Koko Beach,wengine tunakubali inaweza kuwa ni za wakimbizi kweli.Ila sasa na hilo alilosema Zitto kuhusu diwani wa Kibondo aliyechukuliwa na Afisa Usalama wa Wilaya na mpaka leo inakaribia mwaka hajaoenekana,unafikiri linajenga picha gani?

Haya yote,na mengine mengi kama watu kulalamika ugumu wa maisha,kupanda kwa nishati ya umeme na kupaa kwa bei ya sukari,ni malalamiko yanayowagusa hata masikini walio chini kabisa.Hawa huwezi kusema wanaongea eti sababu ya siasa,hawa wansema ule uhalisia wa maisha wanayoyaishi.Kule Lindi zao la mbaazi lilikuwa kilo kwa shilingi 2000,sasa wanauza shilingi 100 hadi 150.Mfuko wa cement ulikuwa shilingi 7000 hadi 10000,sasa unauzwa 22000.Hawa ukipanda jukwaani ukasema yanayolalamika kwa sasa kuwa vyuma vimekaza yalikuwa mafisadi,huyu mwananchi wa Mahuta Newala,atajiuliza na yeye kuuza mbaazi toka shilingi 2000 hadi 150,yeye alikuwa anafisidi nini?

Hili la trilion 1.5 mimi sitaliongelea,maana nasubiri maafisa masuhuli watolee ufafanuzi.Lakini mzee Rais,unapokuwa unasema watu walizoea kuwa mafisadi,majizi na makwapuaji enzi za JK,sio kwamba walikuwa wanaenda hazina na mifuko ya sandarusi na magunia kubeba hela,hata kutumia pesa za hazina bila kufuata utaratibu sahihi wa kisheria na kuidhinishwa na bunge nao ni ufisadi,hata kama aliyechukua pesa hizo alikuwa na nia njema ya kujenga nyumba za polisi na kuwapa askari magereza ghorofa za makazi au kujenga ukuta wa kulinda Tanzanite.Kama alichukua bila utaratibu wenye baraka za bunge,huyu naye ni fisadi tu kama mafisadi wengine.

Mwisho nikuombe radhi kama kuna mahali nimetumia lugha usiyoipenda,hata kama huwezi kuturidhisha wote,lakini kupunguza malalamiko na manung'uniko ya wengi na kuzizingatia kelele za wachache,ndio alama ya hicho wanachosema "Uongozi unaoacha alama".Jitahidi katika haya,ili utipunguzie mzigo wa kukuelezea mtaani.

Wako barafu wa Jf
 
MNIOMBEE
tapatalk_1523945759282.jpeg
 
Ni janga kubwa la Taifa huyo. Hilo wengi tulilijua siku nyingi sana. Ni mwizi, muongo, mbaguzi na fisadi mkubwa sana pia anayependa kukurupuka na kupindisha sheria. Sasa yametimia kile ambacho tulisema kabla na baada ya hili jiwe kuingia Magogoni kimetimia.

Naunga mkono hoja. Kuna vitu JPM anajiangusha mwenyewe! Angeweza kuwa Rais bora kabisa kihistoria Africa! Nafikiri kuna wapambe wanamuingiza chaka mno! Bado naamini ni mtu sahihi na atajifunza kutokana na wakati.
 
Alianzisha vita ya kulinda rasilimali, Hasa madini huyo huyo ametunga sheria ambayo inamzuia mkaguzi mkuu kukagua shughuli za madini, Maana yake afanye bila kukaguliwa. Bado mnasema ni mzalendo???

TRA wameongeza 2.2T ambazo hawakukusanya kwenye Kodi.
 
Barafu,
Msema kweli mpenzi wa Mungu, umefunguka vizuri. Na ni kweli hoja nyingi humu Jamiiforums hujibiwa kwa hoja nzito zenye mashiko.

Hivyo wahusika wanasiasa, viongozi na wapenzi wa vyama vya siasa mnakaribishwa kufanyia kazi hoja za wananchi zinazotolewa hapa JF kwa manufaa ya ustawi wa nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.
 
Kuna hoja ninakubaliana nazo lakini kuna hoja zingine umeweka kisiasa zaidi badala ya uhalisia.

Naomba unioneshe ni kifungu gani cha sheria ambacho kilikuwa kinamruhusu CAG kukagua migodi ya watu/makampuni binafsi.

Naomba pia unionyeshe ni kifungu gani cha sheria mpya ambacho kinamkataza CAG kukagua kampuni binafsi?

Nini nafasi ya TRA katika migodi yenyewawekezaji binafsi?

Tatizo ninaloliona ni baadhi ya watu kuchukua maneno ya wanasiasa bila hata ya vielelezo halisi
 
Back
Top Bottom