SoC03 Mgongano wa Kimaslahi, Sintofahamu kwa Watoa Huduma Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Mamshungulii

Senior Member
May 3, 2023
124
66
MGONGANO WA KIMASLAHI, SINTOFAHAMU KWA WATOA HUDUMA TANZANIA

Mgongano wa maslahi ni dhana pana na haina tafsiri moja. Kwa maana rahisi ni: Hali ya kukinzana kati ya maslahi binafsi ya kiongozi au mtumishi wa umma na kazi au majukumu yake kwa umma. Maslahi binafsi yanatoa ushawishi kwa kiongozi wa umma kufanya maamuzi au kutekeleza majukumu kwa upendeleo na kuathiri upatikanaji wa haki na fursa sawa.

Maslahi binafsi maana yake ni njia binafsi za kiuchumi au zisizo za kiuchumi za kiongozi,mtoa huduma au mtumishi wa umma ambazo zinaweza kumshawishi kufanya uamuzi wa upendeleo katika utekelezaji wa majukumu aliyopewa kusimamia.

Maslahi binafsi ya kiongozi au mtumishi wa umma ni pamoja na manufaa kwake binafsi, kwa familia yake,rafiki zake na washirika wake wa kibiashara.

CHANZO CHA MGONGANO WA KIMASLAHI NI: -
1. Asili ya mwanadamu ya ubinafsi inayosababisha kujipendelea au kupendelea wale walio karibu yake
2. Mtazamo kuwa Serikali ni chombo cha umma amba- cho kimepewa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba na kwa manufaa ya wananchi.
3. Msingi wa imani ya wananchi kwa watumishi wa umma kuwa watafanya kazi kwa manufaa ya umma.Ukasumba ya kwamba mtu hawezi kuwa Jaji kwenye kesi yake mwenyewe.
4. Kukua kwa dhana ya manufaa makubwa kwa watu wengi
5. Kukua kwa Sekta Binafsi na muingiliano kati ya Sekta
6. Binafsi na Sekta ya Umma.

MGONGANO WA MASLAHI UMEGAWANYIKA KATIKA MAKUNDI MAKUU MAWILI:
Mgongano wenye Maslahi ya kifedha na Mgongano usio na Maslahi ya kifedha. Maslahi ya kifedha yanahusisha manufaa halisi au uwezekano wa kupata manufaa ya kifedha kutoka kwa watu wengine, kumiliki mali, kuwa na hisa au kuwa na nafasi ya uongozi katika kampuni inayowania zabuni ya serikali, kupokea zawadi au ukarimu wa kawaida au mapato kutoka katika kazi nyingine. Si lazima kuwe na kupeana fedha. Hata ongezeko la thamani ya mali kwa sababu ya kufanya uamuzi wa makusudi wa kuboresha mazingira ya mahali mali ilipo.

Mfano: kujenga barabara ya lami kuelekea mahali ambapo biashara ya kiongozi ipo, wakati ujenzi huo si kipaumbele cha maendeleo kwa eneo hilo. Maslahi yasiyo ya kifedha hayana manufaa ya kifedha ndani yake. Yanatokana na uhusiano binafsi au wa kifamilia au kushiriki katika michezo au shughuli za kijamii. Mfano: Kiongozi wa Umma anaweka shini - kizo la kubadilisha utaratibu ili ndugu yake apate ajira, hatarajii kupata manufaa yoyote ya kifedha kwa ajili hiyo.

MIENENDO NA MAMBO YANAYOSABABISHA
MGONGANO WA KIMASLAHI:
a. Kushiriki kufanya maamuzi katika suala ambalo kiongozi, familia au jamaa zake wana maslahi binafsi bila kutoa taarifa ya maslahi hayo katika kikao cha maamuzi.
b. Upendeleo kwa watu binafsi, makampuni au mashirika ambayo kiongozi ana hisa.
c. Kutoa au kunufaika na taarifa rasmi za kikazi ambazo hazijatolewa rasmi kwa umma. (Mfano: Taarifa za siri za vikao vya Bodi ya Zabuni).
d. Kudai, Kuomba au kupokea maslahi makubwa ya kiuchumi. (Mfano: kutoka kwa Makampuni yenye mikataba na Serikali).
e. Mwenendo wa kiongozi wa umma ambao unamuweka kiongozi kutumia ofisi kwenye manufaa yake binafsi au unadhalilisha uongozi wa umma kiasi cha kushusha imani ya wananchi kwake.
f. Kuingia mikataba ya kibiashara na Taasisi anayoisimamia.
g. Kujilimbikizia mali isivyohalali.
h. Kujihusisha na shughuli ya kibiashara inayoshabihiana na kazi au majukumu ya kiongozi husika

MADHARA YA MGONGANO WA KIMASLAHI: -
Mgongano wa Maslahi ni miongoni mwa matatizo ya kimaadili yenye matokeo hasi kwa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Tatizo hili linaripotiwa katika nchi nyingi duniani na madhara yake yanatofautiana kati ya nchi moja na nyingine kutegemea na kiwango na ukubwa wa tatizo. Athari za tatizo hili ni pamoja na;
1. Rasilimali za nchi kunufaisha watu wachache.
2. Wananchi kukosa haki zao za msingi kutokana na Taasisi za Umma kuendeshwa kwa misingi ya upendeleo; Kuathiri utendaji kazi na maamuzi yenye maslahi mapana kwa Taifa.
3. Kupungua kwa uzalendo miongoni mwa wananchi; Kuongezeka kwa tofauti ya kipato kati ya masikini na matajiri.
4. Kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
5. Wananchi kupoteza imani kwa Viongozi na mihimili ya dola; na
6. Kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

VIASHIRIA VYA MGONGANO WA KIMASLAHI NI:
A. Mgongano halisi wa maslahi unatokea pale kiongozi au mtumishi wa umma anapotumia madaraka yake kujinufaisha binafsi au kumsaidia mtu mwingine kupata manufaa. Mfano: kupokea fedha ili atekeleze jambo au kutoa huduma.
B. Kuonekana kuwepo kwa mgongano wa maslahi ni hali ya kuwepo viashiria kwamba kiongozi au mtumishi wa umma ametumia madaraka yake kwa maslahi binafsi au amemsaidia mtu mwingine kupata manufaa. Mfano: Kiongozi wa umma kushiriki kufanya uamuzi kwenye jambo ambalo linahusu kampuni ya mke/mume wake.
C. Uwezekano wa kuwepo mgongano wa maslahi ni hali ya kuwepo kwa mazingira yanayoweza kumshawishi kiongozi au mtumishi wa umma kutumia madaraka yake kujinufaisha binafsi au kumsaidia mtu mwingine kupata manufaa siku za usoni. Mfano: Kiongozi wa umma kupokea zawadi yenye thamani kubwa kutoka kwa kampuni ambayo ina suala ambalo analishughulikia.

NJIA ZA KUDHIBITI MGONGANO WA MASLAHI:
Mgongano wa Maslahi unaweza kudhibitiwa kwa njia zifuatazo: -
a) Utoaji Wa Elimu kuhusu Mgongano wa Maslahi kuanzia ngazi ya familia,rika zote , viongozi wa Umma, Makampuni, Watumishi wao, Watumishi wa Umma, Asasi za Kiraia, Vyombo vya Habari na Wadau wengine wa Sekta Binafsi, Makundi mbalim- bali ya Kijamii na Wananchi.
b) Kuimarisha mifumo na miundombinu ya upatikanaji wa huduma mbalimbali ili kudhibiti mgongano wa Maslahi.
c) Kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya umma.
d) Kutoa Tamko kuhusu Maslahi binafsi aliyonayo juu ya suala linalojadiliwa katika kikao cha maamuzi. Kufanya maamuzi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo kwa Masilahi ya Umma.
e) Kuzuia kutokea kwa Mgongano halisi wa Maslahi; uwezekano wa kuwepo na kuonekana kuwepo kwa Mgongano wa Maslahi.

KWAKUMALIZIA, Mgongano wa maslahi ndiyo chanzo kikubwa cha ukiukwaji wa maadili. Usipodhibitiwa una athari kwa ustawi wa jamii. Ni jukumu la kila kiongozi na mtumishi wa umma kupanga mambo yake katika namna ambayo itazuia kutokea kwa mgongano wa maslahi. Kujali maslahi ya umma ndiyo msingi mkuu wa Taasisi yoyote ile ya umma duniani.
 
Back
Top Bottom