Haya wadau tuisikilize serikali yetu, mwenye ushahidi wa vifo vilivyosababishwa na mgomo alete kwa sasa hii ndio kauli ya serikali yetu sikivu;
SERIKALI imesema hakukuwa na ongezeko la vifo ambavyo vinahusishwa moja kwa moja na mgomo wa madaktari uliotokea hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya aliliambia Bunge jana mjini hapa wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), ambaye katika swali la nyongeza, alisema yupo kijana wake alifariki katika mgomo huo huku akihoji ni namna gani Serikali itawapoza walioathirika.
Aidha, katika swali la msingi, Khalifa alitaka kufahamu ni namna gani mgomo uliathiri jamii ya Watanzania, watu wangapi walikufa kwa kukosa huduma na ni maeneo gani ya nchi yaliathirika zaidi.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri alisema hospitali nyingi zilizokumbwa na mgomo huo zimetoa taarifa kuwa hakukuwa na ongezeko la vifo ambavyo vinahusishwa moja kwa moja na mgomo.
Alitoa mfano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwamba kabla ya mgomo, Novemba mwaka huu, kulikuwa na vifo 457, Desemba vifo vilikuwa 537 wakati wa mgomo, Januari vifo vilikuwa 475 na wiki ya kwanza ya Februari vilikuwa 95.
Alisema mgomo wa madaktari ulitokea katika hospitali 13 na maeneo yaliyoathirika zaidi ni Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi yake ya Mifupa (MOI) pamoja na hospitali za Manispaa za Dar es Salaam ambazo ni Amana, Temeke na Mwananyamala.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, hospitali nyingine zilizokumbwa na mgomo ni Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali za Rufaa-Bugando, Mbeya na KCMC. Pia Hospitali za mikoa ya Tanga, Morogoro, Dodoma na Arusha.
Akieleza ni namna gani mgomo uliathiri jamii, Naibu Waziri alisema uliwaathiri wananchi kisaikolojia kutokana na wagonjwa kukosa huduma kwenye maeneo ya hospitali walizotarajia.
Athari nyingine ni ya kiuchumi ambapo baadhi ya wagonjwa ilibidi wapate huduma za malipo kupitia hospitali za watu binafsi. Aidha, alisema wapo watumishi wa afya waliokuwa wakiendelea na kazi wakati wa mgomo ambao walipata usumbufu mkubwa kutoka kwa waendesha mgomo.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (Chadema) aliyetaka kufahamu ni namna gani Serikali imeshughulikia uhaba wa vifaa uliochangia mgomo huo, Dk. Nkya alisema chanzo kikubwa kilikuwa ni maslahi binafsi ya madaktari. Hata hivyo, alisema Serikali imejitahidi kupeleka vitendea kazi
Source:
HabariLeo | Mgomo wa madaktari haukuongeza vifo