Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,353
- 33,190
Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad
Mgogoro unaofukuta ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), umeingia sura mpya baada ya baadhi ya wanachama na waasisi wa chama hicho Wilaya ya Tanga, kutoa tamko la kuunga mkono kauli ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid na kuutaka uongozi wao wa Taifa kutoa maelezo na kuzifanyia kazi dosari zote zilizojitokeza.
Hayo yalielezwa na waasisi hao katika kikao chao na waandishi wa habari jana wakidai kukerwa na malumbano yanayotengenezwa na viongozi waandamizi kupitia vyombo vya habari na hivyo kulazimika kutoa tamko kwa niaba ya baadhi ya wanachama wa Wilaya ya Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama na waasisi wenzake, Salim Daiyah Daiyah, alisema kwanza wanampongeza Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwataka viongozi kuacha kulumbana katika vyombo vya habari.
Hata hivyo, walisema wanasikitika pia kuona wahusika hao bado wanaendeleza malumbano hayo, jambo walilolieleza kuwa ni hatari kwa mustakabali wa Chama hicho.
Muasisi huyo na ambaye alishawahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya Wilaya ya Tanga, alisema kimsingi hawaridhishwi na malumbano hayo kwa kuwa hayana tija kwa Chama hicho na wanachama kwa ujumla na badala yake wanautaka uongozi huo kujibu madai ya
Mbunge Hamad Rashid Mohamed waliyoyaeleza kuwa ni ya msingi.
Tunasikitika kuendelea kuwasikia viongozi hao wakiendelea kutoa tambo mbalimbali mfano kipindi cha baragumu kilichorushwa na televisheni ya Chanel Ten Desemba 19, mwaka huu masjira ya asubuhi. Sasa haya hatukutarajia yatokee tena baada ya kauli ile ya Katibu Mkuu, alieleza Daiyah Daiyah
Kwa upande wake, yeye alishauri viongozi hao kuyafanyia kazi aliyoyasema Mbunge wa Wawi Hamad Rashid kwani ni mambo ya msingi ambayo yanalenga kujenga chama ambacho alidai kuwa suala la kuzorota kwa chama hicho ni la wazi na halina ubishi.
Naye Abdul Alqarney, ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa Wilaya na Juma Mafita, Mwenyekiti wa Vijana Kata ya Makorola, walieleza kushangazwa kwao na viongozi hao waandamizi kwa kile walichodai kupanga mikakati ya kumhukumu Mbunge Hamad Rashid badala ya kujadili jinsi ya kurekebisha dosari alizozieleza.
Sisi tunaona kuwa mambo aliyoyaeleza Mbunge wa Wawi, Mheshimiwa Hamad Rashd, ni ya msingi na tunaona si haki na vyema kujadili jinsi ya kumhukumu, badala yake wajibu na watekeleze yale aliyoyaeleza ambayo ni kuitisha vikao vya chama, kusimamia vizuri fedha na mali za
chama hicho ..huu ndiyo msingi tunaoutaka ufuatwe kwa mujibu wa katiba yetu ya chama, alisema Abdul.
Naye Mafita alisema ufike wakati viongozi kukubali kukosolewa na kukumbuka lengo la chama hicho la kutaka kukiimarisha kuanzia bara na
visiwani na hatimaye kushika dola pande zote mbili za Muungano.
Hata hivyo, katika tamko la wanachama hao walisisitiza umuhimu wa viongozi kutumia vikao halali vya kikatiba vya Chama kutatua matatizo na kujibu madai yaliyotolewa na wa Wawi na kwamba vikao visivyo rasmi vinaweza kuchochea zaidi vurugu ndani ya chama hicho.
CHANZO: NIPASHE