Meneja wa hoteli akana Bobi Wine kuwa na silaha

Return Of Undertaker

JF-Expert Member
Jun 12, 2012
4,572
26,868
Meneja wa hoteli akana Bobi Wine kuwa na silaha


BOBI+PIC.jpg

Mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Kwa ufupi
Meneja huyo ambaye pia ndiye mmiliki wa hoteli hiyo alisema wageni wanaoingia katika hoteli hiyo hukaguliwa

Uganda. Uongozi wa Hoteli ya Pacific umekanusha maelezo ya polisi nchini hapa kuwa walikuta bunduki ndani ya chumba cha hoteli hiyo alichokuwa amepanga mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Agosti 13, 2018 polisi walivamia hoteli hiyo wakimsaka Bobi Wine ambaye ni Mbunge wa Kyadondo na wapambe wake baada ya vurugu zilizotokea katika kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Arua.

Katika vurugu hizo dereva wa mwanamuziki huyo, Yasiin Kawuma aliuawa.

Meneja na mmiliki wa hoteli hiyo, Luiji Candia amelieleza gazeti la Daily Monitor kuwa bunduki zilizotajwa hazikuwa ndani ya hoteli hiyo.

Amebainisha kuwa katika hoteli hiyo kuna utaratibu wa kuwakagua wageni wao wanaofika kupata huduma na kwa wale wanaokuwa na silaha huzihifadhi katika sehemu salama.

“Polisi hawakukuta bunduki yoyote hapa hotelini kwetu, wanatakiwa waone aibu kwa walichosema kwa umma,” amesema.

“Kama kuna mahali wameipata hiyo bunduki wanapaswa kusema ukweli badala ya kuisingizia hoteli yetu kwani wanafanya hivyo kwa maslahi binafsi ya kisiasa.”

Usiku wa Agosti 20, 2018, hoteli hiyo ilivamiwa na wanajeshi na kufanya ukaguzi.

Katika ukaguzi huo, Candia amesema wanajeshi hao waliingia katika vyumba vyote na kuchukua simu, kompyuta mpakato za wateja wao pamoja na fedha na kuvunja milango.

Amebainisha kuwa pia waliwakamata wafanyakazi wao wawili na kuwapiga, mmoja aliachiwa jana Agosti 21, 2018 huku mwingine akiendelea kushikiliwa katika kituo cha polisi Arua.

Kufuatia uharibifu huo, meneja huyo amesema watafungua kesi kudai vitu vilivyopotea na kuharibika katika tukio hilo, akieleza kuwa hoteli hiyo ndio biashara pekee inayomuingizia kipato cha kuendesha maisha yake.

“Nitafungua kesi ya madai kwa uharibifu uliofanyika ikiwemo kupotea kwa mali za wateja wangu. Kama watakuwa tayari tuelewane nje ya mahakama sawa na kama hawatakuwa tayari tutakutana mahakamani na timu yangu ipo tayari kwa hilo,” amesema.

Msemaji wa Jeshi la Uganda (UPDF), Brigedia Richard Karemire amesema jeshi hilo halitalipa chochote kwa uharibifu huo kwa maelezo kuwa hakuna walichoharibu.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom