Mema ya serikali yasiyostahili asante | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mema ya serikali yasiyostahili asante

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Nsololi, Apr 19, 2010.

 1. N

  Nsololi JF-Expert Member

  #1
  Apr 19, 2010
  Joined: Mar 8, 2007
  Messages: 290
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  Kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kusoma makala hii.


  Mema ya serikali yasiyostahili asante

  Ansbert Ngurumo


  KATIKA kufuatilia mnyukano wa nguvu ya hoja na mabavu kati ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Serikali kwa muda sasa, rafiki yangu mmoja alinikumbusha swali moja la msingi ambalo bado limepuuzwa.
  Na kilichoibua swali hilo ni kauli ya Serikali kupitia kinywa cha Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa taifa mwishoni mwa mwezi Machi.
  Katika kuthubutu kuwashawishi (kabla ya kuwatisha) TUCTA wasitishe mgomo wa wafanyakazi kitaifa kuanzia Mei 5, 2010, na katika kusisitiza jinsi serikali ilivyotekeleza wajibu wake, rais alisema:
  “Napenda kuwahakikishia wafanyakazi wote nchini na wananchi wenzangu wote kuwa tunawajali na kuwathamini sana wafanyakazi: wawe wa Serikali au wawe wa sekta binafsi. Kamwe hatujawapuuza na mimi binafsi nitakuwa mtu wa mwisho kufanya hivyo. Tangu tuingie madarakani tumechukua hatua thabiti za kuendeleza haki na maslahi ya wafanyakazi mambo yanayothibitisha ukweli huu kwamba tunawapenda, tunawathamini na kuwajali wafanyakazi nchini. Tumeongeza mshahara wa kima cha chini mara tatu kuanzia mwaka 2006 kutoka shilingi 65,000 hadi 104,000 sasa, na hivi sasa tunajiandaa kuongeza tena katika bajeti ijayo.
  “Kwa upande wa mafao ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa, Serikali imesikiliza kilio chao na kukubali kuubadili mfumo wa malipo baada ya kustaafu kutoka ule wa akiba ya uzeeni na kuwa ule wa pensheni. Mabadiliko hayo yanahitaji shilingi 103 bilioni na Serikali imeamua kuubeba mzigo huo badala ya kuacha wafanyakazi waubebe wenyewe. Kwa ajili hiyo kila mwaka Serikali italipa zaidi ya shilingi 10 bilioni. Hivi asiyekujali anakufanyia mema haya?”
  Katika kujitapa, serikali ilitonesha kidonda cha wafanyakazi. Na kwa sababu hiyo, bila kujua, iliwahamasisha na kuwapa sababu zaidi za kuandaa mgomo.
  Tangu miaka mitatu iliyopita, wafanyakazi wamekuwa wakiishauri serikali ilipe kima cha chini cha walau shilingi 315,000 kwa mwezi. Hakitoshi, lakini kingeweza kusaidia kuboresha maisha yao.
  Bahati mbaya, rais na serikali yake bado wanafikiri kwamba thamani ya shilingi ya leo ni sawa na ya mwaka 2006. Na kama vile haitoshi, wanadhani wamewatendea wafanyakazi mema ya kutosha kwa kupandisha kiwango cha mshahara kutoka Shilingi 65,000 hadi 104, 000; ambayo haifiki hata nusu ya kiwango walichoomba miaka mitatu iliyopita.
  Maana yake ni kwamba kama wafanyakazi wataamua kupitia upya madai yao, watadai kima cha chini kilicho zaidi ya 315,000 kwa sababu thamani ya shilingi imeshuka mno.
  Serikali inajaribu kuwahadaa wafanyakazi kwa kuwachomekea hesabu ya kujumlisha – kutoka 65,000 hadi 104,000; huku ikijua kuwa huko ni kucheza na uhai wa wananchi kwa kuwapa mshahara ambao haulingani na posho wanazopeana wakubwa kwa kazi au safari ya siku moja ndani au nje ya nchi.
  Kama serikali ingekuwa inawajali wafanyakazi, ingepunguza mafungu inayopeleka kwenye posho nono za vigogo; au ingedhibiti ongezeko la posho za vigogo katika bajeti zake.
  Kwa mfano, kati ya mwaka 2007 na mwaka huu, posho za vigogo katika ofisi ya rais na (sekretarieti ya) baraza la mawaziri, imepanda kutoka bilioni 114.1 hadi bilioni 148. Katika kipindi hicho hicho, posho za Bunge zimeongezeka kutoka bilioni 20.8 hadi bilioni 36.8.
  Bado zipo za polisi, magereza, elimu na ufundi, na idara nyingine za serikali zisizosemeka.
  Posho za vikao vya maofisa wa serikali tangu Julai mwaka jana ni Sh 407 bilioni. Mwaka 2008/09 Serikali ilitenga Sh 506 bilioni kwa ajili ya posho; ikiwa imepanda kutoka Sh 423.2 bilioni za mwaka 2007/08. Mwaka huu pekee, imetenga Sh 571 kwa ajili ya posho.
  Safari moja ya ndani ya nchi kwa kigogo inampatia zaidi ya shilingi 80,000 kwa siku. Akikaa mkoani kwa siku mbili anakuwa amevuna zaidi ya mshahara wa mfanyakazi mmoja kwa mwezi.
  Mkurugenzi au katibu mkuu anaposafiri nje ya nchi, anapata posho isiyopungua laki tano na nusu (550,000) kwa siku moja; huku ofisa mwandamizi na ofisa wa kati anapata lakini nne na nusu (450,000) kwa siku moja.
  Kama mabilioni haya yangeingizwa kwenye mishahara, wafanyakazi wangepata ongezeko nono ambalo lingewapunguzia makali ya maisha.
  Na ikumbukwe kuwa wanaopata posho hizi ni vigogo ambao tayari wana mishahara minono. Watumishi wadogo, ambao ndio wangepewa fursa ya kutunisha mishahara yao, wananyimwa stahili hiyo.
  Na kwa unono wa posho hizi, hatushangai wakubwa hawatulii nchini. Ndicho kisa cha safari zao zisizoisha na zisizo za lazima nje ya vituo vya kazi. Na ndicho kisa cha Tanzania kupeleka wajumbe wengi katika mikutano ya kimataifa, ambao wakati mwingine hawahudhurii hata mikutano yenyewe. Wanatafuta fursa ya kutunisha mifuko, si kufufua uchumi wa nchi.
  Na bado zimeachwa fedha nyingi zilizo nje nje, katika idara mbalimbali, na katika mapato ya serikali yanayopotea hovyo hovyo; ambapo serikali kivuli imekuwa ikishauri zibanwe na kuingizwa katika mfumo rasmi.
  Katika mazingira haya, serikali ina haki ya kujitapa kwamba inawajali wafanyakazi? Wakati mazungumzo yakiendelea kati ya TUCTA na serikali, inaweza kudai imetoa hoja za kuridhisha kuzuia mgomo wa wafanyakazi kabla haijaondoa mazingira haya ya utapanyaji fedha, yanayowanyima wafanyakazi utatuaji wa matatizo ya msingi?
  Na kama inawalipa kidogo, ambacho inajua hakiwatoshi hadi mwisho wa mwezi, inadhani wanaishije siku hadi siku, mwezi hadi mwezi, bila kutafuta njia nyingine za kuihujumu serikali yenyewe?
  Tunajua kuwa serikali inaogopa athari za mgomo huu katika mwaka wa uchaguzi, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijitapa kuwa kimetimiza vema ahadi zake za mwaka 2005.
  Tayari, Ofisi ya propaganda ya CCM imeshaungazia umma kuwa inajipanga kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 80.3 za urais walizopata mwaka 2005; eti wananchi wameridhika na utendaji wa serikali.
  Lakini wanasahau kwamba katika kipindi chao cha utawala, Watanzania waishio katika umaskini uliokithiri wanafika milioni 13. Kwa kuzingatia kwamba idadi ya Watanzania haijazidi milioni 50, hii ni sehemu kubwa sana ya idadi ya Watanzania wanaoteseka.
  Wanasema hivyo wakijua kuwa watoto wapatao 600,000 walio chini ya miaka mitano (5) wamekufa kwa utapiamlo katika miaka ipatayo kumi mfululizo. Na watafiti wanasema mwaka huu pekee, watoto wengine wapatao 43,000 wanatarajiwa kupoteza maisha kwa sababu ya utapiamlo – wakati serikali (inayoongozwa na CCM) ikijiandaa kuzoa asilimia 88 za kura za urais.
  Sina shaka baadhi yao ni watoto wa wafanyakazi hawa hawa wanaodhalilishwa kwa kipato duni, na wanaozuiwa kudai zaidi.
  Wazazi hawa hawa ndio wale wale waliokuwa walengwa wa hotuba ya rais, aliposema: ”Hivi asiyekujali anaweza kukutendea mema haya?” Wamemwelewa? Ni mema yanayostahili ”asante” yao?


   
 2. Eliphaz the Temanite

  Eliphaz the Temanite JF-Expert Member

  #2
  Apr 19, 2010
  Joined: Jan 19, 2010
  Messages: 2,836
  Likes Received: 358
  Trophy Points: 180
  Hii ndio serikali inayojiandaa kwenda kuomba kura kwa wananchi wake iliyowadhoofisha kwa utapia mlo. Wafanyakazi hawana sauti, kwa miaka miatano si Bunge wala serikali imeonyesha utashi au mkakati wa kuinua kipato cha mfanyakazi! Bunge letu limekuwa mstari wa mbele kabisa kupigania kushibisha matumbo yao huku wakijua wazi wananchi wanaowawakilisha wako hoi bini taabani!
  Posho ya mbuge inazidi kima cha chini cha mfanyakazi for christ's sake! Wamekuwa mstari wa mbele kupiganaia misamaha ya kodi, huku mfanyakazi wake hata kile kidogo anachopata kinazidi kunyonywa tena na tena! Mfanyakazi wa kibongo ni yatima asiye na baba wala mama!
  Guys this your shot! Nobody will speak for you no one will defend you!

  Will you go home and watch Tv or you will stand and fight?
   
Loading...