Meli yazama Zanzibar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Meli yazama Zanzibar

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MwanaFalsafa1, May 31, 2009.

 1. MwanaFalsafa1

  MwanaFalsafa1 JF-Expert Member

  #1
  May 31, 2009
  Joined: Feb 26, 2008
  Messages: 5,566
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 135
  MELI ya mizigo inayomilikiwa na Kampuni ya Seagul, Mv Fatih imepinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi Zanzibar usiku wa kuamkia jana na watu watatu wamethibitika kupoteza maisha huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

  Mamlaka ya Udhibiti na Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra), ilisema meli hiyo iliyopinduka saa 4:00 usiku wa kuamkia jana, ilikuwa na abiria 25 na mizigo yenye uzito wa tani 76, ilipinduka na kuzama ikiwa tayari imekaribia kutia nanga katika Bandari ya Malindi mjini Zanzibar ikitokea Dar es Salaam.

  Lakini abiria walionusurika kwenye ajali hiyo walisema walikuwa wanafikia 100, huku nahodha wa meli hiyo akisema walikuwa abiria 25 na wafanyakazi 13 na jeshi la polisi limeeleza wasiwasi wake juu ya idadi hiyo.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakari Khatib Shaaban alisema ajali hiyo ilitokea wakati abiria wakitaka kushuka, lakini ghafla waliona inapinduka na kuzama baharini.

  Hadi jana mchana ni maiti tatu zilikuwa zimepatikana ikiwamo ya mtoto mdogo wa kiume, mwanamke na mwanaume ambao hawakuweza kufahamika majina yao.

  Afisa Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema watu 10 waliookolewa katika ajali hiyo, na kuwa wengine 12 walikuwa hawajulikani walipo.

  Polisi waliwataja watu 11 kuwa ndio waliookolewa, akiwamo Machano Mkinai mkazi wa Mkwajuni, Kitiba Mussa Kitiba wa Gamba, Mkoa wa Kaskazini 'A', Halima Mussa wa Arusha, Hassan Omar na Maulid Abdallah, wa Kisiju Mkoa wa Pwani.

  Wengine ni Fatma Ali Salum wa Kinyasini Wete Kisiwani Pemba, Hawa Juma Saleh wa Rukwa, Zainab Ali Kitiba, Tandale Dar es Salaam, Sharifa Hamad wa Wingwi Pemba, Ramadhan Juma Mohammed wa Tandale, Dar es Salaam na Omar Khamis Mohammed wa Vingunguti, Dar es Salaam.

  Polisi wanamshikilia nahodha wa meli hiyo, Ussi Ali, lakini maelezo yake yalielezwa na kuwa na utata hasa juu ya idadi kamili ya abiria waliokuwamo kwenye meli hiyo.

  Kamanda Shaaban alisema kwamba awali nahodha alisema katika meli yake kulikuwa na abiria 25 na wafanyakazi 13, lakini Polisi inatilia shaka taarifa hizo kwani yawezekana meli hiyo ilibeba abiria wengi na mizigo zaidi, hivyo wanaendelea kumhoji hadi wapate maelezo ya kuridhisha.

  “Jeshi la polisi halijaridhishwa na maelezo ya nahodha bado hasa katika idadi ya abiria aliyoitoa, bado tunaendelea kumuhoji,” alisema kamanda huyo.

  Alisema polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na kuwataka wananchi kutulia na kuacha vyombo vya dola kufanya kazi zao kwa wazi.

  Nahodha huyo alisema wakati akiingia bandarini ghafla aliona meli hiyo ikijaa maji na kulala upande wa kushoto.

  Alisema alianza safari yake saa 10:00 jioni kutoka Dar es Salaam na kwenda Unguja ambapo aliwasili saa 3:30 usiku, lakini akiwa njiani alipata tatizo la usukuni kutoenda vizuri akiwa karibu na kufika bandarini hapo.

  Alisema ndani ya meli hiyo kulikuwa na mizigo yenye uzito wa tani 40, abiria 25 na wafanyakazi ni 13.

  Miongoni mwa wafanyakazi hao, alisema watatu aliwaona baada ya meli hiyo kuzama, lakini wakati akizungumza na gazeti hili hakujua mahali walipo.

  Ajali hiyo ilizua taharuki miongni mwa watu wakiwemo wafanyabiashara waliokuwa eneo hilo wakisubiri mizigo yao, hali ambayo ilisababisha watu kujazana katika eneo hilo hadi polisi kuwatawanya kwa kupiga risasi hewani.

  Polisi wakishirikiana na baadhi ya askari wa vikosi vyingine waliimarisha ulinzi katika maeneo yote ili kuzuia vibaka kujipenyeza na kupora mali zilizokuwemo ndani ya meli hiyo.

  Kazi za uokoaji ziliendelea usiku juzi na kutwa nzima jana baada ya wazamiaji zaidi ya 30 wa Kikosi cha Kupambana na Magendo (KMKM) kuifanya kazi hiyo kwa mafanikio kidogo.

  Baada ya miili ya watu watatu kupatikana usiku huo walisitisha hadi jana saa 4:00 asubuhi walipofanya jitihada za kuingia ndani ya meli hiyo bila mafanikio.

  Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa viongozi waliofika katika eneo hilo kushuhudia jinsi uokoaji ulivyokuwa unaendelea.

  Rais Karume aliwaagiza waokoaji kuhakikisha wanawapata watu wote ambao hawakuwa wamepatikana na kama wamepoteza maisha kuipata miili zaidi iliyosadikiwa kuwa ndani ya meli hiyo.

  Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe alimweleza Waziri Kiongozi kwamba juhudi za uokoaji zinaendelea kwa kushirikiana na KMKM, polisi na wadau wengine wanaojitolea kusaidia.

  Jumbe alisema bado ni mapema kuielezea serikali juu ya hatua za kuchukuliwa zaidi, kwa vile wameanza kufanya kazi hiyo ambayo imekuwa ngumu kutokana na meli hiyo kuwa na mzigo mkubwa kiasi ambacho kimekuwa kikiwapa usumbufu waokoaji.

  Jumbe alisema kwamba baadaye watajaza upepo meli hiyo iliyozama kwa kutumia kifaa maalumu ili mizigo na watu waliokuwamo waweze kuja juu, kazi ambayo ingefanywa baada ya maji kujaa kwani kwa wakati huo maji yalikuwa yanakupwa na kufanya zoezi hilo kushindikana.

  Waziri Kiongozi aliwataka viongozi wa Bandari kuieleza SMZ msaada gani wanaohitaji ili kufanikisha uokoaji.

  Hata hivyo, habari zaidi kutoka kwa abiria walionusurika katika ajali hiyo wamedai kuwa ndani kulikuwa na watu wanaofikia 100.

  Halima Mussa mkazi wa Arusha alisema kwamba wakati tukio hilo linatokea alikuwa tayari ameanza kushuka ghafla aliona ikipinduka na kujikuta ndani ya maji akiwa ameshikilia kitu.

  “Mimi namshukuru Mungu kwa sababu nilikuwa nashuka, lakini ghafla nikajikuta nimo katika maji lakini baadaye nikakamata kitu bila kukijua ni kitu gani nilichoshikilia na nikaanza kupiga mayowe ya kutaka msaada na huku nyuma yangu nasikia sauti nyingine watu wakiomba msaada.

  “Kuna watu waliokuwepo katika maji ndio wakaniambia shikilia hivyo hivyo hicho kitu na kunitaka ninyooshe mikono, ndio waliponiokoa na kunileta juu,” alisema huku akihema.

  “Ni dharau ya hali ya mwisho hii, maana ajali tokea saa 4 usiku, lakini hawa watu wa KMKM wanakuja mapema hawana chochote cha kuwasaidia kuokoa abiria, matokeo yake wamekuja na kuondoka kwa kisingizio cha kungojea maji yakupwe,” amesema Ali Haji mkazi wa Jang'ombe ambaye ndugu yake alikuwamo ndani ya meli hiyo.

  Naye Kapteni Juma wa meli ya Sea Bus amesema ipo haja ya kuwa na timu nzuri ya waokoaji pale inapotokea ajali kama hiyo.

  Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwaambia waandishi kwamba, ipo haja kwa serikali hivi sasa kuvifanyia ukaguzi vyombo vya usafiri na kuzitaka mamlaka za usafirishaji na mawasiliano kuwajibika kutokana na uzembe huo ili kuipa heshima serikali ya Karume.

  Meli hiyo inayomilikiwa na Said Mbuzi imeelezwa kuwa ilibeba mizigo mizito ikiwemo trekta, magari mawili, magunia ya unga wa ngano, sukari, mchele, magunia ya viazi, nyanya, mifuko ya saruji, magodoro na bidhaa nyingine mbalimbali.

  Tukio hilo limewakumbusha Watanzania ajali ya Mv Bukoba iliyotokea Mei 21, 1996 na kuua watu zaidi ya 1,000 ilipozama ikiwa karibu kutia nanga katika Bandari ya Mwanza ikitokea Bukoba mkoani Kagera.

  source;Mwananchi Read News
   
 2. MwanaFalsafa1

  MwanaFalsafa1 JF-Expert Member

  #2
  May 31, 2009
  Joined: Feb 26, 2008
  Messages: 5,566
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 135
  May God R.I.P. the souls which were lost.
   
 3. BUSARA6

  BUSARA6 JF-Expert Member

  #3
  Jun 1, 2009
  Joined: Jan 8, 2007
  Messages: 341
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 35
  Sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake ndio marejeo.
   
 4. M

  MzalendoHalisi JF-Expert Member

  #4
  Jun 1, 2009
  Joined: Jun 24, 2007
  Messages: 3,869
  Likes Received: 116
  Trophy Points: 160
  vipi data za karibuni zinasemaje??
   
 5. B

  Bibi Kizee JF-Expert Member

  #5
  Jun 2, 2009
  Joined: Feb 18, 2008
  Messages: 213
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  mungu awape faraja waliopoteza ndugu zao, mungu atupe nguvu ya kupambana na mafisadi watanzania woote, mungu inusuru Tanzania yetu na majanga!!

  mafisadi wanatumaliza jamani, meli ya mizigo imebeba abiria!! imeishajulikana ni abiria wangapi?? hakuna update wazee hali ikoje hukoo, uokoaji unaendelea au ndio chakula cha samaki,
   
 6. m

  mamah Member

  #6
  Jun 2, 2009
  Joined: Apr 8, 2009
  Messages: 31
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 13
  Kila kiumbe hai kitaonja mauti. Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea. Hivi Tanzania tuna kitengo cha kukabiliana na dharura i.e. Emergency Response Unit iliyo na uwezo wa kukabiliana na majanga kwa haraka? Maisha yanapotea ambayo yangeweza kuokolewa lakini utakuta hatuna vifaa stahili, mara wataalamu hawapo mpaka tusubiri waje toka watokako. Siku tukiwahi kwenye tukio, vifaa vibovu kama siku ulipotokea moto kwenye kiwanda kimoja kule mikocheni, mipira inavuja , sasa hilo halikujulikana mapema? Jamani mtu unachoka ukifikiria mambo yanayofanyika humu nchini. Sijui tufanyeje Wa Tz?
   
Loading...