BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,124
Mchumi BoT: Kwanini fedha imepotea mifukoni?
Apr 06, 2017 by Raia Mwema in Habari
MCHUMI katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Lusajo Mwankemwa, amesema muda si mrefu Watanzania wataanza kuona mzunguko wa fedha ukirejea katika hali iliyozoeleka.
Akizungumza na Raia Mwema mjini Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwankemwa alisema Watanzania wanalalamika kuwa fedha hazipo kwa sababu serikali imeelekeza fedha zake katika maeneo mengine muhimu kwa uzalishaji na matokeo yataonekana kabla ya mwaka 2020.
“Kwanza niseme mapema kwamba fedha ipo kwenye mzunguko lakini haipo kwenye mzunguko ambao watu walikuwa wameuzoea katika miaka iliyopita.
“Kwa mfano, labda watu walikuwa wanasafiri sana na wanalipwa masurufu ya safari zao. Au watu walikuwa wanapata posho mara kwa mara kutokana na mikutano ya kikazi.
“Ile hela ambayo mtu alikuwa anapata, labda alikuwa anaitumia kujenga nyumba yake. Akijenga maana yake fundi ujenzi anapata fedha. Fundi akipata hela ananunua vitumbua kwa mama lishe. Huyu mama akipata hela ananunua sukari kwa muuza duka. Hapo utaona namna fedha inavyozunguka. Ndivyo ilivyokuwa huko nyuma.
“Sasa siku hizi hali ni tofauti kidogo. Ile hela ya posho zisizo za lazima na matumizi mengine yasiyo na faida sana imeondolewa huko na kwenda kujenga barabara au kununua ndege.
“Sasa ukinunua ndege inawezekana hela isizunguke kwa sababu ndege inatengenezwa nje ya nchi. Lakini, ukifufua shirika la ndege, unarahisisha usafiri na kuchochea kukua kwa utalii. Vyote hivyo ni vichocheo vya uchumi.
“Kwa maana nyingine, mtu ambaye kwa sasa yuko kwenye sekta ya miundombinu anaona namna fedha inavyozunguka lakini wale wengine hawaioni,” alisema mchumi huyo.
Katika hali ya kawaida, alisema BoT huwa inafahamu kiwango chote cha fedha ambacho kiko katika mzunguko na kwamba kikiwa kimezidi mahitaji, huwa kinapunguzwa na kikiwa pungufu, benki huongeza ujazi wa fedha.
Alisema ujenzi wa viwanda unaoendelea sasa, ufufuaji wa Shirika la Ndege la ATCL, Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na nyinginezo nchini ni mambo yanayohitaji gharama kubwa lakini yakikamilika, uchumi utaimarika na mzunguko utakuwa mzuri.
“Miundombinu ikiboreshwa, maana yake ni kwamba wakulima watakuwa jirani na masoko ya bidhaa zao. Viwanda vikikamilika, maana yake ni kwamba ajira zitaongezeka pamoja na mahitaji ya malighafi.
“Uboreshaji wa bandari zetu utaongeza ufanisi na kuchochea wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuitumia. Nina matumaini makubwa kwamba hali itaboreka mara viwanda vitakapoanza uzalishaji na kila uwekezaji kuanza kazi rasmi,” alisema.
Kuzimua uchumi
Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Itifaki wa BoT, Zalia Mbeo, alisema kitendo cha taasisi hiyo kupunguza kiwango cha amana ambacho benki zilizopo nchini huweka kama dhamana (Statutory Minimum Reserve-SMR) kutoka asilimia kumi hadi asilimia nane, kina lengo la kusaidia kuboresha mzunguko wa fedha nchini.
Alisema kama benki ilitakiwa kuweka shilingi 100 kama dhamana yake BoT, sasa itaweka shilingi 80 na hivyo inaweza kuzitumia shilingi 20 zilizobaki kwa shughuli muhimu za kibenki kama vile kukopesha na kupunguza riba.
“Unajua kama benki ina fedha kidogo, maana yake ni kwamba itakopesha watu wachache na kwa riba kubwa. Lengo la BoT katika kushusha SMR ni kuziongezea benki ukwasi na hivyo kuziwezesha kukopesha watu wengi zaidi na kwa riba nafuu.
“Kama watu wataweza kupata mikopo itawasaidia katika shughuli zao za kibiashara ambazo ndizo huchochea mzunguko wa fedha. Kama riba si kubwa sana, maana yake watu wengi wanaweza kujitokeza kukopa,” alisema Zalia.
Hali ya uchumi nchini
Wakati BoT ikitoa picha hiyo ya matumaini, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, wasomi, wanasiasa na wafanyabiashara kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini.
Mwezi uliopita, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lilitoa ripoti yake iliyosema kwamba ingawa ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni wa kuridhisha, mambo manne yanaweza kuathiri hali hiyo.
Sababu nne kubwa zilizotolewa na IMF kuhusu hofu hiyo kwa Tanzania ni kutotabirika kwa sera zake za uchumi mpana, kutokua kwa sekta ya mikopo, kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya uwekezaji na kubinywa kwa sekta binafsi na serikali.
Sekta binafsi imeathiriwa na baadhi ya vitendo vya serikali ya Rais John Magufuli, likiwamo agizo la kutaka taasisi za serikali zifanye biashara zenyewe kwa zenyewe kabla ya kufikiria sekta binafsi.
Pia, agizo hilo lilitaka taasisi za serikali kufanyia mikutano yake katika kumbi zao za mikutano badala ya hoteli binafsi kama ilivyozoeleka katika miaka ya nyuma.
Hatua hiyo imeiumiza sekta binafsi kwa sababu kwa Tanzania, serikali ndiyo mhimili mkubwa wa uchumi na si sekta binafsi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea. Kwa maana hiyo, wakati inapofunga milango yake kwa sekta binafsi, athari zake huwa kubwa.
Wakati huo huo, serikali pia imeondoa katika benki binafsi kiasi cha shilingi bilioni 500 zilizokuwa zimehifadhiwa na taasisi zake na kwenda kuzihifadhi BoT.
Hatua hiyo imeelezwa kupunguza ujazi wa fedha katika benki za biashara zilizopo nchini; na pengine ndiyo sababu BoT imeamua sasa kupunguza kiasi hicho cha dhamana ya benki.
Mmoja wa wachumi mashuhuri nchini, Profesa Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, ameliambia gazeti hili kwamba kama serikali itaendelea na utaratibu wake wa kubana matumizi hususani yale yanayozimua sekta binafsi, hali ya uchumi itaendelea kubaki kama ilivyo.
Kudhihirisha ukweli wa kauli ya Ngowi, Chama cha Wamiliki wa Hoteli hapa nchini (THA), kimetoa taarifa inayoonyesha kwamba mapato ya hoteli hapa nchini yameporomoka kwa asilimia 40 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mmoja wa viongozi wa THA, Latifa Sykes, alinukuliwa katika baadhi ya vyombo vya habari wiki hii akisema kwamba mwaka jana pekee, takribani hoteli 400 hapa nchini zilipigwa mnada kutokana na kushindwa kulipa mikopo waliyokopa benki kwa sababu ya kuyumba kwa biashara.
Pia, mwishoni mwa mwezi uliopita, Kampuni ya Konyagi ilitangaza kupunguza wafanyakazi 50 kutokana na hali mbaya ya biashara iliyosababishwa na hatua ya serikali kupiga marufuku pombe za viroba.