Mchango wa Uislamu katika maendeleo ya mwanadamu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
Sayansi ya Maumbile (Natural Science)

Katika sayansi asilia, baada ya kuelewa maoni ya waandishi wa Kigiriki, Waarabu nao walianza kuitafakari na kuichunguza (nature) asili ya maumbile na kutoa mahitimisho (observations) yao wenyewe. Kutokana na juhudi zao waliweza kutaja nyongeza ya mimea 2000 katika idadi ya mimea iliyokuwa inajulikana. Taaluma ya Waarabu ya Madawa ilihusisha matumizi ya mimea na michanganyiko ya vitu ambavyo havikujulikana kwa Wagiriki. Matumizi ya sukari badala ya asali yalisababisha kuwepo kwa madawa mbalimbali yenye harufu na ladha ya kuvutia kwa wanywao katika uponyaji. Kwa kutumia sukari, Waarabu waliweza kutengeneza madawa mbalimbali pamoja na uwezo wa kuhifadhi mboga na matunda.

Waarabu ndio waliowaonyesha Wazungu aina mbalimbali za manukato na viungo vilivyotokana na mimea, maua, na mbegu mbalimbali. Kahawa, bidhaa muhimu sasa hivi duniani asili yake ni katika nchi ya Yemen. Miongoni mwa wanyama wa kufugwa, farasi bora anapatikana Uarabuni, na mbuzi bora pia anapatikana Asia ndogo wakati kondoo wazuri wanapatikana nchini Morocco. Waarabu ndio walioiendeleza elimu ya kilimo bora na pia walijishughulisha na taaluma ya miamba (geology)



Elimu ya Madawa (Medicine)

Baada ya hisabati na kemia, elimu ya utengenezaji wa madawa ilikuwa miongoni mwa sayansi iliyowavutia sana Waislam. Wakati wa karne za mwanzo za Hijra, taaluma hii ilifanywa kuwa mojawapo ya sehemu muhimu katika mfumo wa elimu kwa jumla. Ndio maana walitokea madaktari wazuri na maarufu pamoja na tasnifu (makala) zao mbalimbali juu ya taaluma hii.

Madaktari wa Kiislam walileta changamoto muhimu katika sayansi ya madawa kwa nchi za Magharibi. Kwa karne nyingi vitabu vya AL-Razi (Razes), Ibn Sina (Avicenna), Abul Cassis na Ibn Zohar vimekuwa ni msingi wa elimu ya tiba katika Vyuo Vikuu vyote vya Ulaya. Chuo cha Tiba hapo Salerno na hasa Montpellier kilisifika sana duniani. Machapisho ya kazi za tiba ya AL-Razi yaliyojulikana kama Havi (au Maisha Bora), pamoja na kitabu chake kiitwacho Mansuri, viliendelea tena kwa karne nyingi kuwa vitabu vya kiada (miongozo) kwa taaluma ya tiba.

Havi, ni mojawapo ya juzuu tisa (9) zilizokuwa katika Maktaba ya Kitivo Cha Tiba cha mjini Paris, Ufaransa katika mwaka 1395. Humo kunapatikana maelezo ya dalili za homa za magonjwa mbalimbali kama ya ndui na surua. AL-Razi alianzisha matumizi ya dawa baridi za kumharisha mgonjwa katika kulainisha tumbo lake. Pia alitoa dalili za ugonjwa wa kiharusi na matumizi ya maji baridi (sponging) katika kupunguza homa kali. Anahusika pia na ugunduzi wa seton, kwani alikuwa akiitumia mara kwa mara. Vitabu vya AL-Razi vilitafsiriwa katika lugha ya Ki-Latin na kuchapishwa nakala mara nyingi na hasa katika miaka ya 1505 hapo Venice, mwaka 1428 na 1578 hapo jijini Paris, Ufaransa. Makala yake juu ya ugonjwa wa ndui ilichapishwa tena mwaka 1745.

Abu Ali Al-Hussein Ibn Abdallah, aliyejulikana kote Ulaya kama Ibn Sina na kwingineko Ulimwenguni kama Avicenna, bila shaka alikuwa daktari maarufu. Kitabu chake cha Kanuni za Tiba (Canun Fi’l Tib) kilichapishwa kwanza katika lugha ya Kiarabu hapo mjini Roma mwaka 1593. Kilitolewa katika juzuu tano katika fani za fiziolojia (elimu ya viungo), kanuni za Afya, patholojia (elimu ya magonjwa), elimu ya Tiba (therapeutics) na taaluma ya famasia (yaani ya utengenezaji wa madawa (pharmacy)).

Kwa takriban miaka mia sita hivi kuanzia karne ya 12 hadi ya 17, vitabu hivi vilisaidia kuwa msingi wa Taaluma ya Tiba katika Vyuo Vikuu nchini Italia na Ufaransa. Katika karne ya 15 vilihaririwa mara 15 katika lugha ya Ki-Latin na mara moja katika Kiebrania (Kiyahudi). Vilichapishwa tena na tena hadi kufikia karne ya 18 na hata mwanzoni mwa karne ya 19 ambapo mihadhara kutokana na mafunzo yake, iliendeshwa katika Kitivo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha hapo Montpellier. Licha ya hayo, naye Ibn Sina aliandika kitabu chake juu ya Tiba ya ugonjwa wa Moyo na hata mashairi kuhusu elimu ya madawa. Kamusi yake yenye orodha ya madawa na tiba zake iliainisha madawa yapatayo 760.

Mojawapo ya hatua muhimu iliyofikiwa na madaktari wa Kiislam ni katika nyanja ya upasuaji (surgery). Hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya 11 walishaelewa jinsi ya kutibu magonjwa ya macho (hasa mtoto wa jicho), kutokwa na damu puani, na matumizi ya tiba za dawa joto (caustics). Pia wasomi wa Kiislam walishajua matumizi ya ganzi (anaesthetics), ingawa yamekuwa yakichukuliwa kuwa ni uvumbuzi wa siku hizi. Wao, kabla ya kumfanyia mgonjwa operesheni (upasuaji), walimnywesha kwanza dawa ya kumtia usingizi mzito, iliyotokana na mmea ulioitwa ‘danel’, hadi hapo alipoonekana kuzimia.

Daktari wa Kiislam maarufu katika upasuaji aliitwa Abul-Qasim Khalaf bin Abbas (Abulcassis), aliyeishi mjini Cordova na kufariki mwaka 1107. Mwanafisiolojia maarufu Haller anadai kwamba "kazi za Abulcassis ndizo zilizokuwa chanzo ya changamoto kwenye taaluma ya upasuaji hadi kufikia kwenye karne ya 15." Elimu ya upasuaji ya Abulcassis ilichapishwa kama kitabu katika lugha ya Ki-Latin mwaka 1497.

Chini ya tawala za Kiislam, Hispania nayo iliweza kutoa madaktari bingwa na miongoni mwao ni Ibn Zohar na Averroes (Ibn Rushd). Ibn Zohar, alianzisha katika fani ya tiba, kanuni ya uchunguzi kwanza. Jambo muhimu katika matibabu yake ni kuanzia kwenye mwili wenyewe kwamba una uwezo asilia (immunity) wa kujikinga na baadhi ya magonjwa. Alikuwa mtu wa kwanza kuunganisha somo la tiba, upasuaji na madawa na kuliweka kama somo moja. Maandishi yake juu ya taaluma ya upasuaji ndiyo ya mwanzo kuelezea sura halisi ya koromeo (bronchotomy), na maelezo ya kina juu ya magonjwa ya mifupa, viungo na taratibu za tiba zake.

Averroes (Abul Walid Mohammed Ibn Rushd) kama mtu aliyeendeleza kazi za Aristotle, hatimaye alikuja kuwa daktari bingwa, na pia alitoa Tahariri (commentary) juu ya kitabu cha Ibn Sina (Avicenna) kiitwacho "Canun" na pia kile cha Galen. Kwake tumfaidika kutokana na makala yake kubwa kuhusu "theriac" na pia kitabu chake juu ya homa na sumu mbalimbali pamoja na tiba zake. Kazi yake kubwa ni pale alipotoa kitabu cha Tiba kiitwacho Kulliyet, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1490 hapo mjini Venice na baadae kiliendelea kuchapishwa katika nchi mbalimbali duniani.

Tiba ya macho inayoendelezwa hivi sasa duniani asili yake ni katika elimu ya sayansi ya Waarabu. Kitabu cha "kumbukumbu ya Kanuni za Tiba ya Macho", alichotunga Ali Ibn Isaa kiliendelea kutumika kama kitabu cha kiada (reference) hadi majuzi kwenye karne ya 19. Operesheni ya kwanza ya kuondoa mtoto wa jicho ilifanywa kwa mafanikio makubwa na Al Muhsin mwaka 1256, na ndiye aliyegundua sindano (hollow needle) yenye uwezo wa kuingiza dawa katika mwili wa mwanadamu.

Ibn AL-Nafis, Msyria aliyefariki mwaka 1289 hapo Damascus, alikuwa ameshaelezea, tena kwa usahihi kabisa mzunguko wa damu mwilini, miaka ipatayo 300 kabla ya maelezo yaliyotolewa na Mreno aliyeitwa Serget, ambaye dunia imekuwa ikimdhania kuwa mtaaalam wa mwanzo kuelezea jambo hili.

Maelezo juu ya sura ya Mapafu na mzunguko wa hewa ndani yake yalitolewa na msomi kutoka Misri aliyeitwa Muhy Al-Dine Tatarui, katika Tasnifu (thesis) yake aliyoitayarisha kabla ya kuhitimu kwake katika Chuo Kikuu cha Freiburg mwaka 1924.

Maelezo mafupi juu ya somo la afya yanaweza kufanyika kama ifuatavyo. Sote tunaelewa kwamba Dini ya Uislam imejaa kanuni bora kabisa juu ya utaratibu unaomwezesha mtu kuishi kiafya, kama kuoga na kunawa mara kwa mara, makatazo juu ya ulaji wa nyama ya nguruwe na unywaji wa pombe. Zaidi ya hayo, Madaktari wa Kiislam walisisitiza zifuatwe taratibu za kiafya wakati wa kutibu magonjwa. "Hospitali za Waarabu", anaeleza Gustave Le Bo, "zilijengwa katika misingi bora ya afya kuliko hospitali nyingi za siku hizi. Yalikuwa ni majumba makubwa makubwa yaliyoruhusu mzunguko huru wa hewa na zilikuwa na maji ya kutosha kabisa,"



Somo la Falsafa (Philosophy)

Kuna mambo mengi ambayo yametokana na mchango wa Uislam katika fani ya Falsafa, kama mtu akifuatilia historia hatua kwa hatua. Hapa tutaeleza mawazo ya jumla jumla tu ya Kiislam yaliyochangia kuleta maendeleo ya somo la Falsafa hasa yaliyochukuliwa na wasomi wa nchi za Magharibi.

Katika Ulimwengu wa Kiislam, mawazo ya Falsafa yalianza kuibuka mapema sana. Kuna wakati baadhi ya waandishi walikataa kabisa falsafa ya Kiislam. Walidai kwamba dhana yoyoye nje ya maelezo ya Qur’an au mawazo juu ya kuwepo kwa dini nyingine hayakuwa na nafasi katika Uislam. Hivyo kikawa ni kigezo cha baadhi ya wasomi hasa wa Magharibi kukataa utambuzi wa mchango wa Uislam katika maendeleo ya somo la Falsafa.

Hivyo, haikuchukuwa muda mrefu tangu vitabu vya Historia vilipoanza kufundisha kwamba Waarabu walipovamia Misri, Khalifa Omar Ibn Khattab aliamrisha ichomwe Maktaba maarufu ya mjini Alexandria, akidai kwamba "kama vitabu vyake vinaendana na falsafa ya kiislam, basi havina maana yoyote, na kwamba kama haviendani nayo basi ni vya hatari."

Hakuna mtu leo mwenye kujua vizuri somo la Historia ya Uislam, anayeweza kujali tena dai hilo kutokana na ushahidi uliokwishathibitishwa kihistoria wenye kupinga maoni kama hayo. Wala sio haki au vyema kudharau mawazo ya Uislam kwa kuyapendelea mawazo hafifu ya kijakazi ya wanafalsafa wa Kiyunani.

Falsafa ya Waarabu imeweza kuthibitishwa kuwepo kwake tangu karne ya mwanzo ya zama za uislam kama ulivyoenezwa na Mtume Muhammad (S.A.W), ambayo imehusishwa moja kwa moja na theolojia ya uislam. Kuwepo kwa Mwenyezi Mungu mmoja, upekee wake, uwezo wake Mkuu, Mtenda Haki (asiyedhulumu), Mwenye Huruma (kwa viumbe vyake), na sifa nyinginezo nyingi ni miongoni mwa mada ambazo zilihitaji kutafakariwa kwa kina ili kuweza kuzielewa kiusahihi. Mawazo mbalimbali yaliibuka wakati wa mijadala ambayo wakati mwingine ilikuwa mikali kabisa. Makundi yenye mitizamo tofauti yaliibuka kuhusu masuala ya hatima ya watu iliyokwisha kadiriwa (na Mwenyezi Mungu), uhuru wa imani (kuabudu), ukombozi kwa njia ya vitendo au imani, Khalifa wa Mtume kama kiongozi wa muda wa kuiongoza jamii ya Kiislam mara baada ya Mtume kufariki na masuala mengine mengi.

Haya yalikuwa ni makundi ambayo yaliyojulikana kama Kharidji, Murdji na Kadari. Mwanzoni mwa karne ya 2 Hijria, lilizuka kundi la Mu’tazili. Yote haya yalisababisha zidurusiwe tarehe za tafsiri za Wagiriki, ambazo hazikuwa zimefanyika hadi wakati wa Ukhalifa wa AL-Mansur mnamo miaka ya 735 – 774, na pia ni ushahidi wa kuwepo kwa maendeleo tofauti ya uislam yaliyojitegemea.

Kwa kuidurusu, kuisambaza na kuitumia elimu ya watu wa kale, Falsafa ya Uislam ilitokea kuwa changamani (complex) na pambanuzi (subtle). Katika karne ya 3, wakati wa utawala wa AL– Kindi, kundi la wasomi wenye kushabikia somo la Falsafa lilianzishwa. Kundi hili lilichambua mafundisho ya Kiyunani (Kigiriki) na ya Plato. Wasomi wengi wa Kiislam walishughulika zaidi na kuoanisha mawazo ya Plato na Aristotle na kuyahusisha na mafundisho ya Dini. Katika Falsafa, kama ilivyo katika sayansi yoyote, wasomi wa Kiislam walionyesha kila aina ya shauku ya kutaka kujiendeleza kielimu. Matatizo yote yenye kuhusu kiini cha mambo kama yanavyotafakariwa na mwanadamu, aina zote za tafakari, kupitia kwenye Nadharia ya Kushuku na Mantiki, yaliweza kuelezeka katika mitizamo mbalimbali ya kifalsafa.

Tunaweza kuuchunguza usomi wa Kiislam kwa undani zaidi kutokana na umuhimu wa ushawishi (influence) wa wahubiri wake walivyokuwa makini na masuala ya Dini, na pia kutokana na wasomi hawa kuwa misingi ya falsafa iliyojengeka Ulaya kuanzia karne za zama za Kati. Avicenna (Ibn Sina) na Averroes (Ibn Rushd), walisifika sana katika Ulimwengu wa Magharibi kuliko Mashariki, ambako walijulikana tu kama madaktari au watabibu.

Umashuhuri wa Ibn Sina, ambaye alifikiriwa na watu kuwa kigezo cha kilele cha usomi wa karne za Kati, ni kutokana na kazi aliyoitoa katika seti ya vitabu vyenye kuzungumzia mada mbalimbali. Tulishaelezea kazi zake katika taaluma ya Tiba. Pia, alifanya mengi katika fani za Sayansi na Falsafa. Anaheshimika kutokana na kuanzisha taratibu za kisayansi zilizodumu kwa karne nyingi bila ya kubadilishwa. Kama msomi mkuu, alianzisha somo la Falsafa na kulitolea mwelekeo wa siku hizo na za baadae. Mawazo ya Aristotle na Plato pamoja na kuyasoma, hayakuathiri asili ya mawazo yake mwenyewe. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kumjadili Aristotle na pengine aliweza kumkosoa na kutoa hitimisho lenye mantiki. Kazi zake kubwa zilizowekwa katika vitabu ni pamoja na: Kitab AL- Shifa (au Taaluma ya Tiba), AL- Hidayat Fi’l Hikmat (au Mwongozo katika Hekima), Hadithi ya Hayy Ibn Yagzan, Kitab AL-Isharat Wa’al Tanbihat (au Mwongozo wa mafunzo ya Ishara na Tahadhari), n.k. Tafsiri ya kwanza ya Ibn Sina ilifanyika mwanzoni mwa karne ya 12.

Ushawishi wa Ibn Sina katika maendeleo ya somo la Falsafa kwa nchi za Magharibi ulikuwa mkubwa sana. "Hakuna Tasnifu ya msomi yoyote ambaye haikumnukuu Avicenna, kama anavyosema mamaA.M. Gorchon.. Na tafakari zaidi zinaonyesha wazi zaidi kwanba Avicenna alizivutia sana fikra za wanafalsafa wa Ulaya."

Albetus Magnus alimchukulia kama mtu wa mfano mwema ingawa yeye mwenyewe alikuwa msitari wa mbele katika kuishambulia falsafa ya Waarabu. Naye Renan, katika kitabu chake chenye maana ya "Averos na Uaverosi", hakusita kuthibitisha kwamba masomo yaliyotolewa katika Chuo cha Mtakatifu Thomas yalitegemea kwa kiasi kikubwa elimu ya Ibn Sina. Mt. Thomas mwenyewe, ambaye alivutiwa sana na Ibn Sina, hakuwa mgeni wa fikra zake. Papa Yohana wa 21, kabla ya kusimikwa kwake, "alifundisha nadharia ya elimu ambayo aliihusisha na Aristotle badala ya mwenyewe Avicenna." Hayo yamesemwa na wasomi kama akina William mwenyeji wa Auvergne, Alexander wa Hales na wengineo wengi ambao walisoma hapo kwa Mt.Thomas.

Averroce, jina ambalo limepotoshwa kutokana na Abdul Walid Mohammed Ibn Rushd, alikuwa pia na mafanikio makubwa yaliyoonewa wivu na wasomi wa nchi za Magharibi hata kumzidi Ibn Sina. Ni kutokana na Tahariri zake juu ya Aristotle ambazo zilimfanya kuwa maarufu zaidi ya wasomi wenzake wa Kiislam.

Azma ya Averroes (Ibn Rushd) ilikuwa ni kujitwisha dhima ya kihistoria ya kuzifundisha falsafa nchi za pande mbili za ulimwengu yaani Mashariki na Magharibi. Alikubalika kama Mhariri Mkuu wa kazi za Aristotle, msomi mkubwa kabisa, ingawa alishambuliwa na wengine kuwa hakuwa Mcha Mungu. Hata kama Albertus Magnus mara chache sana alimnukuu, kadhia ya Mt. Thomas Aquinas inakanganya. "Mt.Thomas", anasema Renan, "wakati huohuo anaonyesha kuwa adui mkubwa kupita kiasi wa Mawazo ya Ibn Rushd, na mtu anaweza kupata mshangao ulio wazi kuhusu mabadiliko ya ghafla ya mfuasi huyu wa kwanza wa Mwanafalsafa huyo mkuu. Albertus Magnus alitumia mawazo ya Ibn Sina wakati Mt. Thomas yeye alitumia sana mawazo ya Ibn Rushd."

Padri Asin Palacio, aliyesoma sana falsafa ya kidini itokanayo na mafundisho ya Ibn Rushd yaliyofundishwa hapo kwa Mt. Thomas, aliyafananisha na mafundisho yaliyotolewa katika nchi za Latin (Milki ya Kirumi), baada ya kuyachunguza maandishi mbalimbali ya Wanafalsafa wa Cordova na kuyalinganisha na yale ya Ibn Rushd. Kufanana kwa mawazo hayo kunaonyeshwa na matumizi ya misemo inayofanana kiasi kwamba hakuna shaka juu ya mchango (au ushawishi) wa Falsafa ya Mwislam huyu ulivyokuwa mkubwa katika mafundisho ya Wakatoliki.

Karne za 14 na 15 zilishuhudia kilele katika matumizi makubwa ya Falsafa ya Ibn Rushd. Katika Vyuo Vikuu vya Magharibi, Mihutasari yake ilitumiwa kama kiada badala ya makala za Aristotle. Yohana Baconthorp, aliyefariki mwaka 1346, aliyekuwa Askofu wa Jimbo moja nchini Uingereza, na daktari wa Mipango, aliamrisha yaingizwe mafundisho ya Averroes katika mfumo wa elimu katika Chuo chake. Naye Paul mwenyeji wa Venice aliyefariki mwaka 1429, alikiri waziwazi kuzipenda nadharia za Averroes (Ibn Rushd). Alipoliandaa somo la Falsafa mwaka 1473, Louis wa 11 alizifanya nadharia za Aristotle pamoja na Tahariri za Averroes kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wake. Naye Vicomercato alilifundisha somo hilo katika Chuo chake nchini Ufaransa toka mwaka 1543 hadi 1567.

Lakini ni Chuo Kikuu cha Padua kilichokuja kuwa Kitovu cha elimu ya Kiarabu kwa wakati huo. Ibn Rushd ndiye aliyeonekana kuwa bingwa wao. Mafunzo yake yalidumu hadi karne ya 17. Bologna, Ferrara na Venice zililazimishwa kufuata mafundisho ya Kirumi, ingawa hakukutokea pingamizi juu ya Tahariri za Kiarabu juu ya Falsafa ya Aristotle.

Mwaka 1240, Askofu William kutoka mjini Paris aliamuru yaondolewe mawazo ya Kiarabu katika baadhi ya maandishi na vitabu. Mwaka 1269 Etienne Tempier aliyekuwa Askofu wa Paris wakati huo pia, alithibitisha kutekelezwa kwa amri hiyo. Hatua zote hizi hata hivyo, hazikusaidia kuzima harakati za maendeleo ya Falsafa ya Kiislam. Falsafa hii iliendelezwa na Warabu na kuweza kuimarika zaidi. Ukweli Siger de Brabant, anayesemekana kuwa muasisi wa harakati za (Ibn Rushd) Averroes, alikuwa mwalimu wa Falsafa hii katika miaka ya 1266 na 1277 katika Chuo Kikuu cha hapo mjini Paris. Huko kabla mnamo mwaka 1227, aliyekuwa Papa wakati huo, aliamuru yapitiwe upya maandiko, na ndipo makala zipatazo 219 zilizoonekana kuwa za uasi dhidi ya Kanisa zilipopigwa marufuku. Matokeo yake ilikuwa ni kufukuzwa kazi kwa Bwana Siger, na baadaye alihukumiwa na Kanisa kutumikia kifungo cha maisha jela. Pamoja na hatua zote hizi, Uaverosi uliendelea kuimarika zaidi.

Kundi lililokuwa mstari wa mbele katika kuipinga Falsafa ya Averroes ni lile lililoamua kuanza kufuata mafundisho ya Kirumi na Kiyunani tu (lililoitwa the Humanist). Kwa mtizamo wao, walimwona Averroes kuwakilisha fikra za Waarabu, na kwa kuwa sasa walishaelewa moja kwa moja asili ya elimu ya kale, Waarabu wakawa ni watu wa kushambuliwa, tena kwa nguvu zote. Bila ya kujali wala ya kuthamini mchango wao mkubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya mwanadamu baada ya kuichambua na kuiendeleza elimu ya Wayunani (Wagiriki), badala yake walishutumiwa kwa kuudumaza na kuupotosha utamaduni wa kale, jambo ambalo kama tulivyokwishaona kuwa halikuwa la kweli.

Petrarch, aliyedhaniwa, na kwa uhakika zaidi kuwa miongoni mwa watu walioasisi ustaarabu unaoendelea sasa hivi duniani, aliandika katika mojawapo ya barua zake kwa rafiki yake aliyeitwa Jean Dondi maneno yafuatayo: "Mimi binafsi nalichukia sana kabila hili (la Waarabu). Kwani inaniwia vigumu sana kwangu mimi kuamini kwamba Waarabu wanaweza kuleta jambo lolote la manufaa (kwa watu)."

Hata hivyo, pamoja na mashambulizi haya yaliyotoka katika sehemu zote mbili, za walimu wa dini (theologists) na wasomi wa Kirumi na Kiyunani (the humanists), Uaverosi (falsafa ya Ibn Rushd) uliendelea na kusambaa kwa wasomi mbalimbali duniani hadi kufikia kwenye karne ya 17.

Harakati za kuendeleza mawazo ya Averroes (Ibn Rushd) zilikuwa kubwa, na kuwepo kwa uhakiki tofauti tofauti juu ya kazi zake ni ushahidi tosha wa jinsi gani alivyokuwa mwana falsafa makini kabisa wa Kiislam. Kumekuwepo na tofauti kubwa kati ya fikra sahihi za Ibn Rushd na mawazo ya wasomi wengine ambayo amekuwa akihusishwa nayo. Falsafa ya Averroes ni kitu kimoja na Uaverosi (Averroism) ni kitu kingine. Mambo hayo mawili hayana budi kutofautishwa.

Si jambo la kubabaisha tu katika kubainisha tofauti hizo. Tunatumai kutokana na maelezo tuliyoyaona hapo nyuma kwamba Ibn Rushd alikuwa amewazidi katika elimu ya Falsafa, wasomi wa Ulaya tena kwa karne nyingi tu, kiasi kwamba nadharia na mafundisho yake, hata yale yaliyopotoshwa ama kufichwa kwa makusudi, yalisaidia katika kujenga muamko wa kielimu katika bara la Ulaya na pia yalichangia katika kuondoa dhana potofu zilizokuwa zimedumaza na kukwaza uhuru wa watu kufanya tafiti na kutoa fikra mbalimbali.
Tunakaribisha Mijadala ,midaalo au hotuba tuandikie kwa anuani jifunzeuislamu@yahoogroups.com au angalia page yetu http://groups.yahoo.com/group/jifunzeuislamu/
 
Sam Harris katika kitabu chake "The End of Faith" ana argue kwamba Islam has had it's day - the bulk of what you mentioned hapo juu is actually from the medieval era, from translating the Greek Classics to Cordova and the conquering of Europe to cosmology etc- and that today it remains an intolerant, overly militant rigidly backward faith.

To be fair he attacks all faiths so this is not a Christian/Muslim argument, rather it is a faith vs reason one.
 
Back
Top Bottom