Mbowe,lema,mnyika,ndesamburo watikisa rombo

Molemo

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
14,534
13,225

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mustapha Sobodo ametoa Sh10 milioni kwa familia mbili ambazo vijana wake waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi Jijini Arusha wiki iliyopita.

Hatua ya mfanyabiashara huyo ambaye pia ni kada wa CCM, imekuja wakati baadhi ya viongozi wa chama hicho wakionyesha kuunga mkono hatua ya polisi kutumia nguvu za ziada katika kudhibiti maandamano ya Chadema.

Akizungumza katika ibada maalumu ya mazishi ya Denis Shirima aliyeuawa katika vurugu zilizosababishwa na Polisi Jijini Arusha, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kila familia itapatiwa Sh 5milioni.

“Wakati tuko njiani tukitokea KCMC kuchukua mwili wa shujaa wetu, nilipigiwa simu na rafiki yetu Mustafa Sabodo akasema ameguswa sana na kuhuzunishwa na mauaji hayo na kila familia ataipa Sh 5milioni,”alisema Mbowe.
Mbowe ambaye hotuba yake ililingana na ile iliyotolewa na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kwa kugusa hisia za watu hadi kububujikwa machozi alisema, waliokufa wamekufa kishujaa wakitetea maslahi ya Watanzania.

“Watanzania hawa ambao ni mashujaa walipigwa risasi za moto kama wanyama halafu wanatoka baadhi ya viongozi wendawazimu wa CCM wanawapongeza polisi kwa kufanya kitendo hiki cha kinyama. Hii ni aibu,”alisema Mbowe.

Mbowe alisema katika mambo yaliyosikitisha ni kwamba hakuna kiongozi hata mmoja wa serikali na CCM aliyehudhuria ibada ya kuwaombea marehemu hao iliyofanyika katika viwanja vya NMC juzi Jijini Arusha.

“Misiba siku zote inatuunganisha Watanzania lakini mjue serikali yenu isivyokuwa na utu, wakati Chadema tunasema tutagharamia mazishi haya, polisi walizunguka kinyumenyume kuwashawishi ndugu wa marehemu wasikubali”.

Akizungumza kwa uchungu katika viwanja vya Vetinari, kijiji cha Makiidi wilayani Rombo jana, Mbowe alisema baadhi ya maofisa wa polisi walienda mbali na kutaka kuwahonga ndugu hao wazike kimya kimya.

“Sisi tuliwaambia hapana, tukawaambia ndugu jamaa na marafiki wa marehemu kwamba ni lazima miili ya marehemu ifanyiwe uchunguzi kwa sababu tuna mpango wa kusaidia familia hizi kuidai serikali fidia kwa mauaji haya,”alisema.

Wakati huo huo Paroko wa Parokia ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Padre Henry Mushi amesema damu ya vijana waliouawa kwa kupigwa risasi na Polisi Jijini Arusha, itawaandama polisi waliouhusika katika maisha yao yote.

Padre Mushi ambaye pia ni mwakilishi wa Askofu wa Jimbo hilo katika wilaya ya Rombo, alisema polisi waliohusika na mauaji hayo, hawawezi kujitetea kuwa walitumwa kwani wao sio mashine kiasi cha kuua raia bila kutafakari.

Padre Mushi alitoa kauli hiyo kijijini hapo wakati wa ibada maalumu ya mazishi ya mmoja wa wafuasi wa Chadema aliyeuawa katika tukio hilo, Dennis Shirima.

“Tendo la kumwaga damu lililotokea Arusha ni baya na yeyote aliyefanya kitendo hicho damu hiyo itamsumbua kama ilivyomsumbua Kaini…Huyo aliyefanya hivyo naye atafuata njia hiyo hiyo,” alisisitiza Padre Mushi.

Padre Mushi aliongeza kusema kuwa,” wewe ni binadamu sio mashine kwa hiyo hata kama utasema ulitumwa kufyatua risasi lakini, wewe unayepiga risasi ndiye utakayeulizwa mbele za Mungu kwa kushindwa kutafakari”.

Paroko huyo aliendelea kusisitiza katika ibada hiyo iliyofurika waombolezaji kutoka mikoa ya Kilimanjaro kuwa, Arusha, Dar Es Salaam na Mwanza kuwa polisi aliyefanya kitendo hicho asifikiri atajificha mbele ya uso wa Mungu.

“Huyo aliyefanya kitendo hicho hatujui yuko wapi lakini afahamu yuko chini ya Mwanga wa Mungu na njia pekee ya kuepuka hasira ya Mungu ni kutubu dhambi hiyo vinginevyo damu aliyoimwaga itaendelea kumsumbua,”alisema.

Katika hatua nyingine, ndugu wa raia wa Kenya aliyeuawa katika tukio hilo lililotokea Januari 5 mwaka huu, amelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi maalumu wa nini hasa kilifanyika na kuwachukulia hatua polisi waliohusika.

Akizungumza katika ibada hiyo ya mazishi, Timoth Gitau ambaye ni ndugu wa mkenya Paul Njuguna ambaye aliwafanya waombolezaji kububujikwa na machozi alisema serikali haikutumia njia sahihi kushughulikia jambo hilo.

“Kama ni kuzuia maandamano serikali ya Tanzania ilipaswa kutumia njia sahihi na si kupiga risasi raia…tumeumia sana na tunaomba uchunguzi maalumu ufanyike tujue nini kilifanyika hata ndugu yetu akauawa”alisema Gitau.

Gitau aliwaomba Watanzania wampe ushirikiano kufanikisha kuusafirisha mwili wa ndugu yake hadi nchini Kenya kwa mazishi akisema anahitaji msaada kwani mwili huo bado upo katika chumba cha maiti hospitali ya Mount Meru.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha, Lema pamoja na Mbowe wamesisitiza kuendelea kuwaamsha Watanzania kupigania haki zao na kamwe hawatarudi nyuma na kwamba tukio hilo limewapa nguvu ya kudai haki za Watanzania.

Lema alisema serikali ni lazima ifahamu kuwa risasi na bunduki hazitaweza kurudisha nyuma harakati za kudai maisha bora kwa Watanzania na kwamba wataendelea kupigania haki za hizo kwa gharama yoyote.

“Polisi waongeze bunduki nyingi zaidi na waongeze magari mengi ya maji ya kuwasha lakini hatutarudi nyuma kudai haki za Watanzania…vijana wetu wamekufa wakipinga katiba mbovu, Dowans na mishahara duni”alisema.

Katika Ibada hiyo iliyoendeshwa na Mapdri watatu, Henry Mushi, Pamphil Ngowi na Valerian Shirima, waombolezaji walibubujikwa na machozi kila viongozi walipokuwa wakitoa hotuba zao kwa hisia.

Baadhi ya Wabunge wa Chadema waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Philemon Ndesamburo(Moshi Mjini), John Mnyika (Ubungo) na Grace Kiwelu, Lucy Owenya, Maulida Kommu ambao ni Wabunge wa Viti maalumu.

Katika Ibada hiyo, Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini ambaye alikuwa mshereheshaji, alijikuta akishindwa kujizuia na kububujikwa na machozi, na ulifika wakati akashindwa kuendelea na ushereheshaji huo.

Selasini ambaye ni miongoni mwa Wabunge wa Chadema waliokamatwa katika maandamano hayo na kushitakiwa mahakamani, alionekana mara kwa mara akifuta machozi na wakati mwingine akishikwa na kwikwi kwa uchungu.
 
Back
Top Bottom