Mbowe: Kima cha chini cha Sh. 500,000 kinawezakana | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbowe: Kima cha chini cha Sh. 500,000 kinawezakana

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 13, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 13, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.  Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema kuwa serikali ina uwezo wa kuongeza kima cha chini kwa watumishi wake kutoka Sh. 104,000 hadi Sh. 500,000 kwa kuwa ina vyanzo vingi vya mapato.
  Amesema serikali inaweza kulipa kiasi hicho ikiwa itakusanya kwa makini fedha za madini, mbuga za wanyama pamoja na mapato mengine ya ndani.
  Mbowe alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini hapa ambao pia ulihudhuriwa na wakazi wa mji wa Isebania ulioko nchini Kenya, wakiwemo vijana wanaojishughulisha na kusomba na kuvusha mizigo katika mipaka ya Sirari na Isebania.
  Mamia ya watu walifurika katika uwanja wa Tarafa ya Sirari kumsikiliza Mbowe, ambaye hotuba yake ilijikita zaidi kuzungumzia mgomo kati ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na Serikali kuhusiana na mgomo ulioitishwa na shirikisho hilo kuishinikiza serikali pamoja na mambo mengine, kupandisha kima cha chini kutoka Sh. 104,000 hadi Sh. 315,000.
  Mbowe alisema Sh. 104,00 hazitoshi na kwamba serikali ina uwezo wa kupandisha kima hicho hadi Sh. 315,000 ingawa inakataa kufanya hivyo.

  Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema: “Sisi Chadema tunaungana na madai ya watumishi wanaodai kuongezwa kwa mishahara yao kutoka Sh. 104,000 hadi Sh. 315,000 kwani maisha ya sasa kiasi hicho kwa mtumishi kimepitwa na wakati, hiyo ni nauli tu bado chakula na mavazi na kusomesha watoto.”
  “Tukifanikiwa kuchukua utawala wa nchi hii tutawaongezeni mishahara na kima cha chini kitakuwa laki tano, kwani hakuna uwiano wa mishahara hapa nchini. Polisi hawa mnaowaona hapa analipwa Sh. 150,000 huku akilinda raia na mali zao, TRA wanalipwa hata mfagiaji zaidi ya laki nne haki iko wapi?” alihoji huku akishangiliwa na wakazi wa kitongozi cha Nyamorere na kuongeza: “Watumishi msiipe kura CCM.
  Hivi sasa Tucta na Serikali bado wanavutana huku serikali ikisema haiko tayari kulipa Sh. 315,000 kwa maelezo kuwa ni fedha nyingi wakati Tucta inasisitiza kuwa fedha hizo zinaweza kulipwa ikiwa serikali itapunguza matumizi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato yake.
  Mei 4, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alilihutubia Taifa kupitia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam na kutamka kuwa mgomo wa Tucta uliokuwa umeitishwa Mei 5 ni batili kwa kuwa uliitishwa wakati majadiliano kati ya Tucta na serikali yakiendelea.
  Rais Kikwete aliwashutumu viongozi wa Tucta kwa kutowaeleza ukweli wanachama kuhusiana na suala zima la mazungumzo na uwezo wa serikali kulipa kiwango hicho.
  Licha ya Tucta kuusitisha mgomo huo Mei 5 kwa ajili ya kusubiri Mei 8 ambayo ilikuwa tarehe ya kukamilisha majadiliano hayo, bado pande hizo hazijafikia mwafaka.
  Katika hatua nyingine, Mbowe alisema kuwa Chadema haina chuki na Jeshi la Polisi bali adui yao ni wale wanaowatuma Polisi kuwanyanyasa wananchi kwa kuwakamata bila makosa.
  Mwenyekiti huyo pia ambaye alifika wilayani Tarime kwa ziara ya siku tatu kwa ajili ya kufanya mikutano, alitoa kauli hiyo baada ya kada wa Chadema, Mwita Waitara Mwikwabe, kumweleza kuwa baadhi ya wenyeviti wa vijiji vinne wa Chadema wilayani hapa wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za mauaji na wizi wa mifugo.
  Waitara alidai kuwa wenyeviti waliokamatwa ni kutoka vijiji vya Ganyange, Ngerengere , Kembwi na Manga.
  Katika Ziara hiyo, Mwenyekiti huyo wa Chadema aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Tarime, Charles Mwera; Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mara, Mwikwabe Machage; Mwenyekiti Kitengo cha Wanawake Taifa, Ghati Masole; Mwenyekiti wa Walemavu Chadema Taifa, Shida Salumu na kada wa chama hicho, Benson.
  CHANZO: NIPASHE

  Hata mimi nakubaliana na Mheshimiwa Mbowe kuwa kima cha chini cha Sh. 500,000 kinawezakana umesema kweli mheshimiwa mbowe Ubarikiwe Yes We Can.
   
Loading...