Mbeya makanisa lundo, uhalifu kibao - Miaka 50 ya Uhuru | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mbeya makanisa lundo, uhalifu kibao - Miaka 50 ya Uhuru

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Nov 10, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Nov 10, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145

  Miaka 50 ya Uhuru


  Felix Mwakyembe

  [​IMG]


  Kandoro asifia miundombinu ya usafiri

  Uzalishaji kilimo umepanda, bei bado duni
  Elimu yapanda, vyuo, shule vyaongezeka
  TBL, Coca Cola, Pepsi, Saruji vyapandisha ajira

  TATHMINI ya jumla inaonyesha kuwapo kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa mkoani Mbeya ndani ya miaka 50 ya Uhuru, ambayo hata hivyo yameibua pia changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi.

  Maendeleo hayo yanajibainisha katika sekta mbalimbali zikiwamo za elimu, afya, maji, barabara, majengo, viwanda na shughuli nyingine za kiuchumi.


  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kwa upande wake, anayaelezea mabadiliko hayo kwa kulinganisha hali ilivyokuwa mwaka 1961 na ilivyo leo hii.


  "Ni maeneo machache tu ya Uzunguni, Uhindini, Majengo na Sokomatola, basi, yalikuwa na nyumba za bati za kuhesabu," anasema Kandoro katika taarifa yake ya miaka 50 ya uhuru kwa Mkoa wa Mbeya.


  Pamoja na majengo, Mkuu huyo wa Mkoa vile vile anaonyesha kuwepo kwa mabadiliko makubwa tangu uhuru kwa kurudisha taswira ya miaka 50 iliyopita kwenye sekta ya usafiri, anaposema, "Watu waliozaliwa miaka 20 au hata 30 iliyopita yawezekana wasiamini kwamba safari ya Mbeya hadi Iringa ilikuwa inachukua siku mbili."


  Pamoja na kuirudisha taswira ya hadhi ya majengo, ukubwa wa mji wa Mbeya na usafiri ulivyokuwa mwaka 1961, wakati Tanganyika inapata Uhuru, bado kwa walio wengi inawawia vigumu kuamini kutokana na ukweli kwamba wamezaliwa na kukuta masaibu yote hayo yalikwishakupotea na kilichobakia ni simulizi za kihistoria, kikubwa wanachokiangalia wao ni changamoto zinazowakabili.


  Miongoni mwa changamoto zinazobainishwa na wakazi wa Mkoa huo ni pamoja na uharibifu wa mazingira na mipango miji huku Jiji la Mbeya likielezwa kuongoza katika uharibifu huo kiasi cha kupoteza fahari yake ya ukijani iliyoshawishi wengi wauite "The Green City" au Jiji la Kijani.


  Misitu yote iliyopamba jiji hilo pamoja na vilima vyake imepotea, milima yote leo hii iko wazi tofauti na ilivyokuwa miaka 50 iliyopita ambapo ilipambwa kwa rangi ya kijani kutokana na kufunikwa na miti.


  Matokeo ya uharibifu huo ni kuongezeka kwa joto katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo pamoja na ugonjwa wa malaria, maeneo ambayo huko nyuma yalikuwa na baridi kali huku yakipata mvua kwa kipindi kirefu cha mwaka.


  Kutokana na uharibifu huo mkubwa wa mazingira uliotokea katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Wilaya za Rungwe, Mbeya Mjini na Vijijini ambazo huko nyuma wakazi wake hawakuwahi kuona mbu, sembuse kuugua malaria kutokana na hali ya hewa ya baridi kali iliyokuwapo wakati huo, leo hii wamekuwa miongoni mwa jamii zenye kusumbuliwa na malaria.


  Pamoja na uelewa ulipo hivi sasa kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira bado viongozi wanafumbia macho tatizo hilo huku baadhi wakiwa sehemu ya uharibifu huo, kwa kutoa vibali vya watu kukata miti pamoja na kuruhusu kulima maeneo ya milimani kinyume cha sheria za nchi.


  Mbali ya mabadiliko ya hali ya hewa, uharibifu wa mazingira ya mkoa huo umesababisha kukauka kwa mito mingi, hususani wilayani Chunya, Mbarali na Mbeya, kulikochangiwa na ukataji miti na kilimo kwenye vyanzo vya maji.


  Changamoto nyingine inayotokana na maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka 50 ya uhuru, ni kuongezeka kwa makazi holela ndani ya Jiji la Mbeya kunakochangiwa zaidi na viongozi wa jiji hilo.


  Maeneo yanayotajwa katika tathmini ya Mkuu wa Mkoa yaliyokuwepo mwaka 1961, pamoja na uduni wa majengo yake wakati huo, bado yako kwenye mpangilio mzuri tofauti na maeneo yaliyopimwa baada ya uhuru, hususan kuanzia miaka ya themanini.


  Pamoja na kupimwa, maeneo mapya kama yale ya Forest, Block T, Soweto, Block Y na hata Ikulu, ramani zake zimeharibiwa ambapo baadhi ya sehemu hadi barabara zimefungwa na hata viwanja vya michezo kwa watoto vimejengwa nyumba.


  Mkuu wa Mkoa Kandoro anakiri kuwapo kwa uharibifu wa mazingira ya mkoa huo pamoja na mipango miji ya Jiji la Mbeya, ambapo akijibu swali kuhusu uvamizi katika eneo lililotengwa awali kujengwa Ikulu ndogo anasema,


  "Hatuliangalii in isolation, lipo tatizo la uvamizi wa maeneo mbalimbali katika jiji letu, tunaliangalia tatizo hilo pamoja na jiji."


  Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Juma Iddi aliambia Raia Mwema kwa njia ya simu kuwa hawajabadili matumizi ya maeneo yaliyopimwa kwa madhumuni maalum ikiwamo ilipokuwa ijegwe Ikulu Ndogo, maeneo ya wazi na madimbwi.


  Kuhusu maeneo ambayo yamevamiwa anasema kuwa yapo yaliyohalalishwa lakini yapo pia ambayo hayajahalishwa hivyo sheria itakuchukua mkondo wake.


  Pamoja na ukongwe wake, Mkoa wa Mbeya hauna ofisi za Mkoa zenye hadhi ikilinganishwa na majirani zake wa Iringa, Ruvuma na Rukwa. Ofisi za Mkoa bado zimo kwenye majengo ya zamani ambayo hata kuyakarabati ni hasara tupu.


  Mikakati ya kujenga upya ofisi hizo ipo kwa zaidi ya miaka 20 sasa, ambapo kila awamu ya uongozi wa Mkoa imekuwa ikiahidi kukamilisha kazi hiyo lakini hadi inapondoka inaacha hadithi ile ile, na hata Kandoro naye tayari anatoa ahadi zile zile katika mahojiano yake na Raia Mwema kwa njia ya simu hivi karibuni ambapo anasema,


  "Imetengwa pesa, watu wa MIST (Mbeya Institute of Science and Technology) wanandaa michoro, Ikulu ndogo ipo tayari, residence iliyokuwa ya Mkuu wa Mkoa ndiyo Ikulu ndogo, Mkuu wa Mkoa amejengewa pembeni."


  Eneo jingine ambalo Mkoa huo umepiga hatua kubwa lakini halitajwi katika tathmini ya Mkoa ni pamoja na ongezeko la makanisa, inakadiriwa kuwa Jiji la Mbeya ni la pili baada ya Lagos, Nigeria kwa kuwa na makanisa mengi.


  Ongezeko la makanisa mkoani humo linaenda sambamba na kasi ya ongezeko la vitendo vya uhalifu na ushirikina, vitendo ambavyo vinajenga taswira chafu ya Mkoa iliyo tofauti na tamaduni za wakazi wake, na hii inatajwa kuwa changamoto kubwa kwa Mkoa huo kwamba hata baada ya miaka 50 ya Uhuru bado watu wake wamezama kwenye dimbwi la ushirikina na uhalifu pamoja na wingi wa makanisa uliopo.


  Pamoja na changamoto hizo, bado mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali mkoani humo yanathibitisha maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka 50 ya Uhuru na yanaelezwa kwa kifupi sana na Mkuu wa Mkoa Kandoro akisema,


  "Miaka 50 iliyopita Mbeya haikuwa hivi."


  Miongoni mwa maeneo yaliyobadili sura ya Mbeya ni pamoja na barabara ambapo tathmini inaonyesha kuwa mkoa huo haukuwa na hata kilometa moja ya barabara ya lami tofauti na leo hii ambapo kuna kilometa 833.95, changarawe kilometa 6,160.08 na udongo kilometa 3,518.65.

  Tathmini hiyo inaonyesha pia kuwa asilimia 58 ya wananchi waishio vijijini mkoani humo wanapata maji safi na salama, na kwa Jiji la Mbeya ni asilimia 89.6 kutoka asilimia tano wakati nchi inapata uhuru.

  Katika sekta ya elimu, tathmini ya Mkoa inabainisha kuwepo ongezeko kubwa la shule za msingi, sekondari na vyuo mkoani humo ikienda sambamba na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga nazo na kuhitimu.


  Mathalani, wakati mwaka 1961 Mkoa wa Mbeya ukiwa na shule nne tu za sekondari ambazo ni Iyunga, Sangu, Loleza na Rungwe, leo zipo 298 zikiwemo 19 za kidato cha tano na sita, huku zingine 53 zikiwa ni za watu binafsi na mashirika ya dini.


  Pato la wastani la mwananchi mkoani humo limekuwa kutoka shilingi 1,841 mwaka 1980 hadi 895,366 mwaka 2010.


  Hata hivyo ongezeko hilo la pato la mwananchi linaelezwa kuchangiwa zaidi na viwanda vilivyopo mkoani humo ambavyo ni pamoja na Saruji, Tanzania Breweries ltd, PEPSI, Coca Cola na viwanda vidogo vidogo.


  Mkoa wa Mbeya bado unafanya vema katika uzalishaji wa mazao ya kilimo ambapo katika msimu uliopita wa 2010/2011 mkoa huo ulizalisha tani milioni 3.3 za chakula, wakati mahitaji yake ni tani 750, 677 hivyo kuwa na ziada ya tani milioni 2.5.


  Hata hivyo pamoja mchango mkubwa wa wakulima wa Mkoa huo katika uzalishaji chakula nchini, bado hawajaweza kunufaika na jasho lao kutokana na bei ndogo inayotolewa na soko la ndani kwa mazao ya wakulima.


  Pamoja na kuadhimisha miaka 50 ya uhuru, bado kilio cha wananchi wa Mkoa huo kinaendelea kuwa soko lisilo rafiki wa jasho lao.


   
 2. SILENT WHISPER

  SILENT WHISPER JF-Expert Member

  #2
  Nov 10, 2011
  Joined: Jun 26, 2009
  Messages: 2,231
  Likes Received: 53
  Trophy Points: 145
  basi bomboa haya makanisa ..jenga misikiti
   
 3. Mamndenyi

  Mamndenyi JF-Expert Member

  #3
  Nov 10, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 29,046
  Likes Received: 6,492
  Trophy Points: 280
  mimi sitaki ugomvi na IGWE,
  napita njia.
   
Loading...