Mbetto: Ilani ya CCM imetekelezwa asilimia 99% miaka mitatu ya Dkt. Mwinyi

Hamduni

Senior Member
Apr 25, 2020
155
108
Unguja. Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk Hussein Mwinyi inatekeleza miradi yake kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakati leo Rais Mwinyi akitimiza miaka mitatu madarakani, CCM inaridhika kwa kiasi kikubwa jinsi ilani inavyotekelezwa na kiongozi huyo katika sekta mbalimbali za elimu, maji, afya, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu ofisini kwake Makao makuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM, Khamis Mbetto anasema kwa kipindi cha uongozi wa Dk Mwinyi ametekeleza ilani kwa vitendo na miradi yote inaonekana kwa macho sio tu kwa mdomo.

Mbetto anasema kitu cha kipekee na cha kushangaza katika utawala wa Dk Mwinyi, amehakikisha anagusa kila sekta “kuna viongozi waliingia madarakani wakashughulika na sekta moja tu.”

“Mambo mengi yamefanyika kwa kipindi kifupi cha utawala wake, Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 mpaka sasa imetekelezwa kwa asilimia 99,” anasema Mbetto

Elimu
Akizungumza kuhusu sekta ya elimu, Mbetto anasema ilani ilielekeza wahakikishe inaongezwa miundombinu ya elimu kwa maana ya majengo, walimu vifaa na maslahi ya walimu.

Anasema kwa kipindi cha awamu ya nane tayari serikali imejenga maghorofa tisa “lengo kuhakikisha tunakwenda kwenye darasa wasizidi 40 wakati Dk Mwinyi anaingia madarakani alikuta darasa moja linakaliwa na wanafunzi zaidi ya 80.”

Anasema kwamba baada ya kukamilika maghorofa hayo, sasa serikali inajenga majengo mengine 21.

Pia serikali imejenga shule zenye mahitaji maalumu takribani tano; Unguja tatu na Pemba mbili na serikali imejenga kila wilaya vyuo vya amali ili kuendeleza vipaji vyao.

Pia katika elimu imeimarishwa taaluma kwa kutoa vibali vya kuajiri ambapo tayari matokeo yameanza kuonekana kwa kuongeza ufaulu na kupunguza sifuri katika matokeo. Hilo linapimwa katika matokeo ya kidato cha sita ya mwaka huu ambapo hakukuwa na sifuri.

Serikali imeongeza fedha katika bodi ya mikopo na hakuna mtoto kwasasa atakuwa na sifa ya kusoma akakosa mikopo.

Mbetto anasema shule hizi zimesheheni vifaa vyote vikiwamo vitabu vya sayansi, sanaa na maabara za kisasa. “Kwa maana hiyo sekta ya elimu tumepiga hatua na kwenye ilani tumefikisha asilimia 120.”

Afya
Mbetto anasema sekta ya afya pia imeboreka akitolea mfano hospitali za Mnazimmoja Unguja na Abdalla Mzee Pemba ambazo zilikuwa ndio hospitali pekee zinazotegemewa katika huduma lakini kwa sasa hali imeanza kubadilika baada ya kujengwa hospitali za kisasa za Wilaya 10 na mbili za Mkoa.

Mbetto anasema tiba zilikuwa hazitolewi vyema lakini kwa sasa hospitali hizi zinavifaa vyote vya kisasasa ikiwemo X ray, CIT Scan, MRI na mgonjwa anayetaka rufaa kutoka katika hospitali ya wilaya kwenda Mnazimmoja au hospitali zingine nje ya Zanzibar, mojakwa moja taarifa zake zinakwenda kule kupitia njia ya mtandao.

“Kwa maana hiyo pia tumeboresha sana sekta ya afya na zaidi tumeajiri madaktari bingwa zaidi ya 350 lengo mwananchi asipate shida kupata huduma za afya,” anasema

Katika kutoa huduma bora serikali imetafuta kampuni binafsi inayolipwa kutoa baadhi ya huduma zikiwemo dawa, zamani upatikanaji wa dawa katika hospitli ilikuwa changamoto.

Barabara
“Kwakweli katika sekta hii mtandao wa barabara wote wa Unguja zaidi ya kilomita 275.9 na zingine kilomita 279 kwa mjumuiko wa barabraba za mjini na vijijini, unaona jinsi ambazo zimejengwa ambazo hata hazikutarajiwa kujengwa,”

“Tuna barabara kubwa ya kilomita 48.9 Tunguu Makunduchi imeanza kujengwa na nyingine ya Chake Wete Pemba ambazo serikali imelipa fidia zaidi ya Sh9 bilioni kwa wananchi kupisha ujenzi huo na imelipa Sh800 milioni kwa ajili ya vipando (mazao).

Kuna barabara kutoka ChakeChake hadi Mkoani yenye kilomita 45.8 tayari upembuzi yakinifu umekamilika na kuna barabara za Kiboje, Charawe na Mikongoroni.

Mbetto anasema kuna barabara itakayojengwa ya kilimita 11 kutoka kitogani Paje, nyingine kutoka Makunduchi mpaka Kizimkazi kilomita 13 itajengwa.

Kwa upande wa bandari, inajengwa bandari ya Kizimkazi na bandari jumuishi ya Mangapwani. bandari ya Wete, ikishajengwa mizigo yote itakuwa inakwenda moja kwa moja Pemba.

Mbetto anasema “lakini tunajenga bandari nyingine ya Shumbamjini ambayo itakuwa inasaidia mizigo kwa ajili ya Tanga na Pemba.”

Katika usafiri na usafirishaji, serikali inakarabati meli ya Mapinduzi II kutoa huduma katika kisiwa cha Pemba na Dar es Salaam huku ikiwa na mkakati wa kununua boti za mwendo kasi.

Michezo
Serikali inajenga viwanja vya michezo vya kisasa kila wilaya huku ikikarabati uwanja wa Amani ambao umeingia katika viwango vya shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Alisema uwanja wa Amani utakuwa na michezo jumuishi ya judo na kuogelea na vingine vingi na pale maisara vinajengwa viwanja vya kisasa.

Uwezeshaji
Mbetto anasema katika sekta hiyo tayari serikali imeshatoa zaidi ya Sh50 bilioni kuwezesha wananchi kupata mikopo na vifaa kama boti, wajasirimali na wafanyabiashara wadogowadogo.

“Kwa maana hiyo serikali imegusa kila eneo naona inavyojenga masoko ya kisasa kabisa na vituo vya wajasiriamali 12 katika kila halmashauri na wilaya,” anasema

Mbetto alizungumzia soko la Mwanakwerekwe ambalo alidai tayari limefikia asilimia 80 ujenzi wake kukamilika na masoko ya Jumbi, Mbuzi na soko la mbogamboga kwa mchina huku Machomane Pemba kukijengwa soko pia.

Utaona jisni maendeleo yalivyotamalaki kila eneo

Uchumi wa buluu
Anasema katika kutekeleza ilani ya CCM, limejengwa soko la samaki la Malindi na Tumbe Pemba katika uwezeshaji wananchi

Katika kuupamba mji “tunajenga basi terminal pale Kijangwani na ujenzi unaendelea na tunajenga maegesho makubwa eneo la Malindi ili kuondosha maegesho ya kila eneo kwenye mji.”

Umeme
Katibu Mbetto anasema zaidi ya vijiji 48 ambavyo havikuwa na umeme tayari vimefikiwa na huduma hiyo, lakini kwa wastani, vijiji 65 vimefikiwa huduma hiyo.

Zamani Mwananchi alikuwa ananunua nguzo kwa Sh1 milioni lakini Rais Mwinyi ameondosha gharama hizo na hivyo Mwananchi akitaka kuungiwa umeme nguzo ni bure.

Pia amepunguza gharama ya kuungiwa umeme kutoka Sh400,000 hadi Sh200,000.

Wazee
Wapo wazee waliokuwa katika mfumo rasmi na wengine hawakuwa katika mfumo rasmi, kulikuwa na pensheni jamii waliokuwa wanalipwa Sh20,000 kila mwezi kwasasa Dk Mwinyi ameongeza kiwango hicho wanalipwa Sh50,000 sawa na asilimia 150.

Na amepanidha pensheni ya kawaida ya watumishi kwa asilimia 100. Haya ni mafanikio makubwa lazima tuseme na kumtia moyo Dk Mwinyi, katika ilani, Serikali imefanya vizuri na kuvuka malengo kila unapokwenda lazima uone alama,”

Maji
Mtandao mzima wa maji umefanyiwa marekebisho zaidi Qubiki lita za ujazo milioni 10, yamejengwa matangi makubwa na kujenga miundombinu ya kuunganisha na kusambaza maji hayo kwa wananchi.

Mbetto anasema kutokana na utekelezaji wa ilani, hata wapinzani wamekosa hoja.

“Kwasasa ukiangalia hoja hakuna, wanasema fisadi lakini miradi mingi inatekelezwa, Dk Mwinyi anafanya vitu vizuri hata kama kuna watu hawampendi lakini pendeni anayofanyia wananchi,” anasema

Mwisho.

IMG-20231102-WA0150.jpg
 
Back
Top Bottom