Mawaziri wapya hawana la kufurahia


MziziMkavu

MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Messages
40,027
Likes
5,488
Points
280
MziziMkavu

MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined Feb 3, 2009
40,027 5,488 280

Maoni ya katuni


Jana Rais Jakaya Kikwete aliwaapisha mawaziri na naibu mawaziri ambao aliwateua katika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri aliyoyatangaza Ijumaa iliyopita.
Katika sherehe za kuapishwa zilizofanyika kwenye viwanja vya Ikulu, wawaziri waliokula kiapo chao mbele ya rais ni pamoja na wanane wa zamani walioteuliwa kuongoza wizara nyingine, mawaziri saba wapya, naibu mawaziri sita waliobadilishwa wizara pamoja na naibu mawaziri 10 wapya.
Haya ni mabadiliko ya pili ya mawaziri kufanywa chini ya utawala wa awamu ya nne baada ya yale ya mwaka 2008 yaliyofikiwa baada ya Baraza la Mawaziri kuvunjika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Mabadiliko hayo ndiyo yalimuinua Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, lakini pia yakiwaweka pembeni mawaziri wengine watatu, ambao ni Nazir Karamagi aliyekuwa Nishati na Madini; Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Zakia Meghji aliyekuwa Waziri wa Fedha.
Mabadiliko yaliyofanyika wakati ule yalitokana na kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa dharura uliotolewa kwa njia zenye maswali mengi kwa kampuni ya Richmond.
Ni baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kamati teule ya Bunge Waziri Mkuu aliamua kujiuzulu akifuatiwa na mawaziri waliohudumu Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Msabaha na Karamagi.
Kwa bahati mbaya tena, mabadiliko ya mwaka huu hayakufanyika hivi hivi tu, ni matokeo ya kushindwa kuwajibika kwa baadhi ya watumishi wa umma, wakiwamo mawaziri sita walioachwa. Kushindwa kuwajibika huko kumedhihirika katika ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10.
Lakini pia taarifa za kamati za kudumu za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu wa Mashirika ya Umma (POAC).
Kwa maana hiyo, mawaziri wapya ni lazima wajue kwamba wamepewa kazi mpya yenye changamoto kubwa. Kwamba wameteuliwa kutoka miongoni mwa mamilioni ya Watanzania wenye sifa za kupewa majukumu hayo, lakini wao wamebahatika.
Ni kwa jinsi hii wakati tukiwatakia kila la kheri katika majukumu yao mapya, tungependa viongozi hawa wapya wajione kwanza kama watu waliobahatika, lakini la muhimu zaidi watu waliobebeshwa mzigo mkubwa na mzito katika kuwatumikia wananchi.
Ni hakika watangulizi wao katika nafasi hizo kama wanagelitimiza wajibu wao sawa sawa kusingelikuwa na mabadiliko haya. Na hili ndilo linahitaji kuwa moja ya angalizo kubwa kwa mawaziri wapya, kwamba wanatarajiwa waonyeshe tofauti na watangulizi wao kwa vitendo halisi vya uwajibikaji vyenye tija.
Sababu za kung’oka kwa mawaziri hawa ni utendaji mbaya katika kusimamia matumzi bora ya fedha za umma na wengine kuhusika moja kwa moja kujinufaisha binafsi na ofisi za umma kinyume kabisa cha viapo vyao, kwa kifupi mawaziri hawa wameshindwa kusaidia serikali kutumiza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.
Ndiyo maana sisi tunasema katika mazingira kama haya, inapokuwa unapewa kazi ambayo imemshinda mtu hakika watu wanakutegemea uonyeshe kuwa unaweza na unafaa kuliko mtangulizi wako, ndiyo kusema kwamba mawaziri wapya hawana sababu ya kufurahi, ila wanapaswa kutambua kuwa wana mzigo mzito wa kubeba ili nao wasitoke kama waliowatangulia.
Kitendo cha serikali kukubali kuchukua hatua juu ya ripoti ya CAG kwa hakika kimefungua ukurasa mpya juu ya ofisi hii muhimu ya kusimamia matumizo bora ya kodi za wananchi. Si mara moja wala mara mbili kwamba CAG amekuwa akitoa ripoti chafu ya matumizi kuliko hii ya mwaka 2009/10; kwa miaka na miaka ripoti hizi zimekuwako, nyingine chafu zaidi. Lakini kwa sababu za kizembe tu hakuna hatua zozote za kuwajibishana zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
Ndiyo kusema kuwa mawaziri hawa wajue kuwa kazi ya CAG ni ya kudumu, si kazi ya kamati teule au tume, ni kazi ya kudumu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 143. CAG haombi ruhusa kukagua mahesabu yoyote katika ofisi ya umma.
CAG ataendelea kuwako na atafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria mwaka hadi mwaka na kutoa ripoti ambayo itafikishwa bungeni mwaka hadi mwaka.
Katika mazingira hayo, mawaziri wapya hawana jinsi, hawana sababu ya kusheherekea nafasi hizo mpya, ila wanapaswa kuwaza jinsi ya kuleta tija, kuonyesha tofauti kati yao na watangulizi wao, vinginevyo taarifa ya CAG itakuwa inawasubiri wasinzie na kuzembea ili wakumbwe na kimbunga kama kilichowakuta watangulizi wao.

CHANZO: NIPASHE

 

Forum statistics

Threads 1,273,856
Members 490,528
Posts 30,493,607