Mauaji ya kinyama sasa yaandama makada CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mauaji ya kinyama sasa yaandama makada CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Zak Malang, May 17, 2010.

 1. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #1
  May 17, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Mauaji ya kinyama sasa yaandama makada CCM

  Na Waandishi wetu, NIPASHE

  Limeibuka wimbi la mauaji ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mazingira yanayoacha shaka kwamba huenda kuna mikono ya kisiasa katika vitendo hivyo.

  Wakati wakazi wa Jiji la Mwanza wapo katika simanzi kubwa ya kumpoteza Katibu wa CCM Kata ya Isamilo, Bahati Stephano (49), aliyeuawa kikatili kwa kuchomwa kisu ofisini kwake na mtuhumiwa aliyetambuliwa kwa jina la Jummane Oscar (30), Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Salama A, kata ya Salama wilayani Bunda, Messo Kubuka (46), kupitia CCM naye ameuawa kinyama baada ya kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana.

  Imedaiwa kuwa Mwenyekiti huyo alikutwa na mauti hayo baada ya kutoka katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Bunda ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.

  Imedaiwa kwamba marehemu alikuwa mtu wa karibu na Wasira na amekuwa akiratibu shughuli mbalimbali za kisiasa za Waziri Wasira kama mbunge.

  Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Salama, Mramba Simba, alisema kuwa marehemu aliuawa wakati akitoka kwenye kibanda chake cha biashara akielekea nyumbani kwake.

  Simba, alithibitisha kuwa kabla ya mauaji hayo, Mwenyekiti huyo jioni alishiriki kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Wasira. Tukio hilo ambalo limeibua mjadala mkubwa, linadaiwa kutokea Mei 14, mwaka huu majira ya saa 3 usiku katika kitongoji cha Gabarawa kijijini hapo ambapo watu wasiofahamika idadi walimkatakata kichwani, begani, shingoni na kidole kisha kupoteza fahamu na kufariki dunia papo hapo.

  Habari za uhakika zilizothibitishwa na uongozi wa wilaya hiyo wakiwemo polisi, zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo alikutwa na mauti akiwa anaelekea kwake katika kitongoji cha Mumwalo njiani eneo la kichaka lililopandwa katani. Polisi wilayani hapa wamethibitisha kuuawa kwa mwenyekiti huyo na maiti yake kukutwa asubuhi karibu na eneo la nyumbani kwake. Mmoja wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo, alisema pembeni mwa maiti hiyo walikuta pikipiki ya mwenyekiti huyo.

  Alisema baada ya askari kumpekua, walimkuta akiwa na Sh. 3,000 kwenye mfuko wake wa suruali. Ofisa huyo, alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. “Polisi wameanza upelelezi wa tukio hili ili kujua chanzo cha mauaji hayo,” alisema.

  Wanakijiji kadhaa waliozungumza na mwandishi wa gazeti hili, walisema kuwa aliyeuona mwili wa marehemu ni Mwenyekiti wa zamani wa serikali ya kijiji hicho, Julius Wesaka, wakati anakwenda dukani kwake majira ya saa 11 alfajiri.

  “Alipiga kelele na watu kukusanyika, kwa kweli ilikuwa inashtua jinsi alivyokuwa amekatwa huku suruali yake imelegezwa mkanda, huenda walichukua fedha kwa kuwa alikuwa mfanyabiashara wa ng’ombe, walikuwa wamepasua taa kubwa ya pikipiki yake aina ya Toyo,” alisema mmoja wa wanakijiji waliofika eneo la tukio.

  Baadhi ya wanakijiji walisema kuwa kifo hicho kinahusishwa na mambo ya kisiasa kwa kuwa alikuwa ni mpambe wa karibu wa Mbunge Wasira na siku hiyo alikuwa akifuatana na msafara wa Wasira katika mikutano yake katika maeneo kadhaa. Walisema kuwa siku hiyo walimaliza mkutano wa hadhara kijijini hapo na baadaye aliongozana na msafara wa Waziri Wasira katika maeneo mengine, likiwemo Kurusanga na kurudi jioni.

  Hata hivyo, wapo wanaodai kuwa huenda mauaji hayo yanatokana na sababu za kibiashara kwa kuwa marehemu alikuwa akinunua ng’ombe na kuuza kwenye minada.

  Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwake. Hadi jana, hakuna mtu alikuwa amekamatwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo, ingawa polisi walisema kuwa wanaendelea na msako dhidi ya waliohusika.

  Waziri Wasira alipotafutwa jana kuzungumzia tukio hilo, simu zake zote mbili za kiganjani zilikuwa zikiita bila kupokelewa.

  Hilo ni tukio la pili kwa makada wa CCM kuuawa katika mazingira ya kutatanisha na kikatili katika kipindi cha wiki moja, huku pia kukiwa na hisia zenye utata juu ya kifo cha Nsega Aloyce Ntobi (45) ambaye pia alikuwa kada wa CCM eneo la Pasiansi, jijini Mwanza. Marehemu anadaiwa kwamba alikuwa na mpango wa kugombea ubunge, lakini alianza kuugua ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

  Marehemu Nsega alizikwa juzi kijijini kwao Nsola jimbo la Busega alikokuwa anataka kuwania ubunge.

  Naye Bahati aliuawa kikatili Ijumaa iliyopita kwa kuchomwa kisu tumboni akiwa ofisini kwake. Tukio hilo lilitokea siku hiyo majira ya saa 6:15, muda mfupi baada ya kuwasili ofisini kwake.

  Bahati alifariki dunia baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
   
Loading...