Matokeo Kidato cha Tano ufaulu umeongezeka? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Matokeo Kidato cha Tano ufaulu umeongezeka?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Luteni, Mar 19, 2010.

 1. Luteni

  Luteni JF-Expert Member

  #1
  Mar 19, 2010
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 2,274
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 0
  WANAFUNZI 33,662 kati ya 39,189 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana na kufaulu, wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano katika shule za Serikali na vyuo vya ufundi.

  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, alisema jana kuwa idadi hiyo ambayo ni asilimia 85.90 ya waliokuwa na sifa za kujiunga na kidato cha tano, inajumuisha wasichana 12,622 ikilinganishwa na 12,349 waliojiunga na kidato cha tano mwaka jana.

  Profesa Maghembe alifafanua kuwa wanafunzi wa kike karibu wote wenye sifa wamepata nafasi katika shule za Serikali na kwamba wanafunzi waliobaki 146 ambao ni asilimia 1.24 walikuwa na sifa; lakini masomo waliyofaulu hayakutengeneza unganisho (combination) lolote la masomo katika yanayofundishwa.

  Kwa upande wa wanafunzi waliojiunga na vyuo vya ufundi mwaka huu ambao ni 897 wasichana ni 16 tu, idadi ambayo ni sawa na asilimia 1.78. “Idadi hii ni ndogo, lakini hao ndio waliochagua fani hiyo au kuwa na sifa za kutosha kuchukua masomo ya ufundi,” alisema.

  Alisema waliohitajika kwenye vyuo hivyo walitakiwa kufaulu masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati, “wasichana wengi hawakufaulu masomo haya au walichagua kwanza kusoma kidato cha tano badala ya ufundi.”

  Profesa Maghembe alisema wanafunzi 13,288 wamepangwa kusoma masomo ya Sayansi mwaka huu, idadi ambayo ni sawa na asilimia 40.56 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano.

  “Idadi ya wanafunzi wanaochukua Sayansi inalenga kutosheleza nafasi za masomo ya Sayansi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wanapomaliza ngazi hii ya elimu,” alisema.

  Profesa Maghembe alisema wanafunzi wengi wa kike wamepangiwa kusomea kwenye maunganisho ya masomo ya Historia Jiografia Fasihi (HGL-wanafunzi 2,790), Historia Kiswahili Fasihi (HKL-1,782), Kemia Biolojia Jiografia (CBG-1,522), Historia Jiografia Kiswahili (HGK-1,512) na Fizikia Kemia Biolojia (PCB-1,304).

  Idadi hiyo inaonesha kuwa wasichana 4,112 wamepangiwa kusoma Sayansi ambayo yako kwenye muunganiko wa PCB na CBG. Idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 29.19 ikilinganishwa na 3,183 waliochaguliwa kwa masomo hayo mwaka jana.

  Kwa upande wa wavulana, wengi wamepangiwa Fizikia Kemia Hisabati (PCM-3,417), PCB (2,973), HGL (2,673), HKL (2,430) wakati HGK ni 2,365.

  Profesa Maghembe alisema wavulana waliopangiwa kusoma Sayansi ni 9,176 idadi ambayo ni sawa na asilimia 45.56 ya wanafunzi wote wa kiume waliopangwa kidato cha tano mwaka huu.

  Kuhusu wanafunzi 6,643 wenye sifa ya kupangwa kidato cha tano au vyuo vya ufundi, lakini hawakupata nafasi katika uchaguzi huo wa awali, Waziri alisema wana nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano katika shule mpya za Serikali zinazotarajiwa kufunguliwa kabla ya Mei mwaka huu.

  Fursa nyingine kwa wanafunzi hao ni kujiunga na kidato cha tano katika shule za binafsi. Waziri alisema kuna shule 303 za binafsi zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 16,000 ambazo baadhi yao tayari zimeanza masomo na baadhi ya wanafunzi ni ambao hawakupata nafasi katika shule za Serikali.

  Lakini Profesa Maghembe alisema wanafunzi hao wanaweza kujiunga na kidato cha tano katika shule za Serikali ili kujaza nafasi zitakazoachwa na waliochaguliwa chaguo la kwanza; lakini hawakuripoti katika shule hizo badala yake wamejiunga na za binafsi.

  Wanafunzi hao pia wanaweza kujiunga katika vyuo vya ualimu kusomea ualimu wa cheti daraja la tatu A ambako kuna nafasi 6,000 kwa ajili ya wahitimu wa kidato cha nne.

  Wanafunzi 41,363 wa Tanzania Bara walikuwa na ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu, hata hivyo baadhi yao hawakuwa na sifa zote zilizotakiwa kujiunga na kidato cha tano.
   
 2. Luteni

  Luteni JF-Expert Member

  #2
  Mar 19, 2010
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 2,274
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 0
  MODS naomba ubadilishe heading iwe Matokeo kidato cha Nne badala ya Kidato cha Tano
   
Loading...