MATOKEO HUHALALISHA MBINU au MBINU HUHALALISHA MATOKEO?

Izack Mwanahapa

JF-Expert Member
Apr 21, 2011
497
236
Kuna mazingira yanayonipa wasiwasi sana kwa namna mambo muhimu kwa mustakabali wa taifa na mikoa yake, yanavyoendesha katika awamu ya tano. Inaniumiza kwamba nia, dhamira, na malengo mazuri kabisa ya kufikia matokeo yanayotakiwa yanaharibiwa kwa mbinu (hila, fikra, ubabe, uonevu ) za ovyo kabisa.

Nasikitishwa zaidi na sisi, wenye kuyaona manufaa ya nia, dhamira na malengo mazuri, tunapotekeleza au kutetea mbinu hizo za ovyo kwa kimvuli cha the end justifies the means. Viongozi wetu, kwenye nchi ya utawala wa sheria (siyo wa kidikteta), wanafanya mambo huku wakitoa kauli za “kutokubali kuyumbishwa” na “kuwashughulikia watakaojaribu kukwamisha”, n.k. kwa misingi kwamba matokeo yatahalalisha mbinu.

Ni jambo la busara kujiwekea kanuni na malengo na kukataa kutetereka au kuyumbishwa na wasio na nia nzuri kwako. Lakini ukumbuke pia ili kufanikiwa kwenye hilo ni sharti kuwa na upeo wa kupambanua ni wepi wenye au wasio na nia nzuri kwako. Lakini hili silo ninalolijadili hapa.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba kauli ya “the end justifies the means” ni kauli hasi, kauli ya kuhalalisha maovu katika kufikia “mazuri”. Kauli hiyo ina chimbuko lake kwa Wagiriki wa kale ambao walikuwa wakisema “Matokeo huhalalisha udhalimu”. Karne kadhaa baadae Warumi wakaitafsiri kauli hiyo kuwa “Matokeo huhalalisha matendo”. Sisi wa kileo tunakwenda na fikra kwamba: kama tumekabiliwa na tatizo kwa muda mrefu bila kuonekana ufumbuzi, basi mbinu “yoyote ile” (pasipo mipaka) itumike kutupatia matokeo tunayoyataka.

Kwa maana hiyo Hitler kutumia mbinu ya kuwaua Wayahudi ili asasi za kifedha ziwe mikononi mwa Wakristo huko Ujerumani, kulikuwa halali? Wahutu kutumia mbinu ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watusi Rwanda ili na wao washike madaraka, kulikuwa halali? Kwa maana hiyo mbinu ya kuwaachia Machinga wazagae kwenye barabara za miji ili kuzishinikiza halmashauri kuwatengea maeneo, ni halali? Kwa maana hiyo kiongozi mkuu wa ulinzi na usalama kutumia mbinu ya mikutano na wanahabari badala ya mikutano na wana wa ulinzi na usalama kukabiliana na uhalifu, ni halali?

Utumiapo fursa za kuandaa mbinu, (mikakati, taratibu, kanuni) zinazoeleweka na wahusika na washiriki wote, na utekelezaji wa mbinu ukawa ndani ya mwenendo unaotambulika, matokeo yatakuwa halali.

Kwa hekima, busara, upeo, upembuzi, tathmini na tafakari unaweza kuepusha ubabe, udhalimu, uonevu na uharamu wa “matokeo huhalalisha mbinu” na kuwashinda wapinzani, wahalifu na wanafiki kwa uhalali wa “mbinu huhalalisha matokeo”.

Na: Albert Msemembo
 
Back
Top Bottom