Kwa kawaida unaporipoti kituo cha polisi na kutoa malalamiko kama hayo ya kwako au mengine yeyote ya jinai, unabaki kuwa mlalamikaji na polisi kwa kwa upande wao wanakuwa na jukumu la kufanya upelelezi na kuona kama malalamiko yako yana msingi wa kisheria au la? Lengo la kufanya upelelezi ni kukusanya ushahidi ili kumshitaki mtuhumiwa mahakamani, na kuthibitisha kuwa mshitakiwa ametenda kosa, na polisi wanatakiwa kuthibitisha pasipo kuacha mashaka.
Sheria imewapa polisi, kulingana na aina ya kosa, mamlaka ya kuchambua ushahidi na pengine kuamua kama kesi ifutwe au ipelekwe mahakamani, hivyo katika mazingira hayo si jukumu lako kusema kesi ifutwe au iendelee bali ni jukumu la polisi, japo katika kufanya hivyo, polisi/kurugenzi ya mashitaka wanatakiwa kuamua kwa nia ya kutenda haki au kwa maslahi ya taifa. Na jukumu lako ni kutoa ushirikiano wa taarifa zote muhimu kuhusiana na tukio ili kuwawezesha polisi kukusanya uhahidi wa kutosha ili waweze kuithibitishia mahakama na hatimaye kumtia hatiani mshitakiwa.
Kwa msingi wa maelezo hayo hapo juu, huyo polisi anayekudai pesa na ngono mchukulie kama muhalifu mwingine yeyote sawa na huyo alietishia kukuua. Anadai rushwa badala ya kufanya kazi yake ya kupeleleza na kushtaki. Dawa yake ni kumkamatisha kwa makachero wa TAKUKURU, lakini kuwa makini usije ingia kwenye mtego mwingine wa rushwa ya ngono maana siku hizi kila mahali kumeharibika.
Huhitaji kulipia chochote polisi maana sisi (raia) ndo waajiri wao na sisi ndo tunaowalipa mishahara, kwahiyo asikubabaishe na tamaa zake za pesa na ngono.