Masikio ya Kenge.. based on true story

Nicodemas Tambo Mwikozi

JF-Expert Member
Aug 13, 2016
663
1,047
MASIKIO YA KENGE

Kenge huwa hasikii kabisa mpaka pale masikio yake yatakapotoka damu. Na ukiona masikio ya kenge yanatoa damu basi ujue yameanza kusikia.

Kama hujui ni kwamba kusikia kwa kenge ni mpaka pale anapokuwa amepigwa vizuri kichwani kiasi cha kutoa damu masikioni. Hapo utamuona amekuwa mtulivu, msikivu na mwenye adabu. Anakuwa amekufa!
Vinginevyo kenge ataendelea kuwa mjuaji, mjanja, mtukutu na asiyejali lolote....

Ukishauriwa au kuonywa na wakubwa, au yeyote mwenye kukutakia mema kuhusu mwenendo wa maisha yako ukapuuza, hautofautiani na kenge.
Bahati mbaya au nzuri ni kuwa ushauri au maonyo ya namna hiyo ni sauti ya Mungu; ambayo huwa haipotei bure, ipo siku masikio yako yatakuja kusikia tu; walau yakiwa yanavuja DAMU!

*****

Niliingia benki ya CRDB tawi la Azikiwe majira ya saa nane mchana. Foleni niliyoikuta pale ndani ilinikatisha tamaa, nikamuuliza mteja mmoja, kulikoni foleni kubwa vile? Akanijuza kuwa mtandao ulikuwa unasumbua. Benki bila mtandao hakuna kazi.

Nikasema isiwe taabu, nikageuka na kuamua kwenda kupata lunch pale Break Point, bar maarufu inayotazamana na 'marehemu club Billcanas'.

Ugali na samaki mkubwa wa kuchoma aliletwa mezani kwangu mpaka nikaanza kujisuta mwenyewe. Huyu samaki ningempeleka nyumbani, akaungwa kwa tui la nazi na viungo vingine, angetutosha wote kusindikizia ugali wa mchana, na ubwabwa wa usiku. Lakini eti nimeletewa nile peke yangu, mlo mmoja...Ubinafsi ulioje!

Nikalifukuza hilo wazo baada ya kuona wateja wenzangu walioagiza kilo nzima za nyama choma na ugali, wakila bila kujiulizauliza maswali. Nikajipa moyo, maisha yanataka nini zaidi ya kula? Pesa yenyewe tunaipata kwa shida na masimango ya mabosi. Acha nile!

Wakati mhudumu amekuja kuondoa masalia ya ugali na miiba ya samaki niliyemteketeza pale mezani, nilimuagiza serengeti mbili za baridi. Nilikusudia kuzipiga fasta kisha nirudi zangu benki, nikiamini mtandao utakuwa umekaa sawa.

Kwenye soksi zangu kulikuwa na vibunda vya pesa zenye thamani ya shilingi milioni tano niliyopaswa kudeposit kwenye akaunti ya mteja wetu aliyetaka kurudishiwa pesa zake, baada ya kupungukiwa na mzigo aliokuja kununua.

Wakati huo nilikuwa nafanya kazi katika kampuni fulani ya mabati ya kisasa iliyomilikiwa na wazungu fulani raia wa Afrika kusini. Bidii yangu, uaminifu na ubunifu katika kazi viliwafanya waniamini na kunipa nafasi ya juu zaidi kati ya wafanyakazi wazawa. Nikaaminika nami nikajiaminisha zaidi kwao.

Siku chache zilizopita kuna wateja walikuja kutoa oda ya mabati mengi sana, nadhani walikuwa na mradi wa kujenga chuo au shule. Bahati mbaya aina ya mabati waliyonunua ilipelea kidogo hivyo wakaahidiwa kukamilishiwa mzigo wao wiki itakayofuata. Lakini siku iliyofuata walipiga simu kuomba warejeshewe hela iliyobaki. Ndiyo hizo milioni tano nilizokuwa nimezificha kwenye soksi, mbili mguu wa kushoto, nyingine tatu mguu wa kulia.

Wakati namalizia bia yangu ya mwisho nilishangaa kuona mhudumu akiniletea bia nyingine mbili za baridi. Nikamtazama usoni kwa mshangao.

"Nimeagizwa nikuletee na yule dada palee..." Mhudumu alinijibu kabla sijamuuliza. Nami nikainua macho yangu kufuata uelekeo wa kidole chake, ndipo yakagongana na macho ya malaika mgeni kabisa machoni mwangu. Ndiyo kwanza alikuwa anatoka kupiga funda jepesi la bia yake aina ya Savanna.

"Yule pale? " Nilimuuliza tena yule mhudumu kwa mastaajabu. Naye akaniitikia kwa kichwa, kisha akazifungua bia zote mbili na kutokomea. Ni kama alikuwa ameingiwa na kijicho.

Hata hivyo sikuacha kushangazwa na muujiza huo. Kununuliwa bia na mwanamke nisiyemjua? Hapa Bongo? Sijawahi kuona. Ndipo nikamuangalia vizuri!

Alikuwa ni msichana mrembo ambaye sikuwahi kuona wa kumfananisha naye. Nywele zake ndefu ambazo ndiyo ugonjwa wangu zilikuwa zimeangukia mabegani na mgongoni mwake, na hazikuonesha kabisa kuwa miongoni mwa zile nywele bandia. Alikuwa shombe shombe!

Akanitazama kwa haya kisha akainamia simu yake huku akitoa tabasamu jepesi lililotaka kuniondoa fahamu.

Nikajikuna kichwani kwa hamaniko. Halafu kabla sijajua nini cha kufanya, nilimuona akiinuka taratibu kuelekea maliwatoni. Makubwa!

Kila mteja aliyekuwemo pale Break Point alijishika kichwa; akimtumbulia macho ya mshangao. Ni kama sote tuliweweseka kwa jazanda la mtikisiko wa maungo yake. Moja kati ya maumbo ya kiafrika ambayo ni ndoto ya kufurahisha kwa kila mwanaume; rijali na asiye rijali, tena yakiacha jinamizi kwa kila mwanadada aliyemtazama kwa husda na wivu. Mvumo mwepesi ukasikika. Ulikuwa ni mguno wa halaiki.

Moyo ulinienda mbio huku nikiwa siamini kilichotokea. Nikazitazama tena zile bia mbili ambazo kwa mujibu wa mhudumu zilitoka kwa yule mrembo aliyepagawisha wateja wote mle ndani.

Wakati anarudi kutoka huko alikoenda, kila mtu alikuwa ametegesha macho yake kama antenna. Ni kama watu walikuwa wameambizana, ili hata wale ambao hawakubahatika kumuona vizuri wakati anaenda, wamshuhudie kwa kujinafasi zaidi anavyorudi.

Alitembea kwa madaha, huku akizihesabu hatua zake kwa maringo. Alijua kutembea kike hasa. Mikono yake akiitupa huku na kule kwa mikogo iliyoturuhusu kulivinjari umbo lake maridadi kwa jinsi tulivyotaka.

Alikuwa na kifua kilichobeba matiti ya wastani huku ncha kali zikichomoza pande zote mbili. Tumbo jembamba chini ya kifua hicho lilidhihirisha kutokuwahi kukumbwa na suluba za ujauzito. Kisha nyonga pana zikaning'inia chini ya kiuno kile chembamba. Huyu binti alikuwa ameumbwa akaumbika.

Alipofika kwenye meza yake alivuta kiti na kukaa taratibu, akiruhusu watu waliosahau milo yao kwa sekunde takribani thelathini kuanza kufukuza mainzi yaliyotumia fursa hiyo kufyonza chochote kilichowafaa kwenye sahani zao.

Nikiwa katika hali ya sintofahamu, yule binti aliinua tena uso wake na macho yake yakagongana tena na yangu. Akang'ata midomo yake kwa aibu kabla ya kuyarudisha mezani kwenye simu yake. Niliganda kama sanamu huku nikiyasikilizia mapigo yangu ya moyo.

Si kwamba nilikuwa mgeni kwa wasichana warembo, la hasha! Huyu niliyekutana naye leo alikuwa na zaidi ya urembo.

Nilikuwa mbishi na nisiyekubali kupitwa na msichana ambaye nafsi yangu ilimtamani, lakini huyu hakuwa hadhi yangu. Ni aina ya wanawake ambao inatosha kuuburudisha moyo wako kwa kuwatazama tu, na kisha kuwaacha waende zao. Kuwaachia wenye visu vikali waweze kula nyama.

Mtaani walikuwa wakiniita kipanga au kiwembe. Lakini leo sikuwa na makali wala uthubutu wa kumsogelea mwanamke huyu, japo kwa uwezo wa shetani bahati ilionekana kuniangukia kabla sijajiandaa kuipokea.

** ** **
Hivi wanaume wengine wakoje? Nilijiwazia. Kumruhusu mtoto mkali kama huyu atoke Arusha kwa ndege, na afikie hotel ya bei mbaya kama New Africa, kisha uje umchungulie kidogo tu na kumuahidi kurudi kesho yake na baada ya hapo umzimie simu, una wazimu?

Nilijikuta nikichefukwa.

Laura, kama alivyokwishajitambulisha kwangu baada ya kupiga moyo konde na kumfuata pale mezani ili kumshukuru kwa 'ofa' yake na kuangalia uwezekano wa kumjoin mezani pake, alikuwa amenisimulia kisa hicho cha mwanaume wake aliyemtambulisha kama mchumba wake.

Mchumba? Mchumba gani asiyejitambua? Nilijikuta nikisonya.

Jamaa yake huyo alikuwa anafanya kazi kwenye ubalozi wa Marekani na kwa muda mrefu alikuwa akimsumbua Laura kumtaka aje Dar es salaam. Ikaja siku hiyo, kwa mapenzi yake, na kwa nauli yake mwenyewe, Laura aliamua kumfanyia surprise mchumba wake ambaye hakutarajia ujio huo wa ghafla. Kwani hata baada ya kumhakikishia kuwa ameshaingia Dar es salaam, na kufikia hotel ya New Africa, bwana yule hakuonesha kufurahia japo aliahidi kumfuata baada ya muda wa kazi.
Na kweli kwenye majira ya saa kumi na mbili jioni, jamaa alimfuata pale hotelini akiwa juu juu sana.
Hata Laura aliposhauri waondoke wote jamaa alikataa katakata akidai kuwa bado alikuwa na kikao cha kiofisi na maofisa muhimu ubalozini. Akaondoka na kumuacha solemba.

Laura hakuwa mjinga, alijua lipo jambo. Aliteremka haraka haraka kumfuata lakini hakumuwahi, akamuona anaingia kwenye gari lake lilokuwa limepaki mbele ya hotel hiyo na kuondoka haraka.

Akaamua kumuulizia mlinzi kuhusu gari aina ya Land Rover Freelander lililoondoka hivyo punde. Mlinzi naye hakumficha, akamueleza ukweli kuhusu msichana aliyekuwa amebaki kwenye gari lile la mchumba wake. Ikawa dhahiri, mwanaume huyo alikuwa na mwanamke mwingine, na alichelea kuwa ujio ule wa ghafla ungeweza kumtibulia kila kitu.

Ndipo mapenzi yalipoingia shubiri. Usiku mzima ulitumika kutumiana jumbe za kulaumiana na matusi tele.

Leo ikiwa ni siku ya pili aliamua kuja kujiondolea stress hapa Break Point, baada ya kutoka kukata tiketi ya ndege ya kumrudisha Arusha kesho yake mchana. Hiyo ndiyo ilikuwa hadithi ya mrembo huyo mantashau, japo kwa kifupi.

Ng'ombe kafia kwa muuza supu. Nilijisemea kimoyomoyo huku nikicheka kwa kugugumia.

Usicheze na hisia za mwanamke. Anaweza kufanya lolote, saa yoyote na mtu yeyote, alimradi tu moyo wake uridhike.

Baada ya kugundua maumivu aliyokuwa amepitia, nilidhamiria kumsaidia kikamilifu. Nilimfariji kwa maneno na vitendo, ukichanganya na asili yangu ya uchakaramu basi Laura akawa amefika. Nilimfanya acheke na kufurahia kila nukta niliyokuwa naye pale. Na akawa amenizoea kupita kiasi.

Macho ya husda yaliyotupapasa na kila aliyepita karibu yetu hayakututoa kwenye upako wa hisia mpya za mapenzi zilizoamua kumea ghafla jioni ile. Hatukuwajali kabisa.

Mrembo akaendelea kuaniagizia pombe mpaka nikajishtukia. Wakati fulani mkojo uliponibana nilijikuta eti nikiingiwa na wivu, kuwa nikienda chooni kuna wakware watatumia muda huo kumfuata Laura wangu na kumrubuni kwa kutoa namba zao au kuchukua namba zake.

Nikamuonya kabla sijaenda msalani, awe makini na mbwa mwitu waliotuzingira. Akacheka kwa huba na deko za kike huku akinithibitishia kuwa shetani hana nafasi wala mamlaka kwenye moyo wake.

Nikiwa chooni, niliinama na kuvuta kiasi fulani cha pesa kutoka kwenye soksi zangu ambacho nilikadiria kisingekuwa chini ya shilingi laki mbili. Japo, nilijua ni fedha za watu lakini sikujali. Nilitakiwa nijitutumue kiume badala ya kuacha mwanamke aendelee kunipiga ofa kama kinabo. Uanaume wangu uko wapi?

Kabla sijatoka huko vijana wawili waliokuwa wakiendelea kujisaidia, walinisabahi na kuniporomoshea sifa lukuki, kwa mrembo niliyekuwa nimekaa naye.

"Aisee bro big up! Yule mtoto balaa sana... Kila mtu anakumwagia saluti hapa Break Point..aisee ni noma...umetisha mkuu!"

Niliwakenulia meno kisha nikawaonesha alama ya dole gumba. Nikatoka nje haraka kumuwahi Laura...ndege mjanja aliyenaswa kwenye tundu bovu.

Akanipokea kwa bashasha huku akinung'unika kwa kuchukua muda mrefu msalani. Jamani nyie...? Acheni tu. Kupendwa raha sana. Tena kupendwa upendwe na mtu aliyewatosa wadosi na wakwasi na kuangukia kwako kapuku usiye na mbele wa nyuma... Dunia ilikuwa imeniinamia kwa salamu ya heshima.

Kwenye saa kumi na nusu simu yangu iliita. Kuitazama nikagundua alikuwa ni bosi wangu mzungu, Mr Bidwell. Moyo ukapiga pah! Baada ya kugundua kuwa nilikuwa bado sijatumbukiza kile kiasi cha watu benki. Nikajikaza kiume na kuipokea.

"Hallo sir! "
"Already deposited that amount?"
"Yes sir, I already did that!"
"Okay, thank you Mr Foroy, have a nice evening!"
"Same to you, Sir...." Simu ikakatwa.

Kwa sekunde chache akili yangu ikawa imehama. Nikawaza kama muda huo ningeweza kuwahi kwenda kuweka hizo fedha, lakini ukweli muda ulikuwa umeenda, milango ya benki lazima ingekuwa imefungwa. Anyway, japo kesho yake ilikuwa jumamosi, najua ningeweza kwenda kudeposit zile fedha mapema asubuhi.

"Baby...unawaza nini? Kuna mtu kakuudhi?" Sauti laini ilinibembeleza na kunivua kutoka kwenye bahari ya fikra nilikoanza kuzama. Nikarejea Break Point, na starehe zikarudi mahala pake.

Nilijitutumia kiume kwa kuagizia Savanna mbili na bia zangu mbili ili asije kuniona 'kitonga'. Nikamuona ananikazia macho na kujaribu kukunja ndita bila mafanikio.

" Don't do that dear, sitaki kabisa kukuharibia bajeti yako. Mimi ndiye host wako this evening, don't bother about bills, okay honey?" Alinilalamikia huku macho yake mazuri yakionesha wazi kuanza kuzidiwa na kilevi.

"Don't mind....niko sawa tu Laura...usijali" Nikamjibu kwa swaga.

Mtungi ulikuwa umekolea hasa wakati Laura ananiomba nimsindikize chooni ili arudi zake hotelini akapumzike.

Saa kumi na mbili hii? Aende wapi na starehe ndo kwanza imeanza kunoga? Sikukubaliana na wazo lake. Nikamshawishi tuendelee kufurahia maisha mahali pale. Ila kwa sauti ya kilevi akalalamika kuwa ameshachoka kukaa hapo na mazingira yalianza kumboa. Isitoshe kulikuwa na joto sana. Akashauri labda nimpeleke maeneo ya ufukweni ili walau upepo wa bahari uweze kupunguza makali ya pombe iliyoanza kumpeleka puta.

Ndipo wazo la kwenda Coco Beach lilipotua mezani. Tukalipokea kwa mikono miwili.

Baada ya kutoka chooni nilikomsindikiza, tulipita mbele ya wateja kwa mara nyingine tukiwaruhusu wayashibishe macho yao kwa mara ya mwisho wakati tunaenda zetu nje. Nilicheka kila nilipofikiria jinsi gani watavyotumisi.

Ndiyo...wangetumiss! Kuna nyakati watu hukaa mahali fulani kutokana na raha ya kumtazama kiumbe mwingine mahali hapo. Laura alikuwa miongoni mwa viumbe hao. Macho yao yakatusindikiza mpaka tulipopotelea nje.

Madereva tax wakatupokea kwa kelele zao, kila mmoja akijaribu kuvutia upande wake. Nikamfuata dereva fulani mtu mzima, aliyesimama mbele ya Carina iliyoonekana kuwa na hali nzuri. Nilihitaji Tax yenye AC. Mtoto kama huyu hafai kuingizwa kwenye gari iliyochoka.

"Shilingi ngapi Coco Beach?" Nikauliza.
" Elfu thelathini tu bosi wangu..." Dereva akanijibu kwa adabu.

Ningalikuwa peke yangu nisingekubali kulipa hiyo bei kwenda coco beach. Nikajua fika mrembo aliyekuwa pembeni yangu ndiye hasa aliyeongeza thamani ya safari hiyo. Tukapanda gari na kukaa siti za nyuma. Laura akaniangukia kifuani huku gauni lake fupi likipanda juu na kuyaacha wazi mapaja yake yaliyonona na kunisabahi kwa mara ya kwanza. Nikavuta pumzi ndefu, na kutikisa kichwa kwa uchu.

Tulitinga kwenye fukwe za coco beach majira ya saa moja na nusu jioni, giza likiwa limeanza kutanda. Huko nako tukapokelewa na umati wa watu waliokuja kufurahia maisha yao baada ya kukuru kakara za wiki nzima.

Kama kawaida tukaendelea kuwa pambo lililoyavutia macho ya wengi tuliowakuta hapo. Kiukweli Laura hakuwa mwanamke wa kawaida. Hakuna aliyeweza kumuangalia mara moja bila kugeuza shingo yake kumtazama kwa mara ya pili. Nilisafisha nyota yangu sana siku hiyo.

Tukatafuta sehemu yenye utulivu tukakaa na kusikilizwa na mhudumu nadhifu. Kama kawaida yangu nikaagiza serengeti baridi, nadhani hii ikiwa ni bia ya kumi. Laura akaagiza mvinyo uitwao Robertson baada ya kulalamika kuwa savanna imeanza kumuumiza kichwa.

" Elfu thelathini na tano..." Mhudumu alitujuza huku akinitazama usoni. Utaratibu wa hapa ulikuwa ni wa 'lipa nikuhudumie'.

Nilimuona Laura akianza kufungua pochi yake lakini nikaingiza mkono haraka kwenye mfuko wangu wa suruali na kutoa noti nne za shilingi elfu arobaini. Nikamlipa mhudumu bila kuonesha kushtushwa na bei kubwa ya vinywaji vile. Laura akanitazama kwa macho yake malegevu, halafu akabetua midomo yake na kupandisha juu mabega yake.

Vinywaji vililetwa tukaendelea kunywa huku tukiburudika kwa muziki uliopangiliwa vizuri na DJ mahiri.

Nikiri tu, sikuwahi asilani kuhisi maisha yangu yamekamilika kama siku hiyo. Nilijiona kuwa kwenye kilele cha furaha na amani ya kuwa binadamu. Laura alinifanya niyaone maisha katika mwanga bora zaidi.

Mtoto mzuri, mwenye uwezo wa kifedha, asiye na majivuno wala ngebe kama wasichana wengi wa kizazi hiki, alikuwa amenidondokea roho na mwili. Alikuwa amejiaminisha kwangu kwa asilimia mia moja. Alikuwa ameamua kuukabidhi moyo wake kwangu bila kutaka mjadala. Machozi yalinitoka.

Wakati huo akiwa ameniegemea kifuani na kuruhusu mkono wangu wa kushoto uliopita nyuma ya shingo yake kuendelea kuzichezea nywele zake laini mithili ya sufi.

"Baby nasikia njaa!" Alinililia.

Bila ajizi nikamuita mhudumu na kumuagizia mchemsho wa kuku kama alivyohitaji. Nami nikajiagizia mishkaki ya samaki aina ya sato. Napenda samaki.

Safari hii sikutaka kabisa aingie mfukoni mwake, alikuwa amenikarimu vya kutosha. Potelea mbali japo bei ya vyakula maeneo ya ufukweni ni kubwa, sikujali. Kuna kitu kikubwa kilikuwa kinafuata baada ya siku ya leo, kati yangu na huyu msichana ambaye ni kama alishushwa kutoka mbinguni.

Ni kweli nina mke na mtoto mmoja, lakini unadhani nani angenicheka au kunishangaa kwa kuwa na hawara kama huyu? Kwanza hakustahili kuitwa hawara...jina baya kama hilo unawezaje kulitumia kwa mtoto mwenye hadhi ya Laura?

Nitamuoa tu, na itabidi mke wangu akubaliane na hali halisi.

Unaweza kusema ni mawazo ya pombe, lakini amini haikuwa pombe. Nilishakata shauri itakuwa hivyo. Kuna binadamu hupaswi kuwapoteza kwa gharama yoyote. Laura alikuwa mmojawapo.

Kwenye saa tano usiku tuliamua kuhama kutoka Coco beach kuelekea maeneo ya mwananyamala kwenye ukumbi wa Mango Garden, bendi ya Twanga pepeta ilipokuwa inatumbuiza. Wazo la kwenda muziki nililitoa mimi. Japo mwenyewe alikuwa kachoka na kunisihi nimrudishe New Afrika, sikukubaliana naye. Nilitaka tuendelee kula bata hadi kuku wakereke.

Laura hakuwa mwanamke mbishi, alijua umuhimu wa kumheshimu mwanaume. Alinikubalia na kunipa busu motomoto.

Tukachukua Tax kuelekea kinondoni. Tukiwa njiani nilishindwa kuvumilia zaidi, nilijikuta nikimtomasa Laura maungoni mwake. Jambo hilo likauwasha moto mkubwa wa ashki ya kufanya jambo jingine, muhimu zaidi. Laura pia akawa hajiwezi. Kalegea kama mlenda.

Kuna mambo yalianza kufanyika huku nyuma ambayo nilijua fika yangeweza kusababisha ajali kama yangeendelea. Kama mara mbili tatu dereva alipoteza umakini barabarani na gari kuyumba vibaya, baada ya kujaribu kuchungulia kilichokuwa kikiendelea huku nyuma kwenye siti za abiria wake.

" Honey....i can't....i cannot hold it anymore! Help me pleaseee...." Laura alikuwa akinong'ona kwa mahaba mazito.

Ni wazi safari ya Mango garden ikawa imekufa. Lakini pia wazo lake la kwenda New Afrika sikuliafiki. Hata kama nilikuwa nimelewa lakini sikuwa nimepoteza umakini kiasi cha kutokujua hatari za kwenda kulala nae Hotel New Africa. Kisa cha kuja kufumaniwa na kumuliwa risasi? Kwamba huko kugombana na mpenzi wake ndiye iwe tiketi ya mimi kujipeleka shimoni kichwa kichwa?

Nilikataa kata kata, badala yake nikamuamuru dereva atupeleke Hotel De Mag iliyopo maeneo ya mwananyamala komakoma. Laura hakubisha.

Nililipia Tax kiasi cha shilingi elfu ishirini na tano, kisha tukajitoma ndani ya Hotel De Mag.

Mapokezi tulipokelewa na mhudumu ambaye macho yake yote aliyatumbua kwa Laura niliyembana kiuno chake barabara. Elfu arobaini zikanitoka, sikujali.

Moja kwa moja mpaka orofa ya kwanza kwenye chumba moja nadhifu kilichotulaki kwa harufu nzuri ya manukano na ubaridi murua wa kiyoyozi kilichoendelea kupuliza upepo mwanana.

Katikati ya chumba hicho Laura hakutaka kunipa pumzi, kama mtu aliyekuwa anakaribia kufa kwa kukosa hewa ya oksijeni alinikumbatia kwa nguvu na kunasisha mdomo wake mdomoni kwangu. Ndimi zikakamatana na kuzungushana kwa mitindo anuai, miguno ya kimahaba ikirindima.

Dakika tatu zilipotea kabla hatujapeana nafasi ya kupumua kidogo.

Laura akavirusha viatu vyake, kimoja huku kingine kule. Kisha ukafuatia mkoba wake, nao akautupia huko. Akilini mwake aliwaza kitu kimoja tu, ambacho pia nilikiwaza.

"Pls....let me just take a little shower...nakuja mme wangu...najimwagia kidogo nitoe uchovu okay?"

Laura aliongea haraka haraka huku akipambua nguo zake na kuzitupia juu ya meza. Kufumba na kufumbua akabaki na nguo moja tu mwilini mwake ambayo ama hakika sijui kama ni halali kuiita nguo. Maana vilikuwa ni vijikamba vyembamba vilivyopita hapa na pale kuzunguka maeneo yake ya siri. Ni sehemu ya mbele tu ndiyo ilikuwa imesitiriwa na kijitambaa chekundu chenye umbile la sambusa. Bikini!

Niliwaza kwa sauti. Maana sikuwahi kushuhudia kabla nilichokiona mbele yangu.

Alikimbilia bafuni huku akiniacha nimepigwa na bumbawazi kwa mitikisiko niliyoishuhudia. Mdomo wangu sikukumbuka kuufumba. Kazi ipo!

Nikaona nisiwe mzembe, nami nikavua nguo zangu ili nimfuate bafuni. Lakini kabla sijaingia bafuni nilikumbuka kuichungulia simu yangu ambayo mara ya mwisho niliondoa mlio wake ili kuondoa bughudha. Nikakutana na missed calls yapata hamsini za mke wangu. Nikaizima kabisa na kuirushia kwenye kochi dogo lilikuwemo chumbani humo.

Nilipotaka kufungua mlango wa bafu ambalo tayari lilishaanza kutiririsha maji nilishangaa kuona Laura amejifungia kwa ndani.

"Baby nifungulie tuje tuoge wote..." Nilimsemesha lakini hakunijibu. Nikajiongeza, pengine anajisaidia. Nikarudi kitandani na kujilaza chali huku nikihisi kichwa kikizunguka kwa pombe.

Maji yaliendelea kutiririka kule bafuni kwa muda mrefu sana. Mpaka nikashawishika kumwita kwa mara nyingine. Lakini safari hii nguvu ya kuita sikuwa nayo. Usingizi mzito wa pombe ulianza kunikandamiza. Jitihada zangu za kuinuka ziliishia kukigeuza kichwa changu huku na kule bila hata kufumbua macho.

Mpaka usingizi mzito unanichukua na kufuatiwa na koromo zito la kilevi, nilikuwa nikiendelea kusikia maji ya bomba yalivyokuwa yakitiririka bafuni.

** ** **
Mlango ulikuwa umegongwa karibu mara tano. Na nilikuwa nausikia kabisa lakini kuamka ndiyo ikawa shida.

Safari hii ukagongwa kwa nguvu sana mpaka nikaamka.
"Nani?" Niliita kwa sauti yenye mikwaruzo bado nikiwa na wenge la usingizi.

"Kaka, saa nne na nusu saa hizi, tunataka kufanya usafi...unatakiwa kuachia chumba!"
Sauti ya mhudumu ndiyo iliyonizindua kwenye wenge hilo. Nikasimama wima na kuangaza huku na kule.

Laura? Yuko wapi?
Ndilo swali lililonijia safari hii. Mbio mbio nikaenda hadi bafuni na kujaribu kuusukuma mlango wa bafu ambao ulifunguka kiulaini tofauti na nilivyotarajia. Nikaingiza kichwa changu kwa hofu kuchungulia kilichokuwemo humo ndani.

Hakukuwa na mtu. Tena sakafu ilikuwa kavu kabisa utadhani bafu hilo halijatumika kwa majuma kadhaa.

Laura yuko wapi? Nilirudi mbio na kuanza kukagua hiki chumba. Hakukuwa na nguo wala alama yoyote ya Laura. Moyo ukaanza kupoteza baadhi ya mapigo.

Nikainamia viatu vyangu uvunguni. Nikavivuta taratibu na kuvitoa nje. Nikashusha pumzi ndefu baada ya kuona soksi zipo ndani ya viatu kama nilivyokuwa nimezifundika jana usiku. Nikazichomoa moja baada ya nyingine.

Yes! Zilikuwa nyepesi kama zimetoka kuanuliwa kwenye kamba. Hakukuwa na hata senti. Ndipo ukafuata wazimu wa kukagua kila kona ya chumba kile. Nikafunua hapa na pale, nikapanda kule na kuchungulia huku. Wazimu mtupu. Milioni tano za watu zilikuwa zimeenda na maji.

Tumbo na mkojo vikanibana ghafla. Nikarudi msalani kwa pupa. Nilikojoa bila kulenga tundu huku nikijamba mfululizo bila kujizuia.

Nilitoka nje jasho likiwa linanitoka. Japo nilijizuia kuonesha hali ya kuchanganyikiwa lakini ni wazi wenyeji wangu walijua fika kuwa nimepagawa. Japo kilichonipagawisha hawakukijua.

Pale mapokezi nikakutana na yule dada aliyetupokea jana usiku. Kabla hata sijamsalimu alinichangamkia kwa bashasha na kuniambia kuwa ana ujumbe wangu.

Nilijizuia kutetemeka japo sina hakika kama nilifanikiwa.

"Aliniachia hii bahasha wakati anaondoka akaniambia nikuhifadhie. Yeye kasema anawahi ndege ya alfajiri." Dada wa mapokezi aliyasema hayo na kunikabidhi hiyo bahasha. Nilitaka kuisomea hapo lakini akili nyingine ikasema ni bora nikaisomea nje. Nisije nikaangua kilio cha mbwa hapo na kujaza nzi. Tumbo lilininguruma mfululizo.

" Kaka hongera, una mwanamke mzuri kweli halafu mkarimu. Mimi mwenyewe kaniachia elfu kumi wakati anaondoka...." Aliendelea kubwabwaja.

Nilimtazama mara moja kisha nikasonya kwa hamaniko na kutoka nje. Alibaki amepigwa na butwaa. Ni dhahiri hakujua kilichonikuta.

Nje ya hotel De Mag, hotel ambayo kwa sasa niliiona kama pango linaloficha wevi na wanyang'anyi, kulikuwa na miti mikubwa iliyotengeneza kivuli. Nikaamua kujificha kwenye moja ya miti ile na kuirarua ile bahasha kwa pupa.

Ujumbe niliokuta humo ndani ulinifanya nilie machozi. Laura alikuwa ameniaga kwa maneno mazuri, na mwisho akaniasa niwe makini na wanawake wa mjini.

Pia aliambatanisha na shilingi elfu moja na mia mbili ambazo alidai ni nauli yangu ya kunirudisha mbagala.

"Mpende sana mkeo, na kuwajali watoto wako!"

Huo mstari wa mwisho ulikuwa kama msumari wa moto kifuani. Nililia kama punguwani na kamasi zikanitoka. Nikajilaumu sana kuliko ninavyoweza kusimulia.

Mwisho wa siku ilinibi nitembee taratibu kutafuta kituo cha daladala ili nirudi tu nyumbani. Sikuwa na pengine kwa kukimbilia.

Njaa ilikuwa kali. Niliwaona watu waliokuwa wakila supu asubuhi hii kwenye mabaa, nikajikuta nawatamani. Nilitamani nikawaombe waniachie hata mchuzi wa supu, lakini sikuweza. Nani angenielewa? Acha niyaone mwenyewe....

** ***

Baada ya wiki mbili nilikuwa choka mbaya. Sikuwa na hata kumi ya kuweza kusogeza siku.
Kazini nilikuwa nimetimuliwa baada ya kutiwa ndani kwa wiki moja na wenye ofisi yao, wakiamini kuwa nilifanya utapeli. Hata hivyo baada ya wiki moja , waliamua kufuta kesi lakini kibarua kikawa kimeota nyasi.

Mke wangu naye aliondoka pamoja na mtoto na kwenda nisipopajua, huku simu yake ikiwa haipatikani.

Leo usiku nikiwa nimepania kunywa sumu ya panya, mke wangu alirejea nyumbani akiwa na mwanangu aliyenilaki kwa shangwe na furaha asijue lolote liloendelea kati yetu.

Alikuwa na matunda kama mananasi, mapapai na machungwa.

Baada ya kula chakula cha usiku, aliahidi kunisamehe na kunisisitiza kesho yangu kuingia barabarani kutafuta kibarua kingine ambacho kingetusaidia kujikimu kimaisha.

Haikuwa kazi rahisi!

#Take_care
FB_IMG_1527201744538.jpg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Wewe ni mwandishi mzuri sana mkuu. Endeleza kipaji chako. Yote uliyoandika ni matukio yanayotokea katika jamii. Binafsi siku zote huwa ninapokutana na msichana wa aina hiyo ambaye simfahamu cha kwanza huwa nakumbuka maandishi ya A. E. Musiba katika vitabu vyake vya Willy Gamba. Mara zote anahusia kuwa wanawake wa aina hiyo ni mtego na hata Gamba mwenyewe ameshanaswa mara nyingi tu. Sasa sijui ni kitu gani kinacho tufanya wanaume tushindwe kubaini mtego huu .
 
Hizo style wanapigwa maboya sana!! Dem wanaangalia sura bana
 
Back
Top Bottom