Masahihisho kidogo katika hotuba ya mwalimu kuhusu siku za awali za TANU

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,265
Wanamajlis,
Kiasi cha kama miaka miwili iliyopita palikuwa na mjadala mkali sana
hapa ukumbini kuhusu hotuba ya Mwalimu Nyerere alipomtaja Abdul
Sykes.


Yericko Nyerere, Maalim Faiza Foxy na wengineo walichangia sana
lakini hakuweza kuileta ile hotuba.

Hotuba imepatikana lakini ile sehemu ilosababisha mjadala mkali haimo.

Nakuombeni ingieni hapo chini msikilize hii hotuba na msome niliyoongeza
kuiweka vizuri hotuba hii ya Baba wa Taifa:

Mohamed Said: Nyerere Alipomzungumza Abdul Sykes

Katika hotuba hii ya Mwalimu Nyerere kuna jambo kakosea. Anasema safari ya kwanza kutangaza TANU alikwenda Mbeya. Hapana safari ya kwanza alikwenda Morogoro akiongozana na Zuberi Mtemvu 1954 na hii safari ya Mbeya aisemayo alozungumza na wanachama mkutano wa ndani ilikuwa mwaka 1955 alipokwenda Lindi akifuatana na Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani. Mbeya TANU ilikuja baadae sana. Ukisoma kitabu cha Abdul Sykes utayakuta haya na ithibati yake ni nyaraka nilizosoma katika majalada ya akina Sykes.

''Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.

Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.

Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii ''maalum'' ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam.

DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika ya jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.''

Huenda mkutano aliokusudia Mwalimu Nyerere kuufanya Mbeya ni huu aliofanya Mkindani nyumbani kwa Ahmed Adam baada ya kutoka Lindi:

''Julius Nyerere, Ali Mwinyi Tambwe na Rajabu Diwani waliwasili Mikindani kutoka Lindi siku ya Jumamosi. Kabla ya kuwasili ujumbe huo, kazi kubwa kuliko zote waliyokuwanayo uongozi wa TANU Mikindani ilikuwa kutafuta mahali pa kumlaza Nyerere. Walimwendea Ahmed Adam, Mnubi mmoja tajiri na mtu wa makamo, aliyemiliki nyumba moja ya fahari. Nyumba hii ilikuwa ya ghorofa moja na ilijengwa kwa mawe na chokaa. Ahmed Adam aliombwa awe mwenyeji wa Nyerere na ujumbe wake. Nyumba hii tayari lilikuwa na kisa chake. Ilijengwa na hayati kaka yake Ahmed Adam baada ya Vita Kuu ya Kwanza. Kaka yake alikuwa askari wa Kinubi aliyekuwa katika jeshi la Wajerumani. Huenda alichukuliwa Misri mwishoni mwa mwa karne ya kumi na tisa na Wajerumani kuja Tanganyika kama mamluki katika jeshi la Wajerumani wakati wa vita vya Maji Maji. Baada ya vita alilipwa kiinua mgongo na serikali ya Ujerumani na kwa kutumia fedha hizo alijenga nyumba hiyo. Katika Vita Kuu ya Kwanza yeye alipigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza. Baada ya vita Wajerumani wakiwa wameshindwa vita, Waingereza waliitikadi nyumba hiyo kama mali ya adui wa himaya ya Kiingereza na kwa hiyo ilibidi itaifishwe. Hii ilikuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa nzuri yenye kumilikiwa na Mwafrika na kwa ajili hii haikuweza kukosa kuhusudika.

Utawala wa Waingereza ulikuwa katika taratibu ya kuitaifisha nyumba hiyo wakati ilipofahamika kwamba serikali isingeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kifungu cha sheria ambacho kilisema kuwa mali ya Waafrika waliokuwa wakitumika katika majeshi ya watawala wao haiwezi kutaifishwa. Hii ilinusuru nyumba hiyo na hivyo ilibakia mikononi mwa mwenyewe mpaka alipofariki na nyumba hiyo ikaja kuwa katika miliki ya mdogo wake, Ahmed Adam. Ahmed Adam alikubali kumpokea Nyerere na ugeni wake nyumbani kwake. Nyumba hiyo ilikuja kuwa tawi la kwanza la TANU Mikindani. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, usiku Nyerere aliitisha mkutano na wanachama kama thelathini hivi walihudhuria. Nyerere aliwaeleza kwa ufupi juu ya ile safari yake ya Umoja wa Mataifa na hali ya siasa kwa ujumla mjini Dar es Salaam. Nyerere aliwahakikishia waskilizaji wake kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Tanganyika itakuwa huru katika uhai wao.''

Kuhusu kuandika katiba ya TANU. Katiba ya TANU haikuandikwa na yeyote katika viongozi wa TANU bali ilinakilikwa neno kwa neno kutoka katiba ya Convention People'sParty (CPP) ya Kwame Nkrumah wa Ghana:


''Kasella Bantu ndiyo mtu aliyempeleka Julius Nyerere kwa Abdulwahid kumtambulisha. Hii ilikuwa mwaka wa 1952.Bantu na Nyerere walifahamiana toka huko nyuma walipokuwa wakifundisha Tabora. Chama hakiwezi kupinga ukweli kwamba Kasella Bantu alikuwa miongoni mwa wale wanachama 17 waasisi wa TANU. Hali kadhalika chama hakiwezi, kupinga ule ukweli wa historia kuwa Kasella Bantu alishiriki katika ''kuandika'' ile katiba ya TANU. Kasella Bantu anakerwa sana na kupotoshwa kwa historia. Kila alipopata fursa kuanzia alipokuwa ng?ambo uhamishoni na hata baada ya kurudi nyumbani kutoka uhamishoni, Kasella Bantu ameeleza kuhusu mambo haya mawili ya kihistoria, kuwa ''aliandika,'' katiba ya TANU na ni mmoja wa waasisi wa TANU. Bantu kama waanzilishi wengine wengi anahisi kwamba mchango wake katika harakati za uhuru wa Tanganyika haujathaminiwa.

Uongozi wa TAA haukurasimu katiba mpya. Katiba ya TANU ilinukuliwa neno kwa neno kutoka Convention People?s Party (CPP) ya Kwame Nkrumah, kwa kutia TANU mahali pa CPP (Maelezo kutoka kwa Tewa Said Tewa).''


20151219_124937.jpg
Nakala ya kwanza ya kitabu cha Abdul Sykes kwa Kiingereza kilichochapwa
London mwaka wa 1998 maelezo hayo hapo juu yanatoka katika kitabu hiki

20151219_124737.jpg



DSCN0073.JPG


Waasisi wa TANU mbele ya Makao Makuu ya TAA New Street 7 July 1954
Nyuma waliosimama aliyevaa miwani ya jua ni Abdulwahid Kleist Sykes


DSC03392%252520%2525281%252529.JPG





DSCN0108.JPG
Ilipokuwa ofisi ya TAA na TANU sasa lipo jengo hili jipya la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lumumba Avenue
 
Safi sana wakristu kukubali waislam kuingia kanisani. Ingekua vice versa sijui!
 
tatizo hivi vitabu kwa kuvipata sijui hata naanzia wapi!

Nelson,

Kitabu cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes kinapatikana Tanzania
Publishing House (TPH), Ibn Hazm Media Centre Msikiti wa Mtoro na Manyema,
A Novel Idea Slip Way Masaki na Soma Book Milocheni.
 
Hizo ni hisia tu za kidini zinakupeleka mputamputa.Hoja ni kwamba alilindwa na wanachama wa chama cha TANU siyo waislam.
 
Back
Top Bottom