MOTOCHINI
JF-Expert Member
- Jan 20, 2014
- 27,778
- 30,749
MAREKANI imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kuelekea baadhi ya maeneo ya Kenya hasa yale yanayopakana na Somalia wakihofia mashambulizi ya Al-Shabaab pamoja na uhalifu.
Ilani hiyo ilichapishwa Ijumaa kwenye mtandao wa Idara ya Marekani inayoshughulikia Usafiri ikiwataka Wamarekani wawe waangalifu zaidi kutokana na vitisho kutoka kwa kundi hilo la kigaidi pamoja na taarifa za kukithiri kwa visa vya uhalifu katika maeneo kadha.
“Msisafiri kuelekea Kaskazini-Mashariki mwa Kenya katika kaunti za Mandera, Wajir na Garissa pia msithubutu kwenda kaunti za Pwani za Tana River na Lamu wala kaskazini mwa Malindi iliopo Kilifi na mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi,” ilinukuliwa ilani hiyo.
Isitoshe, ubalozi wa Marekani uliwashauri raia wao wazuru mtaa wa Old Town, Mombasa nyakati za mchana pekee na watahadhari dhidi ya kuabiri feri katika kivuko cha Likoni.
Idara hiyo ilieleza hofu yake kuhusiana na kuendelea kuwepo kwa vitisho vya ugaidi humu nchini katika maeneo hayo na pia Nairobi na Pwani kwa jumla.
Aidha ilisema visa kadha vya uhalifu vimekuwa vikiripotiwa ambapo baadhi ya raia wa Marekani na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani humu nchini wanalengwa kuibiwa magari, kuvamiwa, kuporwa au kutekwa nyara.
Vifo vya watu 122
Mwaka 2016 mashambulizi ya kigaidi yakiwa ni ufyatulianaji risasi, kurushwa maguruneti na vilipuzi vinginevyo yaliwaangamiza jumla ya watu 122 nchini.
Visa hivyo vingi vilitokea katika kaunti za Wajir, Garissa, Lamu na Mandera.
Mashambulizi ya kigaidi aghalabu yamekuwa yakilenga asasi za Kenya pamoja na zile za kigeni zikiwemo vituo vya polisi, magari, mikahawa, usafiri wa umma, vilabu na mabaa.
Vilevile baadhi ya taasisi za kidini, maduka na miradi ya miundombinu pia imo hatarini.
Ilani hii inafuatia ile iliyotolewa na idara hiyo mara ya mwisho mnamo Juni 30, 2016.