Mapenzi kitu ajabu, ni shani yake Manani
Hayahitaji sababu, sababu ilo makini
Hujimwaga bubububu, bububu maji ya pwani
Watu wakataajabu, kilichokupata nini!
Hayahitaji dhahabu, mapambo mingi mwilini
Au wingi wa adabu, adabu za kizamani
Jamani mapenzi tabu, tabu yake huioni!
Mpaka uwe karibu, karibu yake mwendani!
Mapenzi yakikusibu, yakasibu mtimani
Wageuka kuwa zubu, kwa wingi wa hamkani!
Wataraba kama dubu, dubu lisilo makani
Bila wako mahabubu, hakika umashakani.
Mapenzi kama zabibu, zabibu mbivu mtini
Hata yawe ughaibu, utayafata kwa kani
Humsemesha na bubu, mapenzi akibaini
Wala hayana ubabu, ujana wa kizamani!
Mapenzi si madhehebu, ya fikira au dini
Mapenzi si ustarabu, si haiba wala fani
Mapenzi si ukatibu, cheo hakina thamani
Mapenzi yanaghilibu, ajabu hii jamani!
Hayana utaratibu, mapenzi ni maluuni!
Mapenzi kisebusebu, na kiroho mkononi!
Mapenzi ni merikebu, isiyo nahodha ndani!
Au punda mwenye nabu, hatari iso kifani.
Mapenzi hayana jibu, mapenzi si mtihani!
Mapenzi sio kitabu, cha kusoma darasani
Mapenzi si aghalabu, kuwa sawa duniani
Imechoka yangu nibu, kalamu naweka chini.