Mapendekezo ya Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Dec 10, 2015
22
70
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHESHIMIWA WILFRED MUGANYIZI LWAKATARE (MB) AKIWASILISHA MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BENGENI KUHUSU BAJETI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018

*(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016)*
_____________________
1. *Utangulizi*

Mheshimiwa Spika, nasimama tena mbele ya Bunge lako tukufu kwa neema za Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukurani kwa uongozi mzima wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Wabunge wote wa Kambi ikiongozwa na Mheshimiwa Freeman A. Mbowe (Mb) kwa kuendelea kutuamini mimi na Mheshimiwa Salma Mwasa (Mb) kuisimamia na kuisemea Wizara hii kwa kipindi chote hiki. Mungu aendelee kuwapa nguvu na uvumilivu ya kuyakabili yote na naamini kwa nguvu zake yeye TUTAVUKA na kuvishinda vikwazo vyote.


Mheshimiwa Spika, Kwa moyo mkunjufu niendelee kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Bukoba Mjini (Bukoba Town) kwa ushirikiano wanaonipa kwa kuliwakilisha na kuliongoza Jimbo lao. Kwa dhati kabisa nimshukuru Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba, Chief Karumuna, Madiwani wote wa Manispaa ya Bukoba bila kujali tofauti zao za kivyama, Mkurugenzi na Watendaji wake wote, Mwenyekiti wa Chadema Bukoba Mjini Victor Sherejey na Kamati yake yote ya utendaji kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa.

Mheshimiwa Spika, ushirikiano ninaopata kutoka kwa viongozi wenzangu unalifanya Jimbo la Bukoba na Manispaa kwa ujumla kuwa sehemu ya kuigwa ambapo figisu na tofauti za kivyama haziwi kikwazo cha kuwaletea wananchi maendeleo wanayoyahitaji kutoka kwetu tuliochaguliwa kuwaongoza na kusimamia shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Mshikamano wetu ndio utaendelea kuwa chimbuko la kuipata na kuiona Bukoba Mjini waitakayo. Kipekee naomba niishukuru familia yangu yote ambayo imeendelea kunipa moyo katika kazi hii ambayo inaninyima muda mwingi wa kuwa nao.

Mheshimiwa Spika, Nitoe pole kwa wote waliopatwa na majanga mbalimbali tetemeko, njaa, mafuriko, ukame, ajali mbaya, ugumu wa maisha n.k kubwa ni kuwa na subira na kuyaombea na kuyaunga mkono yale tunayoyaaininisha kama sababu na kikwazo cha maisha na maendeleo yao.

2. *Migogoro ya Ardhi Nchini*

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 01 Novemba mwaka 2013 Bunge lako tukufu liliunda Kamati Teule kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha migogoro ya ardhi nchini na hatimaye kuja na mapendekezo ili Bunge liazimie na kuielekeza serikali kwa ajili ya mustakabali wa taifa letu kwa ujumla. Hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule iliridhiwa na Bunge baada ya malalamiko ya muda mrefu yaliyokuwa yanawasilishwa Bungeni na Wabunge kwa niaba ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa iliwasilisha taarifa yake Bungeni tarehe 06 Februari 2015. Pamoja na mambo mengine taarifa ya Kamati ilieleza aina ya migogoro ya ardhi nchini, uchambuzi wa mipango, sera na sheria zinazohusiana na masuala ya ardhi, uchunguzi wa Kamati pamoja na mapendekezo ya muda mfupi, kati na muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kurejea baadhi ya masuala muhimu yaliyoibuliwa na Kamati Teule ya Bunge wakati huo;


(a) *Aina ya Migogoro*

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule iliainisha aina kadhaa za migogoro ya ardhi nchini kuwa ni migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro kati ya wakulima na wawekezaji, migogoro kati ya wafugaji na wawekezaji, migogoro kati ya wakulima/wafugaji dhidi ya maeneo ya hifadhi na migogoro kati ya wananchi na serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na uainishaji huo wa migogoro lakini ingependa kuongeza mgogoro mwingine ambao ni mgogoro unaotokana na mipaka ya maeneo ya utawala kama vile Vijiji/Mitaa na hata ngazi zingine za maeneo ya utawala.

(b) *Hali ya Migogoro*

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ya Bunge iliweka bayana kuwa hali ya migogoro ya ardhi nchini baina ya wakulima na wafugaji au baina ya makundi hayo na wawekezaji imekuwa ya muda mrefu pamoja na kuwa serikali imekuwa ikileta mipango, sera na hata sheria mbalimbali kukabiliana na tatizo hili. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaunga mkono kauli ya Kamati Teule ya Bunge kuwa hali ya migogoro ya ardhi nchini isipotafutiwa ufumbuzi inaweza kuhatarisha amani na mustakabali wa nchi yetu.

(c) *Sababu ya Migogoro*

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ya Bunge ilieleza sababu nyingi ambazo ni chanzo kinachosababisha migogoro ya ardhi nchini ambapo pamoja na sababu zingine ni kama ifuatavyo;

(i) Kutokutengwa kwa maeneo mahususi ya Kilimo na Ufugaji.
(ii) Kutokupimwa na kutokubainishwa kwa mipaka ya Vijiji
(iii) Watu wachache kumiliki maeneo makubwa ya ardhi
(iv) Wawekezaji kutokuzingatia na kufuata sheria za uwekezaji kwenye ardhi
(v) Rushwa miongoni mwa watendaji wa serikali
(vi) Kutowalipa wananchi fidia kamilifu
(vii) Tofauti ya sera ya ardhi na sera ya mifugo

Mheshimiwa Spika, kuhusu watu wachache kumiliki maeneo makubwa ya ardhi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kwa mara nyingine kuikumbusha serikali juu ya hoja binafsi ya aliyekuwa Waziri Kivuli wa Ardhi Mheshimiwa Halima Mdee (2010-2015) ambaye alieleza kwa undani juu ya uwekezaji kwenye mashamba makubwa nchini ambao utaleta tishio la uhaba wa ardhi na pia serikali kushindwa kusimamia uwekezaji wenye tija katika sekta ya ardhi. Ieleweke kuwa serikali ilikubali kufanya ukaguzi kwenye mashamba makubwa nchini na kuleta taarifa yake Bungeni, hata hivyo mpaka leo taarifa hiyo haikuwahi kujadiliwa ndani ya Bunge lako tukufu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuleta Bungeni taarifa ya ukaguzi wa mashamba makubwa nchini ili ijadiliwe na Bunge na pia kuzingatia ushauri kama ulivyotolewa na Kamati Teule ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa nyakati tofauti tuliweka bayana orodha ya watu wanaomiliki mashamba makubwa na kusababisha uhaba wa ardhi kwa wananchi. Ukiangalia kwa makini orodha ya wanaohodhi mashamba makubwa ambayo hata hivyo imeonekana wanashindwa kuyaendeleza wapo pia wanasiasa (vielelezo vimeambatanishwa). Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda serikali kutoa kauli juu ya mashamba hayo ambayo yalionekana ni muhimu kurudishwa serikalini kama agizo la Bunge limeshatekelezwa. Katika hili tofauti za kiitikadi ziwekwe pembeni vinginevyo serikali itakuwa ikifanya kazi zake kwa upendeleo na kwa hila.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wawekezaji kukodisha mashamba kwa wananchi kinyume na taratibu za kisheria za kubinafsishwa ardhi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kueleza kuwa tatizo hilo bado lipo na serikali inashindwa kuchukua hatua hata baada ya kushauriwa hivyo na Kamati Teule ya Bunge. Ieleweke kuwa hata baadhi ya waheshimiwa Wabunge wametoa malalamiko kwa niaba ya wananchi juu ya tabia za wanaoitwa wawekezaji kuwakodisha ardhi wananchi.

Mheshimiwa Spika, hata baadhi ya kauli na matendo ya viongozi wa serikali zimekuwa zikichangia kutozingatiwa na kuheshimiwa kwa taratibu na sheria za ardhi nchini ambapo inakuwa pia chanzo cha migogoro ya ardhi. Itakumbukwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliutangazia umma kuwa amekabidhiwa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda lakini baada ya muda mfupi Waziri mwenye dhamana akatangaza wazi kuwa mwekezaji huyo sio mmiliki wa ardhi ambayo imetangazwa kutolewa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa viongozi wa serikali ambao hawahusiki na masuala ya ardhi kuacha kutafuta umaarufu kupitia ardhi ya watanzania. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangaa na kuhoji kama utaratibu wa viongozi wa serikali hiyohiyo na Chama hichohicho kushindania umaarufu kwenye vyombo vya habari kama unatupeleka sehemu salama kama taifa.

(d) *Mapendekezo ya muda mfupi ya Kamati Teule kwa serikali*

Mheshimiwa Spika, pamoja na mapendekezo mengi ya Kamati kuhusu masuala ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, baadhi ya mapendekezo ya muda mfupi ambayo yalipendekezwa na Kamati Teule ya Bunge ni kama ifuatavyo;

(i) Serikali iharakishe usuluhishi wa mgogoro baina ya wakulima na wafugaji wanaogombania maeneo Wilayani Kiteto.
(ii) Kupima ardhi ya Mkoa wa Morogoro kama mpango wa dharura ili kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji
(iii) Serikali ifute na kuyapima upya mashamba ya wawekezaji ambayo yametelekezwa na wawekezaji ili ardhi hiyo wapatiwe wananchi.
(iv) Serikali ipime upya maeneo ya Vijiji vyenye migogoro ya mipaka
(v) Serikali iangalie upya uamuzi wa kupanua mipaka ya maeneo ya hifadhi na kuangalia upya maeneo ambayo kwa sasa yamepoteza hadhi ya kuitwa hifadhi ili makazi na shughuli za kiuchumi za wananchi zipanuliwe.
(vi) Serikali itwae maeneo ambayo yalibinafsishwa bila kuzingatia mipaka na hivyo wawekezaji kuingilia ardhi ya wananchi.
(vii) Serikali ilete Bungeni marekebisho ya Sheria kwa ajili ya kuweka vigezo vya usajili wa Vijiji ambapo pamoja na mambo mengine Kamati iliitaka pia serikali kuzingatia historia na uwepo wa ardhi ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaikumbusha serikali kuhusu ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa Bungeni wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa serikali italeta taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge. Kamati Teule ya Bunge kuhusu maula ya migogoro ya ardhi inapaswa kuletwa Bungeni haraka.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu taarifa ya serikali kuhusu maazimo ya Bunge kuhusu migogoro ya ardhi ikaletwa Bungeni ili ijadiliwe kwa sababu toka maazimio haya yatolewe ndani ya Bunge lako tukufu tumeshuhudia mgogoro wa Kiteto ukiwa bado haujapatiwa ufumbuzi, huko Kilosa Mkoani Morogoro Mkulima mmoja Ndugu Augustino Mtitu wa Kitongoji cha Upangwani, Kijiji cha Doma Isanga, Kata ya Masanze, Jimbo la
Mikumi Wilaya ya Kilosa alipigwa mkuki na wanaodaiwa kuwa wafugaji. Kama hiyo haitoshi baada ya muda mfupi mkulima mwingine Ndugu Rajab Ayoub wa Kijiji cha Mbigiri Wilayani Kilosa alijeruhiwa kwa sime akiwa shambani mwake na wanaodaiwa kuwa ni wafugaji. Aidha yapo matukio kadhaa ya mifugo ya wafugaji kupewa sumu au kujeruhiwa moja kwa moja na wanaodaiwa kuwa ni wakulima.

Mheshimiwa Spika, Ni ishara kuwa matukio kama haya ya mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi yanazidi kutokea kwa sababu serikali imeyafungia maazimio ya Bunge kabatini bila kuchukua hatua za dharura kama ilivyokuwa imeazimiwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kuwa moja ya sababu za migogoro ya ardhi hasa kwa Mkoa wa Morogoro ni baadhi ya viongozi wa serikali za Vijiji na Mitaa ambao sio waaminifu kuuza ardhi mara mbili kwa wakulima na wafugaji na hivyo kuchochea migogoro. Aidha baadhi ya wakulima huuza ardhi kwa wafugaji na baadae kuikana mikataba/makubaliano ya awali waliyofanya na wafugaji.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi na watu wote ambao wamekuwa sehemu ya migogoro ya ardhi kwa kufanya mambo ambayo hayana uadilifu na kusababisha migogoro isiyoisha ndani ya jamii.

3. *Kodi ya Majengo (Property Tax)*

Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha unaokwisha mwezi Juni 2017 serikali iliweka utaratibu wa kisheria kuondoa mamlaka ya Halmashauri kukusanya kodi ya majengo (property tax)na kuipa haki hiyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku serikali ikijua kuwa kodi hiyo ilikuwa sehemu muhimu sana ya mapato ya Halmashauri nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililiona jambo hili kama mkakati wa kuondoa mapato kwa Halmashauri ili kuzipunguzia nguvu Halmashauri nyingi za Majiji ambazo zinaongozwa na Wapinzani. Ieleweke kuwa halmashauri hapa nchini zimekuwa zikikusanya mapato kwa ajili ya kuendesha miradi yake ya maendeleo na shughuli nyingine za kawaida kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato kwa mujibu wa sheria ya fedha ya Halmashauri (Local Government finance Act, 1982) Haukuwa uamuzi sahihi kutunga sheria ya kuondoa chanzo cha mapato cha kodi ya majengo kutoka katika halimashauri nchini .

Mheshimiwa Spika, Kufutwa kwa kifungu kilichokuwa kinazipa Halmashauri jukumu la kukadiria na kukusanya kodi za majengo na kulihamishia TRA kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2016, kifungu cha 38 baada ya kufanya marekebisho kwa kuvifuta vifungu vya 31A na 31B vya sheria ya fedha ya

Serikali ya Mitaa sura 290 kumeziyumbisha sana halimashauri katika kutekeleza majukumu yake kutokana na ukweli kwamba chanzo cha kodi ya majengo kilikuwa ni mojawapo ya chanzo kikubwa cha mapato ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa Ofisi ya Rais TAMISEMI tulieleza wazi kuwa taarifa ya Serikali inaonyesha kuwa kodi ya Majengo iliyokusanywa ni shilingi milioni 4,762.37 kati ya mIlioni 29,004 sawa na asilImia 17.4 tu ambayo ilitarajiwa kukusanywa na TRA.

Mheshimiwa Spika, kwa takwimu ambazo nimerejea katika hotuba hii, ni ishara kwamba hoja niliyoielezea mwaka jana katika Bunge hili ilikuwa ni muhimu kuzingatiwa na serikali kwa sababu ni wazi kuwa TRA haina uwezo wa kufanya kazi ya kukusanya chanzo hiki cha mapato. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kulieleza Bunge hili sababu za kuipa TRA mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo wakati haikuwa imejipanga kimikakati na kimfumo kufanya kazi hiyo, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuleta tena marekebisho ya Sheria ya Fedha ili kurudisha chanzo hiki cha mapato katika ngazi ya Halmashauri kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kuwa baada ya kuziondolea Halmashauri haki ya kutoza kodi ya majengo, Halmashauri nyingi hasa za Vijijini zimeanza kutoza kodi ya majengo kwa wananchi huko vijijini jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi wetu ambao kwa waliowengi hawana vipato vizuri.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kupitia Wizara hii kulieleza Bunge lako tukufu, ni kwa nini wameondoa kodi ya majengo kama chanzo cha mapato na kuruhusu Halmashauri kuanza kuwatoza wananchi wa vijijini kodi ya majengo yao.

Mheshimiwa Spika, Kama serikali bado inang’ang’ania chanzo hiki, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri majengo yagawanywe kwenye madaraja kama vile majengo makubwa ya kibiashara, residential apartments, na majengo mengine makubwa kama itakavyoamuliwa kodi zao zikusanywe na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) lakini majengo madogo ya biashara na nyumba za makazi kodi yao ikusanywe na Halmashauri ili kuongeza ufanisi wa TRA katika ukusanyaji.


4. *Kodi ya Ardhi*

Mheshimiwa Spika, ni takwa la kisheria kupitia kifungu cha 22 cha Sheria ya Ardhi sura 113 kuwa ardhi yoyote inayomilikiwa kwa mujibu wa sheria kulipiwa kodi ya ardhi kama sehemu ya masharti ya miliki ya ardhi nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitambua jukumu hili kwa sababu imekuwa ikilipigia kelele kwa miaka mingi sasa kuwa wamiliki wengi wa ardhi hasa wanaomiliki mashamba makubwa wamekuwa hawalipi kodi ya ardhi wala kuendeleza ardhi ambazo wamemilikishwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina tatizo na hatua zinazochukuliwa na Wizara kuhakikisha kuwa kila mwenye miliki ya ardhi nchini analipa kodi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa. Itakumbukwa kuwa Aprili mwaka huu 2017 Waziri mwenye dhamana ya ardhi alitoa maelekezo kuwa wananchi wote wanaomiliki ardhi iwe imepimwa au haijapimwa wanatakiwa kulipa ardhi.

Mheshimiwa Spika, ni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa agizo hilo la Waziri linaenda kinyume na sheria ya ardhi kwa kuagiza kodi hiyo kulipwa kwa ardhi ambayo haijasajiliwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kusitisha agizo hilo kwa sababu wanakwepa jukumu la kupima ardhi badala yake wanatoa maelezo ambayo ni kinyume cha sheria. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa kama serikali inaona uamuzi wa kutoa maagizo hayo ni tija kwake ni vema ikaleta marekebisho ya sheria hapa Bungeni kuliko kuendelea kufanya hivyo kinyume na taratibu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunapenda kusisitiza kuwa tamko hilo la Waziri linakiuka sheria ya ardhi Na. 4 na Na. 5 ya mwaka 1999 inayotaka kodi ya ardhi ilipwe kwenye maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa kwa kipindi maalum (miaka 33, 66 na 99) tunataka Serikali itoe ufafanuzi juu ya maeneo ambayo hayajapimwa yatalipishwaje kodi na kwa utaratibu upi kwani watu hao hawana nyaraka zozote za umiliki.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka seriakali kuacha kutafuta njia za mkato za kuwakamua wananchi pesa badala yake serikali inatakiwa kuwekeza katika kusimamia maeneo yote ambayo hayajapimwa ili kutoa miliki kwa wahusika kwani kwa kufanya hivyo:-

(i) Itapanua wigo wa mapato ya Serikali
(ii) Itapandisha thamani ya ardhi
(iii) Itapunguza au kuondoa kabisa migogoro ya ardhi
(iv) Itawapa fursa wananchi kutumia ardhi zao kama dhamana katika Taasisi za kifedha
(v) Itavutia Uwekezaji
(vi) Itasaidia utunzaji bora kumbukumbu za ardhi
(vii) Itaweka mandhari nzuri za maeneo husika na mpangilio mzuri wa matumizi yote ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa tamko hilo la serikali ni kukimbia jukumu lake la msingi la kuhakikisha ardhi yote inapimwa na badala yake wanatafuta njia ya mkato ya kuongeza mapato. Kama njia hii itatumiwa na serikali ni maoni ya Kambi Rasmi Upinzani Bungeni kuwa itazalisha migogoro ya ardhi lukuki hasa kwenye Miji, Manispaa na Majiji nchini kwa sababu udanganyifu utakuwa mkubwa na matapeli watatumia sababu za kulipia kodi ya ardhi kama sehemu ya kutaka kupewa miliki ya ardhi.


5. *Watumishi wa Ardhi Katika Halmashauri*

Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge la kumi serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Ardhi wakati huo Mheshimiwa George Simbachawene alitoa ahadi ya serikali kuwa kutokana na malalamiko mengi ya wananchi pamoja na tuhuma na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na watumishi wa idara ya ardhi ya Halmashauri nchini, serikali itahakikisha kuwa watumishi hao wanapokea maelekezo ya moja kwa moja kutoka serikalini na watakuwa wanapokea malipo kama watumishi wa Wizara ili iwe rahisi kupokea maelekezo na usimamizi moja kwa moja kutoka Wizarani pamoja na kuendelea kufanya kazi katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, serikali haikutoa ahadi hiyo kwa bahati mbaya, hiyo ilitokana na hoja za waheshimiwa Wabunge kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja katika Wizara na watumishi wa idara ya ardhi katika Halmashauri mbalimbali nchini jambo linalopelekea watumishi wa ardhi katika ngazi ya Halmashauri kutokuwa na ufanisi na kujihusisha na vitendo visivyo vya uadilifu wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepigwa na butwaa kwa sababu serikali ya awamu ya nne ilikuwa chini ya CCM na serikali ya awamu ya tano ipo chini ya CCM lakini kwa utendaji wa serikali ya awamu ya tano inaonekana kama vile imeshuka kutoka mwezini. Hii ni kutokana na sababu zilizotolewa za kushindwa kutekeleza ahadi ya serikali ya kushindwa kuanzisha mchakato wa kuhamisha ajira ya sekta ya ardhi kutoka serikali za mitaa kwenda serikali kuu.

Mheshimiwa Spika, serikali kupitia randama ya Wizara imeeleza yafuatayo kuhusu kutekeleza ahadi hii;

“Serikali inaendelea na utekelezaji wa dhana ya kugatua madaraka (Development by Devolutions) kwenda katika ngazi za msingi. Hivyo, utaratibu wa kuhamisha ajira za watendaji wa sekta ya ardhi kutoka Halmashauri utakinzana na dhana hii”

Mheshimiwa Spika, hii ni ishara kuwa ahadi na commitment za serikali wanazozitoa Bungeni wanazitoa kwa ajili ya kuwashawishi waheshimiwa wabunge kupitisha bajeti na mipango mingine ya serikali tu na si kuzingatia wanachoahidi mbele ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, Wabunge waliishauri serikali kutokana na uzoefu wa masuala wanayokumbana nayo katika utekelezaji wa shughuli zao majimboni na Waheshimiwa Wabunge walitoa ushauri huo wakizingatia kuwa ipo dhana na mfumo wa D by D na kwa upande wa serikali walitoa ahadi hiyo wakijua kuwa mfumo huo wa utawala upo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kulieleza Bunge lako tukufu sababu za ziada zilizopelekea kutotekeleza ahadi yake iliyoitoa katika Bunge hili.

6. *Kuundwa kwa Mamlaka ya kusimamia Sekta ya Milki nchini (Real Estate Regulatory Authority) *

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 wakati wa mkutano wa kwanza wa Bajeti wa Bunge la kumi, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alishauri umuhimu wa kuundwa kwa mamlaka ambayo itasimamia sekta ya ujenzi hasa ujenzi wa majengo makubwa ambayo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya serikali ikiwa serikali itakitumia vizuri.

Mheshimiwa Spika, hoja hiyo ilitolewa kwa sababu ya hali ya wakati huo iliyoonesha kuwa kulikuwa na ongezeko kubwa la majengo makubwa hasa katika miji mikubwa nchini lakini pamoja na ukuaji huo bado sekta hiyo ilionekana kutochangia fedha za kutosha katika pato la taifa.

Mheshimiwa Spika, katika randama za Wizara hii kwa mwaka wa fedha uliopita , serikali iliahidi kuwa mwaka wa fedha 2016/2017 muswada utakaounda mamlaka ya sekta ya miliki nchini ungeletwa Bungeni na hatimaye kuundwa kwa mamlaka hiyo. Aidha randama za Wizara kwa mwaka huu zinaonesha kuwa muswada huo wa sheria utaletwa kwa mwaka ujao wa fedha. Kambi Rasmi ya Upinzani inaunga mkono kuundwa mamlaka hiyo kama ilivyokuwa imeshauri miaka iliyopita lakini inapata mashaka na nia ya serikali ya kuendelea kuchelewa kuleta muswada huo Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuacha ahadi za mara kwa mara za jambo hilo na sasa ifanye kwa vitendo ili jambo hilo lifike mwisho.

Mheshimiwa Spika, aidha kupitia randama za Wizara serikali imeeleza kuwa tayari imekamilisha maandalizi ya utungwaji wa Sheria ya Mawakala wa Ardhi (Real Estate Agents Act). Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Sheria hiyo ihuishwe ili masuala ya msingi ya sheria hiyo yaunganishwe na Sheria ya Real Estate Regulatory Authority na kuwa sheria moja ambayo itakuwa inasimamia sekta ya miliki na mawakala kwa ujumla.

7. *Malipo ya fidia kwa wananchi*

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Bukoba napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Waziri na Naibu Waziri wa Maji na uongozi pamoja na wasimamizi wa BUWASA (Bukoba Urban Water Supply), kwa kutimiza ahadi iliyotolewa katika Mkutano wa Bunge la Bajeti wa mwaka uliopita wakati nilipoomba ufafanuzi kwenye mshahara wa Waziri ili serikali ianze kulifanyia kazi suala la fidia kwa wananchi wa Kata ya Kahororo waliopisha mradi wa mfumo wa maji taka walipwe fidia zao na serikali.

Mheshimiwa Spika, napenda kushukuru kwa kuwa wananchi hao walilipwa fidia zao ingawa bado wanadai riba za ucheleweshaji malipo ambazo nazo Naibu Waziri wa Maji ameahidi kufuatilia ili walipwe. Napenda kumkumbusha Waziri kuhusu ahadi hii ya serikali ya kulipa riba ya fidia yao ili kumaliza kabisa malalamiko yao dhidi ya serikali.

(a) *Malipo ya Fidia ya Hisani kwa Wananchi wa Mloganzila*

Mheshimiwa Spika, kuhusu mgogoro wa toka kabla ya mwaka 2004 kati ya wananchi wa Mloganzila waliohamishwa kupisha ujenzi wa MUHAS Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati ikijibu swali la Mbunge wa Kibamba John Mnyika tarehe 3 Februari 2017 ilieleza kuwa Serikali pia ililipa kiasi cha Sh. 8,067,904,700 kwa ajili ya fidia ya maendelezo katika ardhi kwa wananchi 1,919 katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2010. Aidha ilijibu kuwa mwaka 2011 Serikali ilitenga kiasi cha sh. 1,610,374,700 kwa ajili ya fidia ya wananchi 619 waliosalia. Hata hivyo, kwa kipindi chote Serikali imekataa kuwalipa wananchi hao fidia ya ardhi pamoja na wananchi hao kupewa ardhi hiyo na Serikali yenyewe na kupatiwa hati ya kijiji cha Kwembe.


Mheshimiwa Spika Tarehe 20 Mei 2015 Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa maelekezo ya Rais ilitoa ahadi ya kuwalipa wananchi hao fidia ya hisani au mkono wa kwaheri ya shilingi milioni mbili kwa kila mwananchi ahadi ambayo miaka miwili imepita bila ya kutekelezwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepitia vitabu vya bajeti na kubaini kwamba hakuna fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya kufanya malipo hayo. Serikali itoe maelezo ni kiasi gani kwa sasa kinatarajiwa kutolewa kwa wananchi, ni kwanini hakuna fedha zilizotengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na ni lini malipo hayo yanatarajiwa kufanyika?

(b) *Bomoa Bomoa ya Kimara- Kiluvya Jijini Dar es Saalam*

Mheshimiwa Spika, Katika miaka 1970, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya utawala wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere ikiwa inatekeleza sera za chama cha TANU ilianzisha Vijji vya Ujamaa katika kutekeleza mpango kabambe wa “Operesheni Vijiji” ambapo wananchi waliondolewa pasipo hiari yao toka ardhi, mashamba na makazi yao na kuhamishiwa katika vijiji vya ujamaa vilivyoanzishwa na kisha halmashauri za vijiji zilizokuwa na mamlaka kisheria ya kugawa ardhi, kuwagawia ardhi kwa ajili ya makazi na kilimo kuanzia yalipo mawe yanayoonyesha mwisho wa hifadhi ya barabara ya wakati huo yaliyokuwa mita 22.85 tu toka katikati ya barabara, pande zote mbili.

Mheshimiwa Spika, Katika Mkoa wa Dar es Salaam miongoni mwa vijiji vya ujamaa vilivyoanzishwa kando kandao ya barabara ya Morogoro ni pamoja na:-


1) Vijiji vya Kimara A na B

2) Kijiji cha Mbezi kilichokuwa na hati ya usajili namba DSM/VIJ/08.

3) Kijiji cha Kibamba kilichokuwa na hati ya usajili namba DSM/VIJ/36

4) Kijiji cha Kiluvya, ardhi yake ilipimwa na kijiji kupatiwa hati miliki ya kijiji yenye namba 34125 iliyotolewa tarehe 2 Julai 1988.

Mheshimiwa Spika, Uthibitisho wa kwanza kuwa upana wa hifadhi ya barabara ya Morogoro kwa eneo la Ubungo hadi TAMCO Kibaha ni mita 22.85 tu na sio hadi mita 121.92 ni kitendo cha, Wizara iliyokuwa na dhamana ya usimamizi wa barabara kupanda mawe yaliyoonyesha mwisho wa hifadhi ya barabara mita 22.85 na sio hadi 121.92 toka katikati ya barabara, pande zote mbili. Hatua hiyo iliashiria kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo ilikamilisha utwaaji wa ardhi kwa upana wa mita 22.85 tu kati ya 121.92 zilizokuwa zimetambuliwa awali kwa ajili ya kutwaliwa kupitia Government Notice 161 ya 5/5/1967 kwa kulipia fidia.

Mheshimiwa Spika, Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana wakati wa ujenzi wa barabara ya Morogoro mwanzoni mwa miaka ya 1970 nyumba za wananchi zilizoangukia ndani ya mita 22.85 ndio zilizotakiwa kuondolewa, baadhi yao kutakiwa na mamlaka za serikali kujenga upya nyumba zao nje ya mita 22.85 hadi leo baadhi ya wananchi hao bado wapo hai.

Mheshimiwa Spika, Uthibitisho wa pili, pale Serikali ilipowahamishia wananchi katika vijiji vilivyotajwa hapo juu, ikawajengea majengo ya huduma mbali mbali za kijamii kama vile Shule ya Msingi ya Mbezi katika Kijiji cha Mbezi. Zahanati ya Kibamba Hospitali na nyumba za watumishi katika Kijiji cha Kibamba n.k. Majengo haya yalijengwa nje kidogo ya mita 22.85 toka katikati ya barabara. Mheshimiwa Spika, Hivyo basi ujenzi na uwepo wa majengo ya Serikali ndani ya eneo ambalo baadaye toka mwaka 2000, lilianza kudaiwa ni sehemu ya hifadhi ya barabara ya Morogoro ni uthibitisho kuwa hifadhi ya barabara halali kwa barabara ya Morogoro kwa eneo la Ubungo hadi Tamco Kibaha ni mita 22.85 tu, toka katikati ya barabara, pande zote mbili.

Mheshimiwa Spika, Kuanzia mwaka 2000, sambamba na makazi na majengo ya wananchi, majengo ya Serikali yaliyoko nje ya mita 22.85 toka katikati ya barabara yamekuwa mara kwa mara yakipata misukosuko ya kuwekewa alama za X na hata kubomolewa kwa madai eti yako ndani ya hifadhi barabara ya Morogoro.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuhoji hivi kweli Serikali inaweza kuvamia hifadhi za barabara na kujenga majengo ya shughuli zingine za maendeleo? Na kwanini Serikali ifanye hivyo wakati Tanzania bado ina ardhi tele?

Mheshimiwa Spika, Uthibitisho wa tatu, ni taasisi za kiserikali yaani Halmshauri ya Jiji la Dar es Salaam, na maafisa ardhi wa Wilaya na Jiji kuwapimia wananchi wa vijiji vilivyotajwa katika hotuba hii ambapo ardhi waliyogawiwa wakati wa operesheni vijiji kwa kuacha hifadhi ya barabara ya upana wa mita 22.85 tu; na Wizara hii yenye dhamana ya masuala ya ardhi kutoa hati miliki ambazo zinaendelea kulipiwa kodi ya ardhi hadi sasa. Hii ni licha ya kuanzia mwaka 2000, kuwepo madai kutoka Wizara yenye dhamana ya barabara kuwa hifadhi ya barabara kwa eneo hilo ni mita hadi 121.92 toka katikati ya barabara, pande zote mbili kwa eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, Uthibitisho wa nne, Mwaka 1985, mkazi mmoja wa Kimara aitwaye Ndg Joseph Marwa aliiandikia barua Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi akitaka kufahamu kama amejenga ndani ya eneo la hifadhi ya barabara ya Morogoro, na kujibiwa kwa barua yenye Kumb. Na TRM/0.10/9/47, kutoka Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi ya Tarehe 20 Agosti 1985 iliyowekwa saini na Ndg A.K Fuko kwa niaba ya Katibu Mkuu iliyosema kuwa”Mnamo tarehe 14/08/1985 Tumetuma vijana toka ofisi ya Chief Engineer Matengenezo kwenda kupima na kubaini wewe upo mita 33 toka katikati ya barabara hivyo upo nje ya hifadhi ya barabara kwa mita kumi {10.m} hivyo hukuhusika na fidia na hupaswi kuondoka”.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inajiuliza licha ya uthibitisho wote huu wa nyaraka, matendo ya wizara, idara na taasisi mbalimbali za kiserikali kutambua kuwa upana halali wa hifadhi ya barabara ya Morogoro kwa eneo la Ubungo hadi TAMCO Kibaha ni mita 22.85 tu, pande zote mbili na sio hadi 121.92.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na mazingira maalum ya kutaka kulinda umiliki wa ardhi ya wananchi waliohamishiwa katika vijiji vya ujamaa, mwaka 1999 Serikali iliwasilisha muswada wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na 5 ya 1999, ambao ulipitishwa na bunge na kuridhiwa na Rais Benjamin Mkapa tarehe 15 Mei 1999.

Mheshimiwa Spika, Kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2000 hadi 2004 wananchi wanaoishi pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kati ya Ubungo na TAMCO Kibaha ndipo wamejikuta katika sintofahamu juu ya hatma ya mali na maisha yao baada ya mkandarasi kutumwa kupanda mawe na miti ili kuonyesha mwisho wa hifadhi ya barabara ni mita 121.92 kutoka katikati ya barabara, badala ya mita 22.85 bila kulipwa fidia stahilifu. Aidha yaliwekwa pia mabango yakuonyesha hivyo, huku mawe yaliyopandwa na COMWORKS miaka ya 1970 yanayoonesha hifadhi ya barabara hiyo ni 22.85 kutoka katikati ya barabara, ambayo hadi leo yapo na yanapuuzwa.

Mheshimiwa Spika, Kutoka wakati huo nyumba za wananchi wanyonge zikaanza kukosa wapangaji, wamiliki wa ardhi wakashindwa kuendeleza ardhi zao, wawekezaji mbali mbali wakashindwa kuwekeza n.k. Ni kutokana na vitendo hivi vya ardhi ya wananchi kutwaliwa isivyo halali na pasipo wamiliki kulipwa fidia yoyote kwa kupandwa mawe, na mabango ya barabara eneo lote toka Ubungo mwisho hadi Kiluvya, hakuna huduma ya kijamii kama vile mabenki, maduka makubwa [Shopping malls] wala shughuli kubwa za kiuchumi zinazofanyika, na hivyo kuleta athari mbaya za kijamii na kiuchumi kama vile kukosekana kwa ajira na njia za wananchi kujikimu kimaisha.

Mheshimiwa Spika, Kibaya zaidi zoezi la upandaji mawe na mabango husika wakati huo halikuheshimu ardhi inayomilikiwa kwa hati miliki na zinazolipiwa hadi na Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Ardhi hizo ziliingiliwa isivyo halali na wamiliki wake wamekuwa wakizuiwa kuendeleza maeneo yao wanayoyalipia. Yote haya yamekuwa yakifanyika isivyo halali kwa njia za vitisho vya kubomolewa. Idadi kubwa sana ya makazi ya wananchi yamebomolewa isivyo halali kwa madai kuwa yako katika hifadhi za barabara, kitu ambacho si kweli.

Mheshimiwa Spika, Tatizo lingine linalojitokeza ni utekelezaji wa kibaguzi wa Sheria ya barabara Namba 13 ya 2007 na Kanuni zake, Sheria na Kanuni hizo ziko wazi kuwa hifadhi ya barabara ya Morogoro ni kama ifuatavyo:-

a) Jengo la Umoja wa Mataifa (la Zamani) hadi Km 10 (Dar es Salaam) ni Mita 60

b) Km 10 hadi 16 ni mita 90

c) Km 16 hadi 37 ni mita 120 (Mbezi hadi Tamco baada ya barabara ya (TAMCO –Vikawe-Mapinga)

d) Km 37 hadi Km 69 mita 60

e) Km 69 hadi Km 70 ni mita 60 (Ruvu darajani) na inayobaki kwenda Morogoro ni mita 60

Mheshimiwa Spika, pamoja na kurejea kwa urefu kuhusu mgogoro wa kuongeza upana wa barabara hiyo wakati huo ukiwa ni wa mita 22.8 na kuongezwa hadi 121.9, hivi karibuni Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam ilitoa notisi ya siku 28 kwa wakazi wa Kimara hadi Kiluvya kuwataka kubomoa nyumba na kuondoa mali ambazo inadaiwa kuwa majengo na mali hizo yapo katika hifadhi ya kipande hicho cha barabara ya Morogoro.

Mheshimiwa Spika, pamoja na notisi hiyo kutolewa kwa wananchi ieleweke kuwa Wizara hii ilishatoa hati za miliki ya ardhi na leseni mbalimbali za makazi kwa wananchi hao toka miaka ya 70, 80 na 90. Aidha TANROADS imeongeza upana wa barabara kutoka mita 60 katikati ya barabara kila upande hadi 121.9. Hii maana yake ni kuwa upana wa barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kiluvya itakuwa mita 240 kutoka 121.9 za awali.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kuwa kuna shauri lililopo Mahakamani kuhusu jambo hili lakini ingependa serikali ieleze Bunge lako tukufu kuwa ni upana upi hasa wa barabara ya Morogoro ambao upo kwa mujibu wa sheria unaotambuliwa na serikali zaidi ya ule ambao nimeurejea katika hotuba? Hii ni kutokana na upana wa barabara hii kubadilika mara kwa mara jambo ambalo linaathiri makazi na shughuli za kiuchumi za wananchi.

(c) *Migogoro ya Ardhi ya Pugu Kajiungeni, Kipawa na UVKIUTA*

Mheshimiwa Spika, mgogoro mwingine wa ardhi upo pia katika Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Ukonga, kata Pugu eneo la Pugu Kajiungeni. Hili lilikuwa eneo la wazi ambalo lilikuwa linatumiwa kwa matumizi ya mnada na michezo kwa vijana wa Pugu. Hata hivyo jambo la kushangaza ni kuwa eneo hilo limeuzwa kinyemela na huku ikifahamika kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri aliwapa wajasiliamali wadogo vijana na akina mama ili waweze kufanya biasharaza ndogo ndogo.


Mheshimiwa Spika, jambo ambalo limewastua wananchi wa eneo hilo ni uvamizi wa usiku wa manane ambao ulipelekea kuvunjwa kwa mabanda yote ya wafanyabiashara ndogondogo na hadi sasa mali za waliokuwa wanafanya biashara eneo hilo zimepotea. Mgogoro huo umekuwa mkubwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dae Es Salaam inazo taarifa za mgogoro huu lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.


Mheshimiwa Spika, mgogoro mwingine wa ardhi ni wa wananchi wa Kipawa ambao walihamishwa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Baada ya wananchi kuhamishwa katika eneo hilo walipelekwa maeneo ya Zavala, Kinyamwezi Nyeburu na Kipawa mpya kwenye Kata ya Buyuni. Waliohamishwa kutoka Kipawa kupisha ujenzi wa ndege hawakulipwa na wala kupewa maeneo mapya na kule walikopelekwa baadhi yao wamepewa maeneo ya watu wa Buyuni. Huu ni mgogoro mkubwa na hadi sasa hakuna majibu ya serikali na wananchi wanaendelea kugombania ardhi.

Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro mwingine mkubwa wa tangu 1998, maarufu kama UVKIUTA. UVKIUTA ulikuwa ni Umoja wa Vijana wa Kikristo Tanzania ambao wanahusisha Kata za Chamazi Wilaya ya Temeke na Kivule Wilaya ya Ilala.

Mheshimiwa Spika, UVKIUTA wanalalamikiwa na wananchi kuwa wameongeza eneo ambalo awali hawakuwahi kuwa nalo ambapo baada ya kuongeza eneo lao limewaathiri wananchi wa Mtaa wa Magole Mkombozi katika Kata ya Kivule ambao awali eneo lao halikuwa la UVKIUTA.

Mheshimiwa Spika, Eneo hili anayetajwa kuhusika na mgogoro huo ni anayedaiwa kuwa mlezi wa UVKIUTA ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ndg Jordan Rugimbana. Wananchi walipewa eneo wakati wa Mwalimu Nyerere lakini Ndugu Rugimbana na timu yake wameongeza kwa nguvu eneo hili kwa kuchukua maeneo ya wananchi na kwa sasa nguvu kubwa imekwisha tumika na kuvunja nyumba zaidi ya 700.

Mheshimiwa Spika, Ndugu Rugimbana ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa ujanja ujanja anadai eneo hilo liko Wilaya ya Temeke lakini wananchi katika eneo hilo walipiga kura zao Kata ya Kivule wilaya ya Ilala. Lakini kwenye suala hili la uporaji wa ardhi yao inadaiwa kuwa eneo hilo liko Temeke hali inayopelekea Mbunge wa Ukonga na Mwenyekiti wa mtaa wa Kivule Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara ashindwe kutetea maslahi ya watu wake. Aidha, zipo taarifa kuwa hata UVKIUTA yenyewe kwa sasa haipo kitaasisi bali ni ujanja wa watu wachache.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri kuangalia ni jinsi gani atawarudishia imani wananchi wa maeneo hayo kwa kuwa Serikali ipo na kimsingi inatakiwa kusimamia sheria kwa kuwa hakuna mtu aliyepo juu ya sheria na haki za wananchi zinalindwa.


(d) *Mgogoro wa Mipaka kati ya Vijiji na Hifadhi ya Wanyama ya Serengeti*

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Wanyama ya Serengeti ilianzishwa mwaka 1968 kwa mujibu wa sheria za nchi huku mipaka ya Hifadhi hiyo ikitajwa na kuwekwa wazi kwenye gazeti la serikali lililoanzisha rasmi mbuga huyo.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mgogoro kati ya Hiafdhi ya Serengeti na Vijiji vya Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikiri na Bonchugu kutokana na Hifadhi hiyo kuhamisha mipaka mara kwa mara tangia Hifadhi hiyo ianzishwe.

Mheshimiwa Spika, ipo ramani mpya ya mwaka 2008 ambayo imelalamikiwa na wanachi kwa kuwa ramani hiyo inapingana na mipaka ya awali ambayo iliwekwa kuonesha mipaka ya Hifadhi jambo ambalo linafanya maeneo makubwa ya Vijiji hivyo kuwa sehemu ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa serikali iliunda Tume inayohusisha Wizara tano lakini cha kushangaza Halmashauri za Vijiji wala Wilaya hazikuhusishwa wakati Tume ikitafuta suluhisho la mipaka ya hifadhi na Vijiji. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inaunda Tume nyingine huru kushughulikia mgogoro huu na ambayo itawahusisha viongozi wa Vijiji na Halmashauri ili kupata suluhisho la mgogoro na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao.

(e) *Mgogoro wa Mipaka kati ya Mitaa ya Kisopwa, King’azi na Mloganzila*

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu kabla hata ya kuundwa kwa Manispaa mpya ya Ubungo katika Mkoa wa Dar es Salaam kumekuwa na mgogoro wa mipaka katika Mitaa ya Kisopwa, King’azi na Mloganzila ambapo pamoja na taarifa kuhusu mgogoro huo kuwasilishwa na Mbunge wa Ubungo wakati huo Mheshimiwa John Mnyika bado kuna hali ya sintofahamu kuhusu mipaka ya Mitaa ambapo mamlaka za serikali za mitaa hiyo zimekuwa zikigombania mpaka kukusanya mapato kutoka kwa wananchi huku suala la mipaka likiwa bado halijaamuliwa.

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Kinondoni wakati huo pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe zilishindwa kufikia muafaka kuhusu mipaka ya Mitaa hiyo mpaka leo ambao imeundwa Manispaa mpya ya Ubungo. Aidha ieleweke kuwa wananchi waliowengi wa Mitaa wameandikishwa kupiga kura katika Jimbo la Kibamba katika Manispaa ya Ubungo na iliyokuwa Manispaa ya Kinondoni ilijenga huduma za kijamii ikiwemo shule, zahanati na kulipa fidia katika maeneo hayo. Hata hivyo linapokuja suala la kukusanya tozo mbalimbali Halmashauri ya Kisarawe hukusanya tozo hizo na kuleta mgogoro. Aidha, utata mkubwa zaidi unaibuka baada ya ujenzi wa Chuo na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishu cha Muhimbili (Muhimbili University of Health and Allied Science- MUHAS) ambapo hulazimika kuwajibika kwa halmashauri mbili tofauti.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imeshangazwa na serikali kuchukua muda mrefu kupata suluhu ya tatizo hili la muda mrefu huku serikali yenyewe kupitia TAMISEMI ikiwa ndiyo inaratibu suala la kutangaza maeneo ya utawala nchini.

Mheshimiwa Spika, Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa kuna Kamati iliyoundwa na Naibu Waziri wa Ardhi kwa ajili ya kuchunguza na kushauri serikali kuhusu mgogoro huo wa mipaka ya maeneo ya utawala. Kambi Rasmi ya Upinzani inashangwaza na hatua hiyo ya Serikali kutaka ushauri upya wakati ambapo aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda walishatoa majibu ya kwamba maeneo hayo yalipaswa kuwa Manispaa ya Kinondoni ambayo sasa imegawanywa na kuzaliwa Manispaa ya Ubungo.

(f) *Mgogoro kati Wananchi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi*

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa za mgogoro kati ya Wananchi wa Vitongoji vya Nzuguu, Nzegamila na Milumbi vilivyopo Kata ya Idodyandole Wilaya mpya Itigi ambapo wanamlalamikia Mkurugenzi wa Halmashauri kuamua kuwaondoa wananchi katika Viitongoji vyao ili eneo hilo litumike kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na malalamiko mengine dhidi ya Mkurugenzi wao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona ni vema iwasilishe jambo hili ili ikiwezekana serikali ichukue hatua za kuona njia bora za kufuatilia malalamiko haya kabla mgogoro haujawa mkubwa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kuwa ofisi ya Waziri Mkuu imeandikiwa kwa kina mgogoro huu na kwa hiyo inaamini hatua stahiki zitachukuliwa. Taarifa zinaonesha kuwa takribani kaya 250 zimeamriwa ziondoke katika Vitongoji hivyo ili kupisha mwekezaji.



8. *Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuingilia majukumu ya Mabaraza ya Ardhi*



Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Ardhi yameanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 167(1) cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na kifungu cha 62 (2) cha Sheria ya Ardhi ya Kijiji Namba 5 ya mwaka 1999 ambapo vifungu hivyo vimeelekeza namna ya kuundwa kwa Mahakama za ardhi.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 22 cha Sheria ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ardhi kinampa mamlaka Waziri kuunda Mabaraza ya ardhi kwa ajili ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, Ieleweke kuwa ukiachia Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi na Mahakama ya Rufaa kama zilizotajwa kwenye sheria nilizorejea, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya, Baraza la Kata na Halmashauri ya Kijiji zina hadhi ya Mahakama (quasi-judicial) katika kushughulikia migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Mabaraza ya Ardhi kupewa mamlaka hayo ya kisheria kushughulikia utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini kumekuwa na tabia ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuingilia mamlaka za Mabaraza ya ardhi kwa kauli au kutoa maelekezo kwa Wenyeviti ambao wamepewa mamlaka ya kuamua masuala ya migogoro.

Mheshimiwa Spika, tabia hii ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuingilia Mabaraza ya Ardhi haijaanza hivi karibuni, Gazeti la Nipashe la tarehe 17 April 2010 liliripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wakati huo aliamuru kumtoa ofisini Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kigoma Mheshimiwa R.J Kim kwa kuwatumia Usalama wa Taifa na Polisi.

Mheshimiwa Spika, sababu za Mkuu wa Kigoma kutoa amri ilidaiwa kuwa ni kitendo cha Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi kukiuka maelekezo ya Mkuu wa Mkoa mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, tabia hiyo ya wakati huo haijaachwa kutokana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kuingilia utendaji wa Mabaraza ya Ardhi kwa kauli au kwa kutoa maelekezo. Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni alinukuliwa akitoa maelezo ya kupinga maamuzi ya Baraza la Wilaya la Kinondoni kwenye moja ya hukumu za Baraza hilo akijua kuwa njia ya kupinga maamuzi hayo ni kwa njia ya rufaa.

Mheshimiwa Spika, aidha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro mwezi Aprili mwaka 2017 alinukuliwa na kituo cha radio cha Abood cha Mkoani Morogoro akiwataka wananchi wa Wilaya hiyo kuwa wanaweza kupeleka taarifa za migogoro kwake kabla ya kuiwasilisha kwenye Mabaraza ya Ardhi.

Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa hata Bungeni inakatazwa kuzungumzia mwenendo wa mashauri yaliyopo Mahakamani. Aidha serikali imekuwa ikitoa sababu za mashauri kuwa Mahakamani au kwenye Mabaraza ya maamuzi na kukataa kujibu hoja mbalimbali. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa kauli hapa Bungeni kama kwa sasa Wakuu wa Wilaya wamekuwa sehemu ya Mabaraza ya Ardhi nchini. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia waraka wa TAMISEMI kama ilivyoazimiwa na Bunge kutolewa kuweka wazi kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa kutoingilia utendaji wa Mabaraza ya Ardhi waache utaratibu wa rufaa ufuatwe.

9. *NHC na Nyumba za Bei Juu*

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linafanya kazi zake kibiashara na hivyo ni lazima shirika hilo litengeneze faida kutokana na mauzo au upangishaji wa nyumba zake nchini kote.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilishatoa maoni hapa Bungeni kuitaka serikali kuondoa baadhi ya kodi kwenye nyumba za NHC ili kuiwezesha NHC kujenga nyumba za bei nafuu na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki nyumba bora na hivyo kupunguza changamoto ya wananchi kuwa na makazi duni nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakumbushia ushauri wake mwingine iliyotoa katika Bunge la kumi kuhakikisha kuwa serikali inashusha kodi ya vifaa vya ujenzi na kupunguza bei ya vifaa hivyo ili kuwezesha wananchi wenyewe kujenga nyumba zao kuliko kutegemea nyumba za NHC ambazo kimsingi hazimgusi mwananchi wa hali ya chini.

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi hasa wa mijini kukosa makazi na wengine kulala mitaani kwa sababu ya kushindwa kulipa pango la nyumba. Kambi Rrasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kulieleza Bunge lako tukufu ni hatua gani ambazo wamezichukua kuhakikisha kuwa wanapunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM inapaswa kutambua kuwa kuna ukuaji wa kasi wa Sayansi na Teknolojia. Leo hii ukitafuta taarifa kupitia mtandao wa google utapata taarfia nyingi juu ya uwepo makampuni mengi katika nchi zinazoendelea na za uchumi wa kati yanayojenga nyumba za bei ya thamani hata dola 4500 zenye kutumia teknolojia ya vifaa nafuu lakini nyumba imara na maridadi.

Mheshimiwa Spika, Kama NHC upeo wao ni hizo nyumba wanazoziita za bei nafuu (milioni 40) ambazo watanzania masikini hawawezi kuzimudu, kwanini Seriklai isiruhusu hayo Makampuni yakaja hapa Tanzania na kupata fursa ya kuonesha namna wanvyoweza kujenga nyumba za bei nafuu?

Mheshimiwa Spika, Na kwa kuanzia kama Pilot Study hizo kampuni ziruhusiwe zije Bukoba kwa gharama za watu wenyewe, ili ziwajengee wananchi walioathiriwa na tetemeko na kwani bado baadhi yao wanalala kwenye maturubai kwa kukosa uwezo wa kuzijenga upya au kuzikarabati nyumba zao.

10. *Mradi wa Kuwezesha Umilikishaji wa Ardhi (Land Tenure Support Programme)*

Mheshimiwa Spika, Mradi huu ambao unafadhiliwa kwa pesa za nje (Billioni 15) na za ndani (Billioni 2) ulioanza kutekelezwa Mkoani Morogoro (Ulanga, Malinyi na Kilombero) unasuasua sana kutokana na ukosefu wa fedha. Bajeti ya 2016/2017 ulitengewa shilingi bilioni 13 fedha za ndani na shilingi bilioni 10 fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, Jambo la kustaajabisha ni kuwa hadi kufikia Februari, 2017 fedha za ndani zilizotolewa ni milioni 400 tu ambazo ni sawa na 29.2% na fedha za nje ambazo ni bilioni 3.4. Kambi ya Upinzani inapenda kujua hivi kwanini Serikali inaendela na mambo yake ya kujipangia mambo makubwa isiyokuwa na uwezo wa kugharamia au kuyafanya?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa tabia hii ya kutenga fedha nyingi wakati fedha hazitolewi kwa ukamilifu wake ni kuwaghilibu wananchi. Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji serikali, ni kwa nini isijipangie mambo machache na kwa priorities (vipaumbele) yanayoendana na mapato halisi ya kifedha? Hii tabia imeendelea kutupeleka kwenye usemi wa “mtaka vyote hukosa kwa pupa vyote” tunatawanya kidogo tulichonacho au tunachopata pasipo ufanisi wowote.



11. *Kufutwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA)*

Mhehsimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inashukuru hatimaye CDA imefutwa kwa tamko la Mheshimiwa Rais baada ya mapambano ya muda mrefu ya wananchi wakiongozwa na Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na UKAWA kwa ujumla. Lakini lazima tuyajua matatizo yaliyoachwa na CDA ili wale waliokabidhiwa (Manispaa ya Dodoma) wayajue wayaepuke na yaliyopo ili ufumbuzi kama ifuatavyo;

(i) Wapo wananchi takribani 1000 ambao hawana makazi baada ya nyumba zao kuvunjwa bila fidia. Maeneo hayo ni pamoja na Njedengwa nyumba 270, Msangalale nyumba 35, Itega nyumba 200, Amani nyumba 107, Kisasa nyumba 5, Chinyoza nyumba 63 na Mkabama nyumba 10 na Mbuyuni nyumba 37. Serikali ituambie inaielekeza nini Manispaa ya Dodoma kulitatua hili?

(ii) CDA ilishindwa kusimamia kwa haki upimaji wa viwanja na kulipa fidia stahiki kwa wananchi wenye mashamba yao yaliyoingiliwa.

(iii) CDA iliviruhusu au kufumbia macho baadhi ya maofisa wake kufanya ufisadi wa viwango vya juu na baadhi ya maofisa kujimilikisha viwanja lukuki. Je Serikali inaielekeza nini Manispaa ya Dodoma kukabiliana na mambo hayo?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inaielekeza Manispaa ya Dodoma kufanya tathmini ya miradi ya iliyotekelezwa na CDA kwa ujumla ili kuona namna ya kutatua mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, Manispaa ya Dodoma ihakikishe kuwa inawashirikisha wananchi wa Dodoma wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya kusimamia ardhi ili kuepuka migogoro ya ardhi (nimeambatanisha baadhi ya migogoro ya CDA na wananchi kama ilivyoelezwa na Kamati Teule ya Bunge).

12. *Miradi ya Urasimishaji*

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za kibajeti Wizara imeshindwa kuhudumia miradi ya urasimishaji kama vile Mradi wa Dar es Salaam maeneo ya Kimara ambao ulikuwa wa majaribio (pilot area) ili baadaye uende nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, Mradi huo umekwama kwa kukosa fedha. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri Serikali kuongeza nguvu kwa utaratibu wa kutumia sekta binafsi kuwezesha huo urasimishaji kwa mfumo wa (PPP). Aidha, tunashauri Serikali iweke utaratibu wa kuingia ubia na Sekta binafsi katika mpango wa PPP ili kuja kurejesha gharama za washirika kupitia kodi zitazokusanywa baada ya urasilimishaji huo.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na wananchi wengi kuhangaika na kujibana kununua ardhi na wengine kupenda kujenga nyumba na hata kuitikia wito wa kurasimisha mashamba na makazi kwa kutumia wapimaji wa Makampuni binafsi, wengi wanakwazwa kupata hati miliki kutokana na gharama kufikia huko kuwa juu sana hasa gharama ya kitu kinachoitwa “premium” Mfano mwananchi anaweza kununua ekari moja ya ardhi kwa shilingi Milioni 2 akajigharamia upimaji lakini Serikali ikamtoza gharama za kuandaa hati kwa zaidi ya milioni 2.5.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kuitaka Serikali kuangalia upya viwango mbalimbali vya tozo zinazotozwa katika kuipata Hati miliki. Pia tunashauri Serikali iweke utaratibu unaoainisha bei elekezi kwa Makampuni binafsi yanayofanya shughuli za upimaji na gharama hizo za shughuli ya upimaji kuwekwa wazi kwa wananchi ili kuweka uwiano ulio sawa wa bei kwa maeneo yote ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Aidha tunashauri makampuni haya binafsi yapewe ushirikiano mzuri na ofisi za Serikali na hasa Halmashuri kwani imethibitika wapo Maafisa wa Serikali hasa Idara za ardhi ambao wanaziona Kampuni hizi zimeingia kuzuia maslahi yao waliyokuwa wamezoea hapo kabla.

Mheshimiwa Spika, Misimamo na ushindani wa itikadi za kisiasa nao umeonekana kuwa kikwazo kwa badhi ya maeneo. Mfano mzuri ni Mji mdogo wa Katoro Geita ambapo ramani imeandaliwa tangu mwaka 2015 ambapo Mtaa wa Califonia ulipimwa na kupatikana viwanja 1462 ikapelekwa wizarani na ikarudi. Kazi iliyokuwa imebaki ilikuwa ni kupima kwa maana ya kuweka becons.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kazi hizo zote kugharamiwa na kampuni binafsi iliyopewa kazi hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa mkataba pale Katoro siasa za vyama za ushindani zimechukua nafasi kubwa kuliko kazi inayopaswa kufanyika.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuyatolea tamko maeneo kama hayo ambayo Viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia mambo wanakuwa sehemu ya kukwamisha michakato ya urasimishaji makazi kwa wananchi kwa sababu ya itikadi kisiasa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tunayashukuru na kuyahimiza maeneo yote ambayo yamekuwa na mwamko katika utekelezaji wa mpango huu wa urasimishaji ili waendelee kwa kasi zaidi, kwa mfano Kata mbalimbali za Bukoba Town, Karagwe Mtaa wa Katome- Ruzinga, Kyaka Wilaya ya Misenyi, Mwanza Wilaya ya Ilemela na Nyamagana na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Spika, Aidha tunatoa shukurani kwa Waziri wa Ardhi kwa hamasa ambayo amekuwa akiitoa katika zoezi hili la urasimishaji wa makazi na hata kuhudhuria yeye binafsi kwenye hafla mbalimbali za kukabidhi hati. Tunaendelea kusisitiza kuhusu Wizara kuendelea kutoa hamasa na elimu kwa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kurasimisha makazi na ardhi zao.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuondoa ukiritimba na kero ambayo imejitokeza kwa baadhi ya Wilaya zinazowataka watu waliopima maeneo yao kufuata hati zao ofisi za Kanda wao wenyewe. Tunashauri maafisa wa ardhi ndani ya Halmshauri wawe wakizifuatilia hati hizo kwenye Ofisi za Kanda ili wananchi waweze kuzichukua kwenye ofisi za Halmashauri zao.

13. *Hati za Kimila*

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kutambua umuhimu wa hati za kimila hasa kwa wananchi wa Vijijini lakini Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa zoezi hili linasuasua na haliendi kwa kasi inayotakiwa na sehemu nyingi utoaji wa hati hizi umesimama. Serikali ilieleze Bunge hili ni kwanini zoezi hili haliendelei kama inavyopaswa?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona sababu mojawapo inaweza kuwa ni kutothaminiwa kwa hati hizo katika taasisi nyingi za kifedha zinazotoa mikopo kama zilivyo hati za kawaida. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunaitaka Serikali ndani ya muda muafaka ilete ndani ya Bunge takwimu zinazoonyesha ni hati za kimila ngapi na maeneo zilizopo na ni wa mabenki gani zimetumika kuchukulia mikopo. Na mikopo hiyo ni ya kiasi gani cha fedha.

Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zitasaidia wananchi kuona umuhimu wa kuwa na hati hizo lakini pia kuwafanya Waheshimiwa Wabunge kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi kuunga mkono zoezi hili na hatimaye kujipatia hati zao kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.

14. *Upungufu wa Watumishi wa Sekta ya Ardhi*

Mheshimiwa Spika, Halmashauri nyigni zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa Sekta ya Ardhi kitu kinachofanya huduma za ardhi yaani kupanga Miji na kufanya uthamini na kutoa Hati Miliki kuwa duni.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kutoa mfano mmoja tu wa Halmashauri ya Ngara ambayo haina mtaalam yeyote wa Sekta ya Ardhi. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa tatizo hili liko katika Halmashauri nyingi nchini jambo ambalo linarudisha nyuma shughuli mbalimbali za sekta ya ardhi nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inakuwa na mpango endelevu wa kuhakikisha Halmashauri zote zinakuwa na Watumishi wenye utaalamu wa masuala ya ardhi ili kurahisisha huduma kwa wananchi lakini pia kuepuka migogoro isiyo ya lazima kutokana na kukosekana wataalamu hao.

15. *Mashamba ya Ushirika Yarudishwe kwa Wananchi*

Mheshimiwa Spika, pamoja na kutambua kuwa masuala ya ushirika yanashughulikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lakini Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi msimamo wake kuwa kwa kuwa miliki ya ardhi nchini husimamiwa na Wizara hii ni vema tukaonesha japo kwa ufupi masuala ya ardhi yaliyopo chini ya Ushirika ili serikali ichukue hatua za dharura.

Mheshimiwa Spika, Lipo shamba la Garagagua lilipopo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro ambalo lina ekari takribani 3400 ambalo awali lilikuwa chini ya Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU). Kutokana na ushirika huo kushindwa kulipa deni la mkopo uliotolewa na Benki ya CRDB, Benki hiyo ililazimika kuliuza kwa mnada kwa mwekezaji ambae pia ni mmiliki wa mashamba ya Kifufu maarufu kwa kilimo cha maparachichi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na tuhuma hizo za ufisadi kutoka kwa vyama vya msingi dhidi ya KNCU wananchi wa maeneo yanayozunguka shamba hilo wana uhitaji mkubwa wa ardhi na wameiomba serikali hata kabla ya shamba hilo kupigwa mnada ili serikali iweze kupima shamba hilo na kuwamilikisha baada ya KNCU kushindwa kuliendeleza na kulitumia kama collateral kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha. Taarifa kuhusu shamba hili na ufisadi wote uliofanyika zinajulikana katika ngazi zote za serikali kwa sababu ni za muda mrefu zikiwemo idara ya Usalama wa Taifa na TAKUKURU.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na sakata la mali za KNCU ikiwemo waliohusika na kuhujumu shamba la Garagua na kuona namna gani wanaweza kuzungumza na mwekezaji aliyeuziwa Shamba hilo kwa mnada kama anaweza kuachia wananchi shamba hilo.

Mheshimiwa Spika, mashamba mengine ya ushirika ni yale yaliyopo Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro ambapo baadhi ya vyama vya msingi wameyatumia kwa muda mrefu kuyakodisha kwa wananchi kila msimu wa kilimo kwa maslahi binafsi na sio kwa manufaa ya ushirika. Kwa kuwa kuna uhaba mkubwa wa ardhi kwa wananchi wa Jimbo la Hai, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa serikali iyachukue mashamba hayo na kuyapima na kuwapa wananchi hasa wenye kipato cha chini ili wayamiliki kihalali kuliko kuyaacha kuwa sehemu ya mapato kwa viongozi wachache wa vyama vya msingi. Aidha, mashamba haya yanaweza kutumiwa na wananchi kuzalisha kwa wingi kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji na kuwa chanzo cha mali ghafi za viwanda vinavyoshughulika na mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Waziri anatambua maombi ya muda mrefu ya wananchi wa Hai kupitia kwa Halmashauri ya Wilaya kuomba sehemu ya ardhi ya Kiwanda cha Machine Tools ambacho kwa sasa hakizalishi. Msingi wa maombi ya wananchi ni kutaka sehemu ya ardhi ijengwe ofisi za Mji Mdogo wa Hai ambao utakuwa ni sehemu ya kuendeleza biashara za wananchi lakini kikubwa zaidi ni ujenzi wa Kituo cha Polisi ambacho kitaimarisha ulinzi katika eneo hilo ambalo limekuwa likiathiriwa kwa kiasi kikubwa na matukio ya ujambazi. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuhoji kama maombi hayo Wizara imeyafanyia kazi.


16. *Mapitio ya Bajeti ya Mwaka 2016/2018 na Mwelekeo wa Bajeti ya Mwaka 2017/2018*

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Wizara ilitengewa jumla ya shilingi 61,873,949,000/= kati ya fedha hizo, miradi ya maendeleo ilitengewa shilingi 20,000,000,000/= ambazo shilingi 10,000,000,000/= zikiwa fedha za ndani na shilingi 10,000,000,000/=. Fedha za matumizi mengineyo zilizotengwa ni shilingi 25,531,158,000/=

Mheshimiwa Spika, takwimu za wizara zinaonesha kuwa hadi mwezi februari, 2017, fedha za matumizi mengineyo (OC) zilizopokelewa ni shilingi 9,994,249,148/- sawa na asilimia 39.2 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Aidha kwa miradi ya maendeleo fedha zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi 7,626,219,314/= sawa na asilimia 38, lakini katika hizo fedha za maendeleo kuna shilingi 3,301,058,684.65 kwa ajili ya kulipia deni la Mkandarasi aliyeandaa Mipango Kabambe ya Majiji ya Arusha na Mwanza

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo ni kwamba fedha halisi zilizopokelewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha bajeti ya mwaka 2016/17 ni shilingi 4,325,160,629.4 tu sawa na asilimia 21.62 pekee.

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2017/18 Wizara inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 68,030,880,526/- kwa ajili ya kutekeleza kazi zake. Kati ya fedha hizo shilingi 21,470,166,074/- ni matumizi mengineyo, ikiwa ni pungufu ya shilingi 4,060,991,926/- kwa kulinganisha na maombi ya mwaka jana kwa matumizi mengineyo. Fedha za maendeleo zinaombwa jumla ya shilingi 25,400,000,000/-

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa wizara hii bado inao uwezo wa kukusanya mapato mengi, lakini haiwezi kufanya hivyo kama uwekezaji hautafanyika. Hii inaonekana wazi kwa kuangalia kiasi kilichotengwa mwaka jana na kilichotolewa. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri fedha za maendeleo ziongezwe ili upimaji wa ardhi na umilikishwaji ufanyike kwa haraka ili kodi ya ardhi ikusanywe. Uwezi kuvuna usipowekeza!!

17. *Hitimisho*

Mheshimiwa Spika, imekuwa dhamira na dira yetu ya Kambi Rasmi ya Upinzani kutochoka kutimiza haki na jukumu letu la kikatiba, kisheria na kikanuni la kuikosoa na kuishauri Serikali ya CCM japo tunapata masimango, mabezo, dharau n.k Tunaamini Mungu anaona na siku moja atatenda. Na kama sio leo au kesho vizazi vyetu vijavyo vitatoa hukumu ni yupi alikuwa kikwazo.
Mheshimiwa Spika, hotuba zetu za miaka ya nyuma tumekuwa tukishauri na tunaendelea kushauri kuwa;
1. Tukae kama Taifa kujipanga upya kutengeneza dira kupitia katiba mpya inayozungumzia namna ya kusimamia na kugawa rasilimali Ardhi.
2. Ni vyema Wizara hii na Serikali kwa ujumla ikapanga katika bajeti zake. Mambo machache ya kufanyiwa kazi (Kwa kuangalia vipaumbele) kuliko utaratibu wa sasa wa kujirundikia majukumu mengi ambayo kwa ufinyu mkubwa wa mapato ya Serikali yamekuwa yanatekelezwa kwa uhafifu na hivyo kuonekana kama ghilba kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoshauri, tungelikamilisha mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (Intergrated land Management of land information system) tungelipunguza au kuondoa kabisa migogoro ya ardhi nchini. Pia Serikali ijitazame upya juu ya utaratibu wa kugawa maduhuli yake kwa ofisi, Wizara na taasisi zake; je inatoa kwa uwiano ulio sawa au inatolewa kwa mfumo wa utaratibu wa “mwenye kisu kikali ndiye mla nyama”.


Mheshimiwa Spika, kama hatujaliona hilo la kujipanga upya na kuendelea kufanya kazi kimazoea kwa kutegemea umahiri au zaidi mitizamo ya mtu mmoja aliyeko katika nafasi ya kimaamuzi kwa wakati huo, ni wazi marathoni yetu ya utatuzi wa kero za ardhi haitakuwa na mwisho.

Mheshimiwa Spika, kwa staili hii, ni kwamba tutaendelea kubadilisha chupa lakini mvinyo utaendelea kuwa ni uleule.


________________________
*WILFRED MUGANYIZI LWAKATARE (Mb)*
*MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA WAZIRI* *KIVULI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI*
*25 Mei 2017*
 
Mh. Nashukuru umeliongelea vizuri. naisoma hotuba yako. Asante sana. Nakuomba uwe na appointment na Lukuvi mliongelee hilo maana litaleta floodgate of litigation!
 
Sawa Ndugu yangu. Asante
Mkuu heshima kwako...... ombi langu mkiwa mnapost hotuba zenu humu mtusaidie pia kuweka na format ya pdf ili mtu aweze kuipakua na kuisoma hta baadae na kwenye format nzuri zaidi otherwise hotuba ni nzuri sana na mnatupa sababu ya kuendelea kuwaombea makamanda wetu huko bungeni
 
Haya utasikia miaka saba ijayo (kama magamba watapita kwenye tundu la sindano) yakianza kutekelezwa na wakishangilia!
 
Back
Top Bottom