Mapambano FFU na wananchi Hanang | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mapambano FFU na wananchi Hanang

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Ex Spy, Dec 18, 2009.

 1. Ex Spy

  Ex Spy Senior Member

  #1
  Dec 18, 2009
  Joined: Jan 15, 2007
  Messages: 139
  Likes Received: 82
  Trophy Points: 45
  ASKARI wa FFU wamesalimu amri dhidi ya vijana wa kibarbaig wilaya ya Hanan'g mkoani Manyara na kuomba msaada wa askari wengine kutoka mjini Babati kufuatia maofisa waliopelekwa kupima ardhi kudhibitiwa na vijana wa kibarbaig waliojificha msituni kwa ajili ya mapambano.

  Taarifa zinaeleza zaidi kuwa askari wa FFU walilazimika kutumia risasi za moto pamoja na mabomu kupambana na vijana hao wa kibarbaig wanaotumia silaha za kijadi kupambana na askari hao lakini walishindwa na kulazimika kukimbia eneo hilo la tukio. FFU wanalazimisha eneo la malisho la wafugaji hao kupimwa kwa lazima na kugawiwa wakazi waliovamia mlima Hanang'.

  Hata hivyo hakuna mtu yoyote aliyejeruhiwa licha ya wapambanaji wa kibarbaig kutokwa machozi kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakirushwa na askari wa FFU Wilaya ya Hanang' kwa lengo la kuwatawanya wananchi hao waliozingira eneo zima la shamba la Warret.  Na Mwandishi Wetu, Hanan'g

  [​IMG]

  Vikosi mbalimbali vya vijana wa Kibarbaig wapato 2000 wakielekea kujificha katika pori ndani ya shamba la NAFCO wakilinda eneo hilo na kujitayarisha kwa mapambano dhidi ya askari wa FFU. Morani hao wanapinga eneo hilo kuchukuliwa na Serikali ya wilaya kwa nguvu na kugawiwa wananchi waliovamia mlima Hanan'g.(Picha na Mpiga picha wetu).

  VIJANA wa kibarbaig zaidi ya 2000 wa vijiji vya Mogitu, Min'genyi na Gidagamo katika kata ya Mogitu, tarafa ya Mulbadaw wilayani Hanan'g, Manyara wameingia msituni kujiandaa kwa mashambulizi dhidi ya Serikali ya wilaya ya Hanan'g kwa kile walichodai Mkuu wa Wilaya hiyo Winifrid Lugubi kutangaza kuchukua maeneo yao ya kufugia kwa kutumia nguvu za jeshi na kuyagawa kwa wakazi waliovamia mlima Hanan'g.

  Aidha vijana hao wamesema wako tayari kufa kwa ajili ya kutetea haki yao ya kumiliki ardhi hiyo waliodai kurejeshewa na Serikali hivi karibuni baada ya lililokuwa shirika la taifa la chakula NAFCO kushindwa kuendesha mashamba hayo waliyopokonywa miaka ya sabini.

  Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo juzi wafugaji hao waliokuwa wamejificha ndani ya vichaka wakilinda shamba hilo linalojulikana kwa jina la Warreet walisema siku ya nne sasa ndugu zao 17 wamekuwa wakishikiliwa na jeshi la Polisi akiwemo Mwenyekiti wa kijiji cha Mogitu Israel Dawii kwa madai ya kuchochea mgogoro na kuwazuia maafisa ardhi kupima ardhi ya vijiji hivyo.

  Walisema kufuatia hali hiyo vijana wa jamii hiyo wameamua kuungana na kuunda vikosi zaidi ya tisa kila kimoja kikiwa na watu wasiopungua mia mbili wakiwa na silaha za kijadi mikuki, fimbo na marungu wakizunguka eneo hilo la shamba la waret walilogawiwa hivi karibuni na viongozi wao wa vijiji kuhakikisha mtu yoyote haingii ndani ya shamba hilo.

  Faustine Mafa wa kijiji cha Mogitu anayeongoza moja ya kikosi chenye zaidi ya vijana mia mbili alisema viongozi wa wilaya wakiongozwa na Mkuu wa wilaya amekuwa wakishinikiza kugawa ardhi yao kwa lazima bila ya wao kushirikishwa.

  Alisema viongozi hao wa wilaya wanataka kugawa eneo hilo kwa wakazi waliovamia eneo la mlima Hanang' ambao sio wahusika wa eneo hilo huku wenyeji wakiendelea kuteseka kwa kukosa malisho na maeneo ya kilimo.

  "Leo ni siku ya nne tupo nje kwa ajili ya mapambano na mtu yoyote atakaejipendekeza kuja kupima ardhi yetu tena, hakika tutamdhibiti hatuko tayari kabisa kwa hilo na hatutarudi nyumbani hadi ndugu zetu waliowakamata wawaachie,"alisema Gidumur Marja mkazi wa kijiji cha Gidagamor.

  Kwa upande wake kiongozi wa vikosi vyote Bw.Mangi Gitagurenda alisema kufuatia viongozi wa Wilaya ya Hanang wakiongozwa na Mkuu wa wilaya kulazimisha kugawa maeneo yao waliyoyatenga kwa ajili ya kilimo na ufugaji kwa wakazi waliovamia mlimani ambao sio wenyeji wa eneo hilo baadhi ya wakazi wamekuwa wakitaka kujinyonga kwa hasira.

  " Hatutaki jamii yetu kuendelea kuteseka kwa ukosefu wa ardhi, NAFCO ilipokuja ilituhamisha na kukimbilia mikoa mbalimbali ambayo hivi sasa tunahamishwa na kuambiwa turudi tulipotoka, sasa waende wapi zaidi ya kuja hapa?, tumejipanga hatutatoka hapa kama wanataka kuchukua maeneo yetu askari waje hapa tupambane na watuulie hapa hapa,"alisema Mangi.

  Akizungumzia sakata hilo ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Parmena Sumary alikiri kukamatwa kwa wafugaji hao 17 akiwemo Mwenyekiti wa kijiji cha Mogitu Israel Dawii kwa madai ya kuchochea vurugu na kuzuia watendaji wa Serikali wasifanye kazi zao.

  " Ni kweli tumewakamata na wapo mahabusu hivi sasa na tunaendelea kuwatafuta wengine ambao waliwazuia watendaji wa Serikali wasifanye kazi zao za kupima ardhi kama walivyoagizwa….hata hivyo RC alishafanya mikutano na wananchi hao na kukubaliana kuchukua sehemu ya eneo la mifugo lililotengwa na vijiji na kugawiwa watu waliovamia mlima Hanang',"alisema Mkuu huyo wa Polisi.

  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanan'g Good Pamba na Mkuu wa Wilaya wote kwa pamoja walikataa kuzungumzia mgogoro huo ambapo Mkurugenzi kwa upande wake alidai kutozungumza mpaka mkuu wake wa wilaya atakapokuwepo na Mkuu wa wilaya, Winifrid Lugubi alipopigiwa simu kuelekeza mgogoro huo aligoma na kuwataka waandishi wa habari kuzungumza na watu waliowapeleka katika eneo la tukio.

  Mkuu wa Mkoa wa Manyara Henry Shekifu aliyekuwa jijini Mwanza kikazi alipoulizwa kuhusiana na mgogoro huo alisema wafugaji waliokamatwa walisababisha vurugu kwa kuwazuia watendaji wa Serikali kupima eneo hilo na kwamba alishafanya vikao na wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo la shamba la Warret na kukubaliana kumega sehemu ya eneo la mifugo kwa ajili ya wakazi waliovamia milimani.
   
 2. LiverpoolFC

  LiverpoolFC JF-Expert Member

  #2
  Oct 21, 2011
  Joined: Apr 12, 2011
  Messages: 11,001
  Likes Received: 153
  Trophy Points: 160
  Wandugu! Hii kasheshe ilifikiaga wapi? Mwenye ufafanuzi a2juze wajameni!
   
Loading...