Maoni ya ACT wazalendo miswada ya sheria za madini

procura

Member
Jul 14, 2013
34
25
Maoni ya Chama cha ACT Wazalendo Kuhusu Mabadiliko ya Sheria Zinazohusu Rasilimali za Taifa:

1. Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
2. Sheria ya Uhuru wa Milele wa Utajiri wa Taifa ya mwaka 2017.
3. Sheria ya Mapitio ya Mikataba ya Utajiri wa Taifa ya mwaka 2017.

Utangulizi:

Kwa takribani miaka 10 sasa kumekuwa na harakati za wananchi na wanasiasa wa vyama vya upinzani kupitia Bunge kuleta mabadiliko makubwa kwenye Sheria zinazosimamia utajiri wa asili wa nchi yetu kama madini, mafuta na gesi, ardhi, misitu, na kadhalika.

Juhudi za kuleta mabadiliko ya sheria za madini zilikuwa kubwa zaidi na kuanza kushika kasi kufuatia sakata la Mkataba wa Mgodi wa Buzwagi la mwaka 2007. Agosti, 2017 mjadala wa Buzwagi utafikisha miaka 10. Mjadala huo ulipelekea kutangazwa kwa Azimio la Songea la Septemba, 2007 na kisha kuundwa kwa Kamati ya Bomani, Novemba 2007, iliyopitia mikataba yote ya kuvuna rasilimali madini, kisheria na kisera.

Taarifa ya Kamati ya Bomani iliwezesha sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010 kutungwa, kufuatia sera ya Madini ya mwaka 2009. Tangu mwaka 2010 kumekuwa na mabadiliko ya sheria mbalimbali za masuala ya fedha zilizojaribu kurekebisha hali ya nchi yetu kutofaidika na sekta ya madini. Ikumbukwe kwamba wakati sekta ya madini inachangia takribani 40% ya mauzo yote ya nje ya Taifa, lakini huchangia takribani 4% tu ya Pato la Taifa. Tunauza 40%, lakini mapato yetu ni 4% tu.

Kwa miaka zaidi ya 20 tangu kuanza kuvunwa kwa kiwango kikubwa madini yetu, na hasa dhahabu, umasikini wa Watanzania umekuwa haupungui. Wakati takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 - 2016 tumeuza nje madini yenye thamani ya takribani shilingi 50 trilioni, Taifa lilipata mapato ya takribani shilingi 3 trilioni tu sawa na chini ya 10% ya mauzo yote. Kwa hakika Tumeshindwa kutegua kitendawili cha nchi tajiri yenye watu masikini.

Mwaka 2015, chama chetu cha ACT Wazalendo kiliingia kwenye Uchaguzi mkuu kikiwa na Ilani iliyojaribu kujibu changamoto kuu tatu kwenye sekta ya utajiri wa rasilimali za nchi yetu:

1. Umiliki wa Rasilimali zetu.
2. Mfumo wa uvunaji wa rasilimali zetu.
3. Mfumo wa kodi kwenye sekta ya rasilimali zetu.

Ibara ya 5.2.4 ya Ilani ya Uchaguzi ya chama cha ACT Wazalendo (Ukurasa wa 21) ilianisha hatua 3 muhimu za kuchukua ili kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya maliasili ya nchi. Hatua hizo 3 ni zifuatazo:

1. Maliasili zote za madini, mafuta na gesi asilia ziwe mali ya wananchi KIKATIBA na uchimbaji wake lazima uwe na kibali cha wananchi (free prior informed consent).
2. Mfumo wa uchimbaji wa maliasili hizi ubadilike kutoka mfumo wa sasa wa kutoa leseni na kukusanya kodi kwenda mfumo wa umiliki na ukandarasi (Serikali imiliki, Mchimbaji/Mwekezaji awe Mkandarasi).
3. Mikataba yote ya uvunaji wa maliasili iwe wazi kwa wananchi.

Machi, 2017 Serikali ilipiga marufuku kusafirishwa kwa makontena ya mchanga wenye madini (copper concentrates) kwenda nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji, ili kujenga kinu cha kuchenjua hapa hapa nchini. Kufuatia marufuku hiyo kamati 2 ziliundwa kwa lengo la kutazama kama tunaibiwa katika usafirishaji huo na kupendekeza mabadiliko ya sheria mbalimbali ili kudhibiti hali hiyo.

Kamati zilirejea mapendekezo ya Kamati ya Bomani kuhusu sheria za madini. Juni, 2017 Chama cha ACT Wazalendo kiliwasilisha Serikalini maazimio ya Kongamano la Rasilimali za taifa ili kuboresha sheria za madini na kuwezesha nchi kufaidika na utajiri wake wa rasilimali. Julai 2017 Serikali imeleta mapendekezo ya kubadili sheria mbalimbali ili kuzingatia ushauri wa muda mrefu wa viongozi mbalimbali wa kisiasa na wanaharakati wa asasi za kijamii kutaka nchi imiliki utajiri wake wa asili na kwamba kuwe na uwazi wa mikataba ya kuvuna rasilimali husika.

Kupitia tovuti ya Bunge, chama chetu kimepata miswada mitatu iliyowasilishwa bungeni kwa ajili ya mjadala na kisha kuwa sheria kama itapitishwa na Bunge. Miswada hiyo ni ifuatato:
1. The Written Laws (Miscellanous Amendments) Act, 2017.
2. The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Renegotiation of unconscionable terms) Act, 2017
3. The Natural Wealth and Resources (Permanent sovereignty) Act, 2017.

Kamati mbili za kisekta za chama cha ACT Wazalendo zinahusika na uchambuzi wa masuala ya sheria na mambo ya kisera na utafiti (Kamati ya Sheria na Katiba, pamoja na Kamati ya Sera na Utafiti) zilipewa jukumu la kupitia miswada yote mitatu, kufanya uchambuzi wa kina, na kupendekeza maoni kulingana na Sera za chama chetu. Kamati zilibeba jukumu hilo kwa unyeti mkubwa, na kuwasilisha maoni ya kamati kwa Kamati ya Uongozi ya ACT Wazalendo. Mara tu baada ya maoni haya kuwasilishwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Chama, kujadiliwa na kupitishwa, chama cha ACT Wazalendo kinayaleta mapendekezo yake kama ifuatavyo.

1. MUSWADA WA SHERIA wa 'The Natural Wealth and Resources (Permanent sovereignty) Act, 2017.

ACT Wazalendo inapongeza hatua madhubuti zilizochukuliwa kutangaza rasmi kwamba utajiri wa nchi ni mali ya wananchi wa Tanzania. Hii ni mara ya kwanza tangu nchi yetu ipate Uhuru kwa Serikali kuitangazia dunia kwamba utajiri wa nchi ni mali ya wananchi. Hata Katiba ya nchi ya nchi yetu haikuwahi kutambua Azimio la Umoja wa Mataifa namba 1803 la mwaka 1962 linalotamka kuwa nchi huru zina uhuru wa rasilimali zao.

Hata hivyo muswada huu umeshindwa kung’amua kuwa umiliki wa utajiri bila ya kudhibiti mfumo wa uvunaji ni sawa na bure kwani haina maana yeyote. ACT Wazalendo tunapendekeza maboresho yafuatayo:

a. Kifungu cha 4 (3) kiongezwe – 'Natural wealth and resources shall be extracted in such a manner that the right (mineral right) is held by the state through a designated public entity and that the model shall be a production sharing agreement'.

Madhumuni ya marekebisho haya ni kuwezesha uwepo wa Shirika la Umma ambalo ndio litakuwa na hati ya umiliki (mineral right) badala ya hati hiyo kuitoa kwa Kampuni za uwekezaji. Shirika hilo la Umma litaingia mikataba ya kugawana mapato na wenye mitaji watakaowekeza kwenye kuvuna utajiri wetu. Mfumo huu utaendelea kuyafanya madini kuwa mali ya Taifa, na mchimbaji/mwekezaji kuwa mkandarasi kwenye uvunaji. Mfumo huu tunaoupendeleza ndio unaotumika sasa kwenye sekta ya mafuta na gesi asilia.

b. Kifungu cha 5 (3) kiandikwe upya kwa kuongeza maneno kwamba ni lazima kupata kwanza kibali cha wananchi wa eneo husika kabla ya kupewa leseni ya kutafuta na kuchimba madini kwenye eneo hilo (principle of free prior informed consent). Madhumuni ya mapendekezo haya ni kuwapa nguvu Wananchi watakaoathirika na uvunaji ili wawe na sauti kuanzia hatua ya awali kabisa. Kibali cha wananchi kitawezesha pia wenye mitaji kuingia makubaliano ya kimaendeleo na wananchi kabla ya kuanza kuvuna utajiri. Kifungu hiki kitaondoa kabisa migogoro kati ya wenye mitaji (wawekezaji) na wananchi wanaozunguka migodi.

c. Kifungu cha 12 Maneno “May be” yaondolewe na badala yake maneno “Shall be” yaongezwe. Hii italipa Bunge mamlaka zaidi kwani kitafsiri ya kisheria neno “may” halimlazimishi mtu au chombo kufanya jambo husika lakini neno “shall” linamlazimisha mtu au chombo kufanya jambo hilo. Shall equals Must.

d. Kifungu cha 14 kiongezwe kwamba mabadiliko yeyote ya sheria hii Tatafanywa iwapo tu kutakuwa na kura ya maoni (referendum) ambayo 75% ya watu wenye umri wa kupiga kura wataunga mkono. Madhumuni ya marekebisho haya ni kuufanya muswada huu kuwa wa wananchi na kuzuia uwezekano wowote wa Serikali yeyote kubadilisha sheria hii kirahisi bila kupata ridhaa ya wananchi wenyewe.

2. MUSWADA wa 'The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Renegotiation of unconscionable terms) Act, 2017.

ACT Wazalendo inapongeza hatua hii kubwa ya kuhakikisha kuwa mikataba yote ya rasilimali za nchi itakuwa inawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa (lazima kuidhinishwa kabla ya kuanza kutumika). Ni hatua muhimu sana na ya kimapinduzi na kiukombozi. Chama cha ACT Wazalendo kina pendekezo moja tu kwamba;

Mabadiliko yeyote ya sheria hii, yatakuwa yamepitishwa iwapo theluthi mbili ya wabunge wataunga mkono. Madhumuni ya marekebisho haya ni kuhakikisha kuwa inakuwa ni vigumu Kwa chama chochote cha siasa au Serikali kuchezea sheria hii muhimu na nyeti Sana.

Pia tunapendekeza ili kulipa bunge Mamlaka ya kupitia mikataba husika pamoja na kuingia katika kuitazama upya mikataba hiyo (renegotiation) basi Kifungu cha 4 (1) neno “May” libadilishwe na badala yake liingizwe neno “Shall”. Hili litaipa mamlaka zaidi Bunge ya kupitia mikataba husika kwa mujibu wa tafsiri ya kisheria ya maana ya maneno hayo mawili. Lakini pia itafanya Kifungu hiki kiendane na kubeba maana na uzito sawa na kifungu kinachofuata yaani Kifungu cha 5 .

3. MUSWADA wa 'The Written Laws (Miscellanous Amendments) Act, 2017.

Muswada huu unapendekeza masuala kadhaa ya kuboresha usimamizi wa sekta za rasilimali na haswa sekta ya madini. Tunaleta mapendekezo ya kuboresha vifungu kadhaa ili kuimarisha sheria yenyewe na iwe na faida Kwa Taifa. ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:

a. Kifungu cha 4 kianzishe Mamlaka ya Madini badala ya Tume ya Madini. Mamlaka ya Madini iwe mdhibiti (regulator) wa sekta na ihusike pia na utoaji wa leseni na usimamizi wa migodi. Mamlaka pia isimamie Mfuko wa Maendeleo wa Sekta ya Madini. Mtendaji Mkuu wa Mamlaka aitwe Mkurugenzi Mkuu. Mahala popote panapotaja Tume pataje Mamlaka

b. Kifungu cha 5 (1) kiondoe maneno Rais na kuweka maneno Bunge. Tunajua kuwa kifungu hiki kinaendana na sheria ya ardhi ya sasa ambapo ardhi ipo chini ya milki ya Rais lakini tunadhani ni muhimu sasa kuhamisha milki hii kuwa chini ya wananchi kupitia Bunge. Madhumuni ya mapendekezo yetu yataleta mambo yafuatayo:

1. Yatarudisha umiliki wa madini mikononi mwa wananchi.
2. Yatalipa Bunge, ambacho ni chombo cha wananchi cha uwakilishi, mamlaka ya usimamizi wa rasilimali kwa niaba ya wananchi.
3. Mabadiliko hayo yanajenga mfumo wa usimamizi shirikishi badala ya kumtegemea Rais tu.
4. Yanampa Rais mamlaka kwani bado anamamlaka Kupitia "Mamlaka" itakayoundwa na kusimamiwa na Serikali.
5. Rais bado ana ‘radical title’ ya Ardhi, hivyo atashiriki kutoka siku ya kwanza wakati wa uvunaji kupitia taasisi zifuatazo:
a) Kupitia wizara husika ya Ardhi
b) Wizara ya Madini
c) Mamlaka ya Madini
d) Serikali za vijiji na Mikutano mikuu ya Vijiji

c. Kifungu cha 8 (1) kiongezwe maneno yafuatayo - 'The consent of the licensing authority where it is required shall not be given unless there is a free prior informed consent of the people surrounding the proposed operations subject to guidelines by the minister'. Madhumuni ya marekebisho haya ni kuendana sasa na dhana nzima kuwa utajiri huu ni mali ya wananchi na kwamba wananchi wa maeneo yanayochimbwa madini wawe na sauti kabla ya leseni kutolewa. Kifungu hiki kinaunganisha sheria ya Kwanza hapo juu na sheria yenyewe ya Madini.

d. Kifungu cha 9 – Kifungu hiki kinaendeleza mfumo ule ule wa zamani wa kuvuna utajiri wa Nchi yetu. Tunapendekeza kifungu hiki cha 9 KIFUTWE kabisa, kufuatia kubadili mfumo wa uvunaji kuwa wa kugawana mapato (Production Sharing Agreements - PSAs) kati ya mkandarasi (mwekezaji) na mmiliki. Iwapo tutakuwa tumebadili mfumo wa kuvuna rasilimali za nchi kwenda kwenye mfumo wa PSAs, sababu za kifungu hiki zinakuwa hazipo tena.

e. Kifungu cha 28 (2) - kiongezwe (f) Parliament. Lengo la nyongeza hii ni ili kuweka milki ya utajiri wa rasilimali za nchi kwa wananchi wenyewe kupitia Bunge badala ya Rais.

f. Tunapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya kwamba asilimia 20% ya Mapato yatokanayo na Mrahaba yatarudi kwenye Halmashauri yenye mgodi husika. Madhumuni ya kifungu hiki ni kuwezesha wananchi wanaoishi jirani na migodi kupata sehemu ndogo ya mapato ili kukabiliana na changamoto za shughuli husika.

HITIMISHO:

Chama cha ACT Wazalendo kinakaribisha mapinduzi haya makubwa kwenye sekta ya rasilimali za nchi. Mabadiliko haya yanaendana na Sera za chama chetu zinazojengwa kwenye Misingi ya Azimio la Tabora lililotangaza Siasa ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Mabadiliko haya ni jawabu la swali la muda mrefu kuhusu milki ya rasilimali za Taifa na jawabu hilo litakuwa kuwa ‘Wananchi wa Tanzania ndio wamiliki wa utajiri wao’.

Emanuel Mvula
Mwenyekiti - Kamati ya Sera na Utafiti - ACT Wazalendo

Thomas Matatizo Msasa
Mwenyekiti - Kamati ya Sheria na Katiba - ACT Wazalendo

Stephen Ally Mwakibolwa
Katibu - Kamati ya Sheria na Katiba - ACT Wazalendo

Idrisa Kwekweta
Katibu - Kamati ya Sera na Utafiti - ACT Wazalendo

Omar Said Shaaban
Mwanasheria wa Chama – ACT Wazalendo

Albert Gasper Msando
Mwanasheria wa Chama – ACT Wazalendo

Ado Shaibu Ado
Mwanasheria wa Chama – ACT Wazalendo
Juni 30, 2017

ZINGATIA

Muswada wa Umiliki wa Milele unaibua upya suala la Dola ( sovereignty ). Dola ni Jamhuri ya Muungano lakini kwenye Muswada Zanzibar imeondolewa. Hii Inatukumbusha umuhimu wa Katiba Mpya. Tanzania Bara sio Dola.
 
Zitto bana...aandike yeye kisha aseme ACT....ahahah...msandoooo. hivi skendo ya giggy haikukuvua hivi vyeo kweli...mbona bado unatokelezea?...
 
.... This is our problem, badala ya kujikita kwenye mapendekezo yao wewe unaleta masighara, baadae mkiliwa na wajanja mnaanza kulia lia na kuandamana eti mnapongeza juhudi...
Wewe umeona nini cha maana walichoandika hao ACT?...

tuache utoto na kushabikia upuuzi...ishu iko bungeni wakajadili bungeni sio watuletee taarifa mahala pasipostahili...zito akatoe maoni yake huko bungeni...alisema muda unatosha kupitia hati ya dharula...

yeye anavyotuletea waraka ulioandikwa na chama chake kasoro mama anna mghirwa anataka tumuelewe vip?

acha unafiki kuwa mkweli usishabikie upuuzi wa zito na msando giggy pesa.
 
Zitto bana...aandike yeye kisha aseme ACT....ahahah...msandoooo. hivi skendo ya giggy haikukuvua hivi vyeo kweli...mbona bado unatokelezea?...
Eti wanasema pale alishika Nguo, na sio Nyapu, so actually was not a scandal
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom