Maoni: Mh. Rais, Sera ya Viwanda iendane na Teknolojia

Mtangoo

JF-Expert Member
Oct 25, 2012
6,167
5,610
Mh. Rais na wasaidizi wako. Naomba nikupongeze kwa kuja na sera ya viwanda. Kusema kweli Tanzania tuliyumba sana katika viwanda na usipokuwa na viwanda hata vya kuunganisha vitu (assembly industries) basi utakuwa mtu wa kununua kila kitu na hili si jambo jema.

Lakini naomba nigusie eneo lingine muhimu ambalo halijavunwa vya kutosha. Tukiwa wawazi ni kama halijavunwa kabisa. Nianze na kukumbusha mheshimiwa Rais kuwa baada ya kuwa Rais mteule, Mh. Donald Trump alikutana na watu ambao kwa maelezo yake alidhani wana nafasi ya kukuza uchumi wa Marekani na kuifanya Marekani "Taifa kubwa tena". Alikutana na watu wa viwanda na baadaye makampuni yanayojihusisha na Teknolojia.

Katika hotuba yake kwa Wana Teknolojia hawa Rais Trump aliyasema haya:

"Katika ulimwengu huu hakuna watu kama watu walio ndani ya chumba hiki. Chochote tunachoweza kufanya kuhakikisha hili linasonga, tutakuwepo hapa kuwasaidia/kwa ajili yenu. Mnaweza kuwapigia watu wangu, au kunipigia mimi. Hakuna tofauti yoyote. Hakuna urasimu hapa.

"In the world, there's nobody like the people in this room. Anything we can do to help this go along, we'll be there for you. You'll call my people, you'll call me. It doesn't make any difference. We have no formal chain of command around here."

Mh. Trump aligundua umuhimu wa teknolojia, kwa maoni yangu, kwa sababu ya vitu viwili (Kumbuka trump ni mfanyabiashara hivyo amejifunza kuona fursa). Kwanza haya makampuni yanaajiri watu wengi sana. Zifuatazo ni takwimu za machache ambayo yameajiri wengi zaidi:

Google Inc. - 20,000 (Wafanyakazi wa ndani) - 55,419 (Jumla ya wafanyakazi)
Apple Inc. - 19,000 (Wafanyakazi wa ndani) - 92,600 (Jumla ya wafanyakazi)
Oracle Corp. - 7,315 (Wafanyakazi wa ndani) - 122,000 (Jumla ya wafanyakazi)

Pia Uber ni kampuni ambayo imewekeza nchi nyingi na sasa imeingia nchini kwetu.

Mh. Rais, kitu cha pili ambacho nadhani Mh. Trump alikiona ni kile kiingereza wanaita "Movers and Shakers", yaani wale wanaoathiri na kutoa mwelekeo wa maisha. Kwa sasa kila mtu anajua Teknohama ndio "movers and shakers" wakuu. Kuanzia WhatsApp, Facebook, LinkedIn mpaka kwenye Afya, Utalii, na hata Computer na Security na kwenye vita: Aliyetangulia katika Teknohama katangulia kwenye vingine.

Mh. Rais, kwa maoni yangu ni kuwa kuna umuhimu mkubwa wa sisi kama taifa kujitafakari mwelekeo wetu kiteknolojia na hasa kwa upande wa Teknohama. Bado tuna nafasi nyingi sana za kufanikiwa kama tutawahi kuchukua hatua ya kukuza uwezo wetu nchini.

Mh. Rais, najua unajua mengi ya matatizo yetu. Ila kubwa ambalo sisi watu wa upande huu wa teknolojia tumelikosa ni kuwa tumebaki yatima. Serikali zote zilizopita hazikuwekeza vya kutosha katika Teknolojia. Kuanzia elimu yetu, mpaka kazi zetu, tumekuwa watumiaji zaidi kuliko wazalishaji. Lakini hili lina sababu zake.

Mh. Rais, kwa bahati mbaya baadhi ya sera zimekuwa kinyume nasi na hazijatungwa kwa kuangalia uhalisia wa mazingira ya kwetu. Hazikutushirikisha wadau na zipo kusimamia zaidi kuliko kulea vipawa vya Watanzania.

Mh. Rais, tunatamani siku moja kuwa na mazungumzo nawe au Mwakilishi wako atakayechukua maoni, matatizo na masuluhisho toka kwa wadau wa teknolojia ili serikali yako iyafanyie mapitio na kuyatafutia ufumbuzi na pamoja kama taifa tusogee toka hapa tulipo. Maendeleo ya viwanda yanapendeza yakiendana na ukuaji wa Teknolojia.

Nikutakie kazi njema Mh. Rais na Wasaidizi wako wote. Niombe radhi kwa mpangilio usio wa kupangiliwa sawia. Ni kwa sababu naandika haraka ili niwahi kuendelea na kazi.

Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu wabariki Watanzania!
 
Back
Top Bottom